Monday, March 1, 2021

Waziri Mhagama: Jengeni Viwanda vya kutengeneza Virutubishi vyakula nchini.

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama ameushauri ushirika wa wazalishaji wakubwa wa vyakula nchini kujenga viwanda vya kutengeneza Virutubishi vinavyoongezwa kwenye vyakula badala ya kuviagiza virutubishi hivyo nje ya nchi. Virutubishi hivyo ni madini ya chuma, Zinki, Asidi ya foliki na Vitamini B 12.

Waziri Mhagama ametoa ushauri huo baada ya kutembelea viwanda vya S.S Bakhresa Plant na Murzah Wilmar complex, jijini Dar es salaam, tarehe 1 Machi 2021,  lengo likiwa ni kujionea hali ya urutubishaji, ambapo wamiliki hao wa viwanda vya usindikaji wa chakula (Unga wa ngano, unga wa mahindi na mafuta ya kula) wamebainisha kuwa wamekuwa na changamoto ya kupata virutubishi hivyo kwa wakati kutoka nje ya nchi.

“Sisi kama serikali tupo tayari kushirikiana na nyie na tutatengeneza mazingira mazuri ya kuwawezesha kufanya uwekezaji wa viwanda hivyo. Tunaamini virutubishi hivi vikizalishwa hapa nchini gharama mnayotumia kununua virutubishi hivyo itapungua, lakini pia tutakuwa na uhakika zaidi wa aina ya virutubishi tunavyotumia kwenye vyakula vyetu” Amesisitiza Mhagama.

Ameongeza kuwa uanzishwaji wa viwanda hivyo utaongeza ajira kwa watanzania ambao bado wapo kwenye soko la ajira, pia amebainisha kuwa viwanda hivyo vitapunguza matumizi makubwa ya fedha za kigeni kwa kufanya manunuzi nje na fedha za kigeni zitaongezeka nchini kwa kuwa kuna nchi jirani ambazo wameamza kutekeleza sheria na Programu za kuongeza virutubishi hivyo zitakuja kununua virutubishi hivyo hapa nchini.

“Eneo jingine ambalo tungependa mfikirie ni kutengeneza vifaa vya kurutubisha chakula (dosifier). Mkiweza kuvitengeneza hivi vifaa hapa nchini na mkatumia nyie wenyewe lakini vikatumiwa na wasindikaji wa Kati na wadogo tutakuwa tumetengeneza vizuri mnyororo wa kuongeza virutubishi kwenye vyakula” Amesisitiza Mhagama.

Kwa upande wake mwakilishi wa Viwanda vya S.S Bakhresa, Husein Sufian amefafanua kuwa ujenzi wa viwanda hivyo ni muhimu kwa kuwa kiwanda hicho hutumia gharama kubwa ikiwa ni takribani shilingi bilioni 1.4/=, kwa kila mwaka hutumika kununua virutubishi vya kuongeza kwenye vyakula vinavyozalishwa na kiwanda hicho.

Awali, wakiongea kwa nyakati tofauti  wakati Waziri Mhagama alipokutana na wadau na Taasisi zisizo za serikali zinazojishughulisha na  masuala ya urutubishaji,  kutoka Technoserve Tanzania Meneja Mradi, George Kaishozi pamoja na Meneja Mradi wa urutubishaji vyakula, Gain Tanzania, Archad Ngemela, wamebainisha kuwa wanaendelea kushirikiana na serikali katika ufuatiliaji wa uhakiki wa udhibiti wa ubora wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi nchini.

Aidha; wamesisitiza kuwa wanaendelea kuwasaidia wasindikaji wadogo kupata   virutubishi na vifaa vya kufanyia urutubishaji pamoja na kuhamasisha wasindikaji hao kuzalisha, kusindika na kuyafikisha kwa walaji mazao yaliyorutubishwa kibaiolijia. 

Mwaka 2011 Viwango na kanuni za uongezaji virutubishi kwenye vyakula viliandaliwa, ambapo Mwaka 2013, Uongezaji virutubishi ulizinduliwa rasmi hapa nchini. Hadi sasa jumla ya viwanda vikubwa na vya kati 35 vya ngano, mahindi na mafuta ya kula vinaongeza virutubishi kwenye vyakula. Tafiti zinaonyesha kwamba asilimia 88 ya ngano na asilimia 68 ya mafuta yanayozalishwa na viwanda vikubwa  vinaongezwa virutubiishi ipasavyo.

ENDS.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akipata maelezo ya namna ya Kifaa maalumu cha kuongeza virutubishi kwenye vyakula (dosifier) kinavyofanya kazi wakati alipo tembelea kiwanda cha S.S Bakhresa Plant, tarehe 1 Machi, 2021 jijini Dar es salaam,  lengo likiwa ni kujionea hali ya urutubishaji.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akipata maelezo ya namna kiwanda cha S.S Bakhresa Plant kinavyo hakiki ubora wa virutubishi  kwenye vyakula vinavyozalishwa na kiwanda hicho,  jijini Dar es salaam, wakati alipofanya ziara ya kubaini fursa na changamoto zilizopo kwa wasindikaji wakubwa ili kuimarisha  urutubishaji wa vyakula nchini, tarehe 1 Machi 2021.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akiangalia sehemu ya mitambo ya kiwanda cha S.S Bakhresa Plant jijini Dar es salaam tarehe 1 Machi, 2021,  wakati alipofanya ziara,  lengo likiwa ni kujionea hali ya urutubishaji wa vyakula.

Sehemu ya mitambo ya kiwanda cha S.S Bakhresa inayotumika katika usindikaji wa chakula (Unga wa ngano na unga wa mahindi). Kiwanda hicho ni miongoni mwa  viwanda vikubwa na vya kati 35 vya ngano, mahindi na mafuta ya kula kwa sasa vinavyoongeza virutubishi kwenye vyakula.

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akimsikiliza Mkurugenzi wa Kiwanda cha Murzah Wilmar complex, jijini Dar es salaam, wakati alipotembelea kiwanda hicho lengo likiwa ni kujionea hali ya urutubishaji wa vyakula , tarehe 1 Machi 2021.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akimsikiliza Meneja Mradi, Technoserve Tanzania, George Kaishozi akimueleza namna viwanda vikubwa vinavyoweza kuimarisha urutubishaji wa vyakula wakati walipotembelea  Kiwanda cha Murzah Wilmar complex, jijini Dar es salaam, tarehe 1 Machi, 2021.

Baadhi ya wafanyakazi wa Kiwanda cha Murzah Wilmar complex, jijini Dar es salaam wakiendelea na shughuli za kuzalisha  mafuta ya kula. Kiwanda hicho ni miongoni mwa viwanda vikubwa vinavyongeza virutubishi kwenye mafuta hayo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa  Kiwanda cha Murzah Wilmar complex, jijini Dar es salaam. Lengo la ziara hiyo ni kujionea hali ya urutubishaji katika kiwanda hicho, tarehe 1 Machi 2021.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akisisitiza umuhimu wa kuwa na viwanda vya ndani vya kutengeneza virutubishi vya vyakula wakati alipokutana na wadau na Taasisi zisizo za serikali zinazojishughulisha na  masuala ya urutubishaji,  Jijini Dar es salaam, tarehe 1 Machi 2021.

Meneja Mradi wa urutubishaji vyakula, Gain Tanzania, Archad Ngemela, akieleza namna ya Taasisi hiyo inavyendelea  kushirikiana na serikali katika ufuatiliaji wa uhakiki wa udhibiti wa ubora wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi nchini, wakati wa mkutano wa Mhe. Waziri Mhagama na wadau na Taasisi zisizo za serikali zinazojishughulisha na  masuala ya urutubishaji,  jijini Dar es Salaam, tarehe 1 Machi2021.

Baadhi ya wadau wa masuala ya lishe wakifuatailia mkutano wa Mhe. Waziri Mhagama na wadau na Taasisi zisizo za serikali zinazojishughulisha na masuala ya urutubishaji, wakati alipokutana nao  jijini Dar es Salaam lengo likiwa ni kubaini fursa na changamoto zilizopo kwa wasindikaji wakubwa ili kuimarisha  urutubishaji wa vyakula nchini, tarehe 1 Machi 2021.

Meneja Mradi Technoserve Tanzania , George Kaishozi , akieleza namna ya Taasisi hiyo inavyendelea  kushirikiana na serikali katika ufuatiliaji wa uhakiki wa udhibiti wa ubora wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi nchini, wakati wa mkutano wa Mhe. Waziri Mhagama na wadau na Taasisi zisizo za serikali zinazojishughulisha na  masuala ya urutubishaji,  jijini Dar es Salaam, tarehe 1 Machi 2021.






 



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.