Wananchi
wa Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga wanatarajiwa kunufaika zaidi kiuchumi kupitia
uwekezaji wa Serikali katika sekta ya kilimo cha mwani, hatua inayolenga
kuongeza thamani ya mazao ya bahari na kuboresha maisha ya jamii za pwani.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa kaushio jipya na mashine mbili za kisasa za kusaga mwani
uliofanyika katika Kijiji cha Kichaka Miba, Wilaya ya Mkinga, Naibu Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Ummy
H. Nderiananga, amesema mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuimarisha
uchumi wa wananchi wa maeneo ya pwani.
Mradi
wa Kuimarisha Usalama wa Bahari unaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia
Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja
wa Mataifa (UNDP), na unatekelezwa na Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini
(IRDP) Tawi la Mwanza kwa ushirikiano na Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga ambapo
Lengo lake ni kuimarisha ufuatiliaji na ulinzi wa bahari pamoja na kuongeza
thamani ya rasilimali za baharini kwa manufaa ya jamii.
Mhe.
Nderiananga amesema kupitia mradi huo, Serikali imenunua boti mbili za doria,
kujenga kaushio la kisasa la mwani, kusimika mashine za kusaga mwani na kutoa
mafunzo kwa vikundi vya wakulima. Ameongeza kuwa hatua hizo zitaboresha ubora
wa mwani, kupanua masoko, kuongeza kipato cha wakulima na kusaidia kuzuia
vitendo vya kihalifu baharini.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP), Dkt.
Guvenail Mkonoko, amesema kabla ya utekelezaji wa mradi huo wataalamu walifanya
tathmini iliyobaini changamoto za mbinu duni za kilimo, ukaushaji usio salama
na ukosefu wa miundombinu ya kisasa ya uchakataji.
Naye
mwakilishi wa wakulima wa mwani, Bi. Mwamvua Bwebwe, Ameishukuru Serikali ya
Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kuongeza
uzalishaji, kupunguza upotevu wa mazao na kuboresha kipato chao.


No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.