WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemaliza mgogoro wa ardhi uliodumu kwa miaka 17
kati ya vijiji viwili vya Ortukai na Esilalei na Taasisi ya Tanzania Land
Conservation Trust (TLCT) baada ya kukabidhi hati ya shamba la Manyara
Ranch kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Stephen Ulaya.
Hati
hiyo imetolewa jana jioni (Jumapili, Desemba 4, 2016) na Waziri Mkuu katika
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya Mto wa Mbu kwenye viwanja vya
Barafu baada ya kubadilishwa umiliki wa shamba hilo kwenda kwa wananchi wa vijiji
hivyo vilivyopo kwenye Kata ya Elesilalei Wilayani Monduli Mkoani Arusha.
Hatua
hiyo imekuja baada ya kilio cha muda mrefu cha wananchi hao kudai kuwa Rais wa
Awamu ya tatu, Benjamin Mkapa aliagiza shamba hilo ligaiwe kwa wananchi hao
lakini jambo hilo halikufanyika na badala yake watu wachache walijimilikisha
shamba hilo kinyemela chini ya wenyekiti wa bodi ya TLCT.
Waziri
Mkuu alisema Serikali imeamua kurudisha umiliki wa shamba hilo kwa wananchi wa
vijiji hivyo viwili baada ya Baraza la Madiwani na Uongoziwa Wilaya hiyo ya
Monduli kuridhia kwa pamoja umiliki huo kurudi kwa wananchi kama ilivyoamriwa
hapo awali.
"Shamba
hili lenye ukubwa wa ekari 44,930 sasa si mali tena ya Taasisi ya Tanzania Land
Conservation Trust (TLCT) iliyokuwa inafadhiliwa na Shirika la African Wildlife
Foundation (AWF) sasa ni mali ya wananchi na halmashauri ya wilaya ya Monduli
ndio itapanga matumizi bora ya ardhi ya shamba hili mliloteseka nalo kwa muda
mrefu ," alisema.
Alisema
nyaraka zinazoonyesha kuwa shamba hilo lililotolewa kwa wananchi wa vijiji vya
Elesilalei na Ortukai na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu mwaka 1999 kwa ajili ya
kilimo na ufugaji lakini jambo hilo halikufanyika badala yake taasisi ya
TLCT ikajimilikisha shamba hilo kinyume na maagizo.
Hata
hivyo Waziri Mkuu alisema Serikali inaendelea kufuatilia maeneo yote
yaliyochukuliwa na watu bila ya kuyaendeleza na kuwapa wananchi. "Ni kwa
nini watu wenye fedha wanachukua mashamba mkubwa bila ya kuyaendeleza huku
wananchi wakiteseka kwa kukosa maeneo ya kilimo na ufugaji," alisema.
Awali
kabla ya kuhutubia mkutano huo wa hadhara Waziri Mkuu alitembelea shule ya
msingi ya Laiboni iliyoanzishwa na mzee maarufu wa kimila wilaya huko
Laigwanani Meshuko Ole Mapii ambayo inawanafunzi 102 wakiwemo wajukuu na watoto
wa mzee ambapo alitangaza umiliki wa shamba hilo kurudi kwa wananchi.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa William Ole
Nasha alisema wizaraya yake itaendelea kutekeleza Sera za Kilimo nchini pamoja
na kusimamia matumizi bora ya ardhi kwenye shamba hilo kutokana na ukosefu
mkubwa ardhi kwa ajili ya wafugaji na wakulima.
“Nikuhakikishie
Mheshimiwa Waziri Mkuu kuwa tutaendelea kuhakikisha wananchi wafanya ufugaji wa
kisasa wenye kwa tija kwa kutumia shamba hili. Pia nakupongeza Mheshimiwa
Waziri Mkuu kwa kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa vitendo na maagizo
uliyotupa ya kuhakikisha wananchi wanatumia ardhi hiyo vizuri tutayasimamia,”
alisema.
Baada
ya shamba hilo kurudishwa kwa wananchi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo
alisema ‘’Nashukuru leo umiliki wa shamba hili umebadilishwa na naishukuru
Serikali yangu tulivu kwa kutoa hati hii kwa Mkurugenzi wa wilaya ya
Monduli ili wananchi waweze kunufaika na ardhi yao na sio watu wachache
wanaolipwa mamilioni ya fedha bila ya sababu za msingi’’.
Naye
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Jumanne Maghembe aliwasihi wananchi hao
kuheshimu njia za mapito ya wanyama (ushoroba) katika eneo hilo ambalo
wanyamapori kutoka hifadhi za Tarangire, Manyara na Ngorongoro wanalitumia kwa
ajili ya kupita kwenye hifadhi hizo mara kwa mara.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amempa siku mbili Mkuu wa
Idara ya Ardhi na Mazingira wa wilaya ya Monduli , Adil Mwanga kumuondoa
muwekezaji, Lekisongo Meijo katika shamba lenye ukubwa wa ekari 2,800 lililoko
katika kijiji cha Lemoti tarafa ya Kisongo ambalo alimilikishwa bila ya kufuata
taratibu na kulirudisha kwa wananchi.
Pia
amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Gambo kufanya uchunguzi wa umiliki wa
mashamba mengine makubwa ambayo yana migogoro na hayajaendelezwa mkoani
humo likiwemo la Makuyuni Stein Seed Valley na kuipatia ufumbuzi
migogoro hiyo.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.