Wizara na Taasisi zinazohusiana na masuala ya
lishe nchini zimetakiwa kushirikiana na kubadilishana uzoefu katika mapambano
dhidi ya Utapiamlo kuhakikisha jamii na Taifa linakuwa salama.
Akizungumza katika mafunzo ya kujenga uelewa
kuhusu Mpango wa Pili Jumuishi wa Masuala ya Lishe wa Kitaifa kwa
Menejimenti ya Sekta ya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Ukumbi
wa Wizara hiyo Mei 10, 2022 Jijini Dodoma Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Lishe
kutoka Shirika la Marekani la Maendeleo Kimataifa (USAID) Bi. Debora Niyeha
alisema mpango huo unaanza utekelezaji wake mwaka 2021-2022/ 2025-2026 hivyo
kama sekta ya mifugo ina sehemu ya kufanya kuhakikisha malengo ya mpango huo
yanafikiwa.
Alisema kwamba vipaumbele katika mpango huo ni
Utapiamlo wa chini na wa kuzidi, utapiamlo utokanao na virutubishi na madini
kwa kuzingatia makundi yote ndani ya jamii akisema kuwa afya bora huanzia ngani
ya familia hadi Taifa huku akisema kwamba bado ipo changamoto kubwa ya lishe
hasa kwa watoto chini ya miaka mitano.
“Kwa takwimu za mwaka 2018 zinasema asilimia
ya watoto 32 ya watoto wa Tanzania wana udumavu, ukondefu watoto zaidi ya
500,000 nchini wanakabiliwa na ukondefu wakati asilimia 45 ya kina mama walio
umri wa kuzaa wanakabiliwa na ukosefu wa damu na asilimia 28 ya kina mama
wanakabiliwa na uzito uliokithiri ndiyo maana tumekaa kuona namna gani sekta za
lishe zinaaweza kutusaidia,”Alisema Mratibu huyo.
Pia alihimiza sekta binafsi kuzalisha bidhaa
za vyakula na dawa zenye ubora unaozingatia lishe bora kama hatua ya
kushirikiana na Serikali kutatua changamoto ya utapiamlo pindi mlaji wa mwisho
anapotumia bidhaa hizo badala ya kudumaza afya za walaji.
“Sekta binafsi zina mchango mkubwa sana katika
suala la lishe kwa sababu wao ndiyo wazalishaji wa bidhaa za vyakula au dawa
kwahiyo sisi tunashirikiana nao kwa karibu maana tunataka watengeneze vyakula
au bidhaa zinazosaidia kukabili hii changamoto na zizingatie makundi muhimu ya
chakula na katika mpango huu wa pili tunategemea sana watusaidie,”alisisitiza
Bi. Debora.
Aidha akitaja mikoa inayoongoza kwa utapiamlo
licha ya kuwa na kiwango kikubwa cha uzalishaji wa chakula alitaja kuwa
ni mikoa saba ikiwemo ya Njombe, Ruvuma, Mbeya na Iringa ambapo zaidi ya
asilimia 40 ya watoto wana udumavu unaoathiri hata uwezo wao kimasomo.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Msaidizi Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bi. Devotha Gabriel alibainisha kwamba kuendelea
kupungua kwa udumavu kumetokana na utekelezwaji wa mpango wa kwanza huku
akisema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo waratibu hivyo iko tayari kushiriki
kikamilifu katika jitihada hizo.
Naye Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa
Rasilimali Watu Sekta ya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles
Mhina aliishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo
kutoa elimu hiyo muhimu itakayowajengea uwezo sekta hiyo.
“Kama Wizara tumejipanga kutekeleza vipaumbele
vya sekta ya mifugo inayochangia kwa kiasi kikubwa katika suala la lishe na
niwahimize watanzania kuzingatia ulaji wa mlo kamili tuache kula kwa mazoea pia
wale samaki, nyama kwa aina zake ambazo zinashauriwa kiafya na kunywa
maziwa kwa wingi maana ni azima ya Serikali kila mtanzania awe na afya
bora aweze kufanya shughuli zake na kuchangia pato la Taifa,” alihitimisha Dkt.
Mhina.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.