Waziri wa Nchi Ofisi
ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Mhe. George
Simbachawene azindua program ya education plus inayolenga kuhakisha vijana
balehe (wasichana na wavulana) wanawezeshwa kuishi maisha salama, yenye afya,
na tija - bila ukatili wa kijinsia, VVU na UKIMWI.
Akizindua program hiyo
hii leo novemba 30, 2022 wakati wa halfa ya kuhitimisha wiki ya Vijana katika
kuelekea siku ya UKIMWI Duniani Mkoani Lindi Waziri wa Nchi amesema amefarijika
kwa jitihada za Taasisi ya TACAIDS pamoja na wadau katika utekelezaji wa afua
za masuala ya UKIMWI.
Alitumia fursa hiyo
kuwaasa vijana wote nchini kuzingatia jitihada za Serikali katika mapambano
haya ya VVU na UKIMWI kwa kuendelea kujilinda na kulinda wengine huku
wakijiepusha na tabia hatarishi.
“Rai yangu kwa vijana
wote nchini, hususani wasichana, fanyeni kila muwezalo ikiwa ni pamoja na
kuzingatia maudhui ya kampeni mbalimbali ili kujikinga na maambukizi ya VVU.
Wale mlio shuleni na vyuoni hakikisheni mnaweka mkazo katika Elimu na
kujiepusha na tabia zote hatarishi zinazopelekea kupata maambukizi ya
VVU.”alisema
Aidha, aliwasihi
vijana walio nje ya shule na vyuo, kuzitumia fursa zilizopo katika kuviwezesha
vikundi vya vijana kujiinua kiuchumi hii itasaidia kujiepusha na tabia za kukaa
vijiweni na kushawishika kujiingiza katika vitendo vinavyopelekea kuwa katika
hatari ya kupata maambukizi ya VVU.
Akieleza hali ya
maambukizi nchini Waziri Simbachawene alisema katika kuelekea lengo la sifuri
ya maambukizo mapya, kama nchi maambukizo mapya yameendelea kushuka mwaka hadi
mwaka, japokuwa sio kwa kasi ya kuridhisha. Kwani, hadi sasa takwimu
zinaonyesha kuwa takribani watu 54,000 waliambukizwa VVU mwaka 2021 nchini. Hii
ni sawa na takribani watu 4,500 kwa mwezi au watu 150 kwa siku.
“Vijana wenye umri wa
miaka 15-24 ndio kundi ambalo linaonyesha kuwa na kiwango kikubwa cha
maambukizo mapya, kwani katika watu wote wanaopata maambukizo mapya ya VVU kila
mwaka, takribani Asilimia 30 ni vijana wenye umri wa miaka 15-24 (yaani katika
kila watu 10 wanaopata maambukizo mapya ya VVU watatu ni vijana wa umri
huu),”alisisitiza
katika kundi la vijana
wa miaka 15-24 wanaopata maambukizo mapya, takriban Asilimia 70 ni wasichana.
Katika mwaka 2021, kulikuwa na maambukizi mapya 212 kila wiki kwa kundi la wasichana
wa miaka 15 -24, Inamaanisha maambukizi mapya 30 kila siku.