Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala
ya UKIMWI imeipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI
Tanzania (TACAIDS) kwa mafanikio makubwa katika kutekeleza afua za VVU na
UKIMWI nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati
hiyo, Mhe. Stanslaus Nyongo wakati kamati ilipofanya ziara ya kutembelea na
kukagua Mpango wa Dreams kupitia Mradi wa Epidemic Control (EPIC) unaotekelezwa
na Shirika la Family Health International (FHI360) kwa wasichana balehe na
wanawake vijana (AGYW) katika katika Mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza mara baada ya kukagua vikundi vya
vijana vikiwemo Sitetereki kilichopo Kata ya Old Shinyanga, Jahazi,
Kata ya Ibadakuli na Tunaweza katika Kata ya Kolandoto Mhe. Nyongo amesema
lengo la ziara ni kujionea maendeleo ya mradi huo na kuishauri Serikali maeneo
ya kuboresha ili kuendeleza jitihada za kuwa na vijana wenye afya nzuri
wanaoshiriki katika shughuli za uzalishaji na kujiletea maendeleo yao.
“Tunapongeza kazi kubwa inayofanywa na Rais
wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa maelekezo ya kumlinda mtoto wa kike
hasa katika gonjwa kubwa la UKIMWI, namna ya kumkomboa mtoto wa
kike, kujifunza kazi za ujasiliamali ili kujikwamua katika maisha pamoja
kupaza sauti dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia hivyo sisi kama wabunge
tumeridhishwa na kazi inayofanywa na Serikali,”Amesema Mwenyekiti huyo.
Naye Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,
Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amewaomba vijana wa kike kuendelea
kujiamini na kufanya kazi vizuri kwani Serrikali ya Awamu ya Sita inawajali
vijana na kutambua mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Taifa.
Akizungumzia ziara hiyo Mjumbe wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Hassan Mtenga
ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za kukamilisha na kujengwa kwa miradi mikubwa
ya maendeleo huku akiipongeza TACAIDS na wadau wa maendeleo kuwa na mwamko wa
kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi.
“Tumejifunza kitu kwasababu tunao watu
wako tayari kupiga vita janga kuu la UKIMWI na niishukuru TACAIDS,
Mawaziri wenye dhamana na hawa wadada ambao wameamua kutoka kwenye
sughuli za kuuza bar na kuanzisha biashara zao sasa uwe mfano wa
kuigwa kwa maeneo mengine,”Amepongeza Mhe. Mtenga.
Vilevile Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Christina
Mnzava amesema wazazi na walezi wana wajibu wa kusimamia malezi sahihi ya
watoto ili kuwakomboa katika tabia hatarishi huku akiupongeza Mpango wa
Dream kwa kuamua kuwafikia mabinti katika maeneo yao akishauri mradi huo
kuongeza wigo na kuwafikia vijana wengine waliopo Vijijini .
“Sisi kama wazazi na walezi tunaweza
kuwakomboa watoto wetu katika tabia hatarishi ambazo wanazipata mtaani kuna
wengine walikuwa wanauza miili yao, lakini kutokana na mradi huu wamejikwamua
wamefundishwa ujasiriamali, kuwekeza tumeona wasichana wamejitambua
wanatengeneza sabuni, batiki, vyungu katika vikundi vya Kata za Old
Shinyanga, Ibadakuli na Kolandoto kwa kweli wamefanya vizuri,”Ameeleza Mjumbe
huyo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga Mhe Christina Mndeme amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na
Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kuondoa unyanyapaa na ubaguzi kwa watu
wanaoishi na VVU ambao upo juu, kuwajengea vijana uwezo wa kiuchumi ili muda
mwingi wautumie kwenye uzalishaji na sio kwenye mambo yanayoweza kuwasababishai
maambukizi ya VVU,kuelimisha jamii kuacha mila potofu ambazo zinasababisha
ukatili wa kijinsia.
Kwa upande wake Mshauri Mwandamizi wa Mpango
wa Dreams kupitia Mradi wa Epidemic Control (EPIC) unaotekelezwa na Shirika la
Family Health International (FHI360) Bi. Agnes Junga amefafanua kuwa lengo la
Mpango huo ni kupunguza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa wasichana kuanzia
umri wa miaka Tisa hadi 24.
“Mpango huu ulizinduliwa 2014 ukilenga
kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa Nchi 13 za Bara la Afrika ikiwemo
Tanzania ambapo tulianza na Halmashauri Sita na hadi sasa tumefikia Halmashauri
12. Shirika la (FHI360) kwenye mradi wa EPIC tunatekeleza Dreams katika
Mikoa miwili ya Shinyanga ndani ya Halmashauri Tano na Iringa katika
Halmashauri mbili na tunawafikia wasichana kuanzia miaka 15 hadi 25 walio nje
ya shule pamoja na wazazi au walezi na jamii kwa ujumla tuhakikishe
msichana anafikia ndoto zake.
Aidha akizungumza kwa niaba ya
wanakikundi kutoka Vikundi vya Mabinti Balehe na Wanawake Vijana vya
Sitetereki, Tunaweza na Jahazi mwanakikundi Sungi Leonard amesema uanzishwaji
wa vikundi hivyo vimewasaidia kama mabinti kujitambua, kufahamu elimu ya
afya, kuwajengea uwezo wa kukabiliana na vitendo vya kikatili pamoja na
kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya VVU na kuwawezesha kiuchumi.
“Nilikutana na mwezeshaji kiuchumi na
mwelimishaji rika nikapata elimu ya ukatili wa kijinsia, umuhimu wa
upimaji wa afya, matumizi sahihi ya kinga, magonjwa ya ngono na VVU
ambayo imenisaidia kujitambua kama binti. Pia nilifanikiwa kujiunga katika
kikundi cha Sitetereki nikajifunza kutengeneza batiki kazi ambayo inanipatia
kipato na ninamudu mahitaji yangu tofauti na ilivyokuwa awali,” Ameshukuru
Mwanakikundi huyo.
Read More