Katika
kuhakikisha malengo ya kutatua masuala ya ajira na kazi, yanafikiwa na Serikali
ya Awamu ya Sita inayongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira,
Vijana na Wenye Ulemavu), imepanga mwaka huu kufanya tafiti mbili kubwa ambazo
zitajikita kwenye kubaini nguvu kazi pamoja na rasilimali watu.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama,
wakati akifungua Kongamano la Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo leo
tarehe 27 Mei, 2021, Jijini Dodoma.
Ameeleza
kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia wanaendelea kushirikiana ambapo Wizara hiyo inapitia sera ya elimu
na huku Ofisi hiyo ikifanya tafiti.
“Mwaka
huu tumeamua kufanya tafiti mbili kubwa ambapo tafiti moja tunaendelea nayo
ambayo ni hali ya nguvu kazi nchini. Utafiti huo utatausaidia kujua ni asilimia
ngapi ya vijana wanaofundishwa ndani ya nchi na wanaweza kuajirika nchini na kama hawaajiriki ni kwa nini. Aidha
Utafiti huo utatusaidia kuelewa sekta ipi yenye fursa nyingi kuliko sekta
nyingine ya ajira hii itasaidia mafunzo ya ufundi yaendane na mahitaji yetu ya
ajira” Amesisitiza Mhagama
Aidha,
Mhe. Mhagama amefafanua kuwa serikali imeshakamilisha utaratibu wa kufanya
utafiti wa Hali ya rasilimali watu nchini. Utafiti huo utasaidia kuelewa juu ya
watanzania waliopo nchini na waliopo nje ya nchi kama wanaendana na mahitaji ya
ajira kwa sasa.
Ameongeza
kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikisimamia vibali vya ajira kwa wageni, hivyo
wataelewa sababu ambazo hupelekea wawekezaji kuhitaji kuwaleta watu wao wenye
ujuzi ile hali wenye ujuzi wa viwango hivyo wapo hapa Tanzania, lakini pia itaeleweka
maeneo gani ambayo nchi haina ujuzi na wangependa ujuzi huo upatikane hapa
nchini.
Mhe.
Mhagama amewataka wadau wa elimu ya Ufundi kuendelea kushirikiana na serikali
katika kuhakikisha changamoto za ajira zinashughulikiwa ipasavyo nchini. Amesisitiza
kuwa ili kuweza kuwa na uchumi wa kati endelevu hadi kufikia uchumi wa juu
tunahitaji kuwa na mfumo rasmi wa kuwandaa vijana katika viwango vya juu vya
maarifa, ujuzi, na stadi za kutenda.
Mhe.
Mhagama amefafanua kuwa kwa sasa serikali inaendelea kutekeleza miradi ya
kimkakati kwenye sekta ya nishati ya umeme, Reli ya kisasa, kwenye Sekta ya
Afya na Elimu pamoja na Barabara na hivi karibuni utatekelezwa mradi wa Bomba la
mafuta kutoka Tanzania hadi nchini Uganda. Ameeleza kuwa miradi hiyo ili iwe
endelevu ipo haja ya kuwa na wataalamu wenye ujuzi wa kuendeleza uangalizi wa
miradi hiyo.
Wakati
huo huo, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la (NACTE), Prof. John Kondoro na
Katibu Mtendaji (NACTE) Dkt. Adolf Rutayuga,wamefafanua kuwa Kongamano hilo litalisaidia Baraza hilo kuwa na
mipango ya kuunganisha nguvu ili kuwekeza kiasi cha kutosha katika Elimu ya
Ufundi.
Aidha,
wamefafanua kuwa wataweza kuwa na suluhisho kwenye masuala ya kupata maeneo ya
kutosha ya mafunzo ya vitendo, Upatikanaji wa Takwimu sahihi za wataalamu
kwenye sekta za ajira, Kuimarisha uhusiano kati ya Taasissi za Mafunzo na soko
la ajira, na hatimaye Elimu na Mafunzo ya Ufundi itaweza kutoa mchango mkubwa katika
Maendeleo ya sekta zote za kiuchumi hapa nchini.
Pia,
Mkurugenzi Idara ya Wanachama, Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Zachy Mbenna ameiomba
serikali kushirikiana na sekta Binafsi katika juhudi za kuendeleza kukuza ujuzi
kwa kusimamia tozo inayotozwa ya kukuza ujuzi
kwa kuelekezwa kwenye kukuza ujuzi moja kwa moja kwa kuishirikisha sekta Binafsi kwenye maoni
ya matumizi yake.
Ameomba
kiwepo chombo cha kitaifa kitakacho ratibu juhudi za kukuza ujuzi kwa
kuwaunganisha wanaotoa mafunzo ya kukuza ujuzi. Aidha, ameomba kuwapa motisha waajiri
wenye utaratibu wa kukuza ujuzi katika maeneo yao ya kazi kwa kupewa utambuzi
wakati wa kulipa kodi, ameomba wadau hao wa sekta Binafsi wanaochangia masuala
ya ujuzi kupewa mazingira ya kipaumbele wakati wa uwekezaji. Utekelezaji wa masuala
hayo yatasaidia kuongeza idadi ya wadau wanaotekeleza masuala ya kukuza ujuzi nchini.
Kauli
Mbiu ya Kongamano hilo ilikuwa ni “Kuimarisha Ushirikiano wa Wadau katika Kukuza Ujuzi kwa Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda”
Wadau hao ni Serikali, Taasisi zinazotoa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, na
Waajiri. Kongamano hilo limeandaliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi
(NACTE) kwa ushirikiano na Taasisi ya Sekta Binafsi.
MWISHO.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye
Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, akisisitiza umuhimu wa tafiti za nguvu kazi na
Rasilimali watu, wakati akifungua Kongamano la
Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo leo tarehe 27 Mei, 2021, Jijini Dodoma.
Baadhi
ya wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo wakifuatilia Kongamano la
Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo leo tarehe 27 Mei, 2021, Jijini Dodoma. Kauli Mbiu ya Kongamano
hilo ni “Kuimarisha
Ushirikiano wa Wadau katika Kukuza Ujuzi kwa Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda”
Katibu
Mtendaji (NACTE) Dkt. Adolf Rutayuga akifafanua umuhimu wa Kongamano la Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo litakavyosaidia
kuibua mipango ya kuunganisha nguvu ili kuwekeza kiasi cha kutosha katika Elimu
ya Ufundi.
Mwenyekiti
wa Baraza la Uongozi la (NACTE), Prof. John Kondoro akieleza umuhimu wa Kuimarisha
uhusiano kati ya Taasissi za Mafunzo na soko la ajira, wakati
akifungua Kongamano la Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo leo tarehe 27 Mei, 2021, Jijini
Dodoma.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye
Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa Elimu
ya Ufundi na Mafunzo mara baada ya kufungua Kongamano la Wadau wa Elimu ya Ufundi na
Mafunzo leo tarehe 27
Mei, 2021, Jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.