*Ataka karakana za ujenzi, useremala zianzishwe kupunguza gharama
*Asisitiza ufyatuaji matofali kukabili upungufu wa nyumba za askari
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamishna Mkuu wa Magereza, Dk. Juma
Malewa asimamie zoezi la upimaji wa maeneo yanayomilikiwa na Magereza
kote nchini na kuhakikisha yanawekewa mipaka.
Ametoa
agizo hilo leo mchana (Jumatatu, Februari 13, 2017) katika kikao baina
ya Kamishna huyo mpya na Maafisa Magereza wa Mikoa yote na maafisa
wanaoshughulikia kilimo na viwanda alichokiitisha ofisini kwake mjini
Dodoma.
“Magereza
yetu mengi yako kwenye maeneo ambayo hayajapimwa. Baadhi ya maeneo kuna
migogoro kwa sababu wananchi wamejenga karibu kabisa na maeneo ya
Magereza. Lazima tupime maeneo yote na kuyawekea alama mipakani ili
kubainisha maeneo yetu,” amesisitiza.
Mbali
ya maeneo ya Magereza, Waziri Mkuu amesema, jeshi hilo lina mashamba
makubwa ambayo pia hayajapimwa hali ambayo amesema imechangia baadhi ya
wananchi kulima ndani ya maeneo ya jeshi hilo.
“Natambua
kuwa jeshi hili lina mashamba makubwa lakini nayo pia hayajapimwa. Kila
RPO ni mjumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wake, tumieni
wapima ardhi kutoka kwenye Halmashauri zenu na mhakikishe kuwa maeneo
hayo yanapatiwa hati,” amesema.
Amesema
umefika wakati sasa kila gereza litambue na kuainisha fursa walizonazo
ili waweze kuamua ni kwa kiasi gani wanaweza kujitegemea kwa uzalishaji.
“Kama ni kilimo, ufugaji, au uzalishaji wa umeme, tuangalie ni kipi
kinaweza kuvutia uwekezaji, lakini cha msingi zaidi ni lazima tuwe na
hati za maeneo tuliyonayo,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema kuna baadhi ya magereza yalikuwa maarufu kwa kilimo lakini
hivi sasa hakuna hata moja lenye trekta na kama yapo ni moja au mawili
tu. “Sasa hivi teknolojia ya kilimo imebadilika, ni lazima tutumie zana
za kilimo ili kwenda na kilimo cha kisasa.
Akizungumzia
kuhusu ufugaji na uvuvi wa samaki, Waziri Mkuu aliagiza jeshi hilo
litumie maafisa wake waliobobea kwenye sekta hizo, watumike kuendeleza
na kuhamisha ujuzi wao kwa wafungwa wanaotumikia vifungo ili wanapotoka
gerezani, wawe na ujuzi ambao utawasaidia kujikimu kimaisha wanaporudi
kuishi vijijini.
“Nimetembelea
maonesho ya Nanenane na Sabasaba huko nimekuta wamejenga banda la kuku
juu ya bwawa la samaki. Hii ina maana kuku wanakula na kinyesi chao
kinakuwa ni chakula kwa wale samaki walioko bwawani,” amesema.
Amemtaka
Dk. Malewa aangalie uwezekano wa kuanzisha karakana na ujenzi kwenye
kila gereza ili maafisa na wafungwa waliopo kule watumike kufanya kazi
kwenye karakana hizo. “Nimetembelea gereza la Isanga, nikakuta kuna
milango haina komeo. Kwa vile hakuna karakana, inabidi atafutwe fundi
kutoka mtaani ili aje kutengeneza kitasa au komeo. Tuanzishe karakana na
tuziboreshe,” amesisitiza.
Amesema
uwepo wa karakana hizo ziwe ni za umeme, ujenzi au useremala, utasaidia
kupunguza gharama za uendeshaji kwa jeshi la magereza kwa matengenezo
madogo madogo yatafanywa na watu wa kwenye karakana badala ya kutumia
watu wa nje.
Amesema
ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa nyumba za askari, kila afisa
magareza wa mkoa hana budi kuandaa matofali ya kutoka kwani timu za
wafyatuaji wanazo na nguvukazi wanayo pia.
“Badala
ya kutegemea wazabuni, kule kwenye udongo mzuri, tafuteni vifaa mfyatue
matofali ya hydraform. Kule kwenye mchanga, fyatueni ya saruji. Kuweni
na matofali ya kutosha kulingana na mahitaji yenu, mtakuwa mmepunguza
gharama za ujenzi wa nyumba za askari kwa kiasi kikubwa,” amesisitiza.
Kwa upande wake,
Kamishna Mkuu huyo, Dk. Malewa amesema atafuatilia suala la upimaji wa
maeneo ya magereza kwa sababu wanao wapimaji na vifaa wanavyo. Amesema
kuna magareza 11 yenye migogoro ya maeneo na wananchi.
“Pia
tutafuatilia upimaji wa maeneo ya mashamba ya magereza. Tumeanzisha
mashamba makubwa ya kilimo na tutahakikisha maeneo hayo yote yanapimwa
na kuwekewa alama za mipaka,” amesema.
Kikao
hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Mwigulu
Nchemba; Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Bw. William Tate Ole
Nasha; Kamishna Jenerali wa Magereza, Makatibu Wakuu wa Wizara ya Kilimo
wanaoshughulikia Kilimo na Mifugo pamoja na Katibu Mkuu wa Mambo ya
Ndani.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.