SERIKALI imeanzisha mafunzo
kwa njia ya mtandao ya Afya moja (ECHO) ili kuwajengea uwezo watoa huduma wa
kada za afya ya binadamu, wanyama na mazingira kwa ngazi zote.
Hayo yamebainishwa na Katibu
Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Dk.Jim Yonazi wakati wa
uzinduzi wa mafunzo hayo tarehe 15 Julai, 2025 katika Kituo cha kurushia
Mafunzo kwa njia ya mtandao (ECHO HUB) kilichopo katika jengo la Idara ya
Utafiti na Mafunzo Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali inaendelea
kukabiliana na majanga na dharula zenye athari kwa afya ya binadamu, wanyama na
mazingira hivyo imeona umuhimu wa kuwezesha wataalamu wake kuelewa kwa kina
dhana ya Afya Moja.
“Ofisi ya Waziri Mkuu kwa
kushirikiana na Wizara za Kisekta na mradi wa USAID Usalama wa Afya Duniani
unaotekelezwa na Shirika la CIHEB Tanzania, imeanzisha mafunzo ya mtandao ya
Afya moja (ECHO) ili kujenga uwezo kwa watoa huduma wa kada za afya ya
binadamu, wanyama na mazingira kwa ngazi zote,”amesema Dkt. Yonazi.
Aliongeza kuwa; “Naomba
niwahamasishe viongozi na watumishi kutoka sekta mbalimbali kushiriki katika
vipindi hivi. Wataalamu wabobezi watawasilisha mada mbalimbali zitakazojenga
uwezo wetu katika kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kwa
binadamu na wanyama, visumbufu vya mazao, usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi
ya dawa, usalama wa chakula.
Awali akieleza lengo la
uzinduzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya
Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Brigedia Generali Hosea Ndagala
amesema,Mafunzo haya yanayolenga katika kuongeza ufanisi kwa wataalam katika
kushughulikia magonjwa ya kizoonotiki, usugu wa vimelea dhidi ya dawa (AMR),
hatari za kibailojia, usalama wa chakula na magonjwa yasiyoambukizwa ambayo ni
maeneo muhimu yenye changamoto na yanapewa kipaumbele katika Sekta ya Afya
nchini Tanzania.
Alifafanua kuwa, Mafunzo haya yatawahusu wataalamu wa Sekta
ya Afya moja, Afya, mazingira, mifuko na uvuvi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa
Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Afya na Lishe Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bi.
Suzanne Nchalla amesema mpango huo
utasaidia watoa huduma ngazi ya msingi kupata uelewa wa Dhana ya Afya Moja na
wakati wa utoaji huduma.
Amesema OR- TAMISEMI
itashirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu katika kuhakikisha watumishi wa afya ya
msingi wanashiriki kikamilifu katika mafunzo hayo.
“Tutawasimamia na kuwakumbusha
viongozi wa Halmashauri kuhakikisha wanashiriki vipindi vilivyopangwa ili
kupata matokeo chanya na kutimiza azma la mpango huu,”amesema Bi.Suzanne.
Naye Mwakilishi wa Mganga Mkuu
wa Serikali Dkt.Otilia Gowelle alisema Wizara ya Afya inatambua umuhimu wa
mashirikiano ya wadau na sekta mbalimbali katika kujiandaa pamoja na
kukabiliana na matishio ya mara kwa mara ya magonjwa ya mlipuko pamoja na
matukio yenye athari kwa afya ya binadamu.
“Kwa kuzingatia umuhimu wa
mafunzo haya, Wizara imekwisha fanya uhamasishaji na itaendelea kuhakikisha
wataalam wengi zaidi wanashiriki mafunzo haya wakiwemo wauguzi, madaktari,
wafamasia, maafisa afya, wataalam wa maabara na wengineo waliopo katika vituo
vya kutolea huduma na maeneo mengine mahsusi” alisisitiza Dkt. Gowelle.
Aliongezea kuwa Wizara ya Afya
imekuwa mshiriki na mnufaika mkuu wa ushirikiano uliopo kupitia Ofisi ya Waziri
Mkuu na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kila inapohitajika.
Read More