Monday, March 29, 2021

Waziri Mhagama aiongoza OSHA kukabidhi Tuzo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria


 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, kwa niaba ya serikali, kupitia Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), ameikabidhi Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Tuzo yenye lengo la kutambua mchango wa kamati hiyo katika kuboresha utendaji wa Wakala hiyo.


Waziri Mhagama ameikabidhi kamati hiyo tuzo leo tarehe 29 Machi, 2021 jijini Dodoma wakati kamati hiyo ilipokuwa ikipokea taarifa ya utekelezaji wa Wakala hiyo. Amebainisha kuwa ushauri wa kamati hiyo umeiwezesha wakala kuboresha Utendaji kwa kutengeneza mifumo ya kimtandao ya kurahisisha utendaji wa Wakala hiyo, Kupunguza tozo saba zilizokuwa kero kwa wadau wa OSHA pamoja kuongeza mapato ya Wakala hiyo.


“Mara nyingi tumezoea serikali kupewa tuzo kwa kufanya vizuri lakini tumekuwa tukisahau kuwa kuna baadhi ya walioisaidia serikali kufanya vizuri. Tumepima utekelezaji na utendaji wa OSHA katika kuzingatia ushauri wenu, tumeona kwa sasa hata gawio limeendelea kuongezeka linalotolewa na OSHA kwenye serikali, mifumo ya kimtandao imetengenezwa ya kurahisisha utendaji lakini pia tozo saba zimefutwa, hivyo hatunabudi kuwashukuru kwa mchango huo umeiboresha OSHA” Amesema Mhe. Mhagama.


Tozo saba ambazo OSHA tayari imezifuta kufuatia ushauri uliotolewa na Kamati hiyo ni; Tozo ya Usajili wa maeneo ya kazi, Tozo ya Fomu ya Usajili, Tozo ya ada ya leseni ya kukidhi matakwa ya sharia ya Usalama na Afya Mahali Pa kazi, Tozo ya Ushauri wa mambo Usala na Afya, Faini zinazohusiana na vifaa vya kuzimia moto, Tozo ya elimu kwa umma, Tozo ya Uchunguzi wa ajali ambayo imepunguzwa kutoka shilingi 500,000/= hadi shilingi 120,000/=.


Akiongea baada ya kupokea Tuzo  hiyo,  Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Mohamed Mchengerwa amefafanua kuwa kamati hiyo imekuwa ikitoa ushauri kwa OSHA wa namna ya kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu pamoja na kuongeza kipato. Aidha, amebainisha kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu inayoirtaibu Wakala hiyo, imekuwa sikivu kwa kufuata ushauri wao wa kufuta tozo ambapo kwa kiasi kikubwa imekuwa ni faraja kwa watanzania na wawekezaji nchini.


Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Patrobas Katambi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Ummy Ngeriananga, Katibu Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Andrew Massawe, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda, pamoja na baadhi ya Wakurugenzi wa OSHA.


OSHA ni Wakala wa serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu). Taasisi hii ina wajibu wa kuwalinda wafanyakazi dhidi ya vihatarishi vilivyopo katika sehemu za kazi ambavyo vinaweza kusabisha magonjwa na ajali. Wajibu huu unatekelzwa kupitia usimamizi wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.


Mwaka 2001, ilianzishwa OSHA chini ya Sheria Na. 30 ya Wakala wa Serikali ya mwaka 1997 kama sehemu ya Mpango wa Maboresho katika utoaji wa Huduma za Serikali kwa wananchi. Makusudi ya kuanzishwa kwa OSHA ni kupata chombo cha serikali kwa ajili ya kusimamia Usalama na Afya mahali pa kazi. OSHA ina jukumu la kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanafanya kazi katika mazingira ambayo ni salama na yenye kulinda afya zao kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa katika kuzuia ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.

mwisho.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, akimkabidhi tuzo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ikiwa ni kutambua mchango wa Kamati hiyo katika kuboresha utendaji kazi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), leo tarehe 29 Machi, jijini Dodoma.Wanaoshuhudia ni Makamu mwenyekiti wa Kamati hiyo, Najma Giga (Kulia), Katibu Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Andrew Massawe (wa pili kulia) na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali  Pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda (kulia).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, akifafanua namna ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria jinsi ulivyoboresha utendaji wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), wakati kamati hiyo ilipokutana na  watendaji wa OSHA,  leo tarehe 29 Machi, jijini Dodoma.


Manaibu Mawaziri Ofisi ya Waziri Mkuu; Naibu Waziri, (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Patrobas Katambi, (katikati), Naibu Waziri (Wenye Ulemavu) Mhe. Ummy Ngeriananga (kulia) na Katibu Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Andrew Massawe wakifuatilia kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria na  Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), leo tarehe 29 Machi, jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Mohamed Mchengerwa, (katikati) akifafanua jinsi ushauri wa kamati hiyo ulivyowezesha Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuboresha utendaji wake, kushoto ni  Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Najma Giga na kulia ni Katibu wa kamati hiyo, Ndg. Stanslaus Kagisa, leo tarehe 29 Machi, jijini Dodoma.


Mkurugenzi wa Mafunzo, Utafiti na Takwimu wa OSHA, Joshua Matiko, akiwasilisha mada kuhusu misingi ya Afya na Usalama mahali Pa Kazi, wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ipokutana na na  Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), leo tarehe 29 Machi, jijini Dodoma.


Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na sheria wakifuatilia uwasilishwaji wa mada kuhusu misingi ya Afya na Usalama mahali Pa Kazi, wakati kamati hiyo ilipokutana na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), leo tarehe 29 Machi, jijini Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, akifuatilia uwasilishwaji wa mada ya kuhusu misingi ya Afya na Usalama mahali Pa Kazi wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ilipokutana na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), leo tarehe 29 Machi, jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Mohamed Mchengerwa, wakiwa na Tuzo iliyotolewa na Kamati hiyo kwa kuchangia ufanisi wa utendaji wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA), wengine ni wajumbe wa kamati hiyo, watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu na OSHA, leo tarehe 29 Machi, jijini Dodoma.


Read More

“Serikali kuendelea kudhibiti Dawa za Kulevya na UKIMWI nchini” Mhagama

 



Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, imeihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, kuwa imeweka mikakati ya Kudhibiti UKIMWI na Dawa za kulevya ili kuimarisha ustawi wa wananchi nchini.


Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama,tarehe  29 Machi 2021,  Jijini Dodoma, wakati akiwasilisha kwa kamati hiyo, taarifa ya Utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2020/2021 na makadirio ya  Bajeti ya mwaka 2021/2022  ya  Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya.


“Kazi hii ya kuwaokoa vijana na watanzania kwenye UKIMWI na dawa za kulevya tumeshafanya vizuri. Tumewasaidia waraibu 10,565 ambao wanapatiwa matibabu katika kliniki za Methadone nchini. Tumeandaa mkakati wa kuhakikisha kuwa waraibu hao hawarejei tena katika matumizi ya dawa za kulevya na tunafanya hivyo kupitia Idara ya Kazi na Ajira.” Amesisitiza Mhe. Mhagama.


Mhe. Mhagama amefafanua kuwa, Serikali imetengeneza mtandao wa Asasi ambapo hadi sasa kuna takribani Asasi 52 nchi nzima ambazo zinashirikiana na Serikali Katika shughuli za udhibiti wa dawa za kulevya. Aidha, ameongeza kuwa tayari mwongozo wa namna Kamati za UKIMWI za Halmashauri zitakavyoratibu shughuli za udhibiti wa dawa za kulevya na  Asasi zilizopo kwenye Halmashauri husika umeshaandaliwa.


Amesisitiza kuwa, serikali inaendelea kushirikiana na nchi nyingine kwenye kudhibiti na kupambana na Dawa za kulenya kwa kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa Katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya, amesema Operesheni za Kupambana na biashara ya Dawa za Kulevya zimefanyika kwa umakini, ambapo Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Februari 2021 wamekamatwa  jumla ya watuhumiwa 5,374 wakiwemo wanaume 4,917 na wanawake 457.

 

Kadhalika, amesema Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetoa mafunzo kwa waratibu wa UKIMWI kwa Halmashauri 185 juu ya ukusanyaji, utunzaji na matumizi ya takwimu sizizo za kitabibu TOMSHA. Pia ameeleza kuwa   ufuatiliaji na usimamizi na Ukaguzi wa takwimu za kila robo mwaka umefanyika katika Mikoa yote 26.


“Hadi Desemba mwaka jana, utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kimataifa wa Kudhibiti na Kupambana na UKIMWI wa 90-90-90, ulionesha mafanikio kwenye  WAVIU milioni 1.4, sawa na asilimia 83 ya WAVIU wote walikuwa wanatambua hali zao za  VVU. Tulifanikiwa WAVIU milioni 1.36 sawa na asilimia 98 walikuwa kwenye tiba na matunzo ya ARV na jambo la faraja ni kuwa asilimia 92 ya waliokuwa kwenye tiba ya ARV walikuwa na kiwango cha chini cha VVU mwilini.” Amesema Mhe. Mhagama


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, Mhe. Fatma Tawfiq amebainisha kuwa kamati yake imeridhika na jinsi serikali ilivyozingatia ushauri  wa kamati hiyo uliolenga kuimarisha jitihada za kudhibiti dawa za kulevya na UKIMWI nchini. Amefafanua kuwa matatizo ya dawa za kulevya na UKIMWI ni mtambuka na yanaathiri sekta mbalimbali hivyo serikali haina budi kuendelea kushirikana na wadau katika kuhakikisha wanaimarisha ustawi wa wananchi.


Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Patrobas Katambi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Ummy Ngeriananga, Katibu Mkuu (Bunge na Waziri Mkuu), Tixon Nzunda, Katibu Mkuu (Sera na Uratibu), Dorothy Mwaluko, Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Leonard Maboko, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya.   James Kaji pamoja na Wakurugenzi na Wataalam wa Ofisi ya Waziri Mkuu.

 

Dira ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ni “Kujenga jamii ya Watanzania isiyotumia dawa za kulevya na kutoshiriki katika biashara ya dawa hizo”. Aidha, Dira ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania ni: “Kuwa Taasisi yenye hadhi inayoongoza Tanzania katika kuelekea kizazi kisicho na maambukizi ya VVU na UKIMWI”.

MWISHO.


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, Mhe. Fatma Tawfiq akieleza umuhimu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kushirikiana na wadau katika kuimarisha ustawi wa watanzania wakati kamati hiyo walipokuwa wakijadili utekelezaji majukumu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Jijini Dodoma, tarehe 29 Machi 2021.


Makatibu wakuu na wakuu wa Taasisi za Ofisi ya Waziri Mkuu, wakifuatilia kikao cha Ofisi hiyo na Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, walipokuwa wakijadili utekelezaji majukumu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Jijini Dodoma, tarehe 29 Machi 2021.


Baadhi ya Wakurugenzi na wataalamu wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia kikao cha Ofisi hiyo na Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, walipokuwa wakijadili utekelezaji majukumu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Jijini Dodoma, tarehe 29 Machi 2021.


Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Leonard Maboko, akieleza mikakati waliyoipanga katika kudhibiti UKIMWI nchini wakati wa kikao cha Ofisi ya Waziri Mkuu na Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, walipokuwa wakijadili utekelezaji majukumu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Jijini Dodoma, tarehe 29 Machi 2021.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akiwaongoza Manaibu Mawaziri, Makatibu wakuu, Wakuu wa Taasisi, Wakurugenzi na Wataalamu wa Ofisi hiyo , wakati wa kikao cha Ofisi hiyo na Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, walipokuwa wakijadili utekelezaji majukumu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Jijini Dodoma tarehe 29 Machi 2021.


Read More

Wednesday, March 17, 2021

Waziri Mhagama: Mapato Uwekezaji NSSF yameongezeka kutoka hasi tatu hadi chanya nne

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama ameieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na sheria kuwa mapato katika uwekezaji ya Mfuko wa  Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), yameongezeka kutoka asilimia 3 hasi (-3) hadi  asilimia 4.7 chanya. Faida hiyo imeongezeka baada ya NSSF kutekeleza maagizo ya serikali ya kuhakikisha miradi ya kimkakati inakamilika na inaleta tija.


Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), katika kutekeleza sera yake ya uwekezaji,  Shirika linawekeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo dhamana za serikali, hati fungani za makampuni. Mikopo, hisa katika makampuni mbalimbali, miundombinu na uwekezaji katika miliki (real eststes). Kama sehemu ya uwekezaji katika miliki, mfuko unatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya ujenzi majengo.


Akiongea wakati akiiongoza kamati hiyo, ilipokuwa ikikagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa majengo wa NSSF katika maeneo ya Mtoni Kijichi, Dungu, Toangoma na Mzizima,  jijini Dar es salaam Machi 17 2021.  Waziri Mhagama amebainisha kuwa,  faida hiyo imeongezeka  baada ya serikali na mfuko huo  kuamua kutumia njia mbadala ya kutengeneza matumizi mbadala ya majengo ya NSSF katika miradi, matumizi ya mifumo ya TEHAMA, mabadiliko ya menejimenti pamoja na  watendaji wa mfuko huo kuongozwa na uzalendo na bidii katika kutekeleza majukumu yao.


“Tunaendelea kupima uendelevu wa mfuko hu ili kuhakikisha unaleta tija kwa wananchama na Taifa pia. Tumejiridhisha jitihada za serikali zinasaidia mfuko kukua kwani Thamani ya mfuko kwa mwaka 2018 ilikuwa trilioni 3.2 na kwa mwaka 2020 imeongezeka hadi trilioni 4.8. Makusanyo ya michango ya NSSF kwa mwezi kwa mwaka 2018 yalikuwa ni wastani wa bilioni 60,  na sasa ni wastani wa  bilioni 100 na hii ni sehemu moja tu ya makusanyo ya michango ya wananchama. Daraja la Kigamboni kwa mwaka 2018 lilikuwa linakusanya wastani wa milioni 650 kwa mwezi,  lakini kwa sasa makusanyo ni takribani bilioni 1.2 kwa mwezi” amesisitiza Mhe. Mhagama.


Ameongeza kuwa  sababu ya mfuko huo kujishughulisha na masuala ya uwekezaji ni kwa sababu ya hitaji la kuhifadhi michango sehemu salama kwa faida ya leo, kesho na baadae na  ili wastaafu waweze kulipwa kwa mujibu wa sheria. Aidha, ameongeza kuwa mfuko huo unalo jukumu la kuandikisha wanachama wengi, kukusanya michango kwa wananchama na kuhakikisha michango hiyo inatumika katika uwekezaji.


Ameihakikishia kamati hiyo kuwa serikali itatekeleza ushauri wao kwa kuwa serikali imepewa jukumu kwenye ibara ya 11 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutengeneza mifumo itakayo hifadhi watanzania. Hivyo sheria ya mwaka 2018, NSSF walipewa jukumu la kushughulika na sekta binafsi katika suala la hifadhi ya jamii. Aidha, emesisitiza kuwa serikali inaendelea kuuwezesha mfuko huo ili kuhakikisha wanachama wananufaika, Taifa lakini pia  na uchumi ukue.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Najma Murtaza Giga, amesisitiza kuwa kamati imeridhishwa na utekezaji wa miradi hiyo ambayo uratibu wake kwa upande wa serikali unasimamiwa na Mhe. Mhagama, hivyo na kutaka kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kufikiwa.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo wakiongea wakati wa ziara hiyo, wamepongeza kwa uwekezaji uliofanywa na NSSF huku wakishauri kuwa uwekezaji huo uliofanywa vizuri na NSSF kwenye miradi ya ujenzi wa majengo ni vyema ukafanywa pia  kwenye ujenzi wa viwanda. Aidha, wamebainisha kuwa kuwekeza kwenye viwanda,  kutasaidia kuharakisha kufanikisha adhima ya serikali ya kuijenga Tanzania ya viwanda.


Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio, ameihakikishia Kamati hiyo kuwa ushauri wao watautekeleza. Amefafanua kuwa suala la uwekezaji  kwenye viwanda wataendelea kulitekeleza kwa kuwa tayari NSSF inatekelza uwekaji kwenye viwanda katika mpango kazi wake waliouanza kuutekeleza tangu  Julai 2020. Aidha, ameeleza kuwa wameanza na viwanda viwili vya kuzalisha sukari na wakimaliza kutekeleza miradi hiyo wanao mpango wa kuwekeza kwenye viwanda vya kimkakati vya mafuta ya kula.


Serikali kupitia Ofisiya Waziri Mkuu ndiyo yenye dhamana ya kuratibu shughuli za Mfuko wa  Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeanzishwa chini ya Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Sura ya 50 marejeo ya mwaka 2018 kwa lengo la kutoa huduma ya Hifadhi ya Jamii kwa wafanyakazi walio katika sekta binafsi na sekta isiyo rasmi.Pamoja na majukumu mengine, shughuli za uwekezaji za Mfuko zinafanywa kwa mujibu wa Sera ya uwekezaji ya Mfuko kwa miongozo/kanuni za Benki kuu na Wizara yenye dhamana ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii.

ENDS


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akiwaongoza wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kukagua mradi wa majengo wa NSSF,  tarehe 17 Machi 2021, katika maeneo ya Mtoni Kijichi, na  Toangoma. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Najma Murtaza Giga.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akiwaongoza wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kukagua mradi wa majengo wa NSSF jijini Dar es salam, tarehe 17 Machi 2021, katika maeneo ya Mzizima. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Najma Murtaza Giga.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akifafanua jambo kwa  wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kukagua mradi wa majengo wa NSSF,  tarehe 17 Machi 2021, katika maeneo ya Mtoni Kijichi,na  Toangoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na  wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kukagua mradi wa majengo wa NSSF,  tarehe 17 Machi 2021, mara baada ya katika maeneo ya Mtoni Kijichi,Toangoma na Mzizima. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Najma Murtaza Giga.


Baadhi ya wafanyakazi wanaoshiriki kwenye mradi wa ujenzi wa Mzizima jijini Dar es salaam. Mradi huo unatekelezwa na NSSF.

Sehemu ya Muonekano wa nyumba zilizo katika mradi wa ujenzi wa NSSF jijini Da res salaam. Baadhi ya nyumba hizo zinazomilikiwa na Mfuko huo tayari zimepangishwa  kwa watu binafsi, wanafunzi wa vyuo vikuu, watumishi wa umma na wengine wamenunua nyumba hizo.



Read More

Tuesday, March 16, 2021

Waziri Mhagama aiogonza Kamati ya Kudumu ya Bunge PAC kuukagua mradi wa Mbigiri


 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama ameiongoza kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za serikali (PAC) kuukagua mradi wa uzalishaji sukari katika shamba la Mbigiri,  wilayani kilosa mkoani Morogoro.


Akiongea wakati wa kikao na Kamati hiyo aliihakikishia kuwa nia ya serikali ya Awamu ya Tano ni kukamilisha ujenzi wa kiwanda hicho kwa wakati ili kuweza kupunguza naksi ya mahitaji ya sukari nchini pamoja na kuweza kutengeneza ajira za moja kwa moja na ajira zisizokuwa za moja kwa moja kwa watanzania.


Mradi huo kwa sasa umeajiri moja kwa moja wafanyakazi 387. Kati ya hao, 300 ni vibarua katika mashamba. Inakadiriwa kwamba mradi  tayari umetoa ajira ambazo si za moja kwa moja kwa wananchi zaidi ya 2,000.


Uzalishaji wa sukari utakapoanza jumla ya wananchi zaidi ya 1,200 wataajiriwa, kati ya hao 650 watakuwa mashambani. Pia ajira zisizokuwa za moja kwa moja kwa wananchi zaidi ya 5,000 zitapatikana. Aidha, kwa sasa kilimo cha miwa kwa wakulima wa nje zaidi ya 245 wamehamasishwa na wakulima 1, 000 wanatarajiwa kuwa wamehamasishwa kiwanda kitakapoanza uzalishaji sukari.


Mradi huo unaotarajiwa kuzalisha tani 50,000 kwa mwaka, unatarajia kuanza kuzalisha sukari kwenye kiwanda cha Mbigiri katika kipindi cha mwisho  wa msimu wa  mwaka 2021/2022 ambapo maandalizi ya eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda yamefanyika kwa kutenga eneo la ukubwa wa hekta 35.3.


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za serikali (PAC), Mhe. Naghenjwa Kaboyoka aliwaongoza wajumbe wa kamati hiyo kukagua eneo lililotengwa kwa ajili  ya ujenzi wa kiwanda, mabweni kwa ajili ya mafundi 112 wa awali wa kiwanda, ofisi za kiwanda, ukumbi mdogo wa mikutano, barabara ya kuelekea eneo la kiwanda pamoja na bwawa la kuhifadhi maji ya kumwagilia miwa.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi ya Mradi Dkt. Hildelitha Msita, ameeleza kuwa mradi umejenga zahanati itakayotumiwa na wafanyakazi pamoja na wananchi wanaoishi jirani na mradi. Aidha, ameeleza kuwa wanaendelea kuboresha kazi za kilimo kwa kununua zana za kilimo na vifaa vya kisasa vya kilimo kulingana na mpango mkakati. Lengo la mradi ni kufikia uzalishaji wa sukari kiwango cha tani 110 kwa hekta ifikapo mwaka 2021/2022  na tani 130 kwa hekta ifikapo mwaka 2023/2024.


Kampuni Hodhi ya Mkulanzi ilianzishwa mwaka 2016 kwa lengo la kuanzisha viwanda vyenye uwezo wa kuzalisha jumla 250,000 za sukari kwa mwaka ili kupunguza nakisi ya mahitaji ya sukari nchini. Endapo Mradi wa Mbigiri Estate, ukianza kutekelezwa unatarajia kuzalisha tani 50,000 za sukari kwa mwaka.Uzalishaji huo utasaidia kupunguza naksi ya mahitaji ya sukari nchini.

ENDS.

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akifafanua jitihada za serikali kwenye mradi wa Mbigiri mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), walipotembelea na kukagua mradi wa uzalishaji Sukari wa Mbigiri wilayani Kilosa, Morogoro.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wakiipitia taarifa ya utekelzaji wa Mradi wa Mbigiri wakati walipotembelea na kukagua mradihuo  wa uzalishaji Sukari eneo la shamba la Mbigiri, wilayani kilosa,  Morogoro.


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mhe. Naghenjwa Kaboyoka (katikati) akizungumza wakati Kamati hiyo ilipotembelea na kukagua mradi wa uzalishaji Sukari wa Mbigiri. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama na Kulia ni Makamu Mweyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Japhet Hasunga.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akiwaongoza Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kukagua shughuli za ujenzi wa miundombinu ya mradi wa uzalishaji Sukari wa Mbigiri walipotembelea na kukagua mradi huo  wilayani Kilosa, Morogoro.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akifafanua eneo lililotengwa ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha sukari na mradi wa Mbigiri wakati Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), walipotembelea na kukagua mradi huo wilayani Kilosa, Morogoro.


Sehemu ya shamba la Mbigiri lililopo kweye ya mradi wa uzalishaji Sukari wa Mbigiri walipotembelea na kukagua mradi huo  wilayani Kilosa, Morogoro.  Kwa sasa eneo liliolimwa na kupandwa ni asilimia 81.25. Kiasi cha miwa kilichopo kinaweza kuzalisha sukari tani 22,750.


Sehemu ya uzio wa eneo litakalojengwa kiwanda cha kuzalisha sukari kupitia mradi wa uzalishaji Sukari wa Mbigiri walipotembelea na kukagua mradi huo  wilayani Kilosa, Morogoro. Mradi huo unaotarajiwa kuzalisha tani 50,000 kwa mwaka.


Sehemu ya bwawa la kuhifadhi maji ya kumwagilia miwa. Tayari uchimbaji wa  mabwawa matatu yenye uwezo wa kuhifadhi maji kiasi cha mita za ujazo 50,000 kila moja umekamilika na yamejazwa maji na uchumbaji wa bwawa lenye ukubwa wa mita za ujazo 1,600,000 umekamilika.


Read More

Monday, March 15, 2021

Waziri Mhagama atoa wiki mbili changamoto Mradi wa Mkulazi kutatuliwa


 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama ameiagiza kamati elekezi ya Kusimamia Mradi wa Mkulazi Estate, kuhakikisha ndani ya wiki mbili ujenzi wa barabara na uwekaji umeme kwenye eneo la mradi huo, ili kuruhusu shughuli za utekelezaji wa mradi huo za kuzalisha tani 200, 000 za sukari kuanza kama zilivyopangwa.


Waziri Mhagama ametoa agizo hilo wakati alipokagua shughuli za mradi huo unaotekelezwa katika shamba Na. 217 lililopo eneo la Mkulazi, Morogoro vijijini. Amefafanua kuwa kamati hiyo kushindwa kutatua changamoto za barabara na umeme kwa wakati, kunasababisha matarajio ya mradi huo ya kushindwa  kuzalishwa hapa nchini, hivyo ameitaka kamati hiyo ndani ya siku mbili ikiwa ni Jumanne ya tarehe 16 Machi, 2021 kuwasilisha mpango wa namna watakavyo tatua changamoto hizo  kwa wiki mbili.


“Maamuzi yalifanyika Novemba na hadi leo Machi hakuna kilichofanyika kwenye kufuatilia. Nataka mwezi huu wa tatu kabla haujaisha mitambo ianze ujenzi wa barabara hapa na nataka majibu ya lini shughuli za kuweka umeme hapa zinaanza. Huu ni mradi wa kimkakati kwani tunao upungufu wa tani 200,000 za sukari ambazo zitazalishwa hapa.Kama hakuna kitakacho fanyika nitachukua hatua kwenu, tumekubaliana tunaenda na mwendo wa ujenzi wa viwanda na hiki nikiwanda muhimu sana” Amesisitiza Mhagama.


Akieleza changamoto zinazosababisha utekelezaji wa Mradi huo usianze, Mwenyekiti wa bodi ya Mradi Dkt. Hildelitha Msita, amebainisha kuwa changamoto ya umeme tatizo lake kubwa lilikuwa ni kwenye makubaliano kati ya Mradi na TANESCO juu ya gharama za kujenga njia za umeme huo kwa kuwa TANESCO njia hiyo haikuwa kwenye bajeti yao.  Amesema tayari wamekubaliana na TANESCO kujenga njia ya umeme yenye urefu wa kilomita 3. 


Mradi umekubali utatoa fedha  ambazo TANESCO  itazilipa kupitia  kwenye makato ya ankala za umeme zitakazo kuwa  zikihitajika kulipwa na mradi,  badala ya kulipwa gharama hizo kwa fedha ambazo zingelipwa na wananchi wenye uhitaji wa kujengewa njia  za umeme.


Kwa upande wake Meneja mradi Abdul Mwankemwa, ameeleza kuwa kutokuwepo kwa miundombinu mizuri ya barabara ya kuelekea shamba la Mkulazi, imesababisha mitambo ya kilmo, kazi ya kusafisha mashamba na kupanda kitalu cha miwakushindwa kufanyika. Aidha amefafanua kuwa Mradi umekamilisha kufanya upembuzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 42 na matokeo ya upembuzi huo yametumika kuomba Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuchukua jukumu la kujenga barabara hiyo inayopitia Chalinze-Seregeta kuelekea kwenye shamba.


Akieleza shughuli ambazo tayari zimefanyika kwenye mradi huo, amesema kazi ya kusafisha eneo la  kitalu lenye ukubwa wa hekta 250, imeanza huku eneo lenye ukubwa wa hekta 80 tayarilimesafishwa. Amefafanua kuwa utafiti wa udongo umefanyika na umeonesha kati ya hekta 60,103 za shamba la Mkulazi, eneo  lenye ukubwa wa hekta 28,000 linafaa kwa kilimo cha miwa. Pia uchunguzi wa kiasi na ubora wa maji umekamilika na watajenga mabwawa makubwa kwa ajili ya umwagiliaji.


Kampuni Hodhi ya Mkulanzi ilianzishwa mwaka 2016 kwa lengo la kuanzisha viwanda vyenye uwezo wa kuzalisha jumla 250,000 za sukari kwa mwaka ili kupunguza nakisi ya mahitaji ya sukari nchini. Endapo Mradi wa Mkulazi  Estate, ukianza kutekelezwa unatarajia kuzalisha tani 200,000 za sukari.

ENDS.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akikagua eneo la shamba la Mkulazi lililopo eneo la Mkulazi, Morogoro vijijini. Shamba hilo linaloendeshwa na Kampuni Hodhi ya Mkulazi linatekelezwa kupitia mradi wa Mkulazi Estate, unaotarajiwa kuzalisha tani 200,000 za sukari.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akikagua  eneo la mto  Ruvu litakalo tumika kama chanzo cha maji kwa shamba la Mkulazi lililopo eneo la Mkulazi, Morogoro vijijini. Shamba hilo linaloendeshwa na Kampuni Hodhi ya Mkulazi linatekelezwa kupitia mradi wa Mkulazi Estate, unaotarajiwa kuzalisha tani 200,000 za sukari.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi  wa Kampuni Hodhi ya Mkulazi, Dkt. Hildelitha Msita,  akimueleza changamoto ya barabara kuwa imesababisha mitambo ya kilimo kushindwa kufikishwa kwenye   eneo la  shamba la Mkulazi lililopo eneo la Mkulazi, Morogoro vijijini. Katikati ni Katibu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Meshack Bandawe.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akimsikiliza Meneja wa mradi wa Mkulazi Estate, Abdul Mwankemwa akimueleza changamoto ya kutokuwa  na  umeme imesababisha kutokufanyika kwa  ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji  kwenye   eneo la  shamba la Mkulazi lililopo eneo la Mkulazi, Morogoro vijijini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akiongea na wafanyakazi wa shamba la Mkulazi lililopo eneo la Mkulazi, Morogoro vijijini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akiwasikiliza wafanyakazi wa Mradi wa Mkulazi wakati alipotembelea shamba hilo  lililopo eneo la Mkulazi, Morogoro vijijini.

Baadhi ya wafanyakazi  wa mradi wa Mkulazi  Estate, wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama wakati alipotembelea shamba hilo  lililopo eneo la Mkulazi, Morogoro vijijini.


Read More