Serikali
kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imesema itaendelea kuimarisha
ushirikiano na sekta mbalimbali katika kukabiliana na maafa ili kuhakikisha
wananchi wanaishi katika mazingira salama.
Kauli hiyo imetolewa
Mkoani Singida na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya
Waziri Mkuu Meja Jenerali Charles Mbuge wakati akifungua
kikao kazi cha Watalam waliokutana kwa lengo la Kuhuisha na Kutafsiri Mwongozo
wa Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja.
Meja Jenerali Mbuge
amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la mwingiliano wa binadamu, wanyama na
mazingira ambao husababisha kutokea kwa magonjwa mbalimbali
yanayotoka kwa wanyama na kwenda kwa binadamu hivyo ipo haja ya
kuwepo kwa ushirikiano wa sekta mbalimbali katika kujiandaa, kuzuia
na kukabiliana na majanga hayo.
“Tunahuisha mwongozo
huu kwa sababu ya mabadiliko ya sheria na kanuni za usimamizi wa
Maafa. Mwongozo huu ni muhimu katika kurahisisha ushirikiano wa
kisekta ili kujenga na kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya milipuko ya
magonjwa na dharura zingine zenye madhara kwa afya ya binadamu, wanyama na
mazingira,” Amesema Meja Jenerali Mbuge.
Ameongeza kuwa kwa
mujibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa husisitiza yakiwemo Shirika la
Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Shirika la Afya Ulimwenguni
(WHO), Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Wanyama (WOAH) na Programu
ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) kwa pamoja husisitiza ushirikiano wa sekta
mbalimbali ili kuwa na mikakati na sera za pamoja katika kuimarisha
afya ya wanadamu, wanyama na mazingira.
“Ili kutekeleza dhana
ya Afya moja, ni muhimu kuwa na miongozo mbalimbali ili kurahishisha uratibu na
utendaji katika ngazi zote. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru FAO ambao
walianzisha mchakato wa kutengeneza mwongozo huu ambao katika kikao hiki
utauhuishwa na kutafsiriwa,” Ameeleza.
Aidha amebainisha kuwa
Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa ina
wajibu wa kuratibu utekelezaji wa dhana ya Afya Moja kwa kuzingatia
Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya 2004, Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na.
6 ya Mwaka 2022 na kanuni zake za mwaka 2022 pamoja na Mkakati wa Afya Moja
2022-2027.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.