SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kuweka mikakati madhubuti katika masuala ya menejimenti ya maafa nchini ili kuhakikisha inapunguza madhara yatokanayo na maafa.
Kauli hiyo imetolea na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti
ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Charles Mbuge wakati akifungua
kikao kazi cha wadau cha kupitia na kujadili Rasimu ya Mpango wa Taifa wa
Mawasiliano ya Dharura kilichofanyika katika ukumbi wa
mikutano wa hoteli ya African Dream Jijini Dodoma.
Kikao kazi hicho kililenga kupitia na kujadili rasimu ya
mpango huo wenye malengo ya kusimamia
mawasiliano na kuweka utaratibu wa matumizi ya huduma za mawasiliano ndani ya
Serikali, Umma, Wadau wa Mawasiliano na Mashirika Binafsi.
Meja Jenerali Mbuge alisema, upo umuhimu wa kuendelea
kufanya kazi kwa ushirikiano na wadau wote wa masuala ya maafa nchini kwa lengo
la kuhakikisha wanaendelea kuwa na mikakati madhubuti ya mawasilino wakati wa
dharura.
“Hakikisheni kuwa mpango unazingatia Sheria ya Usimamizi wa
Maafa Na. 6 ya mwaka 2022, Kanuni za Usimamizi wa Maafa za mwaka 2022 na
Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wakati wa Maafa 2022 ili kurahisisha
utekelezaji wake,”alisisitiza Meja Jenerali Mbuge.
Akieleza kuhusu Mpango huo, alisema utarahisisha mawasilino
ya haraka, sahihi na kwa wakati unaohitajika kwa kuzingatia mfumo huo
uliojikita kidijiti na unahusisha vyombo vya habari ikiwemo matumizi ya radio,
televisheni na mitandao ya kijamii.
Katika hatua nyingine Idara imeendelea kuchukua hatua za
kupunguza madhara kwa kuhakikisha usimamizi na uratibu wa maafa na huduma za
dharura zinatolewa kwa wakati kwa kuzingatia mipango, miongozo na mikakati ya
kitaifa na kisekta. Juhudi hizi zimekuwa zikifanyika kwa kushirikiana na
Wizara, Taasisi, Mashirika ya kimataifa na Asasi zisizo za kiserikali.
“Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa
kuzingatia Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya Mwaka 2004 na Sheria ya
Usimamizi wa Maafa, Na. 6 ya mwaka 2022 inajukumu la kuratibu na kusimamia
masuala ya maafa nchini,”alisema.
Idara ya maafa ilizindua nyaraka za usmamizi wa maafa nchini ikiwemo; Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano ya Dharura 2022 ambao umelenga kuhakikisha utendaji kazi, ushirikiano, na mwendelezo wa mawasiliano vinaimarika wakati wa maafa ili kuruhusu watoa huduma za dharura kufanya mawasiliano baina yao na ngazi nyingine za serikali wakati wote, hata pindi miundombinu ya mawasiliano itakapoharibiwa
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.