Thursday, June 26, 2025

WAZIRI LUKUVI AITAKA BODI YA ATF KUFIKIA MALENGO KUTOKOMEZA UKIMWI 2030


 

Serikali inategemea Bodi ya Mpya ya Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI italeta fikra mpya, mbinu mpya, na weledi wa hali ya juu ili kuhakikisha Mfuko huo unakuwa chombo madhubuti cha kuhakikisha Tanzania inafikia malengo yake ya kutokomeza UKIMWI ifikapo Mwaka 2030.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. William Lukuvi (MB) wakati akizinduza Bodi ya Tatu ya Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (AIDS Trust Fund - ATF) jijini Dodoma.

 Waziri Lukuvi ameeleza kuwa, Bodi hiyo inapaswa kutambua kuwa dunia ipo katika hatua mpya na muhimu ya kimkakati katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI ambapo Tanzania kama sehemu ya jumuiya ya kimataifa imesaini na inatekeleza ahadi na makubaliano mbalimbali ya kimataifa na kikanda.

 “Tumejidhatiti kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs 2030), hasa lengo la tatu linalohusu kuhakikisha afya njema na ustawi kwa wote, vilevile, tunaitekeleza kwa dhati Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063, pamoja na Azimio la Kisiasa la Umoja wa Mataifa la mwaka 2021 kuhusu UKIMWI” amefafanua Waziri Lukuvi.

Aidha, Mhe Lukuvi ameitaka Bodi hiyo kutambua kwamba kwa sasa dunia inashuhudia mabadiliko makubwa katika namna ya kufadhili mapambano dhidi ya UKIMWI.

 “Wahisani wakuu wa Kimataifa kama PEPFAR na Global Fund wameshaanza kupunguza kwa awamu michango yao huku wakisisitiza umuhimu wa nchi kuchukua umiliki wa ndani na kuhakikisha uendelevu wa kifedha kwa juhudi zake. Mwelekeo huu unatutaka sisi kama Taifa kuongeza uwezo wetu wa ndani wa kifedha ili kuhakikisha mwitikio wa VVU na UKIMWI unaendelea kwa nguvu, kasi, na mafanikio makubwa”.

“Katika muktadha huu, Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI (ATF) ni nyenzo muhimu sana katika kuhakikisha Taifa linakuwa na uhakika wa kifedha na usalama wa afya ya wananchi wake” amebainisha Waziri Lukuvi.

 Vilevile ameeleza kuwa, Mfuko huo ni alama ya dhamira ya kweli ya Serikali kuhakikisha kuwa huduma za VVU na UKIMWI zinadumu, hata katika mazingira ambapo michango ya wahisani inapungua.

 “Kupitia Mfuko huu, tunasisitiza umiliki wa kitaifa ambapo Serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia, taasisi za dini, vijana, watu wanaoishi na VVU na jamii kwa ujumla wanashiriki kikamilifu katika juhudi hizi. Mfuko huu pia unaleta msukumo mkubwa wa uwajibikaji wa kisera na kifedha kwa kuhakikisha matumizi ya fedha yanazingatia uwazi na matokeo yanayoonekana” ameongeza.

 Akimkaribisha mgeni rasmi, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Dkt. James Kilabuko kwa niaba ya Katibu Mkuu wa ofisi hiyo Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa, “mfuko huu ni jitihada za kujenga misingi imara ya uendelevu wa kifedha wa mapambano dhidi ya UKIMWI ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakitegemea zaidi wahisani kutoka nje, tukio hili linaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita  ya kuhakikisha kuwa uendelevu wa mwitikio wa UKIMWI unajengeka kwa msingi wa uhimilivu wa ndani na ushirikiano mpana wa wadau wote wa maendeleo yaa taifa letu”.

 Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bw. Sabasaba Mushingi amemshukuru Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumuamini na kumchagua yeye kuwa Mwenyekiti pamoja na wajumbe wake na hivyo kuahidi kuisimamia na kuingoza bodi hiyo ili kuweza kutimiza malengo ya majukumu waliyopewa.



 

 

 

 

Read More

Tuesday, June 24, 2025

MAAMBUKIZI MAPYA VVU YAENDELEA KUSHUKA


 Imeelezwa kwamba takwimu za maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI katika kipindi cha miaka mitano imeendelea kushuka kulingana na matokeo ya utafiti yaliyofanywa hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Catherine Joachim leo Jijini Dodoma wakati akifungua Kikao cha Wakurugenzi wa Sera na Mipango kutoka katika Wizara za Kisekta na Taasisi ili kuangalia mpango  uendelevu wa mwitikio wa UKIMWI.

Dkt. Catherine amebainisha kuwa, nchi imefanya vizuri kwa takwimu za maambukizi mapya zilizotoka mwaka (2023-2024) ambapo maambukizi mapya yalikuwa watu 60000 kwa mwaka ukilinganisha na kipindi cha miaka mitano iliyopita ambapo maambukizi haya yalikuwa watu 72000 kwa mwaka.

“Halikadhalika ukiangalia vifo vitokanavyo na UKIMWI kwa Matokeo ya Utafiti ya Mwaka (2023-2024) watu 24000 walifariki kulinganisha na watu 28000 waliokuwa wamefariki mwaka (2016-2017),” aliongeza Dkt. Catherine.

Ameongeza kusema, ubaguzi na unyanyapaa kwa WAVIU umepungua kutoka 14% hadi kufikia 5%, hatua ambayo ni muhimu kwa sababu inaongeza muitikio wa watu kupima na kujua afya zao.

Aidha, ilikuendelea kuimarisha mapambano, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania imekutana na Wakurugenzi wa Sera na Mipango kutoka katika Wizara za kisekta na Taasisi ili kuangalia mkakati wa  usimamizi na utawala kutoka ngazi ya msingi mpaka ngazi ya Taifa kwa kuangali gharama ya fedha za UKIMWI kulingana na mikakati ya Serikali katika kuongeza fedha za ndani ya Nchi na kutoka kwenye Sekta Binafsi.

 Vilevile, Dkt. Catherine alisema “tutaangalia namna ya kuimarisha utoaji wa huduma na mifumo ya afya na kuongeza uwajibikaji wa wananchi wenyewe katika muitikio”.



 

 

 

 

Read More

Monday, June 23, 2025

ELIMU KUHUSU OWM SERA, BUNGE NA URATIBU KUENDELEA KUTOLEWA

Mkurugenzi wa Idara ya Uwezeshaji Kiuchumi na Maendeleo ya Sekta Binafsi Bw. Conrad Milinga amesema, maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yamewezesha Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kutoa elimu juu ya fursa mbalimbali za kiuchumi kupitia mikopo na mifuko ambayo iko katika sekta mbalimbali zinazohusiana na uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Mkurugenzi Milinga ametoa kauli hiyo leo wa kilele cha Maadhimisho Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali park Jijini Dodoma.

Ameeleza, Ofisi ya waziri Mkuu imetumia maadhimisho ya wiki hiyo kueleza wananchi na wadau mbalimbali kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Ofisi hiyo ikiwemo Uwezeshaji wananchi kiuchumi, namba ya kujikinga na maafa na Alama za Taifa ambazo ni Wimbo wa Taifa, Ngao ya Taifa na Bendera ya Taifa.

 “Tumeweza kuelimisha wananchi kuhusu mfumo unaotumiwa na Idara ya Menejimenti ya Maafa unaoweza kutambua majanga mapema kabla hayajatokea ili kuwapa wananchi tahadhari ya kujiandaa kabla hayo majanga hayajatokea, tumetoa uelewa kwa wananchi kuweza kufahamu maatumizi sahihi ya Alama za Taifa ikiwemo Ngao sahihi ya Taifa , Beti za wimbo wa Taifa ambapo wimbo huo unatakiwa kuimbwa beti zote mbili na rangi sahihi za Bendera ya Taifa”, amebainisha Bw. Milinga

 Aidha, ameongeza kuwa, Ofisi imeweza kutoa elimu kwa umma kuhusu Idara ya Ufutiliaji na Tathimini ya shughuli za Serikali inavyohusika katika kutoa taarifa za utekelezaji wa miradi mabalimbali inayotekelezwa hapa nchini.

Mbali na hayo, Mkurugenzi Milinga ametoa wito kwa wananchi kujitokeza katika Maonesho ya Kimataifa ya Sababa ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu itashiriki maonesho hayo yanayotarajiwa kuanza tarehe 28 Juni, 2025 Jijini Dar Es Salaam.

“Katika maonesho hayo Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na taasisi zetu zote itanatarajia kushiriki hivyo niwasihi wananchi kutembelea maonesho hayo ili kuweza kupata elimu kuhusu shughuli zote zinazofanya na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Madhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yalianza tarehe 16 Juni, 2025 mpaka tarehe 23 Juni, 2025 chini ya kauli mbiu isemayo “Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidigiti ili Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji”



Read More

Saturday, June 21, 2025

SERIKALI YATOA MFUMO WA RAMANI KUONESHA MAENEO YENYE VIASHIRIA VYA MAJANGA

 


Serikali imeandaa mfumo wenye ramani inayoonesha maeneo yenye viashiria vya majanga katika mikoa na maeneo yake ili kuweka mikakati ya kukabiliana nayo yanapotokea.

Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi, katika kikao kilichohusisha Kamati ya Wataalamu ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa kilocholenga kujadili Mfumo wa Ramani ya Majanga; Mwongozo wa Utumiaji wa Ramani ya Viatarishi vya majanga nchini; na Mkakati wa Taifa Ugharamiaji wa viatarishi vya Maafa, pamoja na Mwongozo wa Uhawilishaji Fedha za Misaada ya Kibinadamu. 

Dkt. Yonazi Alisema, Tanzania inaendelea kuweka mikakati mahsusi kuhakikisha kuwa jamii ya Kitanzania inazuia majanga na inajandaa ipasavyo kukabiliana na majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi.

“Serikali imeandaa mfumo mahsusi ambao una ramani mbalimbali zinazoonesha viashiria vya hatari za majanga katika mikoa na maeneo yake. Mfumo huu unasaidia Sekta zote, Mikoa na Halmashauri zote kujipanga na kuweka mikakati ya namna bora ya kukabiliana na vihatarishi vya majanga katika maeneo yao.” Taarifa za vihatarisha katika ramani hiyo, zitasaidia kila mdau katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo mipango ya matumizi wa ardhi.  alisema.

Aliongeza kuwa: “Mfumo huu utatusaidia kujenga uwezo wa kukabiliana na majanga ndani na nje ya nchi.”

Vilevile, Dkt. Yonazi alisema kikao hicho cha Kamati ya Kitaifa kimepitisha miongozo mbalimbali ya kukabiliana na majanga. Aidha, alieleza miongozo iliyopitishwa itatekelezwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kitaifa na kimataifa.

Alieleza kuwa kikao hicho kilihusisha Kamati ya Wataalam ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa ambao wajumbe wake ni Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi zinazohusika zinazohusika na Usimamizi wa Maafa.

Kwa mujibu wa Dkt. Yonazi, lengo ni kuhakikisha kuwa miongozo ya kukabiliana na majanga inapitiwa na kupelekwa katika sekta zote na kusimamiwa ili iweze kutekelezwa

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na  Uvuvi Profesa. Riziki Shemdoe, alisema  ramani hizo zina mchango mkubwa katika kusaidia sekta ya mifugo na uvuvi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Alibainisha kuwa kupitia matumizi ya ramani hizo, nchi itaweza kupanga kwa ufanisi maeneo ya shughuli za uvuvi na ufugaji kwa kuzingatia maeneo yasiyo na hatari kubwa ya majanga kama ukame, mafuriko au mmomonyoko wa ardhi.

"Ramani hizo zitasaidia kuonesha maeneo yaliyo hatarini kwa mabadiliko ya tabia nchi hivyo kutusaidia katika upangaji wa maeneo kwa ajili ya mifugo, malisho, na miundombinu ya maji.



 

 

 

Read More

Wednesday, June 18, 2025

SERIKALI YAWEKA MIKAKATI YA KUIMARISHA SEKTA YA KILIMO KUPITIA ASDP II

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu, Bw. Omary Ilyas, ameongoza kikao maalum cha Wakurugenzi wa Wizara na Taasisi zinazotekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo awamu ya pili (ASDP II).

Kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma kimejadili utekelezaji wa programu hiyo kwa kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, sambamba na kuanza maandalizi ya mpango wa mwaka ujao wa 2025/2026.

Bw. Ilyas amesema ASDP II inalenga kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza tija kwa wakulima na kusaidia ukuaji wa uchumi wa vijijini kupitia ushirikiano wa kisekta.

Kikao kimehusisha wadau kutoka sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi, pamoja na taasisi za fedha na maendeleo, ili kuhakikisha utekelezaji wa pamoja unaolenga mafanikio ya mkakati wa Taifa wa kilimo.

Read More

Tuesday, June 17, 2025

DKT. YONAZI AMEONGOZA KIKAO CHA KAMATI YA TAIFA YA USHAURI YA SENSA YA WATU NA MAKAZI YA MWAKA 2022


 Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi (mwenyekiti wa kikao) cha Kamati ya Taifa ya Ushauri ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kilichofanyika tarehe 17 Juni, 2025 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere JIjini Dar es Salaam.

 Kikao hicho kimeudhuriwa na Matibu Wakuu wa Wizara za Kisekta, Makamisaa wa Sensa pamoja na baadhi ya wakuu wa Taasisi.Lengo la kikao hicho ni kupokea na kujadili ripoti mbalimbali za utekelezaji wa Awamu ya Tatu na ya Mwisho ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.

 Aidha miongoni mwa ripoti hizo ni pamoja na ile ya Utekelezaji wa Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa kipindi cha kuanzia Desemba 2024 hadi Mei 2025, na Hali ya Utekelezaji wa Anwani za Makazi.

 Pia kikao kimejadili na kupokea Rasimu za Ripoti Tano za kina za Matokeo ya Sensa, na Ripoti ya Makadirio ya Idadi ya Watu kuanzia mwaka 2023 hadi 2050 ngazi ya Mikoa.





Read More

WAZIRI SIMBACHAWENE ATEMBELEA BANDA LA OFISI YA WAZIRI MKUU






Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene (Mb) leo June 17, 2025 ametembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu lililopo katika maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park Jijini Dodoma ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) ikijumuisha idara na taasisi zilizo chini yake inashiriki maonesho hayo. 






 

Read More

Saturday, June 14, 2025

SERIKALI KUIMARISHA MIKAKATI YA KUKABILIANA NA MAAFA NCHINI

 

Serikali y


a Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepiga hatua kubwa kwa kuweka mifumo, sera na mikakati madhubuti ya kuzuia, kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali ya pindi baada ya maafa yanapotokea, ili kuimarisha usalama na ustawi wa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi, wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya wakufunzi kuhusu usimamizi wa hatari zitokanazo na maafa Mafunzo hayo yaliandaliwa na Jumuiya ya Nchi Zilizopo kwenye Mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) kwa ushirikiano na Shirika la Maendeleo la Uturuki (TİKA), Shirika la Msalaba Mwekundu la Uturuki, na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania.

Dkt. Yonazi amesema kuwa mafunzo hayo yamekusudia kuimarisha uwezo wa kitaifa na wa kikanda katika kudhibiti maafa na kuwalinda wananchi. Alibainisha kuwa mafunzo hayo yanaonesha umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kupunguza hatari za maafa (DRR), sambamba na kujenga jamii imara na endelevu.

“Kuwajengea uwezo viongozi wa jamii ni jambo la msingi, kwani wao ndiyo wahusika wa kwanza kutoa mwitikio wakati wa majanga, kusaidia kuratibu misaada na kuhakikisha usalama na ustawi wa jamii,” amesisitiza Dkt. Yonazi.

Aidha, amewapongeza wadau wote waliowezesha mafunzo hayo kufanyika kwa mafanikio, akiwemo TİKA, Sekretarieti ya IORA, Msalaba Mwekundu wa Uturuki, pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwa mchango wao mkubwa na ushirikiano thabiti.

“Ni faraja kubwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mafunzo haya muhimu kwa maendeleo ya ukanda huu. Nawatakia kila la heri na natumai mmefurahia uwepo wenu hapa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla. Tunawakaribisha tena na tena,” amesema.

Kwa upande wake, Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Mheshimiwa Bekir Gezer, alieleza kuwa Serikali ya Uturuki itaendelea kushirikiana na Tanzania, hasa katika masuala yahusuyo maafa. Amesisitiza kuwa nchi yao iko tayari kusaidia kwa kutoa vifaa muhimu vya kukabiliana na maafa.

Naye, Bi. Filiz Sahinci, Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la TİKA nchini Tanzania, amesema shirika hilo limejikita kusaidia juhudi za kukabiliana na maafa kwa kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika kutatua changamoto zinazotokana na maafa.

Mafunzo hayo yamehusisha wakufunzi kutoka Mataifa Kumi na Moja zilizopo kwenye Mwambao wa Bahari ya Hindi na yameweka msingi muhimu wa kuimarisha utayari wa jamii dhidi ya majanga na magonjwa ya kuambukiza, hususan katika mazingira ya baada ya maafa.



Read More

Monday, June 9, 2025

TUME HURU YA UCHAGUZI YAPONGEZWA MAANDALIZI UCHAGUZI MKUU 2025

 




Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi ameipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kukamilisha zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuendelea vyema na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

 Dkt. Yonazi ametoa pongezi hizo leo tarehe 09 Juni, 2025 Kisiwani Unguja, Zanzibar wakati wa kufungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la INEC, ambapo imewaasa viongozi wa Tume kuendelea kuwa imara na kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano ili kuhakikisha kuwa uchaguzi unakwenda vizuri.

 “Kwanza niwapongeze sana kwa kukutekeleza jukumu hili kubwa ambalo mmekabidhiwa na Taifa letu na kwa namna ya pekee kabisa Mwenyekiti wa Baraza unifikishie salamu za pongezi kwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele pamoja na wajumbe wa Tume kwa kazi kubwa ambayo mmeifanya katika kuhakikisha kuwa shughuli za uchaguzi nchini kwetu zinakwenda vizuri,” amesema Dkt. Yonazi.

 Ameeleza kuridhishwa na jinsi Tume ilivyotekeleza kwa ufanisi zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuongeza kuwa ni matarajio ya Serikali kuwa utendaji huo mzuri wa Tume utaendelea kwa viwango vya juu kwa mujibu wa katiba, sheria na taratibu mbalimbali ambazo zimewekwa.

 Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndugu. Kailima Ramadhan amesema tayari Tume imekamilisha awamu ya kwanza ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo kwa sasa inaendelea na uboreshaji wa awamu ya pili.

 “Tume imeshakamilisha uboreshaji wa awamu ya kwanza na imeshachakata na kutoa daftari la awali na imeshakamilisha uboreshaji wa awamu ya pili mzunguko wa kwanza na mzunguko wa pili. Tunategemea kuanzia tarehe 28 mwezi huu (tarehe 28 Juni, 2025) tutaanza mzunguko wa tatu wa uboreshaji katika Vyuo vya Mafunzo Tanzania Zanzibar na Magereza Tanzania Bara kwa wanafunzi na wafungwa waliohukumiwa kifungo chini ya miezi sita,” amesema Kailima.

 Katibu huyo wa Baraza amesema mzunguko huo wa tatu utahusisha vituo 140 vya kuandikisha wapiga kura ambapo 130 vipo kwenye magereza Tanzania Bara na vituo 10 vipo kwenye vyuo vya mafunzo Tanzania Zanzibar. Zoezi hilo linatarajiwa kufanyika kwa siku saba hadi tarehe 04 Julai, 2025.

 Ameongeza kuwa Tume imekamilisha maandalizi ya nyaraka mbalimbli kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ikiwa ni pamoja na Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025, Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025 na maelekezo mbalimbali kwa ajili ya watendaji wa uchaguzi na wadau wa uchaguzi kupata miongozo kwa ajili ya utekelezaji wa uchaguzi.

 Alimkumbusha mgeni rasmi kuwa tayari Tume imekamilisha zoezi la ugawaji wa majimbo na kwamba kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kutakuwa na jumla ya majimbo 272 yatakayofanya uchaguzi wa wabunge katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kata 3960 kwa ajili ya uchaguzi wa madiwani kwa Tanzania Bara.

 


Read More

Friday, June 6, 2025

MAMLAKA YA HALI YA HEWA DUNIANI KUENDELEA KUUNGA MKONO JITIHADA ZA TANZANIA KUKABILIANA NA MAAFA

 


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization - WMO) Bi. Celeste Saulo ameahidi kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha mfumo wa Tahadhari ya mapema (early warning systems) kwa ajili ya kuchukua hatua za haraka kuzuia na kukabiliana na maafa pindi yanapotokea.

Ameyasema hayo wakati wa kikao cha pembezoni mwa Jukwaa la Nane la Dunia la Kupunguza Madhara ya Maafa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi pamoja na ujumbe alioongozana nao kwa lengo la kuzungumza mikakati na mipango ya kuendeleza ushirikiano mapema 05 Juni 2025 mjini Geneva Uswizi.

Bi. Celeste Saulo amesema wapo tayari kuwezesha maeneo mbalimbali ikiwemo ya kuongeza ueleza kupitia mafunzo kwa wataalam kwenye masuala ya Matumizi ya Taarifa za  hali ya hewa pamoja na masuala muhimu kama elimu na kuona namna wanavyoweza kuunga nguvu za Pamoja katika matumizi ya vifaa vya kisasa vya utabiri wa hali ya hewa na matumizi ya taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya hewa kwa lengo la kuendelea kuwa na tahadhari za mapema.

“Tunaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa kuwa tuna ushirikiano wa muda mrefu.Aidha, tunazingatia umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa maafa kwa kuzingatia hatua zinazochukuliwa na Tanzania ya kujenga uwezo pamoja na kushirikiana na nchi zingine na kuandaa miradi ambayo inazingatia vipaumbele vyenye maslahi kwa wote,” alisisitiza Bi. Saulo

Kwa hatua hiyo Bi. Saulo ameipongeza Tanzania kwa namna imeendelea kuwa ya mfano katika kuratibu, masuala ya menejimenti ya maafa na kuhakikisha wanakuwa na mifumo ya tahadhari za mapema inayowasaidia katika kupeana taarifa za mapema zinazosaidia kuzuia madhara yanayoweza kutokea wakati wa maafa.

Aidha alifafanua kuwa mifumo ya tahadhari za mapema ni muhimu kwani inasaidia kuandaa mifumo jumuishi ya kupeana taarifa za tahadhari za mapema; kupata taarifa mapema zinazosaidia kupunguza madhara ya majanga, kuwezesha upatikanaji wa taarifa za awali zitakazosaidia kuimarisha mfumo wa maisha ya jamii ambayo iko katika hatari ya kuathirika na majanga na kupunguza madhara katika kujiandaa kwa ajili ya maafa yanayoweza kutokea.

Katika mazungumzo hayo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi amesisitiza dhamira ya Serikali ya Tanzania kuendeleza ushirikiano na Mamlaka ya Hali ya Hewa Duniani katika kuimarisha masuala ya usimamizi wa maafa inayolenga kuwawezesha kuwa na jamii stahimilivu na majanga na kuifanya Dunia kuwa sehemu salama ya kuishi.

 

Akiongelea namna Tanzania inavyoendelea kuratibu masuala ya Menejimenti ya maafa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo ili kuendela kulinda jamii isipatwe na madhara yatokanayo na maafa huku akiainishsa mafanikio makubwa ikiwemo la uwepo wa Kituo cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga na Tahadhari ya Mapema (National Emergency Operation and Communication Center Situation Room) katika Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura nchini Tanzania chenye tija kwa Taifa kwani kimerahisisha utekelezaji na utendaji wa haraka katika masuala ya maafa.

Viongozi hao wamejadili umuhimu wa kuweka mikakati madhubuti ya maendeleo jumuishi ili kuhakikisha juhudi za pamoja katika kukabiliana na maafa kwa kushirikiana na wadau wengine ili kuinufaisha jamii nzima.

Read More

Tuesday, June 3, 2025

“USHIRIKI WA TANZANIA JUKWAA LA DUNIA WAONGEZA FURSA ZA KIMATAIFA KUKABILIANA NA MAAFA” DK. YONAZI



TANZANIA imeshiriki Jukwaa la Nane la Dunia la Kupunguza Madhara ya Maafa lenye jukumu muhimu katika kuhamasisha na kukuza ushirikiano kati ya Serikali, Wadau na Mfumo wa Umoja wa Mataifa ili kuharakisha utekelezaji wa hatua za kupunguza madhara ya maafa.

Akizungumza wakati wa Mkutano huyo unaoendelea Mjini Geneva Uswisi kuanzia tarehe 02 hadi 6 Juni 2025, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri, Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Dkt.Jim Yonazi alisema jukwaa hilo ni chombo cha kutathmini, kujadili maendeleo ya utekelezaji na kuimarisha masuala ya usimamizi wa maafa kimataifa kupitia makubaliano ya hiyari ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ambayo yameridhiwa na Makubaliano ya hiyari ya kimataifa yanayotekelezwa kwa sasa ni Mkakati wa Sendai wa Kupunguza Madhara ya Maafa 2015 – 2030

“Jukwaa hili hutumika kama chombo muhimu cha kukuza ushirikiano katika utekelezaji wa ajenda nyingine za kimataifa zinazochangia kupunguza madhara ya maafa, ikiwa ni pamoja na mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi na malengo ya maendeleo endelevu.

Aliongeza kuwa, Matokeo ya jukwaa hilo yanatumika katika kutoa muelekeo wa masuala ya usimamizi wa maafa katika maazimio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, baraza la umoja wa mataifa la kiuchumi na kijamii na jukwaa kuu la kisiasa la umoja wa mataifa kuhusu maendeleo endelevu.

Kwa mujibu wa Dkt. Yonazi ameelezwa kuwa, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Madhara ya Maafa imepewa jukumu la kuandaa Jukwaa la Dunia na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Jukwaa hufanyika kila baada ya miaka miwili ambapo tangu mwaka 2007, limefanyika mara saba.

Vilevile alisema jukwaa hilo limejumuisha ajenda kuhusu kuimarisha utekelezaji wa mkakati wa Sendai kwa kuzingatia maendeleo na changamoto zilizoainishwa katika mapitio yake ya muda wa kati na Azimio lake kupitia Baraza la Umoja wa Mataifa 2023,

Ajenda nyingine ilihusu kuimarisha mikakati ya kitaifa na serikali za mitaa na mipango ya kupunguza madhara ya maafa, kwa kuzingatia athari za maafa ya hivi karibuni;

“Jukwaa limejadili namna ya kuimarisha mitandao iliyopo na kuanzisha ushirikiano mpya katika ngazi za kimataifa, kitaifa na wadau wa ndani, kubadilishana ujuzi, teknolojia na uzoefu kuhusu sera, programu na uwekezaji kuhusu kupunguza hatari ya maafa.

Dk.Yonazi alisema matokeo ya ushiriki wa jukwaa hilo ni kuimarisha utekelezaji wa Mkakati wa Sendai kupitia Sheria na Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa kwa kupata uzoefu na fursa za kimataifa na wadau.

Matokeo mengine ni kuimarisha uratibu na ushiriki wa pamoja wa sekta na mtazamo wa wadau katika kutekeleza shughuli za maeneo ya maendeleo endelevu, kuibua fursa za rasilimali fedha na mipango ya kiuchumi, kuimarisha miundombinu, hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda mifumo wa ikolojia katika maeneo ya kupunguza hatari ya maafa, tahadhari ya mapema na kurejesha hali.

“Jukwa hili litasaidia kuongeza uwekezaji katika usimamizi wa maafa na tahadhari ya mapema kwa wote kupitia ushirikiano na taasisi za Umoja wa Mataifa na Kimataifa,”alisema.



Read More

Monday, June 2, 2025

DKT. YONAZI ATEMBELEA UWAKILISHI WA KUDUMU WA TANZANIA KATIKA OFISI ZA UMOJA WA MATAIFA GENEVA, AAZIMIA KUIMARISHA USHIRIKIANO

 



Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ametembelea Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Uswisi, ikiwa ni ziara yake ya kikazi nchini humo, lengo ni kushiriki Jukwaa la Nane la Dunia la Kupunguza Madhara ya Maafa linalofanyika kuanzia tarehe 2 hadi 6 Juni, 2025 Jijini Geneva Nchini Uswisi.

Dkt. Yonazi ameongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaoshiriki Mkutano huo huku akiambatana na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Brigedia Jenerali Hosea Ndagala, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Ofisi hiyo Bi. Stella Mwaiswaga, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini, Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Charles Msangi pamoja na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Menejimenti ya Maafa sehemu ya Utafiti, Ofisi hiyo Bw. Vonyvaco Luvanda.

Aidha, amepokelewa na kufanya mazungumzo na Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa na Mashirika mengine ya Kimataifa Geneva Uswisi Mhe. Dkt. Abdallah Possi na kumweleza kuwa ushiriki wa Tanzania katika Jukwaa hilo unatija na manufaa makubwa kwa Taifa.

Alifafanua kuwa Jukwaa hilo linalenga kutathmini, kujadili maendeleo ya utekelezaji wake na kuimarisha masuala ya usimamizi wa maafa kimataifa kupitia makubaliano ya hiyari ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ambayo yameridhiwa.

Sambamba na hilo, Dkt. Yonazi ameupongeza ubalozi huo na kuahidi kuendeleza ushirikiano masuala mbalimbali ili kuona fursa zilizopo Uswisi na kuzichangamkia fursa za kibiashara sambamba za zinazoendana na mabadiliko ya Kiteknolojia.

Akitoa maelezo kuhusu utekelezaji wa shughuli za ubalozi, Mhe. Dkt. Possi amesema amepongeza ushiriki wa Tanzania katika Jukwaa hilo la Nane na kusisitiza kuwa Tanzania ina kila sababu ya kuendelea kushiriki katika mikutano hiyo ili kuwa na mwendelezo mzuri utakaowezesha nchi kupata na kutumia fursa mbalimbali zinazotokana na Majukwaa hayo.



 

Read More