Serikali imesema maandalizi ya
Sensa ya Watu na Makazi yamefika zaidi ya asilimia 95 hivyo ni vyema kuendelea
kushirikiana kwa pamoja kwa kuzingatia muda uliobaki ili kulifikia lengo lililopo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu
Mhe. George Simbachawene katika Mkutano Maalum wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alipokutana na sekta binafsi kwa
lengo la kutambua mchango wao katika kuelekea siku hiyo ikiwemo ya rasilimali
fedha, huduma na vifaa kwa ajili ya zoezi la Sensa ya watu na makazi ya Mwaka
2022.
Alisema kuwa, Serikali
inatambua mchango wa sekta binafsi hivyo ni vyema kwa kila mdau kushirikia
katika zoezi hili kwa kadri awezavyo kwa
kuchangia rasilimali fedha, huduma na
vifaa vitakavyosaidia kufanikisha zoezi la sensa.
“Karibu kila mdau ameshiriki
katika maandalizi ya sensa kupitia taasisi ya sekta binafsi (TPSF) na
tumekutana hapa ili kuonesha mshikamano wetu na kutambua michango yenu
ninawapongeza sana," alisema Simbachawene.
Naye katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu amesema serikali
imeshirikiana sekta binafsi katika
maandalizi ya kuelekea siku ya sensa kwa namna mbalimbali ikiwemo, kugharamia
matangazo yanayotoka kwenye vyombo vya habari.
“Kampuni za simu zilisaidia
kutoa ujumbe mfupi wa kuhamasisha wananchi na kuelimisha wananchi juu ya zoezi
la sensa ya watu na makazi na baadhi kuahidi kuchangia fedha na vifaa
mbalimbali ili kufanikisha zoezi la sensa ya watu na makazi” alisisitiza Dkt.
Jingu
Naye Kamisaa wa Sensa ya Watu
na Makazi Mhe. Anne Makinda ameshukuru sekta binfasi kwa mchango wao katika
kuwezesha maandalizi ya kuelekea siku ya sensa ya watu na makazi inayotarajiwa
kufanyika tarehe 23 Agosti, 2022.
“Tumejipanga kusimamia
matumizi yote tunayopewa na kuhakikisha tunapata matunda tunayotegemea.”
aliesema Mhe. Makinda
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.