Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Bi. Stella Mwaisaga, amekutana na kufanya
mazungumzo na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Kimataifa la Helen Keller
International, Bw. William “Bill” Toppeta.
Mazungumzo hayo yalilenga
kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na shirika hilo katika
utekelezaji wa masuala ya lishe, ambapo Bw. Toppeta aliipongeza Serikali kwa
juhudi kubwa katika kusimamia na kuratibu lishe, huku akisisitiza dhamira ya
Helen Keller International kuendelea kushirikiana na Serikali katika
kuhakikisha jamii inapata huduma bora za lishe.
“Tunaishukuru Serikali ya
Tanzania kwa usimamizi wake imara katika masuala ya lishe. Tutaendelea kuwa
wadau wa karibu katika kusaidia juhudi hizi muhimu kwa afya ya wananchi,”
alisema Bw. Toppeta.
Ujumbe huo wa Helen Keller International upo nchini kwa
ziara ya kukagua na kutathmini utekelezaji wa miradi ya shirika hilo, hususan
katika sekta ya lishe, ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu ni mratibu mkuu wa kitaifa
wa masuala hayo.