Tuesday, August 20, 2024

WAZIRI MHAGAMA AKABIDHI OFISI KWA WAZIRI LUKUVI


Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi katika maeneo ambayo atahitaji kupata taarifa za ziada wakati wa kuratibu shughuli za serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu.

Mhe. Jenista amesema hayo, Jijini Dodoma wakati wa makabidhiano ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) kwa Mhe. William Lukuvi aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo.

Aidha, Waziri Mhagama amewashuruku watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Watumishi wa Ofisi Binafsi ya Waziri Mkuu pamoja na Watumishi wa Ofisi Binafsi ya Naibu Waziri Mkuu kwa ushirikiano waliotoa wakati alipokuwa katika Ofisi hiyo.

“Naomba niwashukuru kwa dhati Watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Watumishi wa Ofisi Binafsi ya Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu kwa ushirikiano Mkubwa mlionipa, Watumishi wa ofisi hizi wako tayari kufanya kazi kwa moyo na kukupa ushirikiano ili kuhakikisha kwamba malengo yale tuliojiwekea ndani ya serikali yanatekelezwa”

“Tumefanya kazi usiku na mchana kama ni uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Mheshimiwa Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ni pamoja na watumishi waliopo kwenye Ofisi hii katika uratibu wa shughuli za serikali,” alibainisha Waziri Mhagama.

 Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi amesema alikabidhi Ofisi hiyo kwa Waziri Mhagama 2014 na kurudi Mwaka 2024 hivyo amekaa nje ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa miaka tisa (9) na kabla alishawahi kuitumikia kama Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu kwa miaka tisa (9).

“Nimeondoka 2014 na kurudi 2024 na kukabidhiwa Ofisi na Waziri niliyemkabidhi wakati huo ambaye ni Waziri Mhagama, aidha nimefanya kazi kwa karibu na Mhe. Mhagama wakati nikiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, wakati Mhe Mhagama akiwa Katibu wa Chama Bungeni hivyo ni Mapenzi ya Mungu tumekutanishwa tena watu walewale tunaofahamiana, niwahakikishie tutaendelea kushirikiana na Katibu Mkuu na Watumishi wote ili kuhakikisha kwamba tunafanya kazi zetu vizuri,” alisema waziri Lukuvi.

 Awali Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi amewapongeza Waziri wa Afya na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kwa kuaminiwa na kuteuliwa kwa nafasi walizopewa.

 “Sisi watumishi wenu tunapenda kuwaahidi kwamba tutaendelea kushirikiana nanyi kutekeleza majukumu yetu lakini kuwatumikia wananchi wa Tanzania,” alisema Katibu Mkuu.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.