Wednesday, March 20, 2024

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA KATIBA NA SHERIA YAPITISHA MAKADIRIO YA BAJETI YA MWAKA WA FEDHA 2024/2025 KWA MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA NA OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA

 


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imepitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25 ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Florent Laurent Kyombo akikaimu nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo hii leo  katika Ukumbi wa Mikutano wa Bunge Jijini Dodoma mara baada ya wajumbe kujadili na kuridhia Bajeti katika kikao kilichohusisha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Alisema baada ya majadiliano mazuri  na maelezo ya ziada kutolewa kuhusiana na  Bajeti iliyotengwa,  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala  Katiba na Sheria imeridhia.

 “Tunawatakia matumizi mema ya fedha hizi pale zitakapokubaliwa kupitishwa katika vikao vya Bunge la Bajeti na tunahitaji kuona Bajeti ya fedha hizi inaakisi matarajio ya msingi ya nchi yetu,” alibainisha.

Kwa Upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu ameishukuru kamati kwa ushauri na kupitia Bajeti hiyo kifungu kwa kifungu na kutoa maelekezo ambayo yatasaidia Bajeti hiyo kukaa vizuri wakati kusomwa Bungeni kwenye vikao vya Bunge la Bajeti.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.