Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imeshauri
serikali kuongeza nguvu ya mapambano dhidi ya virusi vya UKIMWI katika maeneo
ya migodi; vituo vya magari makubwa, maeneo ya mialo ya samaki na maeneo ya
starehe kwa kuangalia namna ya bora kutoa elimu kwa wananchi ili kujenga uelewa
wa pamoja.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo ya kudumu ya
Bunge ya Afya na Masula ya UKIMWI Mhe. Mhe. Stanslaus Nyongo katika Ukumbi wa
Mikutano wa Bunge Jijini Dodoma mara baada ya wajumbe kujadili na kuridhia randama
ya Bajeti ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI
Tanzania –TACAIDS kwa Mwaka wa fedha
2024/2025.
Ameongeza kusema upo umuhimu wa kuweka vituo vya kisasa vya
kusambazia mipira (kondomu) ambazo mhitaji anaweza kuweka tokeni na kupata, utaratibu
ambao ni mzuri kabisa na utaondoa
utaratibu wa kuchukua mipira hiyo kiholela.
“Kuna baadhi ya sehemu wameanza kutumia mfumo huo wa kisasa wa
kusambaza mipira, nasi tuna nafasi ya kuhimiza kuwekwa kwa vifaa hivyo maeneo mbalimbali ya
uwekezaji na maofisini kwa sababu
tumepitisha Bajeti hii ili muweze kufanya Kazi vizuri ,” alibainisha.
Tunahitaji malengo mliyoyakusudia yatekelezwe na yanatimizwe
vizuri ili wananchi wapate mazingira mazuri ya kuishi na kuondokana na hali ya
maambukizi ya UKIMWI ambayo yanafanya watu waishi katika hali ya wasiwasi.
Aidha niipongeze Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mapambano dhidi ya Virusi
Vya UKIMWI na nimpongeze Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
Mafanikio tuliyoyapata kwenye yale malengo ya 95, 95, 95.
“Utafiti umeonesha kwamba kiwango cha maambukizi ya Virusi Vya
UKIMWI kinazidi kupungua na tunakazi kuendelea kusimamia sekta nyingine kuhakikisha
mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI yanafanikiwa, “Alifafanua.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge
na Uratibu ) Mhe. Jenista Mhagama alisema serikali inaendelea kutoa elimu kwa
wananchi juu ya umuhimu wa kupima hususani kwa wanaume kwa kuwa wamekuwa
wakijitokeza kwa idadi ndogo.
“Tunahitaji kurudisha tena ile kampeni ya FURAHA YANGU iliyoongozwa
na Mhe. Waziri Mkuu, kuanza tena kwa
mwaka ujao wa fedha angalau tuhamasishe kiwango kikubwa cha wanaume wajitokeze
kupima VVU,” alifafanua
Serikali kwa kushirikiana na Baraza la watu wanaoishi na Virusi
Vya UKIMWI; Viongozi wa dini na Vongozi wa kijamii tutaendelea kutoa elimu ya
kupinga unyanyapaa na ubaguzi kupitia majukwaa yao, makongamano na vipindi vya
redio.
Awali Mhe. Dkt. Christina Mnzava aliomba serikali kutenga fedha zaidi
kwa ajili ya kuongeza mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI ili kufikia lile
lengo la kufikia 95 ya Mwisho.
Naye Mhe. Cecil Mwambe aliomba serikali kuweka mazingira wezeshi
kwa wakinababa WAVIU kuwa na uwezo wa kushiriki na kujihusisha katika vikundi
kwenye shughuli za miradi ya maendeleo.