Watanzania wameaswa
kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotokana na ujenzi wa uwanja mpya
wa mpira wa miguu unaoendelea kujengwa Jijini Arusha kwa ajili ya michuano ya
Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.
Wito huo umetolewa leo, na Mwenyekiti wa
Kamati ya Makatibu Wakuu, ambaye pia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, wakati wa ziara ya kamati
hiyo ya kukagua maendeleo ya mradi huo unaoendelea Jijini Arusha.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Dkt. Yonazi
ameeleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 74,
huku akisisitiza kuwa uwanja huo ni uwekezaji wa kimkakati utakaoleta tija kwa
taifa hata baada ya kumalizika kwa mashindano hayo.
"Ujenzi huu umefikia hatua nzuri na
utakamilika kwa wakati, niwaombe Watanzania wachangamkie fursa zinazojitokeza
sasa wakati wa ujenzi na hata baada ya kukamilika kwani uwanja huu utaendelea
kutumika kwa mashindano ya ndani na kimataifa," amesema Dkt. Yonazi.
Aidha, Dkt. Yonazi amebainisha kuwa, usimamizi
wa mradi huo unazingatia viwango vya juu vya ubora, ikiwemo kuweka miundombinu
rafiki kwa watu wenye mahitaji maalum, ili kuhakikisha huduma zote zinapatikana
kwa usawa kwa wageni na wenyeji watakaotembelea eneo hilo.
Uwanja wa Arusha ni miongoni mwa miundombinu
muhimu inayotayarishwa na Serikali ya Tanzania, ambayo ni mshiriki mwenza
katika uenyeji wa michuano ya AFCON 2027, ikishirikiana na nchi za Kenya na
Uganda.
Kukamilika kwa uwanja huo kunatarajiwa
kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii wa michezo jijini Arusha, kutokana na
nafasi ya jiji hilo kama kitovu cha utalii katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.