Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuhitimisha Hoja yake ya Makadirio ya Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka 2017/2018, bungeni mjini Dodoma Aprili 12, 2017. |
1.0. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
- Naomba nianze
kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kutupa Afya njema hadi
leo ninapohitimisha Majadiliano ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi
zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
- Mheshimiwa
Spika, ninapohitimisha hoja yangu, katika siku ambayo Taifa letu
liliondokewa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Hayati Edward Moringe Sokoine,
aliyezaliwa tarehe 1 Agosti 1938 na kufariki kwa ajli ya gari siku kama ya
leo mwaka 1984. Ninalazimika kuwakumbusha Watanzania wote kumuenzi
mpambanaji huyo wa haki za wanyonge kwa kuunga mkono jitihada za Serikali
ya Awamu ya Tano za kupambana na rushwa na ubadhilifu wa mali za umma.
Namuomba Mwenyezi Mungu aendelee kumpumzisha kwa amani Edward Moringe
Sokoine. Amen.
- Natoa shukrani
zangu za dhati kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria; Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Bajeti kwa michango yao mizuri kwenye Hoja yangu.
- Kipekee
ninakushukuru sana wewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wote wa
Bunge kwa kusimamia kwa umahiri mkubwa majadiliano ya Hotuba ya Ofisi ya
Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge.
- Ninawashukuru
pia Waheshimiwa Wabunge kwa pongezi
zenu kwa Serikali na kwa michango yenye dhamira njema ya kuboresha
mipango na kazi zilizokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha
2017/2018. Mjadala huu umedhihirisha namna ambavyo Bunge linaendelea
kuimarika na kutekeleza wajibu wake wa Kikatiba kuishauri na kuisimamia
Serikali kikamilifu.
- Ninawashukuru
Makatibu Wakuu wote, Makamishna na watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu
pamoja na Wizara nyingine walioshiriki kuandaa taarifa hii.
2.0. WACHANGIAJI
Mheshimiwa Spika,
- Mjadala huu, ulichangiwa
na Waheshimiwa Wabunge 148, ambapo Waheshimiwa Wabunge 99 walichangia kwa kuzungumza moja
kwa moja hapa Bungeni na Waheshimiwa Wabunge 49 wamechangia kwa njia ya maandishi.
- Ninawashukuru
sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia Hoja yangu. Hata hivyo,
kutokana na muda naomba uridhie nisiwataje na majina yao yaingizwe katika Hansard.
- Niko mbele yenu
kuomba ridhaa yenu ili tupitishe bajeti hii tuweze kufanya kazi katika
maeneo mbalimbali nchini.
- Serikali
imejibu hoja hizo kupitia Mawaziri na Naibu Mawaziri. Hoja zilizosalia
zitajibiwa kwa maandishi. Aidha, baadhi ya hoja zitajibiwa na Mawaziri wa sekta
husika watakapowasilisha bajeti zao.
3.0. UTENDAJI WA SERIKALI KWA UJUMLA
Mheshimiwa Spika, kabla ya kuanza
kujibu Hoja za Waheshimiwa Wabunge, naomba uniruhusu nibainishe baadhi ya
mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa
Dkt. John P. Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nianze kwa
kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu
Hassan na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein kwa namna
wanavyoendelea kuiongoza nchi yetu kwa uzalendo uliotukuka na dhamira njema
isiyotiliwa shaka.
Mheshimiwa Spika, nina hakika Watanzania wote ni mashuhuda
wa kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Dkt.
John P. Magufuli katika kuiongoza Nchi yetu kwa weledi mkubwa na kwa mipango iliyo imara
ili kuboresha maisha ya Watanzania. Katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi
wake tumeshuhudia kuanza kwa miradi mikubwa na yenye tija kwa nchi yetu.
A: HUDUMA ZA KIJAMII
Elimu bila malipo
Mheshimiwa Spika, chini ya Serikali ya Awamu ya Tano ambapo
watoto wote wa Tanzania wanapata elimu ya Msingi na Sekondari bila malipo. Kila
mwezi Serikali inapeleka shilingi bilioni 18.77
kwenye shule zote za Serikali nchini Tanzania. Aidha, ni chini ya Serikali hii,
kiasi cha shilingi bilioni 3.3
zinatolewa kila mwezi kwa Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule kama motisha kwa
viongozi hao na kufanya kila mwezi kutuma shilingi bilioni 22.7. Tunajua zipo
changamoto zilizojitokeza, hasa uandikishaji mkubwa uliosababisha uhaba wa
madawati. Kipekee, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kujitolea kusimamia
suala hili kwa dhati.
Mheshimiwa Spika, huu ni utekelezaji wa Ilani ya CCM
wenye lengo la kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata urithi ulio bora,
ambao ni elimu.
Maboresho kwenye
Sekta ya Afya
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inatoa
kipaumbele kikubwa kwenye sekta ya afya. Tunatambua kwamba jamii yenye afya
njema ndiyo inayoweza kuzalisha kwa tija. Kutokana na ukweli huo, Serikali
imeendelea kuboresha huduma za afya kwa kuongeza bajeti ya kununua vifaa tiba
na dawa kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/2016 hadi shilingi bilioni 251 mwaka 2016/2017. Hadi leo, tumenunua ambulance 67, tumeanza kuzigawa kwenye
Kanda ya Ziwa. Pia tumeagiza kila Halmashauri hapa nchini, zitenge fedha kwa
ajili ya ujenzi wa nyumba moja ya mganga, nyumba ya muuguzi na maabara ya damu.
Aidha, Serikali
imebuni utaratibu wa kununua dawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa
wazalishaji badala ya kununua kutoka kwa wasambazaji. Pia, Serikali imeanzisha
utaratibu wa kujenga maduka ya madawa ya MSD kwa lengo la kuwezesha upatikanaji
wa dawa na vifaa tiba kwa bei nafuu kwa wananchi. Tayari maduka manane (8)
yamejengwa na mengine yanaendelea kujengwa kote nchini.
Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kuboresha huduma za afya
nchini, Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
amefanya uamuzi wa kusambaza magodoro 25, mashuka 50 na vitanda 25 vya hospitali katika Halmashauri
zote 184 nchini. Kati ya vitanda hivyo, 5 ni kwa ajili ya wajawazito. Pia
Serikali imetoa seti tano za vifaa tiba katika kila Halmashauri. Serikali
itaendelea kuboresha huduma za afya nchini, ikiwemo kusambaza watumishi katika
sekta ya afya.
B: SEKTA ZA UZALISHAJI
Ujenzi wa Reli ya Kati
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na jitihada za
kuimarisha reli ya kati kwa lengo la kurahisisha usafiri na usafirishaji wa
mizigo ndani na nje ya nchi. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali ilitenga shilingi trilioni moja kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa reli hiyo.
Nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, leo hii tarehe 12 Aprili, 2017
Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameweka
jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge. Ujenzi wa reli ya kati
ambayo ni mradi wa kipaumbele katika Dira ya Taifa ya Maendeleo, kuchochea
ukuaji wa uchumi na ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini.
Ujenzi wa Viwanda
Mheshimiwa Spika, Serikali pia inaendelea kuhamasisha ujenzi
wa viwanda na kuvutia uwekezaji nchini. Ndani ya mwaka mmoja jumla ya viwanda 2,169
vimesajiliwa, ikiwa ni pamoja na viwanda vya mbolea, saruji, chuma na
usindikaji wa mazao. Uhamasishaji wa ujenzi wa viwanda nchini ni dhahiri na
tayari tumeanza kuona matokeo. Kwa mfano, Mkoa wa Pwani pekee una viwanda vikubwa 83 na vingine vidogo vidogo zaidi ya 200. Huu ndio mwelekeo wa
Serikali ya Awamu ya Tano.
Maboresho kwenye
Sekta ya Usafiri wa Anga
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea na
jitihada za kulifufua Shirika la Ndege la Tanzania kwa kununua ndege mpya sita,
ambazo zinawasili kwa awamu mbalimbali. Serikali imekamilisha upanuzi wa uwanja
wa ndege wa Dodoma pamoja na kuendelea kujenga jengo la tatu la abiria
(Terminal III) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, upanuzi
wa uwanja wa ndege wa Mwanza na ukarabati wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa
Kilimanjaro na Uwanja wa Songwe – Mbeya.
Vilevile, Serikali
inaendelea na ujenzi wa uwanja wa ndege
wa Mkoa wa Geita na kukamilisha maandalizi kwa ajili ya upanuzi na
ujenzi wa viwanja vya ndege vya Tabora, Kigoma, Sumbawanga, Lindi na Shinyanga.
Serikali imeanza maandalizi kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa viwanja vya
ndege vya Musoma, Mtwara, Iringa na Songea.
Jitihada hizi ni kudhihirisha
dhamira ya dhati ya kuboresha usafiri wa anga ili kurahisisha usafiri kwa
wananchi pamoja na kuchochea utalii nchini.
Miradi ya Barabara
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kukarabati na
kuboresha barabara zinazounganisha mikoa nchini. Aidha, Serikali inaendelea kuimarisha
barabara kote nchini ikiwa ni pamoja na kujenga barabara zitakazofungua fursa
za kiuchumi katika maeneo mbalimbali. Baadhi ya barabara hizo ambazo ziko
katika hatua mbalimbali za ujenzi ni Barabara ya Itoni – Mkiu – Ludewa – Manda
(km 211); Barabara ya Tabora –
Sikonge - Ipole- Koga – Mpanda (km 259); Barabara ya Mbeya – Makongorosi – Rungwa – Itigi – Mkiwa (km 528); Manyoni – Itigi – Tabora (km 259.7); Barabara ya Dodoma – Babati (km
261); Barabara ya Iringa – Dodoma (km
260); Barabara ya Masasi – Songea – Mbamba Bay (km 866.7); Barabara ya Makutano
– Nata – Mugumu – Loliondo – Mto wa Mbu (km 338); na Barabara ya Kigoma –
Kidahwe – Uvinza- Kaliua – Tabora (km 491);
Madeni ya
makandarasi, wazabuni, watumishi na watoa huduma:
Mheshimiwa Spika, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge,
wamejadili kuhusu madeni ya makandarasi, wazabuni, watumishi na watoa huduma
wanaoidai Serikali kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie Waheshimiwa
Wabunge kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuwalipa wakandarasi na wadeni wote
wa Serikali. Hata hivyo, kabla ya kufanya malipo hayo, Serikali inabidi
kujiridhisha kuhusu uhalali wa madeni hayo, na mara moja tunapokuwa
tumejiridhisha kuhusu uhalali wa madeni hayo tumekuwa tukilipa bila kusita.
Hadi kufikia mwezi Desemba, 2016 jumla ya shilingi
bilioni 2,934.2 zilikuwa zimehakikiwa, ambapo shilingi bilioni 555.2 zililipwa. Ninawaomba makandarasi, wazabuni,
watumishi na watoa huduma wote wanaoidai Serikali, watuwie radhi na watuvumilie
wakati tunapojiridhisha kuhusu madeni yao. Serikali isingependa mdeni wake
apunjwe lakini pia ingependa Serikali ilipe madeni halali.
Napenda kuliarifu
Bunge lako tukufu kuwa Serikali imeongeza shilingi bilioni 21 kwa shughuli za
Bunge ili liweze kufika tarehe 30 Juni, 2017.
Mheshimiwa Spika, niliona ni vyema nianze mjadala huu
kwa kubainisha masuala muhimu yaliyofanywa na Serikali ili kuweka kumbukumbu
vizuri kutokana na baadhi yetu kuchangia kana kwamba hakuna jambo lolote
lililofanywa na Serikali tangu iingie madarakani.
4.0. MAJIBU YA HOJA
Mheshimiwa Spika,
·
Kwa
mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, Kanuni ya 99 (13) ya Kanuni za Kudumu za
Bunge, Toleo la Januari 2016, naomba nitumie nafasi hii kujibu na kufafanua
baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge kama ifuatavyo:
1. HOJA
Serikali itoe maagizo kwa Wakurugenzi wote wa
Halmashauri kutengeneza ajira angalau 20,000 kila mwaka katika miradi
mbalimbali inayotekelezwa katika Halmashauri zao, na taarifa ya utekelezaji wa
agizo hilo iwe inatolewa kila mwaka kwenye Bunge la Bajeti.
MTOA HOJA: Mheshimiwa Freeman
Aikaeli Mbowe (Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni); Mheshimiwa Juma
Hamidu Aweso (Pangani)
JIBU:
Mheshimiwa Spika,
Napenda, kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa Ilani ya
Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 Ibara ya 59 inazielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa zote nchini
kuzingatia viashiria vya ukuzaji ajira katika mipango ya maendeleo ya ngazi
husika pamoja na kutoa taarifa za mwenendo wa ajira kila robo mwaka.
Aidha, maelekezo haya, yanazingatiwa katika
Mwongozo wa kuandaa Bajeti ya Serikali unaotelewa na HAZINA kila mwaka
unaozitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara na Taasisi zote kubainisha
fursa za ajira zinazotarajiwa kupatikana kila mwaka kutokana na utekelezaji wa
miradi ya maendeleo. Vilevile Mwongozo huo unazitaka Taasisi hizo kutoa taarifa
za ajira zinazozalishwa kutokana na utekelezaji wa Miradi hiyo kila robo mwaka.
Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Wizara na Taasisi zote ziendelee kuzingatia
maelekezo haya.
2. HOJA: Kuhusu hali ya upatikanaji
wa chakula nchini.
MTOA HOJA:
Mheshimiwa Kunti Yusuph Kajala (Viti Maalum); Mheshimiwa Zuberi Zitto
Kabwe (Kigoma Mjini); Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete (Chalinze)
JIBU
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye hotuba yangu ya
Bajeti ya 2017/18 ukurasa wa 21, katika msimu wa kilimo 2016/17 hali ya
upatikanaji wa mvua katika Mikoa inayopata mvua za vuli haikuwa ya kuridhisha
na hivyo kusababisha ukame na upungufu wa mavuno katika baadhi ya maeneo. Ili
kukabiliana na hali hiyo, Serikali inahamasisha sekta binafsi kununua mazao ya
chakula kutoka maeneo yenye ziada na kuyauza katika maeneo yenye uhaba hasa
kwenye wilaya 55 tulizozibaini.
Aidha, wafanyabiashara
waliohifadhi nafaka katika maghala, wazisambaze katika masoko ya ndani. Katika
kuunga mkono juhudi hizo, Serikali imesambaza tani 1,969 za mbegu bora za mazao
yanayostahimili ukame kwenye Halmashauri mbalimbali. Natoa wito kwa wakulima
kuendelea kutumia vizuri mvua zinazonyesha katika msimu huu wa masika kwa
kupanda mazao yanayokomaa kwa muda mfupi na kutumia mbegu bora za mazao ya
kilimo zinazostahimili ukame.
3. HOJA:
Kutokana nchi yetu kuwa na mipaka mingi yenye
vipenyo vingi pamoja na ukanda mrefu wa bahari ambavyo hufanya udhibiti wa
uingizaji wa dawa za kulevya kuwa mgumu, Serikali imeshauriwa kupitia Kamati za
Ulinzi na Usalama za Mikoa kutoa elimu kwa jamii zinazoishi mipakani ili
zishirikiane na vyombo vya dola hatua ambayo itasaidia udhibiti wa uingizwaji
wa dawa hizo hatari nchini.
MTOA HOJA:
Mheshimiwa Dkt. Haji Mponda (Kamati ya Kudumu ya Bunge, Masuala ya
UKIMWI)
JIBU
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa
za Kulevya imeshaanza kutoa elimu kwa Kamati za Ulinzi na Usalama katika maeneo
ya mipaka ya Tunduma, Kasumulo, Namanga, Horohoro na Mtukula ili kuweza kutoa
elimu juu ya athari za dawa za kulevya kwa jamii inayoishi mipakani. Aidha,
elimu hii itatolewa kwa wananchi kadri hali itakavyo ruhusu ili wananchi wote
kwa pamoja washiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya badala ya
kuviachia vyombo vya dola pekee.
4.
HOJA: Mapambano dhidi ya
dawa za kulevya, kulinda watoa taarifa na pendekezo la kutaifisha mashamba ya
bangi.
MTOA HOJA:
Mheshimiwa Dkt. Haji Mponda (Kamati ya Kudumu ya Bunge, Masuala ya
UKIMWI); Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq (Viti Maalum)
JIBU
Mheshimiwa Spika, tatizo la dawa za kulevya ni janga kubwa la
kitaifa linaloathiri ustawi wa Nchi yetu. Serikali imedhamiria kwa dhati
kupambana na mtandao wa dawa za kulevya nchini. Mafanikio katika mapambano ya
dawa za kulevya yanahitaji ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wananchi. Hivyo,
napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, watoa taarifa za wahusika wa
dawa za kulevya wanaendelea kulindwa na watalindwa kwa mujibu wa Sheria ya
Kulinda Watoa Taarifa na Mashahidi ya Mwaka 2015 (Whistleblower and Witness Protection Act of 2015).
Mheshimiwa Spika, Serikali inalipokea pendekezo
la kutaifisha mashamba ya bangi na itaendelea kutafakari utekelezaji wake. Pale
tutakapojiridhisha kuwa adhabu hii itatoa fundisho kwa wananchi wanaojihusisha
na kilimo cha bangi, Serikali haitasita kuleta Bungeni muswada wa mabadiliko ya
sheria ili kuongeza suala hilo.
5. HOJA: Kuongeza vituo vya tiba ya Methadone na Sober Houses za Serikali angalau moja kila Mkoa.
MTOA HOJA:
Mheshimiwa Dkt. Haji Mponda (Kamati ya Kudumu ya Bunge, Masuala ya
UKIMWI); Mheshimiwa Abdallah Ali Mtolela (Temeke)
JIBU
Mheshimiwa Spika, uanzishwaji wa
vituo vya tiba kwa kutumia Methadone
unategemea ukubwa wa tatizo la matumizi ya dawa za kulevya na uwepo wa
miundombinu ya msingi katika Mkoa husika. Hadi sasa kuna vituo vya Methadone katika hospitali za Muhimbili,
Mwananyamala na Temeke - Dar es Salaam. Vilevile, Serikali inakusudia kufungua
vituo kama hivyo katika Mikoa ya Arusha, Dodoma, Kilimanjaro, Mbeya, Morogoro,
Mwanza, Pwani naTanga.
Kwa kuwa matibabu ya
Methadone yanawasaidia watumiaji wa
dawa za kulevya aina ya Heroin pekee,
Serikali inatarajia kuanzisha nyumba za upataji nafuu (Sober Houses) kila Mkoa. Huduma hii itakuwa ni kwa ajili ya
kuwasaidia waraibu (addicts) wengine
wa aina zote za dawa za kulevya, badala ya kuwaachia watu binafsi ambao mpaka
sasa wanaendesha nyumba 17 za upataji nafuu
nchini. Vilevile, Serikali imeandaa Mwongozo wenye lengo
la kusimamia na kuratibu Sober Houses
za watu binafsi.
6. HOJA: Serikali iongeze vituo
vya afya, vifaa tiba, wahudumu wa afya wenye weledi na kupunguza umbali wa
kupata huduma kwa Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU).
MTOA HOJA:
Mheshimiwa Dkt. Haji Mponda (Kamati ya Kudumu ya Bunge, Masuala ya
UKIMWI);
JIBU
Mheshimiwa Spika, Ilani ya Uchaguzi ya CCM na Sera ya
Maendeleo ya Afya ya Msingi vinaelekeza Serikali kuboresha huduma za afya ya
msingi kwa kujenga zahanati kila kijiji, kituo cha afya kila kata na Hospitali
kila Wilaya. Aidha, Serikali ina mkakati wa kuongeza idadi ya wataalam wa afya
nchini kote. Kupitia mikakati hii, wananchi wakiwemo WAVIU watapata huduma
karibu na maeneo wanayoishi.
7. HOJA: Serikali itoe elimu ya
kujikinga na VVU kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo elimu kwa njia ya Sinema
na kuanzisha vilabu vya mapambano dhidi ya VVU katika shule zote kuanzia msingi
pamoja na kuandaa mitaala ya elimu ya UKIMWI katika ngazi zote za elimu (elimu
ya msingi hadi vyuo vikuu).
MTOA HOJA:
Mheshimiwa Dkt. Haji Mponda (Kamati ya Kudumu ya Bunge, Masuala ya
UKIMWI);
JIBU:
Mheshimiwa
Spika,
Nia ya Serikali ni kuona elimu ya UKIMWI inawafikia
wote wanaostahili. Serikali ina magari ya Sinema katika mikoa ishirini ya
Tanzania Bara ambayo hutoa elimu ya UKIMWI kwa njia ya sinema. Tanzania
Visiwani nayo sasa inapatamagari ya sinema katika mikoa yake yote. Wizara ya
elimu imetoa mitaala ya kufundisha wanafunzi kuhusiana na elimu ya UKIMWI
shuleni.
Serikali inatoa wito kwa Makatibu Tawala wa Mikoa
na Wakurugenzi wa Halmashauri kuyatumia ipasavyo magari hayo na kuhakikisha
Walimu wapya wanapitishwa vyema katika mitaala hiyo pamoja na kuanzisha klabu
za kuhamasisha mapambano dhidi ya UKIMWI katika shule na vyuo vyote nchini.
8. HOJA: Serikali ibuni chanzo mahususi cha kutunisha Mfuko
wa UKIMWI (AIDS TRUST FUND) kama ilivyo kwa mifuko mingine kama vile REA na
maji, ili kufanikisha mapambano dhidi ya UKIMWI.
MTOA HOJA:
Mheshimiwa Dkt. Haji Mponda (Kamati ya Kudumu ya Bunge, Masuala ya
UKIMWI);
JIBU:
Mheshimiwa
Spika,
Ushauri uliotolewa umepokelewa na Serikali itaufanyia kazi.
9. HOJA: Kuweka utaratibu wa kufuatilia fedha zinazotolewa na
wafadhili kwenye Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) zinazojihusisha na
masuala ya UKIMWI.
MTOA HOJA:
Mheshimiwa Dkt. Haji Mponda (Kamati ya Kudumu ya Bunge, Masuala ya
UKIMWI);
JIBU
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa
kufuatilia fedha zinazotolewa kwenye NGOs upo na tumekuwa tukisisitiza ufuatwe.
Mathalan, nilipofanya ziara Mkoani Arusha hivi karibuni nilirudia wito wa
kuzifanyia kaguzi za mara kwa mara NGOs zinazofanya kazi nchini. Hivyo, ushauri
wa Kamati kuhusu hitaji la kufanya ukaguzi kwenye NGOs zinazoshughulikia UKIMWI
utaendelea kuzingatiwa.
Natoa wito kwa
Wakurugenzi wote wa Halmashauri waendelee kuhakikisha wadau wa UKIMWI
wanaofanya kazi kwenye maeneo yao wanakaguliwa kulingana na Sheria ya UKIMWI ya
mwaka 2008 na Sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2002. Nia yetu
ni kujua wanapata nini, kwa ajili ya huduma zipi ili wanufaika waweze
kujulishwa.
10.
HOJA: Serikali ijiridhishe
kuhusu masuala ya kitaalam na kufanya mapitio na maboresho ya Sheria stahiki
katika kutekeleza Mpango wa kuunganisha Mifuko ya Pensheni.
MTOA HOJA: Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama (Kamati ya
Bunge ya Katiba na Sheria)
JIBU
Mheshimiwa Spika, zoezi la
kuunganisha Mifuko ya Pensheni linafanyika kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu.
Katika kutekeleza jukumu hilo, Mifuko yote ya Pesheni imefanyiwa tathmini
(Actuarial Valuation), ambayo pamoja na mambo mengine, imebainisha kuwa
kuunganisha Mifuko ya Pensheni ndio njia bora ya kuimarisha Sekta ya Hifadhi ya
Jamii nchini.
Aidha, Serikali
imeandaa Andiko la mapendekezo ya kuunganisha Mifuko. Kazi hii imefanyika kwa
kushirikisha wadau muhimu katika Sekta husika. Serikali itaendelea kutoa
taarifa za mara kwa mara kwa hatua zinazofikiwa.
11.
HOJA: Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwekeza kwenye
uchumi wa viwanda.
MTOA HOJA:
Mheshimwia Zuberi Kuchauka (Liwale)
JIBU
Mheshimiwa
Spika,
uwekezaji ni kazi mojawapo ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Lengo la uwekezaji ni
kulinda thamani ya michango ya wanachama pamoja na kukuza uwezo wa Mifuko kulipa
mafao kwa wanachama wake pale wanapopatwa na majanga mbalimbali
yanayowasababishia kukosa kipato. Majanga hayo ni kama vile maradhi, uzee na
kifo. Kwa msingi huo, uwekezaji kwenye viwanda unaofanywa na Mifuko ya Hifadhi
ya Jamii sasa una manufaa mtambuka kwani pamoja na kulinda thamani ya fedha za
michango ya wanachama, uwekezaji huu unakuza mapato ya Serikali, unatoa fursa
za ajira na hivyo kusaidia kuongeza idadi ya wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii. Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba uwekezaji unaofanywa na Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii unazingatia Miongozo ya Uwekezaji ili mifuko hiyo isiweze
kupata hasara.
12.
HOJA: Uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura.
MTOA HOJA:
Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama (Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na
Sheria)
JIBU
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Taifa ya
Uchaguzi ina jukumu la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Katika Mwaka
wa Fedha 2017/2018 Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaweka kipaumbele katika
uboreshaji wa Daftari la Wapiga kura.
Aidha, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepewa jukumu la kutoa elimu ya mpiga
kura Nchi nzima na kusimamia na kuratibu Asasi, Taasisi au watu wanaotoa elimu
ya mpiga kura. Tume imeendelea kutoa elimu ya Mpiga Kura kwa njia mbalimbali
ikiwemo kutumia Redio, Televisheni, kukutana na wadau kupitia maonyesho
mbalimbali, pamoja na kushiriki mikutano katika ngazi za Mikoa na Halmashauri.
13.
HOJA: Mgogoro wa Uongozi
ndani ya CUF
MTOA HOJA: Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama (Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria) Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (Msemaji
wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni); Mheshimiwa Cecilia Danel Paresso (Viti
Maalum); Mheshimiwa Rashid Ali Abdallah (Tumbe); Mheshimiwa Khatibu Said Haji
(Konde); Mheshimiwa Juma Kombo Hamad (Wingwi); Mheshimiwa Masoud Abdallah Salum
(Mtambile)
JIBU
Mheshimiwa Spika, Hoja hii
imejadiliwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni na Waheshimiwa Wabunge mbalimbali.
Serikali
haifurahishwi na migogoro ndani ya vyama vya siasa, kwani inadumaza demokrasia
nchini na kusababisha mifarakano isiyokuwa na tija. Ofisi ya Msajili wa Vyama
vya Siasa kama mlezi wa vyama vya Siasa imekuwa ikishiriki kikamilifu katika
kuhakikisha migogoro ndani ya vyama vya siasa inatatuliwa kwa majadiliano.
Mheshimiwa Spika, Katika mgogoro uliopo ndani ya chama cha
CUF, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilitoa ushauri kulingana na taratibu
zilizopo. Hata hivyo, wakati usuluhishi ukiendelea baadhi ya wanachama wa CUF
ambao hawakuridhika na usuluhishi uliofanywa na Msajili walipeleka shauri
Mahakamani, ili kudai haki kwenye Mhimili wa Mahakama ikiwa ni pamoja na suala
la ruzuku ambalo Mahakama imetoa zuio la muda mpaka shauri la msingi lililoko
mahakama itakapolitolewa uamuzi. Kwa kuwa masuala hayo yapo Mahakamani, ni
vizuri tukaiacha Mahakama ifanye kazi yake. Hiyo ni rai yangu.
5.0.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Kama nilivyosema hapo awali, muda
usingeweza kutosha kujibu hoja zote zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wote
waliochangia hoja. Tumejifunza mambo mengi kutoka kwenye michango yenu, na tupo
tayari kuendelea kujifunza zaidi kutoka kwenu Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa
Spika, Nchi hii ni yetu sote, na kila mmoja wetu anao wajibu wa kulisukuma
mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu. Kila mchango wa Mheshimiwa Mbunge una
thamani kubwa sana kwetu, na ninawashukuru sana kwa ushauri, maangalizo na
mafunzo. Endeleeni kutoa ushauri kwa Serikali, hata kwa maandishi siyo lazima
kusubiri Bungeni, nasi tutaupokea na kuona namna bora ya kufanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, kila Mtanzania ikiwemo Waheshimiwa Wabunge,
anawajibika kuiacha Tanzania ikiwa ni nchi bora zaidi ya alivyoikuta. Ili
kuifikia azma hiyo, inabidi tuanze kuwa tayari kujinyima mambo mazuri
tuliyoyazoea, angalau kwa muda, ili kuimarisha misingi ya ujenzi wa Tanzania
yetu. Ninawasihi waheshimiwa Wabunge wenzangu muielewe dhamira ya Serikali na
mtuamini katika kusimamia rasilimali za nchi yetu kwa manufaa yetu na vizazi
vijavyo. Serikali imejipanga vizuri katika kulinda maslahi ya nchi hii na
wananchi wake, hivyo nawaomba muendelee kutuunga mkono kwa kupitisha Bajeti ya
Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.