Mnufaika
wa mafunzo ya Uanagenzi Pili Hussein (wa pili kutoka kulia) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri
Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi (wa pili
kutoka kulia) alipotembelea fani ya ushonaji katika Chuo cha
Ufundi Stadi cha Help to Self Help.
Na:
Mwandishi Wetu - ARUSHA
Vijana
wameaswa kuthamini na kutumia ipasavyo fursa ya mafunzo ya ufundi stadi
yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu maana ni suluhisho la kuzalisha
wataalamu mahiri wenye ujuzi na stadi zinazohitajika soko la ajira ndani na nje
ya nchi ili kuwawezesha kujiajiri, kuajirika na kuajiri wenzao.
Ameyasema hayo Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi
aliposhiriki katika mahafali ya 22 ya Chuo cha Ufundi Stadi cha Help to Self
Help kilichopo Mtaa wa Sakina, Arusha Novemba 19, 2021.
Naibu Waziri Katambi alieleza kuwa, Serikali kupitia
Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inatekeleza Programu ya Taifa ya
Kukuza Ujuzi nchini ambayo inalenga kuimarisha nguvukazi iliyo katika soko la
ajira kwa kuipatia ujuzi na stadi za kazi.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa
Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu
imeendelea kuwatengenezea vijana mifumo maalumu ya kupata ujuzi ili waweze
kuondokana na changamoto ya ajira kwa kuwapatia mafunzo yenye ujuzi staki
unaohitajika katika soko la ajira,” alisema Naibu Waziri Katambi
Alifafanua
kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu iliingia makubaliano na Vyuo 72 ambavyo vinatoa
mafunzo ya ufundi stadi na jumla ya vijana 14,440 katika mikoa yote ya Tanzania
bara wamenufaika na programu hiyo kwa kulipiwa ad ana serikali asilimia 100.
“Mafanikio
tunayoyaona katika utekelezaji wa programu hii yanatupa hamasa ya kuendelea
kutoa fursa zaidi ya mafunzo haya ili kuwezesha nguvukazi ambayo asilimia kubwa
ni vijana kujiajiri na kujikwamua kiuchumi,” alisema
Alieleza
kuwa mafunzo hayo yamekuwa na mchango mkubwa kwa vijana hususan katika
kuongezeka kwa fursa za ajira na uwezo wa kuajirika pamoja na baadhi yao
wamepata ajira kwenye miradi ya kimkakati ya maendeleo inayotekelezwa na
Serikali ya Awamu ya Sita.
“Ukienda kwenye mradi wa kufua umeme wa mto Rufiji - Julius
Nyerere, mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na mradi wa ujenzi wa bomba la
mafuta asilimia kubwa ya vijana walioajiriwa ni wanufaika wa mafunzo haya ya
uanagenzi,” alisema
Aidha, Naibu Waziri Katambi ametaka vijana
wanaohitimu mafunzo hayo kutumia maarifa na ujuzi wao kujiajiri na kujikwamua
kiuchumi ili kuondokana na umaskini. Sambamba na hayo amezitaka Halmashauri
zote nchini kuwa na kanzi data ya vijana wanaopatiwa mafunzo ya ufundi stadi
katika meneo yao ili kuwawezesha mikopo ya asilimia 4 kupitia mapato ya ndani.
“Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Kassim Majaliwa alielekeza wakati wa uzinduzi wa programu hii ya awamu ya tatu
kule Jijini Mbeya vijana hawa waliosomeshwa kwa ufadhili wa serikali wapatiwe mikopo
hiyo ili waweze kuanzisha miradi au shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazo
wawezesha kujiajiri, kuajiri wenzao na kujiingizia kipato,” alisema Katambi
Pamoja
na hayo alitumia fursa hiyo kuwapongeza vijana hao waliohitimu mafunzo hayo na
aliwasihi kuwa mfano wa kuigwa katika utendaji wa kazi zao kwenye jamii
zinazowazunguka kwa kuonyesha uwezo wao katika kumudu kazi.
Naye
Mkurugenzi wa Shirika la Help to Self Help Bw. Amani Sam alitumia fursa hiyo kuishukuru
Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwapatia nafasi ya kutoa mafunzo ya uanagenzi.
“Tunaishukuru
Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kutekeleza mpango huu wa kuwapatia vijana ujuzi katika
fani mbalimbali na jumla ya Vijana wapatao 150 wamepatia mafunzo ya uanagenzi toka
mwezi juni 2021,” alisema
Mnufaika
wa Mafunzo hayo Bi. Dina Lukasi ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajali na
kutambua mchango wa vijana katika jamii kwa kuwapatia ujuzi ambao utakuwa na
manufaa katika kuwawezesha kuondokana na changamoto ya ajira.
“Tunamshukuru
Rais wetu Samia Suluhu Hassan pamoja na wasaidizi wake kwa kutupatia fursa hii,
hakika mafunzo tuyopata yamekuwa na faida mno kwetu,” alisema Mwanagenzi huyo.