Sunday, May 29, 2022

HALMASHAURI ZATAKIWA KUTENGA PESA ZA MIKOPO KWA VIKUNDI VYA WAVIU

 


Naibu Ofisi yaWaziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu  Mhe. Ummy Nderiananga amepongeza Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa kupunguza  kiwango cha maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka 3.5%  mwaka 2020 hadi kufikia  3.2% kwa  mwaka 2021.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Samia Suluhu Hassan kwenye bajeti Mpya ya serikali 2022-2023 itakayoanza mwezi wa saba ameongeza fedha eneo kutoka Billion 1 Mpaka Billion 1.8”

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi yaWaziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga alipokuwa akipokea taarifa ya Mkoa wa Tanga ya Mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi.

Aidha Naibu Waziri Mhe. Ummy Nderiananga ameshauri Halmashauri za wilaya kuona umuhimu wa kutenga fedha za Mapambano Dhidi ya Virusi vya Ukimwi. Hii itasaidia  kuwawezesha katika miradi ya vikundi vya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi (WAVIU) kufanya shughuli zao za maendeleo vizuri.

Wananchi msiogobe kujitokeza kupima virusi vya ukimwi, mpime mjitambue afya zenu. Kama Kauli mbiu inavyosema pima VVU, Jitambue ishi alisema Naibu Waziri Ummy

“Mabinti mnao toa elimu rika, endeeleni kuwaelimisha mabinti wenzetu. Asilimia kubwa ya maambukizi ya virusi vya ukimwi yapo kwa vijana na asilimia 80% ya hao vijana ni mabinti lazima tuendele kuelimishana,  Naibu waziri Ummy”

Naye Naibu katibu Mkuu Bwn. Kaspar Mmuya amesema Baraza la Watu Waoishi na Virusi Vya Ukimwi ambao wamejitokeza na kujitangaza  na kusema wako tayari kushirikiana na serikali kutoa elimu (NACOPHA) ni baraza muhimu.

“Hili baraza ni rasilimali kubwa sana kufikia malengo yetu,  wanaishi kwa mfano na wanamalengo na wanatusaidia hata wale walioachaa dawa kwa sababu mbalimbali wanawatafuta na kuongea nao na kuwarudisha kwenye dawa alisema, Naibu Katibu Mmuya”

Ninaomba hizi afua mbalimbali za ukimwi zinazofanyika, maelekezo yatoke mradi wowote unahusu mambo ya ukimwi washirikiane na NACOPHA. Hawa wanauwezo wa kufikia walengwa  mpaka ndani kijijini na wanatusaidia kufikia malengo ya taifa  kwa kutumia muda vizuri na fedha vizuri.

Thursday, May 19, 2022

TAARIFA ZA MFUMO WA ANWANI ZA MAKAZI, KUTUMIKA KWENYE MAWASILIANO

 


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Bwn. Kaspar Mmuya ameshauri watendaji kuanza kutumia taarifa za mfumo wa Anwani za makazi Postikodi kwenye barua za ofisi ili kurahisha mawasiliano kwa watu kujua eneo zinapopatikana Ofisi

“Watendaji tuanze kujitambulisha kwenye mikutano kwa mfumo wa Anwani za makazi ili kutoa hamasa zaidi kwa wananchi alisema Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu”

Naibu Katibu Ofisi ya waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu ametoa ushauri huo  Katika ziara yake ya kikazi Mkoani Pwani Halmashauri ya Kibaha Mji, alipoenda kujionea utekelezaji wa Operesheni Anwani za makazi.

Afisa Mtendaji mtaa wa mkoani A Kibaha Bwn. Jakson Mwakalima amesema tayari wameshapata mtengenezaji wa vibao vya nyumba, ambavyo mwananchi anaenda kununua kwa shilingi elfu Mbili na kubandika kwenye nyumba yake.

Tuesday, May 17, 2022

TUKUSANYE TAARIFA ZA KIJOGRAFIA KWA KILA NYUMBA TUNAYOITAMBUA

 


NA MWANDISHI WETU

Naibu katibu mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Bwn. Kaspar Mmuya amekemea tabia ya wachukua taarifa wasio waadilifu wanaochukua taarifa za kijiografia  (GPS) za sehemu moja kutolea taarifa kwenye eneo jingine. Jambo hilo linaharibu kazi data na linasababisha mfumo kutoa taarifa zisizosahihi.

“Watendaji mkagaue na kujiridhisha kuhusu taarifa za kijiografia (GPS), hasa pale inapotokea taarifa hizo kufanana eneo moja na jingine allisema Naibu Katibu Mkuu Mmuya.”

Hayo yamesemwa katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa operesheni ya anwani za makazi katika wilaya ya Kilwa na Rufiji. lazima tukusanye taarifa za kijiografia kwa kila nyumba ambayo inaenda kutambuliwa kwa sababu taarifa hizo za kijografia  zinatofautiana.

ninawapongeza wananchi wa Kilwa na Rufiji kwa uelewa na muitikio wao katika kutekeleza Operesheni ya anwani za makazi, na umuhimu wake kwa Sensa ya watu na makazi. Tuendelee kuhamasisha wananchi juu ya umuhimu wa operesheni ya anwani za makazi.

“Ninatoa wito kwa wananchi wote, kujiwekea namba ya kudumu kwenye mageti au milango ni jukumu lao alisema Naibu Katibu Mkuu Mmuya.”

Akihitimisha Injinia wa Tarura Agatha Mtwangambate amesema kwa awamu ya kwanza  idadi ya vibao vya barabara ni kwa ajili ya barabara zote zilizosajiliwa, na vitawekwa katika mwanzo wa barabara na mwisho wa barabara. Kadri operesheni ya anuani za makazi inavyoendelea tutaanza kuzitambua barabara mpya na kuziwekea vibao.

 

Monday, May 16, 2022

SERIKALI YAENDELEA KUHIMIZA WANACHI UWEKAJI ANWANI ZA MAKAZI





NA MWANDISHI WETU-LINDI

Naibu Katibu Mkuu Bwn. Kaspar Mmuya amehimiza wananchi ambao bado maeneo yao hayajatambuliwa kwenye zoezi uwekaji anwani za makazi kujitokeza kwenye Ofisi za serikali za Mitaa au Kijiji kueleza ili uongozi uwawekee namba.

Amezungumza hayo katika ziara yake ya kikazi Mkoa wa Lindi alipotembelea kujionea utekelezaji wa zoezi la anwani na makazi ambalo limeweza kutambua barabara na mitaa 7972 na majengo na viwanja 334771 vimeweza kutambuliwa na kuingizwa kwenye mfumo wa NAPA.

“ Mkoa wa Lindi umefaulu vizuri sana katika kuweka miundo mbinu hasa ya barabara na wamefanikiwa vizuri kuyatambua maeneo yake na kuyapa namba ikiwa inamaanisha nyumba na barabara nyingi kutambuliwa kwa majina alisema Naibu Katibu Mkuu “

Ameongeza kusema Mitaa ambayo haijabandikwa kibao na jina nimepewa mpango kazi na miundo mbinu inatengenezwa kwa kushirikiana vizuri na TANROAD pamoja TARURA katika barabara zinazohusu taasisi zetu hizi mbili. 

Uelewa wa wananchi katika kulipokea na kulitekeleza jambo hili ni mkubwa kwa sababu wameshirkishwa katika kutafuta majina hayo ya mitaa na wanajua umuhimu wa kuwepo kwa miundo mbinu hiyo.

“Wananchi walio wengi wamekubali kuzichora nyumba zao kwa kutumia rangi ya njano na kuweka namba katika nyumba kwa kutumia rangi nyeusi, ni wajibu wetu kama kanuni za anwani za makazi ambazo zimewekwa na TAMISEMI kanuni namba 20 ambayo inasema ni wajibu wa mwenye nyumba kuweka namba hiyo kwenye nyumba yake alisema, Naibu Katibu Mkuu”

Akihitimisha Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa wa Lindi Injinia Dawson  Paschal amesema watawekwa nguzo na vibao 3042 katika Mkoa mzima wa Lindi. Vibao vitakavyotengenezwa vitafidia sehemu ambazo hazijawekwa ili kuhakikisha zoezi la uwekaji wa miundo mbinu linafanikiwa.


 

 

 

 

 

 


Saturday, May 14, 2022

SERIKALI YAHIMIZA USHIRIKISHWAJI ZAIDI ANUANI ZA MAKAZI

 





Na Mwandishi wetu- Pwani

Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bwn. Kaspar Mmuya amehimiza Ofisi za Umma na Ofisi Binafsi kuweka anuani za makazi katika majengo ya Ofisi zao ili kuwa mfano kwa wananchi wengine. Anuani hizo zitasadia kuonesha jina la Ofisi yenyewe Mtaa iliyopo na eneo ambalo posti kodi hiyo ipo.

Naibu katibu Mkuu Mmuya amesema hayo katika ziara yake Mkoani Pwani tarehe 13 /05/2022 alipotembelea na kupokea taarifa ya Mkoa ya utekelezaji wa Anuani za makazi. Kwa sasa ngazi ya Taifa tumefikia 90% ya matarajio yetu lakini tunazidiana Mkoa na Mkoa.

Amepongeza Mkoa wa Pwani kwa kutekeleza vyema zoezi la uwekaji wa anuani za makazi na kufuata miongozo iliyowekwa katika utekelezaji wa anuani za makazi. “Ziara imelenga kujionea uhalisia ili mwezi huu, tutumie kurekebisha dosari chache tulizogundua kwa kupokea taarifa kwenye mfumo au kwa ziara mbalimbali tunazozifanya au taarifa tunazopatiwa alisema, Naibu Katibu Mkuu Mmuya”

“zoezi la anuani ya makazi ni endelevu, kila mmiliki mwenye eneo ambalo limejengwa au halijajengwa anapaswa kuwa na namba,alisema Naibu Katibu Mmuya”. Hiyo itasaidia kujua mahali eneo lilipo, wananchi wanahitaji kuelimishwa zaidi juu ya umuhimu wa  zoezi la uwekaji wa anuani za makazi na itaongeza dhana ushirikishwaji wa wananchi.

Akihitimisha Kaimu Injinia wa Tanroad Mkoa wa Pwani Meneja Heririsper Mollel amesema utekelezaji wa anuani za makazi umefika katika hatua nzuri ukamilishaji wake kwa sasa wamejikita katika kurekebisha vibao vilivyokosewa.

SERIKALI KUIMARISHA VITA DHIDI YA UKATILI KWA WANAWAKE NA WATOTO

 








Na Mwandishi wetu - Dodoma

Serikali imesema itaendelea kuongeza jitihada katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo pamoja na wizara husika ili kuhakikisha makundi hayo yanakuwa salama.

Kauli hiyo ilitolewa  Mei 12, 2022 na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu wakati akiongoza kikao cha Kamati Elekezi ya Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kilichofanyika Jijini Dodoma kikihudhuriwa na Makatibu Wakuu, wawakilishi kutoka Wizara mbalimbali na wadau wa maendeleo nchini.

Katibu Mkuu huyo alisema ipo haja ya kuongeza nguvu katika mapambano hayo kila mdau kwa nafasi yake ili kuongeza jitihada za utekelezaji wa mpango huo kutokana na kuongezeka kwa vitendo na matukio ya ukatili katika maeneo mbalimbali.

“Inabidi tuongeze nguvu yaani Serikali, Wizara za kisekta , Idara,Taasisi, Asasi za kiraia,wadau  na vyombo vya ulinzi katika mapambano haya wote kwa nafasi zetu ili kuongeza kazi ya utekelezaji wa mpango huu na kufikia hilo lazima tuwe na rasilimali kulinda na kutetea makundi ambayo yamekuwa yakiathirika kutokana na vitendo hivyo,”alisema Dkt. Jingu.

Pia aliongeza kwamba kwa mujibu wa muongozo wa  maandalizi ya mpango na bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023 unaelekeza kutengwa kwa fedha kwa ajili ya kutekeleza afua za MTAKUWWA huku akiziomba taasisi na wadau kuona namna ya kuongeza rasilimali kufikia malengo ya Serikali ya kukomesha vitendo vya ukatili.

“Wenzetu wadau wa maendeleo na Asasi za kiraia nimewaomba tuongeze rasirimali katika vita hii kwa sababu inahitaji ushirikiano wa pamoja kwani inamgusa kila mmoja wetu katika jamii zetu itatusaidia kutatua changamoto zinazokabili juhudi hizi na pia mnaweza kuajiri vijana wenye fani za masuala ya maendeleo ya jamii au zinazofanana na haya mambo kuongeza kasi ya mapambano,” alibainisha Katibu Mkuu huyo.

Aidha Mtaalamu wa Masuala ya Usalama wa Mtoto kutoka Shirika la kuhudumia watoto Duniani (UNICEF) Bi. Vailet Mollel alieleza kwamba kwamba wamekuwa wakitoa elimu katika jamii namna ya kudhibiti vyanzo vya ukatili huku akiahidi kwama shirika hilo litaendelea kuunga mkono Serikali katika uandaji wa mkakati mpya wa 2022/2027 pamoja na kuratibu kamati za ulinzi kuanzia ngazi ya Vijiji hadi Mkoa.

“Tutaendelea kuunga mkono juhudi za serikali hatutaishia hapa tulipo na kuwajengea uwezo wataalamu kama jeshi la polisi, wanasheria, mahakama, maafisa ustawi na maendeleo ya jamii ili waweze kukabiliana na vyanzo vya ukatili kama mila kandamizi na desturi kupitia uanzishaji wa vikundi vya malezi, viongozi wa dini na  viongozi wa kimila,” alifafanua Mtaalamu huyo.

 

Thursday, May 12, 2022

TAASISI NA WIZARA ZATAKIWA KUSHIRIKIANA KUKABILI UTAPIAMLO

 



Na Mwandishi wetu-Dodoma

Wizara na Taasisi zinazohusiana na masuala ya lishe nchini zimetakiwa kushirikiana na kubadilishana uzoefu katika mapambano dhidi ya Utapiamlo kuhakikisha jamii na Taifa linakuwa salama.

Akizungumza katika mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu Mpango wa Pili  Jumuishi wa Masuala ya Lishe wa Kitaifa kwa Menejimenti ya Sekta ya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Ukumbi wa Wizara hiyo Mei 10, 2022 Jijini Dodoma Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Lishe kutoka Shirika la Marekani la Maendeleo Kimataifa (USAID) Bi. Debora Niyeha alisema mpango huo unaanza utekelezaji wake mwaka 2021-2022/ 2025-2026 hivyo kama sekta ya mifugo ina sehemu ya kufanya kuhakikisha malengo ya mpango huo yanafikiwa.

Alisema kwamba vipaumbele katika mpango huo ni Utapiamlo wa chini na wa kuzidi, utapiamlo utokanao na virutubishi na madini kwa kuzingatia makundi yote ndani ya jamii akisema kuwa afya bora huanzia ngani ya familia hadi Taifa huku akisema kwamba bado ipo changamoto kubwa ya lishe hasa kwa watoto chini ya miaka mitano.

“Kwa takwimu za mwaka 2018 zinasema asilimia ya watoto 32 ya watoto wa Tanzania wana udumavu, ukondefu watoto zaidi ya 500,000 nchini wanakabiliwa na ukondefu wakati asilimia 45 ya kina mama walio umri wa kuzaa wanakabiliwa na ukosefu wa damu na asilimia 28 ya kina mama wanakabiliwa na uzito uliokithiri ndiyo maana tumekaa kuona namna gani sekta za lishe zinaaweza kutusaidia,”Alisema Mratibu huyo.

Pia alihimiza sekta binafsi kuzalisha bidhaa za vyakula na dawa zenye ubora unaozingatia lishe bora kama hatua ya kushirikiana na Serikali kutatua changamoto ya utapiamlo pindi mlaji wa mwisho anapotumia bidhaa hizo badala ya kudumaza afya za walaji.

“Sekta binafsi zina mchango mkubwa sana katika suala la lishe kwa sababu wao ndiyo wazalishaji wa bidhaa za vyakula au dawa kwahiyo sisi tunashirikiana nao kwa karibu maana tunataka watengeneze vyakula au bidhaa zinazosaidia kukabili hii changamoto na zizingatie makundi muhimu ya chakula na katika mpango huu wa pili tunategemea sana watusaidie,”alisisitiza Bi. Debora.

Aidha akitaja mikoa inayoongoza kwa utapiamlo licha ya kuwa na kiwango  kikubwa cha uzalishaji wa chakula alitaja kuwa ni mikoa  saba ikiwemo ya Njombe, Ruvuma, Mbeya na Iringa ambapo zaidi ya asilimia 40 ya watoto wana udumavu unaoathiri hata uwezo wao kimasomo.

Kwa upande wake  Mkurugenzi  Msaidizi Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bi. Devotha Gabriel alibainisha kwamba kuendelea kupungua kwa udumavu kumetokana na utekelezwaji wa mpango wa kwanza huku akisema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo waratibu hivyo iko tayari kushiriki kikamilifu katika jitihada hizo.

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Sekta ya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Mhina aliishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kutoa elimu hiyo muhimu itakayowajengea uwezo sekta hiyo.

“Kama Wizara tumejipanga kutekeleza vipaumbele vya sekta ya mifugo inayochangia kwa kiasi kikubwa katika suala la lishe na niwahimize watanzania kuzingatia ulaji wa mlo kamili tuache kula kwa mazoea pia wale samaki, nyama kwa aina zake ambazo zinashauriwa kiafya na kunywa maziwa  kwa wingi maana ni azima ya Serikali kila mtanzania awe na afya bora aweze kufanya shughuli zake na kuchangia pato la Taifa,” alihitimisha Dkt. Mhina.

Saturday, May 7, 2022

SERIKALI YAONYA MATAPELI NAFASI ZA AJIRA SENSA YA WATU NA MAKAZI.

 


Na Mwandishi wetu-Dodoma

Serikali imewaonya  baadhi ya watu au makundi ya watu wenye nia isiyo njema kwa zoezi la sensa ambao wamekuwa wakitoa  matangazo ya ajira za Sensa kwa nia ya kuwatapeli wananchi wanaohitaji kushiriki katika zoezi hilo.

Hayo yalisemwa Mei, 05, 2022 Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuanza kwa mchakato wa Ajira za Makarani na Wasimamizi wa Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23, 2022 Nchi nzima.

Pia Mhe. Simbachawene alisema kwamba mchakato wa ajira za makarani na wasimamizi kuanzia Mei 05 hadi Mei 19,2022 ambao utahusisha ngazi  zote za kiutawala kuhakikisha wanapatikana makarani na wasimamizi wenye sifa stahiki.

“Kumekuwepo na watu au makundi ya watu wenye nia isiyo njema kwa zoezi la sensa ambao wamekuwa wakijaribu kutoa matangazo ya ajira za Sensa kwa nia ya kuwatapeli wananchi wanaohitaji kushiriki katika zoezi hili na pengine kwa nia ya kuvuruga mchakato mzima,”alisema Mhe. Simbachawene.

Vilevile Mhe. Simbachawene aliwahimiza watanzania wote wenye sifa ambao wangependa kuomba nafasi za ajira hizo kufuata utaratibu uliowekwa kwa ukamilifu ili kuomba nafasi hizo.

“Kazi za kufanya pamoja na sifa za mwombaji zimebainishwa katika Tangazo la Ajira za Muda za Makarani na Wasimamizi wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.Hakutakuwa na maombi yatakayofanyiwa kazi zaidi ya yale yatakayofuata utaratibu uliowekwa mtandaoni,”alifafanua Mhe. Simbachawene.

Kuhusu namna ya kufanya maombi hayo alibainisha kwamba waombaji watatakiwa kutuma maombi yao kupitia mtandao (online) ambao hautahusisha malipo yoyote kwa mwombaji wa ajira.

 Mfumo wa kuomba ajira hizi kupitia mtandao unapatikana kupitia tovuti zifuatazo;www.pmo.go.tzwww.tamisemi.go.tz,  www.nbs.go.tz kwa Tanzania Bara na www.ompr.go.tzhttps://www.tamisemim.go.tz au www.ocgs.go.tz kwa wale wanaoomba Tanzania Zanzibar,”Alieleza.

Aidha alihitimisha kuwa mchakato wa kuchambua maombi ya kazi pamoja na usaili utasimamiwa na Kamati maalum itakayoundwa katika ngazi ya kila Wilaya na usaili utafanyika katika ngazi ya kata kwa nafasi za makarani na wasimamizi wa maudhui na katika ngazi ya Wilaya kwa Wasimamizi wa TEHAMA,”alihitimisha Mhe. Simbachawene.