Wednesday, April 12, 2017

UFAFANUZI NA MAJIBU YA HOJA ZA WABUNGE NA KUHITIMISHA HOJA YA BAJETI YA OFISI YA WAZIRI MKUU NA TAASISI ZAKE NA MFUKO WA BUNGE KWA MWAKA WA FEDHA 2017/2018

Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuhitimisha  Hoja yake ya Makadirio ya Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka 2017/2018, bungeni mjini Dodoma Aprili 12, 2017.
1.0.      UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika,
  • Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kutupa Afya njema hadi leo ninapohitimisha Majadiliano ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

  • Mheshimiwa Spika, ninapohitimisha hoja yangu, katika siku ambayo Taifa letu liliondokewa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Hayati Edward Moringe Sokoine, aliyezaliwa tarehe 1 Agosti 1938 na kufariki kwa ajli ya gari siku kama ya leo mwaka 1984. Ninalazimika kuwakumbusha Watanzania wote kumuenzi mpambanaji huyo wa haki za wanyonge kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kupambana na rushwa na ubadhilifu wa mali za umma. Namuomba Mwenyezi Mungu aendelee kumpumzisha kwa amani Edward Moringe Sokoine. Amen.

  • Natoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa michango yao mizuri kwenye Hoja yangu.

  • Kipekee ninakushukuru sana wewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kwa kusimamia kwa umahiri mkubwa majadiliano ya Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge.

  • Ninawashukuru pia Waheshimiwa Wabunge kwa pongezi  zenu kwa Serikali na kwa michango yenye dhamira njema ya kuboresha mipango na kazi zilizokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018. Mjadala huu umedhihirisha namna ambavyo Bunge linaendelea kuimarika na kutekeleza wajibu wake wa Kikatiba kuishauri na kuisimamia Serikali kikamilifu. 

  • Ninawashukuru Makatibu Wakuu wote, Makamishna na watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Wizara nyingine walioshiriki kuandaa taarifa hii.

2.0.      WACHANGIAJI

Mheshimiwa Spika,
  • Mjadala huu, ulichangiwa na Waheshimiwa Wabunge 148, ambapo Waheshimiwa Wabunge 99 walichangia kwa kuzungumza moja kwa moja hapa Bungeni na Waheshimiwa Wabunge 49 wamechangia kwa njia ya maandishi.

  • Ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia Hoja yangu. Hata hivyo, kutokana na muda naomba uridhie nisiwataje na majina yao yaingizwe katika Hansard.

  • Niko mbele yenu kuomba ridhaa yenu ili tupitishe bajeti hii tuweze kufanya kazi katika maeneo mbalimbali nchini.

  • Serikali imejibu hoja hizo kupitia Mawaziri na Naibu Mawaziri. Hoja zilizosalia zitajibiwa kwa maandishi. Aidha, baadhi ya hoja zitajibiwa na Mawaziri wa sekta husika watakapowasilisha bajeti zao.

3.0.      UTENDAJI WA SERIKALI KWA UJUMLA

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuanza kujibu Hoja za Waheshimiwa Wabunge, naomba uniruhusu nibainishe baadhi ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Dkt. John P. Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein kwa namna wanavyoendelea kuiongoza nchi yetu kwa uzalendo uliotukuka na dhamira njema isiyotiliwa shaka. 

Mheshimiwa Spika, nina hakika Watanzania wote ni mashuhuda wa kazi nzuri  inayofanywa na Mheshimiwa Dkt. John P. Magufuli katika kuiongoza Nchi yetu kwa     weledi mkubwa na kwa mipango iliyo imara ili kuboresha maisha ya Watanzania. Katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake tumeshuhudia kuanza kwa miradi mikubwa na yenye tija kwa nchi yetu.

A:      HUDUMA ZA KIJAMII

Elimu bila malipo
Mheshimiwa Spika, chini ya Serikali ya Awamu ya Tano ambapo watoto wote wa Tanzania wanapata elimu ya Msingi na Sekondari bila malipo. Kila mwezi Serikali inapeleka shilingi bilioni 18.77 kwenye shule zote za Serikali nchini Tanzania. Aidha, ni chini ya Serikali hii, kiasi cha shilingi bilioni 3.3 zinatolewa kila mwezi kwa Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule kama motisha kwa viongozi hao na kufanya kila mwezi kutuma shilingi bilioni 22.7.  Tunajua zipo changamoto zilizojitokeza, hasa uandikishaji mkubwa uliosababisha uhaba wa madawati. Kipekee, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kujitolea kusimamia suala hili kwa dhati.

Mheshimiwa Spika, huu ni utekelezaji wa Ilani ya CCM wenye lengo la kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata urithi ulio bora, ambao ni elimu.

Maboresho kwenye Sekta ya Afya
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inatoa kipaumbele kikubwa kwenye sekta ya afya. Tunatambua kwamba jamii yenye afya njema ndiyo inayoweza kuzalisha kwa tija. Kutokana na ukweli huo, Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya kwa kuongeza bajeti ya kununua vifaa tiba na dawa kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/2016 hadi shilingi bilioni 251 mwaka 2016/2017. Hadi leo, tumenunua ambulance 67, tumeanza kuzigawa kwenye Kanda ya Ziwa. Pia tumeagiza kila Halmashauri hapa nchini, zitenge fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba moja ya mganga, nyumba ya muuguzi na maabara ya damu.

Aidha, Serikali imebuni utaratibu wa kununua dawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji badala ya kununua kutoka kwa wasambazaji. Pia, Serikali imeanzisha utaratibu wa kujenga maduka ya madawa ya MSD kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa bei nafuu kwa wananchi. Tayari maduka manane (8) yamejengwa na mengine yanaendelea kujengwa kote nchini.

Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kuboresha huduma za afya nchini, Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya uamuzi wa kusambaza magodoro 25, mashuka 50  na vitanda 25 vya hospitali katika Halmashauri zote 184 nchini. Kati ya vitanda hivyo, 5 ni kwa ajili ya wajawazito. Pia Serikali imetoa seti tano za vifaa tiba katika kila Halmashauri. Serikali itaendelea kuboresha huduma za afya nchini, ikiwemo kusambaza watumishi katika sekta ya afya.

B:      SEKTA ZA UZALISHAJI

Ujenzi wa Reli ya Kati
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na jitihada za kuimarisha reli ya kati kwa lengo la kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali ilitenga shilingi trilioni moja kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa reli hiyo. Nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, leo hii tarehe 12 Aprili, 2017 Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge. Ujenzi wa reli ya kati ambayo ni mradi wa kipaumbele katika Dira ya Taifa ya Maendeleo, kuchochea ukuaji wa uchumi na ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini.

Ujenzi wa Viwanda
Mheshimiwa Spika, Serikali pia inaendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda na kuvutia uwekezaji nchini. Ndani ya mwaka mmoja jumla ya viwanda 2,169 vimesajiliwa, ikiwa ni pamoja na viwanda vya mbolea, saruji, chuma na usindikaji wa mazao. Uhamasishaji wa ujenzi wa viwanda nchini ni dhahiri na tayari tumeanza kuona matokeo. Kwa mfano, Mkoa wa Pwani pekee una viwanda vikubwa 83 na vingine vidogo vidogo zaidi ya 200. Huu ndio mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Maboresho kwenye Sekta ya Usafiri wa Anga
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea na jitihada za kulifufua Shirika la Ndege la Tanzania kwa kununua ndege mpya sita, ambazo zinawasili kwa awamu mbalimbali. Serikali imekamilisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dodoma pamoja na kuendelea kujenga jengo la tatu la abiria (Terminal III) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza na ukarabati wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro na Uwanja wa Songwe – Mbeya.

Vilevile, Serikali inaendelea na ujenzi wa uwanja wa ndege  wa Mkoa wa Geita na kukamilisha maandalizi kwa ajili ya upanuzi na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Tabora, Kigoma, Sumbawanga, Lindi na Shinyanga. Serikali imeanza maandalizi kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Musoma, Mtwara, Iringa na Songea.

Jitihada hizi ni kudhihirisha dhamira ya dhati ya kuboresha usafiri wa anga ili kurahisisha usafiri kwa wananchi pamoja na kuchochea utalii nchini.

Miradi ya Barabara
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kukarabati na kuboresha barabara zinazounganisha mikoa nchini.  Aidha, Serikali inaendelea kuimarisha barabara kote nchini ikiwa ni pamoja na kujenga barabara zitakazofungua fursa za kiuchumi katika maeneo mbalimbali. Baadhi ya barabara hizo ambazo ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi  ni Barabara ya Itoni – Mkiu – Ludewa – Manda (km 211); Barabara ya Tabora – Sikonge - Ipole- Koga – Mpanda (km 259); Barabara ya Mbeya – Makongorosi – Rungwa – Itigi – Mkiwa  (km 528); Manyoni – Itigi – Tabora (km 259.7); Barabara ya Dodoma – Babati  (km 261); Barabara ya Iringa – Dodoma (km 260); Barabara ya Masasi – Songea – Mbamba Bay (km 866.7); Barabara ya Makutano – Nata – Mugumu – Loliondo – Mto wa Mbu (km 338); na Barabara ya Kigoma – Kidahwe – Uvinza- Kaliua – Tabora (km 491);

Madeni ya makandarasi, wazabuni, watumishi na watoa huduma:
Mheshimiwa Spika, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge, wamejadili kuhusu madeni ya makandarasi, wazabuni, watumishi na watoa huduma wanaoidai Serikali kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuwalipa wakandarasi na wadeni wote wa Serikali. Hata hivyo, kabla ya kufanya malipo hayo, Serikali inabidi kujiridhisha kuhusu uhalali wa madeni hayo, na mara moja tunapokuwa tumejiridhisha kuhusu uhalali wa madeni hayo tumekuwa tukilipa bila kusita. Hadi kufikia mwezi Desemba, 2016 jumla ya shilingi bilioni 2,934.2 zilikuwa zimehakikiwa, ambapo shilingi bilioni 555.2 zililipwa. Ninawaomba makandarasi, wazabuni, watumishi na watoa huduma wote wanaoidai Serikali, watuwie radhi na watuvumilie wakati tunapojiridhisha kuhusu madeni yao. Serikali isingependa mdeni wake apunjwe lakini pia ingependa Serikali ilipe madeni halali.

Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa Serikali imeongeza shilingi bilioni 21 kwa shughuli za Bunge ili liweze kufika tarehe 30 Juni, 2017.

Mheshimiwa Spika, niliona ni vyema nianze mjadala huu kwa kubainisha masuala muhimu yaliyofanywa na Serikali ili kuweka kumbukumbu vizuri kutokana na baadhi yetu kuchangia kana kwamba hakuna jambo lolote lililofanywa na Serikali tangu iingie madarakani.

4.0.      MAJIBU YA HOJA

          Mheshimiwa Spika,
·         Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, Kanuni ya 99 (13) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari 2016, naomba nitumie nafasi hii kujibu na kufafanua baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge kama ifuatavyo:

1.   HOJA
Serikali itoe maagizo kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri kutengeneza ajira angalau 20,000 kila mwaka katika miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Halmashauri zao, na taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo iwe inatolewa kila mwaka kwenye Bunge la Bajeti.

MTOA HOJA:  Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni); Mheshimiwa Juma Hamidu Aweso (Pangani)

JIBU:
Mheshimiwa Spika,
Napenda, kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 Ibara ya 59 inazielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa zote nchini kuzingatia viashiria vya ukuzaji ajira katika mipango ya maendeleo ya ngazi husika pamoja na kutoa taarifa za mwenendo wa ajira kila robo mwaka.

Aidha, maelekezo haya, yanazingatiwa katika Mwongozo wa kuandaa Bajeti ya Serikali unaotelewa na HAZINA kila mwaka unaozitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara na Taasisi zote kubainisha fursa za ajira zinazotarajiwa kupatikana kila mwaka kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Vilevile Mwongozo huo unazitaka Taasisi hizo kutoa taarifa za ajira zinazozalishwa kutokana na utekelezaji wa Miradi hiyo kila robo mwaka. Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Wizara na Taasisi zote ziendelee kuzingatia maelekezo haya.

2.   HOJA:     Kuhusu hali ya upatikanaji wa chakula nchini.

MTOA HOJA:  Mheshimiwa Kunti Yusuph Kajala (Viti Maalum); Mheshimiwa Zuberi Zitto Kabwe (Kigoma Mjini); Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete (Chalinze)

JIBU
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye hotuba yangu ya Bajeti ya 2017/18 ukurasa wa 21, katika msimu wa kilimo 2016/17 hali ya upatikanaji wa mvua katika Mikoa inayopata mvua za vuli haikuwa ya kuridhisha na hivyo kusababisha ukame na upungufu wa mavuno katika baadhi ya maeneo. Ili kukabiliana na hali hiyo, Serikali inahamasisha sekta binafsi kununua mazao ya chakula kutoka maeneo yenye ziada na kuyauza katika maeneo yenye uhaba hasa kwenye wilaya 55 tulizozibaini.

Aidha, wafanyabiashara waliohifadhi nafaka katika maghala, wazisambaze katika masoko ya ndani. Katika kuunga mkono juhudi hizo, Serikali imesambaza tani 1,969 za mbegu bora za mazao yanayostahimili ukame kwenye Halmashauri mbalimbali. Natoa wito kwa wakulima kuendelea kutumia vizuri mvua zinazonyesha katika msimu huu wa masika kwa kupanda mazao yanayokomaa kwa muda mfupi na kutumia mbegu bora za mazao ya kilimo zinazostahimili ukame.

3.   HOJA:
Kutokana nchi yetu kuwa na mipaka mingi yenye vipenyo vingi pamoja na ukanda mrefu wa bahari ambavyo hufanya udhibiti wa uingizaji wa dawa za kulevya kuwa mgumu, Serikali imeshauriwa kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa kutoa elimu kwa jamii zinazoishi mipakani ili zishirikiane na vyombo vya dola hatua ambayo itasaidia udhibiti wa uingizwaji wa dawa hizo hatari nchini.

MTOA HOJA:  Mheshimiwa Dkt. Haji Mponda (Kamati ya Kudumu ya Bunge, Masuala ya UKIMWI)

JIBU
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imeshaanza kutoa elimu kwa Kamati za Ulinzi na Usalama katika maeneo ya mipaka ya Tunduma, Kasumulo, Namanga, Horohoro na Mtukula ili kuweza kutoa elimu juu ya athari za dawa za kulevya kwa jamii inayoishi mipakani. Aidha, elimu hii itatolewa kwa wananchi kadri hali itakavyo ruhusu ili wananchi wote kwa pamoja washiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya badala ya kuviachia vyombo vya dola pekee.

4.    HOJA: Mapambano dhidi ya dawa za kulevya, kulinda watoa taarifa na pendekezo la kutaifisha mashamba ya bangi.

MTOA HOJA:  Mheshimiwa Dkt. Haji Mponda (Kamati ya Kudumu ya Bunge, Masuala ya UKIMWI); Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq (Viti Maalum)

JIBU
Mheshimiwa Spika, tatizo la dawa za kulevya ni janga kubwa la kitaifa linaloathiri ustawi wa Nchi yetu. Serikali imedhamiria kwa dhati kupambana na mtandao wa dawa za kulevya nchini. Mafanikio katika mapambano ya dawa za kulevya yanahitaji ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wananchi. Hivyo, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, watoa taarifa za wahusika wa dawa za kulevya wanaendelea kulindwa na watalindwa kwa mujibu wa Sheria ya Kulinda Watoa Taarifa na Mashahidi ya Mwaka 2015 (Whistleblower and Witness Protection Act of 2015).

Mheshimiwa Spika, Serikali inalipokea pendekezo la kutaifisha mashamba ya bangi na itaendelea kutafakari utekelezaji wake. Pale tutakapojiridhisha kuwa adhabu hii itatoa fundisho kwa wananchi wanaojihusisha na kilimo cha bangi, Serikali haitasita kuleta Bungeni muswada wa mabadiliko ya sheria ili kuongeza suala hilo.


5.   HOJA: Kuongeza vituo vya tiba ya Methadone na Sober Houses za Serikali angalau moja kila Mkoa.
 
MTOA HOJA:  Mheshimiwa Dkt. Haji Mponda (Kamati ya Kudumu ya Bunge, Masuala ya UKIMWI); Mheshimiwa Abdallah Ali Mtolela (Temeke)

JIBU
Mheshimiwa Spika, uanzishwaji wa vituo vya tiba kwa kutumia Methadone unategemea ukubwa wa tatizo la matumizi ya dawa za kulevya na uwepo wa miundombinu ya msingi katika Mkoa husika. Hadi sasa kuna vituo vya Methadone katika hospitali za Muhimbili, Mwananyamala na Temeke - Dar es Salaam. Vilevile, Serikali inakusudia kufungua vituo kama hivyo katika Mikoa ya Arusha, Dodoma, Kilimanjaro, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Pwani naTanga.  

Kwa kuwa matibabu ya Methadone yanawasaidia watumiaji wa dawa za kulevya aina ya Heroin pekee, Serikali inatarajia kuanzisha nyumba za upataji nafuu (Sober Houses) kila Mkoa. Huduma hii itakuwa ni kwa ajili ya kuwasaidia waraibu (addicts) wengine wa aina zote za dawa za kulevya, badala ya kuwaachia watu binafsi ambao mpaka sasa wanaendesha nyumba 17 za upataji nafuu nchini. Vilevile, Serikali imeandaa Mwongozo wenye lengo la kusimamia na kuratibu Sober Houses za watu binafsi.


6.   HOJA:  Serikali iongeze vituo vya afya, vifaa tiba, wahudumu wa afya wenye weledi na kupunguza umbali wa kupata huduma kwa Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU). 

MTOA HOJA:  Mheshimiwa Dkt. Haji Mponda (Kamati ya Kudumu ya Bunge, Masuala ya UKIMWI);

JIBU
Mheshimiwa Spika, Ilani ya Uchaguzi ya CCM na Sera ya Maendeleo ya Afya ya Msingi vinaelekeza Serikali kuboresha huduma za afya ya msingi kwa kujenga zahanati kila kijiji, kituo cha afya kila kata na Hospitali kila Wilaya. Aidha, Serikali ina mkakati wa kuongeza idadi ya wataalam wa afya nchini kote. Kupitia mikakati hii, wananchi wakiwemo WAVIU watapata huduma karibu na maeneo wanayoishi.

7.   HOJA:  Serikali itoe elimu ya kujikinga na VVU kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo elimu kwa njia ya Sinema na kuanzisha vilabu vya mapambano dhidi ya VVU katika shule zote kuanzia msingi pamoja na kuandaa mitaala ya elimu ya UKIMWI katika ngazi zote za elimu (elimu ya msingi hadi vyuo vikuu).

MTOA HOJA:  Mheshimiwa Dkt. Haji Mponda (Kamati ya Kudumu ya Bunge, Masuala ya UKIMWI);

JIBU:
Mheshimiwa Spika,
Nia ya Serikali ni kuona elimu ya UKIMWI inawafikia wote wanaostahili. Serikali ina magari ya Sinema katika mikoa ishirini ya Tanzania Bara ambayo hutoa elimu ya UKIMWI kwa njia ya sinema. Tanzania Visiwani nayo sasa inapatamagari ya sinema katika mikoa yake yote. Wizara ya elimu imetoa mitaala ya kufundisha wanafunzi kuhusiana na elimu ya UKIMWI shuleni.

Serikali inatoa wito kwa Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri kuyatumia ipasavyo magari hayo na kuhakikisha Walimu wapya wanapitishwa vyema katika mitaala hiyo pamoja na kuanzisha klabu za kuhamasisha mapambano dhidi ya UKIMWI katika shule na vyuo vyote nchini.

8.   HOJA:  Serikali ibuni chanzo mahususi cha kutunisha Mfuko wa UKIMWI (AIDS TRUST FUND) kama ilivyo kwa mifuko mingine kama vile REA na maji, ili kufanikisha mapambano dhidi ya UKIMWI.

MTOA HOJA:  Mheshimiwa Dkt. Haji Mponda (Kamati ya Kudumu ya Bunge, Masuala ya UKIMWI);

JIBU:
Mheshimiwa Spika,
Ushauri uliotolewa umepokelewa na Serikali itaufanyia kazi.

9.   HOJA:     Kuweka utaratibu wa kufuatilia fedha zinazotolewa na wafadhili kwenye Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) zinazojihusisha na masuala ya UKIMWI.

MTOA HOJA:  Mheshimiwa Dkt. Haji Mponda (Kamati ya Kudumu ya Bunge, Masuala ya UKIMWI);

JIBU
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kufuatilia fedha zinazotolewa kwenye NGOs upo na tumekuwa tukisisitiza ufuatwe. Mathalan, nilipofanya ziara Mkoani Arusha hivi karibuni nilirudia wito wa kuzifanyia kaguzi za mara kwa mara NGOs zinazofanya kazi nchini. Hivyo, ushauri wa Kamati kuhusu hitaji la kufanya ukaguzi kwenye NGOs zinazoshughulikia UKIMWI utaendelea kuzingatiwa.

Natoa wito kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri waendelee kuhakikisha wadau wa UKIMWI wanaofanya kazi kwenye maeneo yao wanakaguliwa kulingana na Sheria ya UKIMWI ya mwaka 2008 na Sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2002. Nia yetu ni kujua wanapata nini, kwa ajili ya huduma zipi ili wanufaika waweze kujulishwa.

10.        HOJA: Serikali ijiridhishe kuhusu masuala ya kitaalam na kufanya mapitio na maboresho ya Sheria stahiki katika kutekeleza Mpango wa kuunganisha Mifuko ya Pensheni.

MTOA HOJA: Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama (Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria)

JIBU
Mheshimiwa Spika, zoezi la kuunganisha Mifuko ya Pensheni linafanyika kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu. Katika kutekeleza jukumu hilo, Mifuko yote ya Pesheni imefanyiwa tathmini (Actuarial Valuation), ambayo pamoja na mambo mengine, imebainisha kuwa kuunganisha Mifuko ya Pensheni ndio njia bora ya kuimarisha Sekta ya Hifadhi ya Jamii nchini.

Aidha, Serikali imeandaa Andiko la mapendekezo ya kuunganisha Mifuko. Kazi hii imefanyika kwa kushirikisha wadau muhimu katika Sekta husika. Serikali itaendelea kutoa taarifa za mara kwa mara kwa hatua zinazofikiwa.

11. HOJA:     Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwekeza kwenye uchumi wa viwanda.

MTOA HOJA:  Mheshimwia Zuberi Kuchauka (Liwale)

JIBU
Mheshimiwa Spika, uwekezaji ni kazi mojawapo ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Lengo la uwekezaji ni kulinda thamani ya michango ya wanachama pamoja na kukuza uwezo wa Mifuko kulipa mafao kwa wanachama wake pale wanapopatwa na majanga mbalimbali yanayowasababishia kukosa kipato. Majanga hayo ni kama vile maradhi, uzee na kifo. Kwa msingi huo, uwekezaji kwenye viwanda unaofanywa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii sasa una manufaa mtambuka kwani pamoja na kulinda thamani ya fedha za michango ya wanachama, uwekezaji huu unakuza mapato ya Serikali, unatoa fursa za ajira na hivyo kusaidia kuongeza idadi ya wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba uwekezaji unaofanywa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii unazingatia Miongozo ya Uwekezaji ili mifuko hiyo isiweze kupata hasara.

12.        HOJA: Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura.

MTOA HOJA:  Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama (Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria)

JIBU
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ina jukumu la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Katika Mwaka wa Fedha 2017/2018 Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaweka kipaumbele katika uboreshaji wa Daftari la Wapiga kura.

Aidha, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepewa jukumu la kutoa elimu ya mpiga kura Nchi nzima na kusimamia na kuratibu Asasi, Taasisi au watu wanaotoa elimu ya mpiga kura. Tume imeendelea kutoa elimu ya Mpiga Kura kwa njia mbalimbali ikiwemo kutumia Redio, Televisheni, kukutana na wadau kupitia maonyesho mbalimbali, pamoja na kushiriki mikutano katika ngazi za Mikoa na Halmashauri.

13.        HOJA: Mgogoro wa Uongozi ndani ya CUF

MTOA HOJA: Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama (Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria) Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni); Mheshimiwa Cecilia Danel Paresso (Viti Maalum); Mheshimiwa Rashid Ali Abdallah (Tumbe); Mheshimiwa Khatibu Said Haji (Konde); Mheshimiwa Juma Kombo Hamad (Wingwi); Mheshimiwa Masoud Abdallah Salum (Mtambile)

JIBU
Mheshimiwa Spika, Hoja hii imejadiliwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Waheshimiwa Wabunge mbalimbali.

Serikali haifurahishwi na migogoro ndani ya vyama vya siasa, kwani inadumaza demokrasia nchini na kusababisha mifarakano isiyokuwa na tija. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kama mlezi wa vyama vya Siasa imekuwa ikishiriki kikamilifu katika kuhakikisha migogoro ndani ya vyama vya siasa inatatuliwa kwa majadiliano.

Mheshimiwa Spika, Katika mgogoro uliopo ndani ya chama cha CUF, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilitoa ushauri kulingana na taratibu zilizopo. Hata hivyo, wakati usuluhishi ukiendelea baadhi ya wanachama wa CUF ambao hawakuridhika na usuluhishi uliofanywa na Msajili walipeleka shauri Mahakamani, ili kudai haki kwenye Mhimili wa Mahakama ikiwa ni pamoja na suala la ruzuku ambalo Mahakama imetoa zuio la muda mpaka shauri la msingi lililoko mahakama itakapolitolewa uamuzi. Kwa kuwa masuala hayo yapo Mahakamani, ni vizuri tukaiacha Mahakama ifanye kazi yake. Hiyo ni rai yangu.

5.0.      HITIMISHO

Mheshimiwa Spika, Kama nilivyosema hapo awali, muda usingeweza kutosha kujibu hoja zote zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja. Tumejifunza mambo mengi kutoka kwenye michango yenu, na tupo tayari kuendelea kujifunza zaidi kutoka kwenu Waheshimiwa Wabunge.

 Mheshimiwa Spika, Nchi hii ni yetu sote, na kila mmoja wetu anao wajibu wa kulisukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu. Kila mchango wa Mheshimiwa Mbunge una thamani kubwa sana kwetu, na ninawashukuru sana kwa ushauri, maangalizo na mafunzo. Endeleeni kutoa ushauri kwa Serikali, hata kwa maandishi siyo lazima kusubiri Bungeni, nasi tutaupokea na kuona namna bora ya kufanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, kila Mtanzania ikiwemo Waheshimiwa Wabunge, anawajibika kuiacha Tanzania ikiwa ni nchi bora zaidi ya alivyoikuta. Ili kuifikia azma hiyo, inabidi tuanze kuwa tayari kujinyima mambo mazuri tuliyoyazoea, angalau kwa muda, ili kuimarisha misingi ya ujenzi wa Tanzania yetu. Ninawasihi waheshimiwa Wabunge wenzangu muielewe dhamira ya Serikali na mtuamini katika kusimamia rasilimali za nchi yetu kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo. Serikali imejipanga vizuri katika kulinda maslahi ya nchi hii na wananchi wake, hivyo nawaomba muendelee kutuunga mkono kwa kupitisha Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naomba kutoa hoja.





EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.