Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na watu wenye ulemavu), Jenista Mhagama amesema Serikali
itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa viongozi wa Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi Nchini (TUCTA) ili kuleta tija na ufanisi katika sekta ya kazi..
Waziri Mhagama aliyasema hayo leo Jijini Dar es
Salaam tarehe 05 Desemba, 2016, wakati wa mkutano wake na Viongozi hao wa TUCTA waliofika ofisini kwake
kwa ajili ya kujitambulisha mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa shirikisho
hilo.
“Tumefarijika sana kwa TUCTA kupata uongozi mpya
ambao tuna uhakika wanachama wamezingatia masuala muhimu katika uchaguzi
wao ikiwemo weledi na kutazama dira ya sekta ya wafanyakazi nchini”.
Aidha aliongeza kuwa Viongozi hao wana jukumu kubwa
la kuleta tija na maendeleo chanya katika sekta ya kazi nchini na kuhimiza kuwa
wafanyakazi ni rasilimali muhimu katika kuleta maendeleo ya nchi.
Kwa mujibu wa Mhagama ameahidi Viongozi hao kufanya
kikao kazi mapema iwezekanavyo kwani uchaguzi umekwisha na sasa kilichobaki ni
kufanya kazi.
Pia amesisitiza ushirikiano wa kudumu kati ya
Serikali, Waajiri na wafanyakazi ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua
migogoro iliyopo.
Kwa upande wake Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamghokya
alimshukuru Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kusimamia utu wa mtumishi kwa
kuhaidi kuwalinda kutokana na baadhi ya viongozi kutoa lugha zisizosahihi.
Aidha, ameishukuru Serikali kwa kuwa karibu nao kwa
muda wote na kuhaidi kuendeleza ushirikiano huo ili kuleta tija katika kazi.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.