WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaomba viongozi na wananchi wa Tanzania Bara na Visiwani kushirikiana kwa pamoja katika kuimarisha na kuulinda Muungano ulioachwa na waasisi wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Aprili 7, 2017) mara baada ya kushiriki hitma na kuzuru kaburi la Sheikh Karume lililoko Afisi Kuu za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui mjini Unguja wakati wa maadhimisho ya kifo cha Rais wa kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Sheikh Abeid Karume sambamba na siku ya Mashujaa Zanzibar
Amesema ni muhimu kwa wananchi kutenga muda wao na kuwaombea viongozi wetu waliotangulia mbele ya haki, lengo likiwa ni kukumbuka na kuenzi mchango mkubwa waliotoa katika kujenga msingi wa maendeleo ya Taifa.
Waziri Mkuu amesema Watanzania wote Bara na Visiwani ni wamoja kiasili, hivyo wanapaswa kushirikiana katika kudumisha misingi iliyoachwa na waasisi wa Taifa ili kuweza kujiletea maendeleo
Pia amewaomba Watanzania wote kuhakikisha wanashirikiana kwa pamoja kuulinda na kuudumisha Muungano ulioachwa na waasisi wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Karume.
“Tuhakikishe Muungano huu tulioachiwa na wasisi wa Taifa letu unadumu ili tuendelee kuwa wamoja na kuzungumza lugha moja ya kuboresha maendeleo na kulinda amani na utulivu wa nchi yetu,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu amesema katika kutambua umuhimu wa viongozi hao Serikali imetenga siku maalumu kwa ajili ya maadhidhimisho ya vifo vya viongozi hao na kutoa fursa kwa wananchi kila mtu kwa imani yake kuwaombea dua na kutafakari namna walivyojitoa kwa taifa letu.
Maadhimisho ya kifo cha Sheikh Karumbe ni Aprili 7 ya kila mwaka na Hayati Mwalimu Nyerere ni Oktoba 14 ya kila mwaka.
Maadhimisho hayo ya kifo cha Sheikh Karume yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.
Wengine ni Rais Mstaafu wa awamu ya Pili, Sheikh Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dkt. Amani Abeid Karume, Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Mohamed Gharib Bilal, wazee wa CCM pamoja na wananchi.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.