Tuesday, May 18, 2021

Serikali Wilayani Kilosa yawataka wanaoishi mabondeni kuhamia Maeneo salama yaliyotengwa

 


Serikali Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro imewataka wananchi  wanaoishi mabondeni kuhamia katika maeneo maalumu yaliyotengwa  na Halmashauri hiyo  ili kuepukana na athari za maafa ya mafuriko.


Hayo yamebainishwa Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Adam Mgoyi wakati wa ufunguzi wa semina ya kuongeza uelewa wa jamii kuhusu maafa yatokanayo na mafuriko.


‘’Natoa wito kwa wananchi wanaojenga katika mapito ya maji wanazuia  maji kufuata mkondo wake na kusababisha maafa ya mafuriko lakini pia wa mabondeni wahamie maeneo ya miinuko na waliojenga kwenye maeneo ya kilimo na waliogeuza maeneo ya kilimo kuea makazi baadala ya kujenga makambi ya muda kwa ajili ya kusimamia mashamba yao warudi katika maeneo tuliyowapatia’’ amesema Mgoyi.


Mgoyi amebainisha kuwa kumekuwepo na utamaduni wa wananchi kutaka fidia maafa yanapotokea bila kutambua wao ni sehemu ya visababishi vya maafa hayo huku akiwasistiza kutokuwepo fidia kwa mwananchi ambaye atakaidi maagizo ya Serikali.


Sambamba na hayo, amefafanua kuwa Serikali Wilayani humo  imeanza mpango mkakati wa kuhuisha miundombinu ya maji ili kusaidia kukabiliana na kasi ya maji ambayo inaleta athari kwa wananchi Wilayani humo.


Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Waziri Mkuu Kituo cha Oparesheni na Mawasiliano ya Dharura, Luteni Kanali,  Selestine  Masalamado, amewataka wananchi wilayani humo kuchukua hatua za kupunguza athari za maafa zikiwemo kutochimba madini kando ya mito, kutofanya shughuli za kilimo na ufugaji kando ya mito hiyo.


Naye Katibu Tawala Msaidizi (Mipango na Uratibu) ambaye pia ni Mratibu wa Usimamizi wa maafa Mkoa wa Morogoro, Anza Ndossa  amebainisha kuwa elimu hiyo ni muhimu kwa wananchi hao kwa kuwa Wilaya ya Kilosa ina kata 40 huku 11 kati ya hizo zinaathirika na mafuriko ambapo kijiji cha Kitete huathiriwa sana na maafa  ambapo Machi 2020 kaya  takribani kaya 791 ziliathirika kwa maafa ya mafuriko.


Akizungumza kwa niaba ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wahamaji (IOM), Reuben Mbugi ameihakikishia Serikali yaTanzania  kuwa wataendelea kushirikiana nao katika kuijengea jamii uwezo wa kukabiliana na maafa yatokanayo na mafuriko.


Katika hatua nyingine, wananchi wa ya Kichangani, Tindiga na Changarawe wameishukuru serikali kwa kuendesha elimu hiyo ambayo itawasaidia katika kujenga uwezo wa kujiandaa, kuzuia na kukabili maafa ya mafuriko iwapo yatatokea.


Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Uratibu wa Maafa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Kilosa chini ya Ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wahamaji (IOM), wanatoa elimu kwa umma inayolenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu maafa yatokanayo na maafa ya mafuriko katika kata  tano za wilaya hiyo zilizo katika hatari zaidi ya kuathirika na maaafa ya mafuriko.

=MWISHO=

 

Mkuu wa wilaya ya Kilosa Mhe. Adam Mgoyi akisisitiza  wananchi wanao ishi maeneo hatarishi ya mafuriko kuhama na kuhamia maeneo salama yaliyotengwa kwa ajili yao, wakati wa ufunguzi wa semina ya kuongeza uelewa wa jamii kuhusu maafa yatokanayo na mafuriko.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati za Usimamizi wa Maafa za kata zinazo athirika kwa kiwango kikubwa na maafa ya mafuriko wakifuatilia semina ya kuwaongeza uelewa wa  jamii juu ya maafa ya mafuriko.
Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Waziri Mkuu Kituo cha Oparesheni na Mawasiliano ya Dharura,  Luteni Kanali;  Selestine  Masalamado, akifafanua  umuhimu wa wananchi  wa wilayani humo kuchukua hatua za kupunguza athari za maafa zikiwemo kutochimba madini kando ya mito, kutofanya shughuli za kilimo na ufugaji kando ya mito hiyo.

 

Baadhi ya wajumbe wa Kamati za Usimamizi wa Maafa za kata zinazo athirika kwa kiwango kikubwa na maafa ya mafuriko wakifuatilia semina ya kuwaongeza uelewa wa  jamii juu ya maafa ya mafuriko.
Mratibu mradi, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wahamaji (IOM), Reuben Mbugi akieleza namna ya shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali yaTanzania   katika kuijengea jamii uwezo wa kukabiliana na maafa yatokanayo na mafuriko.

Mratibu wa Shughuli za serikali Ofisi ya Waziri Mkuu, akiendelea kuwajengea uwezo Baadhi ya wajumbe wa Kamati za Usimamizi wa Maafa za kata zinazo athirika kwa kiwango kikubwa na maafa ya mafuriko wakifuatilia semina ya kuwaongeza uelewa wa  jamii juu ya maafa ya mafuriko.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati za Usimamizi wa Maafa za kata zinazo athirika kwa kiwango kikubwa na maafa ya mafuriko wakifuatilia semina ya kuwaongeza uelewa wa  jamii juu ya maafa ya mafuriko.

Mratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Charles Msangi akifafanua Utaratibu wa Tathmini za Maafa kwa mujibu wa sheria  ya maafa.

Mtaalamu wa Masuala ya Hali ya Hewa, Kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Suleimani Chilo, akielemisha matumizi sahihi ya Taarifa za Hali ya Hewa kwa wajumbe wa Kamati za Usimamizi wa Maafa za kata zinazo athirika kwa kiwango kikubwa na maafa ya mafuriko.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati za Usimamizi wa Maafa za kata zinazo athirika kwa kiwango kikubwa na maafa ya mafuriko wilayani Kilosa wakiwemo Viongozi wa dini wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Adam Mgoyi (Katikati walio kaa)

Baadhi ya wataalamu walioshiriki katika zoezi la kuelimisha jamii juu ya  maafa ya mafuriko kwa kuwaongeza uelewa wa  jamii juu ya maafa ya mafuriko, wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Adam Mgoyi (Katikati walio kaa)
Baadhi ya wataalamu walioshiriki katika zoezi la kuelimisha jamii juu ya  maafa ya mafuriko kwa kuwaongeza uelewa wa  jamii juu ya maafa ya mafuriko, 
wakiwa wakipata maelezo ya namana mito ya wilayani hivyo inavyosababisha mafuriko kutoka kwa Mratibu wa maafa wilayani humo, Maximillian Ndwangila.

Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Waziri Mkuu Kituo cha Oparesheni na Mawasiliano ya Dharura,  Luteni Kanali;  Selestine  Masalamado, akiwakabidhi wenyeviti wa Kamati za Usimamizi wa Maafa za kata zinazo athirika kwa kiwango kikubwa na maafa ya mafuriko mabango na miti kwa ajili ya kuendelea na juhudi za kuhifadhi mito.

 



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.