Thursday, November 23, 2017

WAZIRI MKUU AKABIDHI CARRY KWA TIMU YA AFISI KUU ZANZIBAR

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekabidhi zawadi ya gari aina ya carry kwa timu ya mpira wa miguu ya Afisi Kuu Zanzibar baada ya kuibuka mshindi katika mashindano ya mpira wa miguu ya Majimbo.

Mashindano hayo yaliyohusisha majimbo 18 ya kisiwani Unguja yaliandaliwa na Chama Cha Mapinduzi Zanzibar ambayo yalizinduliwa Machi 23, 2017 na Rais wa Zanzibar Dkt. Mohammed Shein.

Alikabidhi zawadi hiyo jana (Jumamosi, Novemba 25, 2017) katika mechi ya fainali iliyozikutanisha timu ya Afisi Kuu na timu ya Jimbo Kwahani. Katika mechi hiyo ya fainali Afisi Kuu iliibuka na ushindi wa magoli matatu na Jimbo Kwahani iliambulia goli moja.

Waziri Mkuu aliipongeza CCM Zanzibar kwa kubuni mashindano hayo ambayo yaliwakutanisha vijana. Alisema mbali na kuimarisha afya zao pia ni chanzo cha ajira hivyo ameishauri CCM upande wa Bara kuiga ubunifu huo.

“Ubunifu huu wa kuanzisha mashindano ya majimbo unapaswa kuigwa na Tanzania Bara, waanzishe mashindano haya kwa kuyakutanisha majimbo yote. Ni vema jambo hili likawa la Kitaifa ili kunufaisha vijana wengi.”

Pia Waziri Mkuu alimpongeza Muwakilishi wa Jimbo la Uzini, Mohammed Raza ambaye ndiye alikuwa mdhamini mkuu wa mashindano hayo, pia aliwashauri vijana walioshiriki mashindano hayo kuendelea kufanya mazoezi.

Katika mashindano hayo timu ya Jimbo Magomeni ilipewa tuzo ya timu iliyoonyesha hamasa kubwa, timu ya Jimbo Mfenesini iliibuka kidedea kwa kuongoza kwenye nidhamu na golikipa wa timu ya Afisi Kuu, Vuai Makame Jecha alipewa tuzo ya mchezaji bora.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.