Tanzania
imekuwa nchi ya kwanza miongoni mwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini
mwa Afrika SADC, kusaini mkataba wa kuanzishwa kituo cha huduma za kibinadamu
na oparesheni za dharura za kanda.
Akizungumza
mapema hii leo wakati wa hafla ya utiaji Saini iliyofanyika Jijini Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene
amesema, Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
zimeendelea kushirikiana, katika masuala ya usimamizi wa maafa kupitia Kamati
ya Mawaziri wenye dhamana ya Usimamizi wa Maafa.
Aliongeza
kuwa, Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa katika kuendeleza ushirikiano ni
kuanzisha Kituo cha Huduma za Kibinadamu na Operesheni za Dharura cha Kikanda
ambacho kipo Nacala, Jimbo la Nampula nchini Msumbiji. Kituo kilichozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mheshimiwa
Filipe Nyusi tarehe 21 Juni, 2021.
“Lengo
la kuanzisha Kituo hicho ni kusimamia masuala ya huduma za misaada ya
kibinadamu kwa Nchi Wanachama zitakazokumbwa na maafa,na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imeendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa shughuli
za usimamizi wa maafa.” Alifafanua.
Aliendelea
kusema kuwa, mkataba huo umepitishwa na kamati zote zinazohusika ikiwemo Kamati
ya Mawaziri wanaohusika na usimamizi wa maafa Aprili, 2022 Lilongwe, Malawi;
Kamati ya Mawaziri wanaohusika na usimamizi wa sheria na Wanasheria Wakuu
Julai, 2022 Lilongwe Malawi; na Baraza la Mawaziri katika mkutano wa kawaida
uliofanyika Agosti, 2022 Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mkutano wa
Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika tarehe 17 na 18 Agosti, 2022 Kinshasa, Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo uliidhinisha Mkataba huu na kuelekeza kuwa usainiwe na
Mawaziri wanaohusika katika usimamizi wa maafa.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt John
Jingu alisema jitihada hizi zilianzishwa kwa sababu, masuala ya majanga hayana
mipaka na yanahitaji jitihada za pamoja na kushugulika kwa pamoja katika usimamizi.
Awali
mwakilishi kutoka sekretariati ya nchi hizo mwanasheria Dkt Phiness Matto,
alisema, Mkataba huu umekuja katika wakati muhimu ambapo kituo hiki kitakuwa na
jukumu kubwa la kufanya uratibu, kutambua na kushughulikia athari zote kadiri
itavyowezekana.
“Natoa
Pongezi kwa Tanzania kuwa nchi ya kwanza ku sign mkataba huu na tunategemea
nchi 11 kusaini mkataba huu” Alifafanua Dkt Matto.