Serikali ya Tanzania
imeendelea kuonesha umahiri wake katika masuala ya menejimenti ya maafa nchini
kwa kuzingatia mifumo sahihi ya kukabiliana na maafa na matumizi ya teknolojia
ya kisasa pamoja na miongozo, kanuni na sheria mbalimbali zinazoongoza katika
uratibu wa maafa hayo.
Hayo yameelezwa na Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu
Mheshimiwa Ummy Nderiananga wakati akiongea na waandishi wa habari mara baada
ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Nane wa Ngazi ya Viongozi kuhusu masuala ya kupunguza athari za maafa
pamoja na Kikao cha Tisa cha Jukwaa la Kanda la Afrika la Kupunguza Athari za
Maafa na vilivyofanyika jijini Windhoek nchini Namibia kwa muda wa
siku nne kuanzia Oktoba 21 hadi 24 2024.
Mhe.Nderiananga ameeleza kuwa,
uwekezaji mkubwa umefanywa na Serikali ya Tanzania hususan katika kuhakikisha
teknolojia inavusha Taifa katika kukabili maafa ambapo Serikali ilianzisha
Kituo cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga
katika Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura nchini
Tanzania ambacho kimeifanya nchi kuwa
mahiri katika masuala ya menejimenti ya maafa hususan katika kuzuia, kupunguza
kujiandaa na kukabili maafa pindi yanapotokea.
Katika hatua nyingine
Mhe.Nderiananga amezungumzia kuhusu mkakati wa miaka kumi wa Nishati safi ya
Kupikia ambao utekelezaji wake umeanza mwaka 2024 hadi 2034, ameeleza kuwa unalenga kuhifadhi mazingira,
kulinda afya kwa kuzuia matumizi ya kuni na mkaa ili kuepuka athari za
mabadiliko ya tabia nchi.
“Suala ya mabadiliko ya tabia
nchi linaathiriwa na ukataji wa miti inayopelekea uharibifu mkubwa wa mazingira
na kuchagiza ukosefu wa mvua za kutosha, uwepo wa ukame unaoathiri uzalishaji
wa chakula, tunampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuzindua mkakati
huo,”alisema
Amesema moja ya mikakati
ambayo Tanzania imejiwekea ni kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania
wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.
"....Kama nchi
tumejipanga kuhakikisha Taasisi za Serikali na Mashirika binafsi yanawekeza
ipasavyo katika matumizi ya nishati safi kwa maslahi mapana ya mazingira safi
na salama, Afya zetu na Afrika kwa ujumla " amesisitiza Mhe.Nderiananga
Kufuatia hatua huyo Mhe.Nderianga ametoa wito kwa Mataifa mbalimbali duniani kufuata nyayo za Tanzania kwa kuhakikisha zinaweka mikakati madhubuti ya muda mfupi na mrefu ya Nishati safi ya Kupikia ili kuifanya Dunia kuwe mahali safi na salama pa kuishi.
Awali akifungua mkutano huo
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Kazi na Uchukuzi Nchini Namibia Mhe. John
Mutorwa amesema mikutano hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa ambapo awamu hii
imefanyika nchini Namibia na kuwakutanisha wadau zaidi ya elfu moja wa maafa kwa nchi za Afrika wakiwemo wataalamu kutoka katika ngazi za kitaifa, Serikali za mitaa,
Mashirika ya Umoja wa Kitaifa na Kimataifa, Asasi za Kiraia, sekta binafsi,
taasisi za elimu na utafiti na wanahabari, na hii imetajwa kuwa ni mafanikio
makubwa kwa bara la Afrika.
“Tunashukuru kwa namna nchi
zilivyojitokeza kushiriki mikutano hii muhimu katika kuhakikisha masuala ya
maafa yanakabiliwa na kuwa na Afrika stahimilivu katika maafa, tunawashukuru
sana Mawaziri mlioweza kushiriki mikutano hii, nasi tumepata heshima kama nchi,
na tunaahidi kuendelea kuimarisha mashirikiano yetu kama Bara la Afrika,”alisema
Mhe. Mutorwa
Aidha, alitoa rai kwa kila
nchi kuona umuhimu wa kujipanga kukabili maafa bila kujali utofauti na hali za
Mataifa ya Afrika, lengo kuyafikia na kuyaishi malengo na kuwa tayari kusimamia
masuala haya.
“Maafa si jambo la
kulifurahia, yanapaswa kupewa mwitikio mkubwa na mikakati yenye mashiko na
inayotekelezeka lengo ni kulinda jamii zetu na kuweza kuifanya Dunia sehemu
salama ya kuishi,hili litafanikiwa tukiendelea kushikamana kwa umoja wetu wa
Afrika” alisisitiza
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.