Friday, April 7, 2017

MAPITIO NA MWELEKEO WA BAJETI YA OFISI YA WAZIRI MKUU 2017/2018-SEHEMU YA TATU

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe . Kassim Majaliwa akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano kuhusu mapitio na mwelekeo wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.  



61.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na ukarabati na ujenzi wa miundombinu katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya, Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam. Ujenzi wa majengo 20 ya mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,840 umekamilika. Vilevile, Serikali inaimarisha miundombinu katika vyuo vya ufundi vya Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam, Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya na Chuo cha Ufundi Arusha kwa lengo la kuimarisha mafunzo ya Ufundi na Sayansi nchini. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaimarisha Vyuo vya Elimu ya Juu ili kuwezesha upatikanaji wa wataalam mahiri katika nyanja mbalimbali hususan Sayansi na Teknolojia.

Maji


62.       Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kusogeza huduma za maji karibu zaidi na wananchi ili wasitumie muda mwingi kutafuta maji badala yake wajikite katika shughuli za uzalishaji mali. Ili kutimiza azma hiyo, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maji mijini na vijijini ikiwemo miradi ya vijiji 10 chini ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Kati ya mwezi Julai na Desemba 2016, miradi 90 ya maji vijijini ilikamilika na kufanya idadi ya miradi iliyokamilika kufikia 1,301 kati ya miradi 1,810 iliyolengwa. Miradi 509 iliyobaki ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na yote inatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Juni, 2017.

63.              Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji vijijini katika Halmashauri zote nchini ukiwemo mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe unaolenga kuhudumia wananchi zaidi ya 456,000 katika vijiji 38 kwenye miji ya Same, Mwanga na Korogwe Vijijini. Ili utoaji wa huduma ya maji uwe endelevu, wananchi waendelee kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji, uvunaji wa maji ya mvua na matumizi bora ya maji. Nitumie fursa hii kuwakumbusha watendaji katika Halmashauri zote kusimamia kikamilifu sheria inayokataza shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji.

Afya


64.              Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhamasisha wananchi kujikinga dhidi ya magonjwa ikiwemo kuhimiza lishe bora. Aidha, Serikali inaboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini kwa kujenga vituo vya kutolea huduma za afya na tiba pamoja na kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba. Bajeti ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 31 mwaka 2015/2016 hadi Shilingi bilioni 251 mwaka 2016/2017. Vilevile, Serikali imeanzisha utaratibu wa kununua dawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji kwa lengo la kupunguza gharama. Serikali pia imeanzisha maduka ya dawa yanayouza bidhaa zake kwa bei nafuu kwa wananchi katika hospitali za mikoa ambapo hadi sasa maduka manane (8) yameanzishwa, na ujenzi wa maduka mengine katika mikoa iliyobakia unaendelea.

65.              Mheshimiwa Spika, Serikali pia inaimarisha huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto nchini kwa kutekeleza Mpango Mkakati wa Kupunguza Vifo Vitokanavyo na Uzazi na Vifo vya Watoto wa mwaka 2016-2020. Lengo ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020, asilimia 50 ya vituo vya Afya nchini vinakuwa na uwezo wa kutoa huduma za dharura kwa matatizo ya uzazi ikiwemo upasuaji na huduma za watoto wachanga.  Hadi sasa, vituo vya afya 159 vinatoa huduma za upasuaji ambapo vituo 106 ni vya Serikali.

Vilevile, Serikali imeimarisha utoaji wa huduma za kinga na hivyo kuchangia kutokomezwa kwa ugonjwa wa Polio hapa nchini na hatimaye nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi zilizopatiwa hati ya kutokomeza ugonjwa huo. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kuimarisha huduma za afya nchini kwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi na kuimarisha huduma za kinga ili kupunguza vifo vya watoto na akina mama pamoja na makundi mengine. Naomba nitoe wito kwa wote Watanzania wajiunge kwa wingi na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili Serikali iweze kuwachangia kupitia mfumo huo.

BUNGE


66.           Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa. Katika mwaka 2016/2017, Ofisi ya Bunge iliratibu na kusimamia shughuli za Mikutano mitatu ya Bunge ambapo maswali 1,054 ya kawaida, nyongeza na ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu yaliulizwa. Miswada kumi (10) ya Sheria ilijadiliwa na kupitishwa na Bunge. Aidha, Bunge liliratibu na kusimamia shughuli za Mikutano ya Kamati za Kudumu za Bunge, kutoa huduma za Hansard, utafiti, utawala na kutoa mafunzo kwa Waheshimiwa Wabunge na Watumishi wa Ofisi ya Bunge. Ofisi ya Bunge pia ilisimamia kazi ya ukarabati wa jengo la Bunge pamoja na kuratibu ujenzi wa Ofisi za Waheshimiwa Wabunge. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kuliwezesha Bunge kutekeleza majukumu yake ya Kikatiba kama kawaida.

MAHAKAMA


67.      Mheshimiwa Spika, utendaji wa mhimili wa Mahakama nchini umezidi kuimarika. Katika mwaka 2016/2017, Mahakama imesikiliza na kukamilisha mashauri 279,331 kati ya 335,962 katika ngazi zote za Mahakama sawa na asilimia 83.1 ya mashauri yote. Pamoja na kazi kubwa ya kusikiliza mashauri, Mahakama imesogeza huduma zake karibu na wananchi kwa kukamilisha ukarabati na ujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu katika mikoa ya Tanga na Dar es Salaam. Pia, kazi za ukarabati wa Mahakama Kuu katika Mkoa wa Mbeya inaendelea na ujenzi wa Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Mwanzo Kibaha Mkoa wa Pwani umekamilika na kuzinduliwa.

Mheshimiwa Spika, ni matarajio yangu kwamba, katika mwaka 2017/2018, Mahakama itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi ili kupunguza mlundikano wa mashauri yaliyopo mahakamani. Hata hivyo, ili Mahakama ifanye kazi zake vizuri, shughuli za upelelezi wa kesi na uendeshaji wa mashtaka zinatakiwa pia kuimarishwa zaidi. Serikali itafanya kila liwezekanalo kuimarisha taasisi zote zinazohusika katika mlolongo wa utoaji haki ili wananchi wapate haki zao kwa wakati.

MASUALA MTAMBUKA


Mfumo wa Ufuatiliaji wa Shughuli za Serikali


68.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali iliahidi kuanzisha Mfumo wa Wazi wa Kielektroniki wa kufuatilia uwajibikaji na utendaji Serikalini. Mfumo huo utasaidia kuongeza ufanisi katika uratibu wa shughuli za Serikali kwa kuwawezesha Viongozi kutoa maelekezo na kufuatilia utekelezaji wake. Aidha, Mfumo huo utasaidia ufuatiliaji wa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Ahadi na Maagizo ya Mheshimiwa Rais na Mpango wa Taifa wa Maendeleo. Napenda kulialifu Bunge lako Tukufu kwamba, Mfumo huo umekamilika, kuzinduliwa rasmi na mafunzo kutolewa kwa wataalamu katika Wizara zote. Mfumo huo pamoja na mambo mengine utaongeza kasi ya utoaji taarifa za utekelezaji wa kazi za Serikali kwa wakati na pia kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wa Umma. Wizara na Taasisi zote za Serikali zinatakiwa kuutumia Mfumo huo kikamilifu ili kurahisisha ufuatiliaji wa utekelezaji wa kazi za Serikali na kusaidia viongozi kutatua vikwazo pale vinapojitokeza. 
    

Vita dhidi ya Rushwa


69.         Mheshimiwa Spika, Serikali inapambana na rushwa kwa nguvu zake zote na haina mzaha wala uvumilivu na vitendo vya rushwa. Hatua zilizochukuliwa kupambana na rushwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani Novemba, 2015 zimetambulika hata na Mashirika ya Kimataifa yanayojishughulisha na tafiti kuhusu masuala ya rushwa Duniani. Taarifa ya Shirika la Transparency International kwenye utafiti wake kuhusu mtazamo wa rushwa mwaka 2016 imeonesha kuwa viwango vya rushwa vinaendelea kupungua hapa nchini.

70.  Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2016/2017, Serikali kupitia TAKUKURU imefanya uchunguzi wa majalada 306 ya tuhuma za rushwa na kupata kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini kuendelea na mashtaka kwa majalada 104. Katika kipindi hicho, TAKUKURU iliendesha kesi 674 zikiwemo kesi mpya 182, ambapo katika kesi 97 watuhumiwa walipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo au kulipa faini. Kesi 407 zinaendelea kusikilizwa mahakamani. Kutokana na operesheni zilizofanywa na TAKUKURU, kiasi cha Shilingi bilioni 9.75 ziliokolewa. Katika Mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea na mapambano yake dhidi ya rushwa hususan katika eneo la ukusanyaji mapato ya Serikali, kudhibiti matumizi ya fedha za umma, malipo hewa, matumizi mabaya ya fedha za ushirika na kuimarisha ufuatiliaji na ukaguzi wa miradi ya maendeleo.

Vita dhidi ya UKIMWI


71.    Mheshimiwa Spika, mapambano dhidi ya UKIMWI yamekuwa yakitegemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa rasilimali fedha kutoka kwa Wadau wa Maendeleo. Ninapenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa, Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI ulioanzishwa na Serikali miaka miwili iliyopita, ulizinduliwa tarehe 01 Desemba, 2016 ambapo kupitia harambee iliyofanyika kwa ajili ya kuchangia Mfuko huo, shilingi milioni 347 zilipatikana kama ahadi. Vilevile, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 5.6 kwa ajili ya Mfuko wa UKIMWI.

72.    Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutoa huduma kwa Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) ambapo hadi Desemba, 2016 WAVIU 839,574 sawa na asilimia 63 ya WAVIU wote, walikuwa wamepatiwa dawa. Juhudi zinaendelea kufanyika ili kuwahamasisha WAVIU kujitokeza na kuingia kwenye Mpango wa Tiba ya Kufubaza Athari za UKIMWI. Aidha, Serikali imekamilisha uandaaji wa miongozo minne ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI ikijumuisha Mpango Kazi wa Kinga, Mkakati wa Kondomu, Mkakati wa Uwekezaji na Mpango kazi wa jinsia.

73.    Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka 2017/2018, itaimarisha uratibu wa afua za UKIMWI kwa wadau wote wa sekta ya umma na binafsi na kupitia mifumo ya uratibu iliyoanzishwa. Serikali kwa kushirikiana na wadau pia itazijengea uwezo Kamati zilizo katika ngazi ya jamii hususan vijiji na kata ili kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa ya kupunguza na kumaliza UKIMWI ifikapo mwaka 2030 kwa kutumia mfumo ulio katika jamii. Vilevile, Serikali itakamilisha utafiti wa nne wa kubainisha viwango vya maambukizo ya UKIMWI nchini na kuboresha ushiriki wa sekta binafsi ili kuleta ufanisi katika kuchangia mwitikio wa Taifa dhidi ya UKIMWI.

Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu


74.    Mheshimiwa Spika, katika 2016/2017, Serikali imeendelea kutoa huduma pamoja na kuongeza upatikanaji wa haki na fursa kwa watu wenye ulemavu. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali imewaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kuwa Kamati za Watu wenye Ulemavu zinaanzishwa katika ngazi za Mikoa, Wilaya, Mitaa na Vijiji. Aidha, Serikali imeanzisha kampeni za kupinga unyanyapaa na vitendo vya kikatili dhidi ya watu wenye ualbino katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Geita, Simiyu, Kagera, Tabora, Kigoma, Mara, Mbeya, Katavi na Rukwa na kampeni hiyo itaendelea nchi nzima.

75.           Mheshimiwa Spika, Serikali pia inahakikisha kwamba watumiaji wa lugha ya alama wanapata haki ya kupata habari na vituo vyote vya televisheni vimeelekezwa kutumia wakalimani wa lugha ya alama. Napenda kuvikumbusha Vituo vya Televisheni kuweka wakalimani wa lugha katika vituo vyao. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kutoa vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye ulemavu shuleni na vifaa vya kufundishia. 

Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya


76.  Mheshimiwa spika, dawa za kulevya zinaathiri maisha ya vijana wetu wengi na hivyo kuzima ndoto za maisha yao na kupunguza nguvu kazi ya Taifa. Ili kupambana na janga hilo, katika mwaka 2016/2017, Bunge lako Tukufu lilifanya marekebisho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015. Marekebisho hayo yameipa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nguvu ya kukamata, kupeleleza na kushitaki watuhumiwa wanaohusika na biashara ya dawa za kulevya. Aidha, hivi karibuni Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa Watendaji Wakuu watakaosimamia Mamlaka hiyo.

77.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Januari, 2017 watuhumiwa 11,303 walikamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya katika sehemu mbalimbali nchini. Kati ya watuhumiwa hao, watu 9,811, walikutwa na kesi za kujibu ambapo 9,174 wametiwa hatiani, 238 hawakukutwa na hatia na wengine 478 upelelezi wa kesi zao unaendelea. Pia alisema tangu Tume mpya iundwe Februari mwaka huu, jumla ya watuhumiwa 79 wametiwa mbaroni na uchunguzi wa kesi zao unaendelea. Ni imani yangu kuwa, Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya itaendeleza kwa kasi zaidi juhudi za kupambana na uingizaji, uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini. Watanzania wana imani kubwa na Mamlaka hii na ninaomba wote tuipe ushirikiano wakati wote kwani vita hii ni kubwa na ni ya Kitaifa! Aidha, nawasihi wazazi wenzangu, tuwe karibu na vijana wetu na kufuatilia nyendo zao ili wasiingie kwenye mtego huu wa dawa za kulevya.  

Uratibu wa Maafa


78.           Mheshimiwa Spika, Serikali wakati wote inahakikisha kuwa nchi ipo katika hali ya utayari wa kukabiliana na maafa na pia kutoa misaada ya kibinadamu ikiwemo huduma za matibabu, ushauri wa kisaikolojia, na vifaa  pale maafa yanapotokea. Serikali imejenga vituo vipya 20 vya upimaji wa hali ya hewa  katika Halmashauri 11 za Tarime, Nyamagana, Muleba, Longido, Geita, Maswa, Kigoma, Sikonge, Kongwa, Serengeti, na Kahama. Kuwepo kwa vituo hivyo kutaongeza ufanisi katika upatikanaji wa taarifa za tahadhari hasa kwa majanga ya mafuriko na ukame.

79.    Mheshimiwa Spika, kufuatia tetemeko la ardhi lililotokea katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa mwezi Septemba 2016, Serikali kwa kushirikiana na wadau imechukua hatua za kushughulikia athari zilizotokana na tetemeko hilo. Huduma za afya na tiba na za kibinadamu za chakula na malazi zilitolewa kwa walioathirika. Vilevile, Serikali ilirejesha hali ya miundombinu iliyobomoka, yakiwemo majengo ya Serikali na Taasisi za Umma 686, Kituo cha wazee Kilima pamoja na kutoa maturubai 6,237, mahema 367, mabati 7,300 na mifuko ya saruji 1,825 kwa walioathirika. Serikali inaendelea na ujenzi wa Shule za Ihungo, Nyakato na Omumwani pamoja na ukarabati wa Kituo cha afya Kabyaile Ishozi. Ninapenda kuwashukuru sana wananchi wote na wadau waliotoa michango yao kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi.

HABARI NA MICHEZO


Habari


80.   Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu lilipitisha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016 ambayo ni muhimu katika kuimarisha usimamizi na uwajibikaji katika Sekta ya Habari nchini. Kanuni za Sheria hiyo zimeandaliwa na tayari zimeanza kutumika. Natoa wito kwa wadau wa sekta ya habari kuzingatia sheria na kanuni hizo ili kuimarisha weledi katika tasnia ya habari. Aidha, nashauri wadau wa habari kujikita zaidi katika kuandika na kutangaza habari za masuala ya maendeleo na uchumi ili kuwasaidia wananchi kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda na kuboresha huduma za kijamii.

Maendeleo ya Michezo


81.   Mheshimiwa Spika, tumeanza kuona dalili nzuri za kuimarika kwa shughuli za michezo hapa nchini. Mathalan, timu ya Mpira wa Miguu ya Serengeti Boys imefuzu kushiriki Mashindano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 yatakayofanyika Gabon, Mei 2017. Napenda nimshukuru sana Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan ambaye amewaaga na kuwakabidhi bendera ya Taifa tayari kwenda kushiriki vita hiyo. Nawaomba Watanzania wote tuungane pamoja kuiombea na kuiunga mkono timu yetu kwa michango ya hali na mali ili kuiwezesha kushiriki kikamilifu. Kwa upande wa riadha, Mtanzania mwenzetu Alphonce Simbu alipata medali katika mbio za marathon huko Mumbai nchini India. Aidha, mwezi Septemba 2016, Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Wanawake Tanzania (Twiga Stars) iliweka historia ya kuwa timu ya kwanza kutwaa taji la CECAFA. Ninatoa pongezi kwa wale wote walioliletea Taifa sifa kupitia michezo. Naziombea dua ili ziweze kushiriki michuano ya kimataifa.

82.      Mheshimiwa Spika, michezo ni sekta muhimu katika kuongeza ajira, kuimarisha afya, kukuza uchumi, kuimarisha umoja wa Kitaifa na kuitangaza nchi Kimataifa. Nchi nyingi zilizofanikiwa kimichezo ziliwekeza zaidi kujenga vipaji vya vijana katika michezo. Natoa wito kwa TFF ihakikishe kuwa vijana wa Timu ya Serengeti Boys wanawekewa Mpango Endelevu wa Kukuza Vipaji Vyao na kutunzwa vyema ili waweze kuiwakilisha nchi yetu katika mashindano mengine ya kimataifa. Aidha, vyama vingine vya michezo vitoe msukumo mkubwa kwenye kuwekeza zaidi kwa vijana wa shule za msingi na sekondari kwani hao ndio watakuwa wawakilishi wetu katika miaka ijayo. Na mwaka huu, michezo ya shule za msingi na sekondari itarejea na kufanyika mkoani Mwanza kama ilivyotangazwa mwaka jana. Nazisihi wizara husika za TAMISEMI na Wizara ya Elimu zianze maandalizi mapema na kuandaa mpango huo na kutoa taarifa timu hizo ziweze kujiandaa na kushindana ili tupate wachezaji imara wa kushiriki michuano hiyo.

ULINZI NA USALAMA

83.    Mheshimiwa Spika, hali ya ulinzi na usalama nchini ni shwari kutokana na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na vikosi vyetu vya ulinzi na usalama katika kulinda mipaka ya nchi yetu. Serikali imeendelea kuimarisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kulipatia zana na vifaa vya kivita na kukamilisha mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba 6,064 za makazi ya askari ulioanza mwaka 2013/2014. Kwa upande mwingine, Serikali kupitia Jeshi la Magereza inakamilisha ujenzi wa nyumba zilizojengwa kwa njia ya ubunifu katika baadhi ya Magereza ikiwemo ujenzi unaoendelea katika Gereza la Ukonga wa ghorofa 12 zenye uwezo wa kuishi askari na familia 320.

84.     Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha usalama wa raia na mali zao kwa  kufanya operesheni za kuzuia uhalifu nchini, kufanya upelelezi wa kesi kwa kasi ili kupunguza mlundikano wa kesi zilizopo mahakamani,  na kusimamia sheria za barabarani ili kupunguza ajali zinazoleta madhara kwa wananchi. Aidha, Serikali itaendelea kutoa mafunzo kwa askari na maafisa wa jeshi ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, kupambana na vitendo vya rushwa na kupambana na biashara ya dawa za kulevya. 

MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA


85.           Mheshimiwa Spika, kudumisha uhusiano mzuri na mataifa mengine duniani pamoja na mashirika ya kimataifa ni moja kati ya Misingi ya Sera yetu ya Mambo ya Nje. Tumeendelea kuimarisha ujirani mwema baina yetu na nchi jirani, nchi marafiki pamoja na mashirika ya kikanda na kimataifa, jitihada ambazo zimetuwezesha kuvutia mitaji mikubwa ya uwekezaji, utalii pamoja na kupanua fursa za kibiashara. Katika mwaka 2016/2017, Serikali imefungua Balozi mpya sita (6) katika nchi za Algeria, Israel, Korea Kusini, Sudan, Qatar na Uturuki. Balozi hizo zina kazi kubwa ya kuendeleza juhudi za kuitangaza Tanzania kama nchi yenye vivutio vingi vya utalii na rasilimali zinazoweza kutumika kuvuta uwekezaji kutoka mataifa hayo ikizingatiwa utulivu na amani iliyopo. Serikali itaendelea kulinda na kutetea maslahi ya Tanzania nje ya nchi na kuweka mikakati ya kunufaika na nafasi ya nchi yetu kihistoria.  Hivyo, ninatoa wito kwa mabalozi wetu wote waendelee kuitangaza nchi yetu kama eneo mwafaka lenye fursa nyingi za utalii, uwekezaji na biashara.

HITIMISHO


86.    Mheshimiwa Spika, ili kujenga uchumi wa viwanda tunahitaji nidhamu ya kazi, ubunifu, elimu na matumizi makubwa ya sayansi na teknolojia. Vilevile, tunahitaji kuimarisha sekta binafsi, miundombinu ya huduma za kiuchumi na jamii na kuondoa urasimu usio wa lazima. Nafarijika kwamba misingi tunayoendelea kujenga katika kutekeleza azma hiyo imeanza kuzaa matunda kama nilivyoeleza awali. Ili kufanya mafanikio hayo yawe endelevu, naomba nihitimishe hotuba yangu kwa kusisitiza mambo makuu yafuatayo:-

(i)         Mosi, ustawi wa nchi yetu na mafanikio ya mipango yetu ya maendeleo vinategemea amani na utulivu. Hivyo, kila mmoja wetu aweke nadhiri ya kuendelea kuilinda na kuienzi amani ya nchi yetu ili mipango yetu iweze kufanikiwa. Tunalo jukumu la kuhimiza amani ili tufanye kazi zetu kwenye mazingira ya amani na utulivu.

(ii)        Pili, jukumu la kujenga uchumi wa nchi yetu ni wajibu wa kila mwananchi. Njia pekee ya kuijenga nchi yetu ni kufanya kazi kwa bidii, kulipa kodi kwa hiari na kufichua wakwepa kodi wote na wala rushwa.

(iii)      Tatu, ujenzi wa uchumi wa viwanda unahitaji wananchi wenye afya njema na maarifa ya kufanya kazi na ubunifu.  Tujenge utamaduni wa kupima afya zetu na kufanya mazoezi ya viungo ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo yanapoteza nguvu kazi kubwa ya Taifa;

(iv)      Nne, rasilimali tulizonazo ipo siku zitaisha. Hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuzitumia kwa uangalifu ili zitufae sisi na vizazi vijavyo.  Tuepuke matumizi mabaya ya rasilimali zetu kama vile maji, madini na misitu ili zinufaishe kizazi hiki na vizazi vijavyo;

(v)        Tano, tuongeze nidhamu na uwajibikaji katika kila jambo la maendeleo tunalolifanya na kuzingatia matumizi ya muda. Tamaduni na mila zinazohamasisha uvivu na uzembe ni lazima tuzipige vita kwa nguvu zetu zote; na

(vi)      Mwisho, dawa za kulevya ni janga kubwa linaloitafuna kwa kasi nguvukazi ya nchi yetu. Tunahitaji ushiriki wa kila mmoja katika vita hii kwa kufichua mtandao wa wahusika wa dawa za kulevya. Ahadi yetu ni kuwapa ushirikiano na kuchukua hatua kali dhidi ya wote waliohusika.

MAKADIRIO YA  MAPATO NA MATUMIZI  YA  FEDHA  ZA OFISI  YA  WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2017/2018


87.           Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2017/2018, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake inaliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Sabini na Moja; Milioni Mia Sita Sitini na Nne, na Hamsini na Tano Elfu (Sh.171,664,055,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Sabini na Nne, Milioni Mia Sita Arobaini na Tatu, na Mia Tatu Thelathini na Tisa Elfu (Sh.74,643,339,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Tisini na Saba, Milioni Ishirini, na Mia Saba na Kumi na Sita Elfu (Sh.97,020,716,000)  ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.

Vilevile, ninaliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Ishirini na Moja, Milioni Mia sita Hamsini na Mbili na Mia Mbili Sitini na Mbili Elfu (Sh.121,652,262,000) kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Mia Moja Kumi na Nne, Milioni Mia Nne Hamsini na Mbili, na Mia Mbili Sitini na Mbili Elfu (Sh.114,452,262,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Saba na Milioni Mia Mbili (Sh.7,200,000,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.

88.           Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.