WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amekagua eneo la ujenzi wa hospitali ya Uhuru lenye ukubwa
wa ekari 109 lililoko katika wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.
Akizungumza
na wakazi wa kijiji cha Maduma wilayani humo leo mchana (Ijumaa, Januari 18,
2019), Waziri Mkuu amesema uamuzi wa Serikali ya kijiji hicho wa kutenga maeneo
ya maendeleo ni wa kupigiwa mfano na vijiji vya maeneo mengine.
“Uamuzi
wenu wa kutenga maeneo ya miradi ya maendeleo umekuwa na tija, ndiyo maana
Mheshimiwa Rais Magufuli aliposema ijengwe hospitali, hamkupata shida sababu
eneo tayari lilikuwepo. Ninawapongeza wazee waliojitolea maeneo yao ili
kuongeza kwenye eneo la hospitali,” amesema.
Wazee
waliotoa maeneo yao ni Mzee Meshack Njamasi (ekari 5.50), Mzee Jobu Malogo
(ekari 3.50) na Bw. Nehemia Mwikwi (ekari 4.50). Ekari 95.5 zilizobakia,
zimetolewa na Seriakli ya kijiji hicho.
Waziri
Mkuu aliwataka wakazi wa wilaya ya Chamwino wasibweteke bali wajipange na kila
mmoja ajipange kufanya kazi kama ambavyo Rais Magufuli amekuwa akihimiza.
“Ujenzi wa mji wa Serikali unaoendelea hivi sasa ni fursa kwenu. Na ujio wa
hospitali hii ni fursa nyingine kwa wana-Chamwino hasa kwa vile ujenzi wake utatumia
mfumo wa force account ambao unatoa fursa kwa wanajamii kushiriki kazi
za miradi ya eneo husika,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema ujenzi wa hospitali hiyo yenye hadhi ya wilaya ni utekelezaji wa
Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inayoelekeza wananchi wapatiwe huduma za
matibabu huko huko waliko. “Hadi sasa tumeshajenga vituo vya afya 350 ili
kusogeza huduma kwa wananchi na jumla ya hospitali za wilaya 67, zinajengwa
nchi nzima kwa mwaka huu,” amesema.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wakazi wa
vijiji jirani, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Bw. Selemani Jafo
alisema eneo la ujenzi wa hospitali hiyo liko umbali wa kilometa mbili kutoka barabara
kuu ya Dar es Salaaam-Dodoma na kilometa tatu kutoka Ikulu ya Chamwino.
Naye, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Dkt. Faustine aliwataka wakazi hao wachangamkie fursa hiyo kwa
kusomba mawe, mchango, maji na kwamba Kamati za usimamizi wa ujenzi zitapaswa
kusimamiwa na wanakijiji.
Aliwataka
wakazi hao wasiishie kwenye lengo la kuwa na hospitali ya wilaya, bali walenge
kujenga hospitali yenye hadhi ya mkoa kwa kadri bajeti itakavyoruhusu.
Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma, Dk. Bilinith Mahenge alisema ujenzi wa hospitali hiyo ni wa hadhi ya
wilaya ikiwa na nyongeza ya huduma za wagonjwa wa dharura na wagonjwa mahututi
(Emergency Department and Critical Care Unit).
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.