Naibu
Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya amesema hadi sasa urejeshaji wa
miundombinu ya barabara na makalvati iliyokuwa imeharibiwa na maporomoko ya
tope na mawe yaliyotokea Disemba 3, 2023 kwenye Mji wa Katesh wilayani Hanang
mkoani Manyara umefikia asilimia 75.
Kasekenya
amesema hayo Mkoani Manyara mara baada ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa
kazi hizo zinazofanywa na Wakala ya Barabara (TANROADS) wakishirikiana na
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini
(TARURA).
"Hadi
sasa tumefikia karibu asilimia 75 ya kuirejesha Katesh katika hali yake na
tutakachofanya kabla ya kuondoka tutakuwa tumehakikisha tumesafisha barabara
zote na kuzirudisha katika hali yake ya awali kama tulivyokuwa tumeagizwa na
Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan", amesema Kasekenya.
Kasekenya
ameongeza kuwa mitambo na magari imeshafika eneo la Katesh ambapo kuna magari
32 yenye uzito wa tani 13, vijiko 12, doza 3, magari ya kishindilia barabara
mawili, mitambo ya kubeba matope (roller) mawili, na mitambo yote hiyo
inaendelea kufanya kazi usiku na mchana.
"Ninaposema
magari yenye uzito wa tani 13 na yale yenye uwezo wa kubeba magunia 130 kwa
wakati mmoja na mpaka sasa magari hayo yameweza kubeba Tripu za tope na mawe
zaidi ya 4,000 na kazi bado inaendelea", amefafanua Kasekenya
Amesema
Wizara hiyo kupitia Wakala hizo wanaendelea kufungua barabara za mitaa kwa
ajili ya kuhakikisha njia zinafunguka kwa kutoa mawe na magogo ili kuhakikisha
kama kuna mali za watu zilisalia katika makazi yao wanaweza kuingia na kufanya
usafi.
"Kwahiyo
kazi kubwa ambayo tunafanya sisi Wizara, TANROADS na TARURA ni tumejipangia
mpaka kufikia kesho tuwe tumefikia walau asilimia 95 katika kurejesha hali",
amesisitiza Eng. Kasekenya.
Naye
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista
Mhagama amesema kuwa mbali na Serikali kurejesha miundombinu pia imeendelea
kuwa bega kwa bega na Wananchi sambamba na kutoa maagizo kwa Wataalamu wa
Satellite kuanza kuangalia Kaya zote na kuona zipi zimeathirika zaidi huku
ikiendelea kutoa msaada zaidi.
"Kiu
ya Mhe. Rais ni kuona wale ambao wamepoteza makazi tunaipata hesabu yao vizuri
ili Serikali ianze mchakato wa makazi mapya kwa waathirika hao",
amefafanua Mhe. Jenista.
Aidha,
Waziri Jenista ametoa shukrani zake kwa juhudi kubwa za uokoaji lakini pia kwa
ushirikiano wa Viongozi wote wa Mkoa,
Wilaya na Serikali za mitaa kwa kuendelea kutatua changamoto sambamba na
kuwapatia mahitaji muhimu ya kibinadamu waathirika wote wa maporomoko ya tope
na mawe waliopo kambini lengo likiwa ni kurejesha faraja tena," amesema
Jenista.
Wakati
huo huo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais - TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya Afya
Dkt. Festo Dugange amesema kuwa waathirika wa Maafa ya maporomoko ya tope 117
wameendelea kupatiwa matibabu bure tangu kutokea kwa maafa hayo hadi leo kwa gharama ya Serikali katika Hospitali ya
Mkoa, Wilaya na Kituo cha Afya cha Gendabi.
"Mhe.
Rais tayari amekwishaleta fedha zaidi ya Milioni 560 kwa ajili ya kununua dawa
na vifaa tiba lakini pia kununua madaawa kwa ajili ya kinga ya mlipuko wa
magonjwa", amesema Dkt. Dugange.
Wakitoa
neno la shukrani kwa Serikali wakazi wa Katesh akiwemo Emmanuael Joseph
ameipongeza Serikali kwa namna ilivyoratibu suala hilo na kueleza kuwa imewapa
faraja na matumaini mapya kwa kuzingatia misaada waliyopewa na namna
walivyohudumiwa.
“Tunamshukuru
Mhe Rais alivyotusaidia wakati wa maafa na wamefungua barabara sasa tunaweza
kufanya biashara zetu ili kujiletea maendeleo yetu na Taifa kwa ujumla,”
alisema
Naye
Mkazi wa Katesh A, Budila Mkenda ameeleza namna Serikali ilivyowasaidia ikiwemo
kuwafikiwa kwa haraka na kupata misaada kwa wakati hii inaonesha namna viongozi
wetu wanajali.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.