NA.MWANDISHI
WETU
Serikali kwa ushirikiana na wadau wengine imejipanga kuendelea kukabiliana
na majanga yanayoikumba nchi ili kuhakikisha inashughulikia na kutatua majanga
hayo pindi yanapotokea.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Bunge na Waziri Mkuu, Maimuna Tarishi Januari 28, 2019 wakati
akifungua warsha ya kupunguza madhara ya maafa nchini na kuimarisha uthabiti kwa
nchi na jamii dhidi ya majanga ya asili katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la
Sahara.
Tarishi alibainisha jitihada zinazofanywa na Serikali ili kukabili maafa
ikiwa ni pamoja na kuendelea kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kuimarisha
ustahimilivu wa majanga ya asili kwa kuongeza idadi ya wilaya zenye mipango ya kupunguza
madhara ya maafa, kuboresha mifumo ya tahadhari za awali, kuongeza utoaji wa
elimu kwa umma na kuimarisha shughuli za kujiandaa, kukabili na kuimarisha
mfumo wa uratibu wa masuala ya maafa.
“Kwa kuzingatia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka wa Mitano, 2016/17-
2020/21 tutaendelea kuimarisha ustahimilivu wa majanga ya asili pamoja na
kukabili majanga kwa kuzingatia utekelezaji wa malengo ya msingi ya Mfumo wa
Sendai wa Kupunguza Madhara ya Maafa wa mwaka 2015 – 2030, tumedhamiria
kuhakikisha tunakabiliana na majanga ili kujiletea maendeleo,”alisema Tarishi
Aliongezea kuwa, kwa kuzingatia majanga yanayoikabili nchi ikiwemo
mafuriko nchi haina budi kuwa mikakati hiyo ili kuhakikisha inakabili na kuweka
mikakati yenye tija katika masuala ya menejimenti ya maafa nchini.
Tarishi alibainisha kuwa,
mafuriko yamekuwa na athari nyingi kwa kulinganisha na majanga mengine
yanayoikabili nchi mara kwa mara kwa kuzingatia takwimu zilizopo kwa sasa.
“Takwimu zinaonesha kuwa kwa kipindi cha Januari hadi Desemba, 2018
mafuriko yameathiri wilaya 50 na kusababisha vifo kwa watu 71, majeruhi kwa
watu 64, kuharibiwa nyumba 15,802 kwa viwango tofauti, kuathiri miundombinu
katika shule 43, mashamba ya mazao mbalimbali, na vituo vya afya,”alisisitiza
Tarishi
Alieleza kuwa, takwimu zilizopo tangu tupate
uhuru nchi imeathiriwa na ukame zaidi ya mara 18 ikimo yale ya mwaka 2006/2007
na 2007/2008 ambayo yaliathiri zaidi mikoa ya Arusha, Dodoma, Iringa,
Kilimanjaro, Manyara, Shinyanga, Lindi, Singida, Tabora na Mwanza.
Sambamba na hilo Ukame mwingine mkubwa ulitokea mwaka 2008/2009
ulioathiri zaidi mikoa ya kaskazini ya nchi hasa Arusha na Manyara. Mikoa
ambayo mara nyingi huathiriwa na ukame ni Dodoma, Singida, Tabora na Shinyanga,
ambayo kawaida hupata mvua ya chini kwa kiwango cha kati ya milimita 200 - 600
kwa mwaka.
Naye Mkuu wa
Sekretarieti ya Kupunguza Madhara ya Maafa ya Umoja wa Mataifa kwa Kanda ya
Afrika, Amjad Abbashar, alieleza
mipango mikakati ya kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuzingatia
ongezeko la madhara yatokanayo ya maafa ikiwemo vifo, upotevu wa makazi, pamoja
na uharibifu wa mali za watu.
“Tutaendelea kushirikiana na kuhakikisha tunakabili na kuzuia maafa
yasitokee pale itakapotokea ili kuendelea kuwa na maendeleo endelevu katika
mazingira tuliyonayo,”alieleza Abbashar
Kwa upande
wake Mwakilishi Mkazi wa Taasisi za Umoja wa Mataifa nchini Tanzania,Alvaro
Rodriques, aliwataka wajumbe kuitumia
fursa ya warsha hiyo kwa kuzingatia mada zitakazowasilishwa ili kuhakikisha
nchi inaendelea kuwa na wataalam na mikakati yenye kutatua madhara yatokanayo
na majanga na kuahidi kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali
ya Tanzania katika kushughulikia maafa.
AWALI
Warsha ya kupunguza madhara ya maafa nchini na kuimarisha uthabiti kwa nchi na
jamii dhidi ya majanga ya asili katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara
imeratibiwa na Idara ya Usimamizi wa shughuli za Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Sekretarieti
ya Kupunguza Madhara ya Maafa ya Umoja wa Mataifa na Taasisi ya Utafiti ya CIMA
kupitia ufadhili wa Umoja wa Ulaya. Aidha warsha inatarajiwa kudumu kwa siku
tano hadi Februari 01, 2019 Jijini Dodoma.
Warsha hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya
Umoja wa Ulaya (EU) katika nchi za Africa, Caribbean na Pacific (ACP), ambayo
inalenga kupunguza majanga katika nchi hizo.
Mkuu
wa Sekretarieti ya Kupunguza Madhara ya Maafa ya Umoja wa Mataifa kwa Kanda ya
Afrika, Amjad Abbashar akizungumza kuhusu namna bora za kukabili majanga wakati wa warsha hiyo.
|
Mwakilishi Mkazi wa
Taasisi za Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Bw.Alvaro Rodriques akiwasilisha
hotuba yake wakati wa warsha hiyo.
|
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Waziri
Mkuu) Bi.Maimuna Tarishi pamoja na wajumbe wa meza kuu wakifuatilia
uwasilishwaji wa mada wakati wa warsha hiyo.
|
Sehemu ya wajumbe wakifuatilia uwasilishwaji wa
hotuba ya Mwakilishi
Mkazi wa Taasisi za Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Bwana Alvaro Rodriques
(hayupo pichani) wakati wa warsha hiyo.
|
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na
Waziri Mkuu) Bi.Maimuna Tarishi (wa tano kutoka kulia) akiwa katika picha ya
pamoja na baadhi ya wajumbe walioshiriki katika warsha hiyo.
|