Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista
Mhagama (wa pili kutoka kulia) akiangalia nembo na kauli mbiu ya miaka 60 ya
Uhuru wa Tanzania Bara kuelekea maadhimisho
ya Sherehe za Uhuru Kitaifa Disemba 9, 2021. Wa tatu kutoka kushoto ni Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar (Sera na Uratibu) Mhe. Dkt. Khalid
Salum, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Ashatu
Kijaji. Kulia ni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent
Bashungwa. Kushoto ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista
Mhagama akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa ratiba na shughuli za maadhimisho ya Sherehe za Uhuru Kitaifa
zinazotarajiwa kufanyika Disemba 9, 2021.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu
wa Rais Zanzibar (Sera na Uratibu) Mhe. Dkt. Khalid Salum akieleza jambo wakati
wa mkutano huo. Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu,
Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama.
Na:
Mwandishi Wetu - DODOMA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amezindua rasmi nembo maalum ya Maadhimisho ya sherehe za Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara ambazo Kitaifa zitakazofanyika Disemba 09, 2021 katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza hii leo Novemba
01, 2021 na waandishi wa habari Jijini Dodoma Mhe. Mhagama alieleza kuwa sherehe
hizo zitafanyika kati uwanja huo mahali ambapo Tanzania Bara wakati huo Tanganyika
ilipata uhuru wake mwaka 1961 kutoka wa Waingereza.
“Kwa heshima ya mafanikio ya
kihistoria ya nchi yetu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa
na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ipo katika maandalizi ya
sherehe hizo zitakazo tanguliwa na shughuli mbalimbali ambazo zitahusisha
Wizara na Taasisi zote za Serikali kueleza hatua ambazo kila sekta imepiga
tangu nchi ilipopata uhuru, ilipo sasa na inapoelekea” alieleza Waziri Mhagama
Waziri Mhagama alifafanua kuwa,
shughuli za maadhimisho hayo zimeanza rasmi hii leo Novemba 1, 2021 ambapo
Ofisi ya Waziri Mkuu itatoa taarifa kwa wananchi kuhusu taswira nzima za
maadhimisho hayo.
“Leo tunapoanza ratiba ya
maadhimisho ya Sherehe za Uhuru kitaifa, tutazindua rasmi nembo na kauli mbiu
ya miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara. Nembo hiyo itakuwa na picha ya Baba wa
Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekabidhiwa Uhuru wan chi yetu
miaka 60 iliyopita kama heshima na kuthamini mchango wake katika historia ya
Taifa letu,” alisema Mhagama
Aliongeza kuwa, Maadhimisho
hayo yatahusisha mashindano ya Insha kwa Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari, Michezo, Sanaa,
Ngoma za jadi, Makongamano ya Kikanda na Kitaifa, Mdahalo wa Kitaifa, Maonesho
ya Maalum ya Vijana kuonesha Ubunifu na ujuzi katika sekta mbalimbali pamoja na
Maonesho ya Biashara ya Kitaifa yatakayotanguliwa na Mkutano wa Uwekezaji
yatakayofanyika katika Mikoa yote ya
Tanzania Bara Zanzibar kuanzia Novemba
01, 2021 hadi tarehe 30 Novemba, 2021,” alisema Mhe. Mhagama
Aidha Mheshimiwa Mhagama
alibainisha kuwa makongamano yatakayofanyika yataelezea mchango wa waasisi wa
Taifa katika kupigania Uhuru wa Tanzania na kusaidia ukombozi wa nchi
mbalimbali barani Afrika.
Kwa upande wake, Waziri wa
Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar (Sera na Uratibu) Dkt. Khalid Salum alipongeza
hatua ya ushirikishwaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika hatua zote za
maandalizi ya sherehe hiyo.
“Uhuru wa Tanganyika wa
Disemba 09, 2021 ni baba wa Muungano wetu, lakini Mapinduzi Matukufu ya mwaka
1964 nayo pia ni baba wa Muungano wetu. Uhuru na Mapinduzi matukufu ya Zanzibar
ndiyo yaliyotufanya tuwe wamoja hadi hii leo,” alipongeza Mhe. Dkt. Mohamed.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.