Saturday, November 25, 2023

WAZIRI MHAGAMA, AHIMIZA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA UTALII MBINGA

 


Imeelezwa kwamba uwekezaji wa hoteli kubwa na za kisasa unasaidia katika kuchochea shughuli za utali na kuongeza thamani ya Mji wa Mbinga, kwa sababu ya upekee wa vivutio vyake.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama wakati wa Uzinduzi wa Mradi wa Hotel ya One Pacific yenye hadhi ya nyota tatu katika wilaya ya Mbinga.

Waziri Mhagama amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.  Samia Suluhu Hassan amejipambanua kwa kuwa balozi kinara wa sekta ya utalii na uwekezaji kwa ujumla katika sekta ya utalii.

“Mkakati wa Taifa wa ROYAL TOUR na kuifungua nchi yetu Tanzania katika sekta ya utalii ni mkakati mkubwa sana, na uliotukuka na tunaungana na wawekezaji katika kutafsiri ROYAL TOUR ndani ya wilaya yetu ya Mbinga,” Alifafanua

Akieleza kuhusu vivutio vinavyopatikana, Waziri amesema, wilaya ya Mbinga inavivutio vya kutosha; kama safu za milima zilizojipanga kwa kuvutia, zenye maporomoko ya maji, uoto wa asili, unaopendezesha madhari ya milima hiyo.

Aidha hapa ndio mahali ambapo kuna mapango ya kale katika eneo la Litembo, na inaaminika wazee wetu wa zamani waliishi katika mapango hayo.

“Hii historia kama itawekezwa vizuri, ni kivutio na utalii wa kutosha sana katika eneo letu,” Alibainisha.

Kwa upande wake Dkt. Erasmo Nyika akizungumza kwa niaba ya bodi ya wawekezaji wa mradi wa Hotel hiyo amesema wamesukumwa kuja kuwekeza Mbinga kutokana na Msukumo wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amejenga mazingira rafiki ya uwekezaji.

“Tumuwekeza miradi miwili ndani ya wilaya ya Mbinga yenye thamani ya zaidi ya shilingi Billioni 4, na tumeona fursa zipo na tunashukuru Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga kwa kutushawishi kuwekeza Mbinga, mradi umelenga kuzalisha ajira nyingi kwa wazawa,” Alisema

Awali, Mhandisi Selemani Kinyaka katika taarifa yake amesema Ujenzi wa Majengo ya mraadi wa One Pacific Hotel; unavyumba vya kawaida 14, vyumba vya daraja la juu 23 vyumba vya hadhi ya kiutawala 3, Ukumbi mdogo wa mikutano, Migahawa 2, sehemu ya mazoezi, eneo la kuogelea na eneo la kufulia nguo.

 

Katika kipindi cha utekelezaji wa mradi tumetoa ajira zaidi ya 250 ambapo 30 zilikuwa ajira za kudumu, na nyingine ni ajira zilizojitokeza kila siku.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.