Tuesday, March 31, 2026

WANANCHI IDODI WAMLILIA LUKUVI


 WANANCHI wamlilia aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu na Mbunge wa Jimbo la Isimani Marehemu William Lukuvi kwa kazi nzuri alizozifanya wakati akitekeleza majukumu yake katika sekta mbalimbali serikalini na kuwaletea maendeleo katika nyanja mbalimbali.

Hayo yamelezwa kwa wakati tofauti hii leo wakati mwili wa marehemu Lukuvi ulipowasili Kijijini Kwake Kata ya Idodi, Wilaya ya Iringa  ambapo ndipo kunatarajiwa kuwa makazi yake ya milele mara baada ya ibada ya mazishi kijijini hapo.

Wananchi hao wameonesha simanzi kubwa na kumkumbuka kama kiongozi shupavu, na mtetezi wa wanyonge hususan kwa wakazi wa Jimbo Lake la Isimani Mkoani Iringa.

Akizungumza na waandishi wa habari Mmoja wa waombolezaji Bw. Kombo  Jumbe amesema Marehemu William Lukuvi aliasisi utaratibu wa kliniki za ardhi wakati akiwa anahudumu kama Waziri wa Ardhi na hivyo kuwezesha wananchi kuhudumiwa kwa  urahisi na kwa haraka.

“Marehemu Lukuvi alituwezesha sisi hupata huduma kwa haraka hasa zilizohusu masuala ya migogoro ya ardhi na kufanya kufikiwa kwa urahisi na watoa huduma katika wizara ya ardhi  na yeye ndiye aliyezindua upatikanaji wa hati za ardhi na kufanya zoezi lile kuwa endelevu” alieleza

Kwa upande wake Bw. Frank Mbindile Mkazi wa Kijiji cha Magozi Wilaya ya Iringa amesema Marehe William Lukuvi alikuwa ni mtu anayependa kusikiliza shida za watu kwa makundi na hata shida za mwananchi mmoja mmoja na kukiri kuwa wamepoteza mtu muhimu na Lulu kwa Taifa.

“Ni aina ya kiongozi anayeamini katika kusimamia mambo ya msingi kwa ajili ya maslahi mapana ya wananchi na akizungumza jambo alikuwa anauwezo wa kulisimamia, hivyo wanaisimani tumepoteza kiongozi mkubwa,” alieleza.

Read More

Monday, March 30, 2026

MISA YA KUOMBEA NA KUAGA MWILI WA MAREHEMU MHE. LUKUVI MKOANI IRINGA

MISA Takatifu ya kuuaga Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), na Mbunge wa Jimbo la Isimani, Marehemu Mhe. William Lukuvi, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu lililopo Kihesa Iringa leo tarehe 30 Machi, 2026 nakuongozwa na Askofu wa Jimbo la iringa Romanus Mihali.

Misa hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Viongozi wa Vyama vya Siasa, Viongozi wa dini pamoja na Waombolezaji kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Iringa na nje ya mkoa huo.

Mhe. Lukuvi amefariki dunia tarehe 25 Machi, 2026 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Mkoani Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu.

Read More

Sunday, March 29, 2026

MWILI WA MAREHEMU MHE. LUKUVI UKIWASILI KATIKA KIWANJA CHA NDEGE CHA IRINGA


Mwili wa aliekuwa  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), na Mbunge wa Jimbo la Isimani, Mhe. William Lukuvi, ukiwasili katika  Kiwanja cha Ndege cha Iringa tarehe 29 Machi, 2026.

Mwili huo umesafirishwa kutoka Dar es Salaam leo baada ya shughuli ya kuaga iliyofanyika jana Machi 28, 2026 katika Viwanja vya Karimjee.

Read More

Saturday, March 28, 2026

NAIBU WAZIRI UMMY ASHIRIKI IBADA YA KUAGA MWILI WA MAREHEMU WILLIAM LUKUVI


NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Mhe. Ummy Nderiananga akiwa katika ibada ya kuaga mwili aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Marehemu Mhe. William Lukuvi leo katika viwanja vya Karimjee Hall Jijini Dar es salaam.

Mhe. Lukuvi amefariki dunia  tarehe 25 Machi, 2026 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Mkoani Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu.

Read More

DKT. YONAZI AWASILISHA WASIFU WA MAREHEMU WILLIAM LUKUVI

 


WASIFU WA ALIYEKUWA WAZIRI WA NCHI OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE, URATIBU NA WENYE ULEMAVU MAREHEMU WILLIAM VANGIMEMBE LUKUVI 

KUZALIWA

Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi alizaliwa tarehe 15 Agosti 1955 katika kijiji cha Mapogoro, Kata ya Idodi - Wilaya ya Iringa Vijijini, Mkoani Iringa.

Marehemu William Vangimembe Lukuvi alikuwa mwanasiasa mashuhuri alieshika nyadhifa mbalimbali za uongozi na aliesifika kwa ubunifu, uthubutu, uchapakazi, uzalendo, mwenye uwezo wa kujitoa na kujituma katika kazi na aliweka maslahi ya Taifa mbele na wakati wote aliamini katika matokeo chanya katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali. Alijulikana kwa mtindo wake wa kazi wa kutembelea maeneo ya miradi na kusikiliza kero za wananchi moja kwa moja, jambo lililosaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za Serikali. Katika kudhihirisha uchapakazi wake, siku moja kabla ya umauti kumkuta, marehemu alihudhuria na kuratibu Serikali katika Vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge pamoja na kutoa maelekezo mbalimbali ya Serikali. 

ELIMU

Marehemu William Vangimembe Lukuvi alipata elimu ya Msingi katika Shule ya Msingi Kitanewa kuanzia mwaka 1962 hadi 1970. Alijiunga na Chuo cha Ualimu Tabora (TTC) kuanzia mwaka 1974 – 1975 ambapo alihitimu na kutunukiwa Cheti cha Ualimu. Mwaka 1982- 1983 alijiunga na Shule ya Komsomol High School, Moscow nchini Urusi na kutunukiwa Stashahada ya Juu ya Sayansi ya Siasa (Advanced Diploma in Political Science). Alipata Shahada ya Masuala ya Kimatiafa na Diplomasia yaani Bachelor of Arts in International Studies and Diplomacy kutoka Washington International University kuanzia mwaka 1999 – 2001, na baadaye alijiendeleza kimasomo katika ngazi ya shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu Huria Tanzania ambapo alihitimu na kutunukiwa Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Siasa mwaka 2008 – 2011.

 KAZI NA SIASA

Marehemu William Vangimembe Lukuvi alianza safari yake ya kisiasa mwaka 1973 alipojiunga na Chama cha TANU akiwa mwanafunzi wa Chuo cha Ualimu Tabora (TCC) na kuchaguliwa kuwa kiongozi wa chama katika chuo hicho mwaka 1974 - 1975.  Mnamo mwaka 1984 alichaguliwa kuwa mjumbe wa Vikao vya umoja wa Vijana wa CCM katika Ngazi ya Wilaya hadi Taifa. Alichaguliwa kuwa Katibu wa Mkoa na Wilaya wa chama cha CCM mwaka 1980 – 1984. Vile vile, aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM mwaka 1993 – 1994. Aidha, Alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashuari Kuu ya CCM na Mjumbe wa Kamati ya Maadili ya Chama mwaka 2010 hadi sasa.

Marehemu William Vangimembe Lukuvi aliajiriwa kama Mwalimu katika Wizara ya Elimu kuanzia mwaka 1975 hadi 1980.

Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba kuanzia mwaka 1994 – 1995, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma 2006 – 2008 na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam 2008 - 2010.

Katika uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi vya Siasa nchini uliofanyika mwaka 1995, Marehemu Lukuvi alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Isimani na hivyo kuwa mbunge wa kwanza wa jimbo hilo alilolitumikia kwa takribani  miaka 30 hadi umauti ulipomkuta. Akiwa mbunge aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuanzia Mwaka 2005 – 2010.

 

Katika maisha yake ya siasa, Marehemu Lukuvi aliingia katika Baraza la Mawaziri kwa mara kwanza alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Vijana na Ajira mwaka 1995 – 2000, na baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu na Mnadhimu Mkuu wa Serikali (Chief Whip) kati ya mwaka 2000 – 2005, 2010 – 2015 na 2025 - 2026.

Halikadhalika, Marehemu Lukuvi aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi Nyumba, na Maendeleo ya Makazi kuanzia Januari, 2015 hadi mwaka  2022.

Aidha, mnamo Juni 2023, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alimteua kuwa Mshauri wa Rais kuhusu Mahusiano ya Kisiasa na Kijamii.

 MAFANIKIO KATIKA SEKTA ALIZOONGOZA KIPINDI CHA UTUMISHI WAKE

 Akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu),

Alikuwa msimamizi mahiri wa shughuli za Serikali Bungeni na alifanikiwa kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na Bunge, jambo ambalo lilimfanya kuwa mmoja wa Mawaziri wenye ushawishi mkubwa katika awamu mbalimbali za uongozi, na kujenga daraja imara kati ya Serikali, Bunge na wananchi.

 

Alisimamia utekelezaji wa sera mbalimbali zilizolenga kuboresha ustawi wa wenye ulemavu akihamasisha ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika fursa za kiuchumi na ajira na kusisitiza kuwa kundi hili ni sehemu muhimu ya nguvu kazi ya taifa.

 Alisimmamia kikamilifu Ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma ambao hadi sasa umefikia wastani wa asilimia 93 na tayari Wizara 15 zimeshahamia katika mji huo na zinatoa huduma kwa umma kutoka hapo.

 Alisimamia uimarishaji wa mifumo ya kisera kwa kufanya maboresho katika usimamizi wa maafa nchini ikiwemo Mfumo wa Taarifa wa kielektroniki wa Usimamizi wa Maafa (Disaster Management Information System - DMIS), hatua iliyosaidia kupunguza Athari za maafa nchini. 

Alikuwa mstari wa mbele kwa kuhakikisha Wizara zote zinafanya kazi kwa ushirikiano ili kuwezesha ufanisi katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuhakikisha ahadi za serikali kwa wananchi zinatekelezwa.

 Akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Alifanikiwa kutatua migogoro ya ardhi nchini kwa kuanzisha mifumo bora ya kutatua migogoro ya ardhi na kupeleka huduma bora na zilizo karibu na wananchi.

 Alisimamia uanzishwaji wa mifumo ya kidijitali ya usimamizi wa ardhi iliyolenga kupunguza urasimu na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa kodi ya pango la ardhi, hatua iliyosaidia kuongeza mapato ya Serikali.

 Alisimamia utoaji wa hati miliki za ardhi zaidi ya 1,992,245 kwa Watanzania hatua iliyosaidia kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutumia hati hizo kama dhamana za mikopo.

 Alifanikiwa kutenga ardhi yenye ukubwa wa ekari 224,439.4 kwa ajili ya uwekezaji kupitia Mipango Kabambe ya miji, mipango ya matumizi ya ardhi ya Wilaya na Vijiji. Hatua hii ilisaidia kuongeza uwekezaji nchini na kutoa ajira kwa wananchi.

 Akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM

Alianzisha mfumo wa mbio za mwenge kwa kushindanisha mikoa katika maandalizi, hamasa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mikoa husika. Suala hili lilileta chachu ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa ufanisi na kuleta matokeo makubwa kwa wananchi. 

Alibuni na kuanzisha mradi wa mabasi ya wanafunzi katika Mkoa wa Dar es Salaam jambo ambalo lilipunguza adha kubwa ya usafiri kwa wanafunzi wa Jiji la Dar es Salaam. 

Akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma

Alifufua na kuimarisha kilimo cha mtama na kuanzisha shamba la ushirika la zabibu akishirikiana na benki ya CRDB ambapo mradi huo sasa unasimamiwa na Wizara ya Kilimo ukijulikana kama BBT (Bulding a Better Tommorow).

 Alihakikisha kuwa mipango ya upanuzi wa mji wa Dodoma inazingatia sheria na taratibu za mipango miji ili kuzuia ujenzi holela, jambo ambalo lilikuwa ni msingi muhimu wa ukuaji wa Mji mkuu wa kisasa. 

Alisimamia Ujenzi wa Chuo Kikuu cha UDOM, hatua iliyosaidia kuongeza udahili wa Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini.

 FAMILIA

Enzi za uhai wake, Marehemu Lukuvi alifunga ndoa takatifu tarehe 28 Julai, 1990 na Bi. Germina Lukuvi katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Jijini Dar es Salaam na kujaaliwa kupata watoto watatu ambao ni Nobert William Lukuvi, Brown William Lukuvi na Anifisye Vanessa William Lukuvi. 

Marehemu Lukuvi ameacha mjane, watoto watatu na mjukuu mmoja aitwae Donovan.

 UGONJWA NA KIFO

Marehemu William V. Lukuvi alifariki dunia tarehe 25 Machi, 2026 saa 1:00 asubuhi katika Hospital ya Benjamini Mkapa Jijini Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kupata ugonjwa wa mshtuko wa Moyo.

Tunamsukuru mwenyezi Mungu, kwa maisha ya Willian V. Lukuvi ambaye hakika aliitumikia nafasi yake ya Ubunge na nafasi nyingine alizoaminiwa na serikali kwa bidii, ufanisi na uadilifu wa hali ya juu. Tunaomba Mungu ampe pumziko la Amani. 

RAHA YA MILELE UMPE EE BWANA NA MWANGA WA MILELE UMWANGAZIE, APUMZIKE KWA AMANI, AMINA.

Read More

Thursday, March 26, 2026

SERIKALI YAIMARISHA HUDUMA KWA WENYE ULEMAVU: WATENDAJI WAJENGEWA UWEZO MATUMIZI YA MFUMO WA (PD-MIS) RUVUMA

Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuboresha huduma kwa watu wenye ulemavu kwa kuwajengea uwezo watendaji wake katika matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji na usimamizi wa taarifa za watu wenye ulemavu (PD-MIS), hatua inayolenga kupata takwimu sahihi kuanzia ngazi ya kaya hadi mkoa.

Mafunzo hayo yamehusisha Maafisa Tehama na Maafisa Ustawi wa Jamii kutoka Mikoa ya Ruvuma, Mtwara, Lindi na Njombe, yakifanyika mkoani Ruvuma kwa lengo la kuwawezesha washiriki kutambua na kusimamia matumizi ya mfumo huo katika maeneo yao ya kazi.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa kutoka Kitengo cha Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Bw. Jackob Mwinula, alisema kuwa uwezeshaji huo ni muhimu katika kuhakikisha watendaji wanakuwa na uelewa wa kutosha wa mfumo huo na kuwafikia wananchi kwa ufanisi zaidi.

“Baada ya mafunzo haya, tunatarajia kuona watu wenye ulemavu wakisajiliwa, kupata namba za utambulisho na hivyo kuwezeshwa kufikia huduma mbalimbali za kijamii pamoja na kuunganishwa na mifumo mingine ya Serikali,” alisema Bw. Mwinula.

Aliongeza kuwa zoezi la usajili ni endelevu na litahusisha maafisa kuwafikia walengwa moja kwa moja katika maeneo wanayoishi ili kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma.

Kwa upande wake, Bi. Suzana Mayengo, mwezeshaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, alisema mafunzo hayo pia yanalenga kuwajengea watendaji uwezo wa kutambua aina mbalimbali za ulemavu na namna ya kushirikisha kundi hilo katika mipango ya maendeleo ili kuhakikisha ushirikishwaji jumuishi na unaozingatia mahitaji yao.

Aidha, upatikanaji wa taarifa sahihi utaiwezesha Serikali kutekeleza kikamilifu Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2006 unaosisitiza kauli mbiu ya “Nothing About Us Without Us”, inayolenga ushirikishwaji wa moja kwa moja wa kundi hilo katika maamuzi yanayowahusu.

Naye Mchambuzi wa Mifumo kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Bw. Antony Nchimbi, alieleza kuwa mfumo wa (PD-MIS) umesanifiwa kwa ushirikiano kati ya e-GA na Ofisi ya Waziri Mkuu, na umeunganishwa na mifumo mingine 11 ya Serikali ili kurahisisha upatikanaji na ubadilishanaji wa taarifa.

Alibainisha kuwa mfumo huo una uwezo wa kuwasiliana na mifumo muhimu ikiwemo wa wanafunzi (SIS) kutoka TAMISEMI, mfumo wa afya (GoTHOMIS), mfumo wa mikopo (Wezesha) na Mfumo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), hatua itakayosaidia kuthibitisha na kuboresha huduma kwa watu wenye ulemavu nchini.




Read More

Monday, March 23, 2026

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YAPITISHA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA BAJETI YA OFISI YA WAZIRI MKUU KWA MWAKA WA FEDHA 2026/27

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imepitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya bajeti ya kiasi cha 168,540,287,000 kwa mwaka wa fedha 2026/27 ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizopo chini ya Ofisi hiyo.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.) leo katika Ofisi za Bunge Jijini Dodoma mara baada ya wajumbe kujadili na kuridhia makadirio hayo ya bajeti katika kikao kilichohusisha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo, wataalamu  kutoka Idara na Vitengo vya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Awali akiwasilisha Taarifa kuhusu Utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/27 mbele ya kamati hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge,Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. William Lukuvi ameishukuru kamati kwa kujadili na kupitisha makadiri ya bajeti hiyo huku akisema Ofisi yake itaendelea kufanya kazi kwa weledi zaidi kwa kuzingatia jukumu la msingi la Uratibu wa Shughuli zote za Serikali.

Ameongeza kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu inaahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Kamati hiyo ikiwa ni pamoja na kutekeleza maoni na ushauri wa kamati.



Read More

Thursday, March 19, 2026

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA AFYA NA MASUALA YA UKIMWI YAIPONGEZA SERIKALI KUWAWEZESHA KIUCHUMI WAISHIO NA VVU

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI ambaye pia ni Mbunge wa Arumeru Magharibi Mhe. Johannes Lukumay ameipongeza  Serikali kuendelea kusaidia kundi la Watu waishio na Maamubikizi Virusi vya UKIMWI kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kujikwamua kiuchumi.

Mhe. Lukumay ameyasema hayo mara baada ya ziara ya kutembelea Baraza la Watu waishio na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI akiwa ameambatana na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI katika (Konga ya Jiji) iliyofanyika   katika Viwanja vya Pugu Mnadani Jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa watu waishio na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ni sawa na watu wengine hivyo yapaswa kuwapa kipaumbele katika fursa mbalimbali za kimaendeleo.Pia Mwenyekiti huyo amelipongeza kundi hilo kwa namna wanavyojituma katika kuhakikisha wanajikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini hivyo  kuziagiza  sekta husika kusaidia katika kuwatafutia masoko kwa ajili ya bidhaa zao.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga amesema kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wataendelea kuunga mkono jitihada zao kwa kuongeza nguvu zaidi kwa Wanakonga ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Mhe. Nderiananga amempongeza Mkurugenzi wa Jiji, Mkuu wa Wilaya pamoja na Katibu Tawala wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam na timu nzima kwa kuwawezesha Wanakonga katika fursa mbalimbali na kuwataka kuendelea na desturi hiyo ya kuwawezesha kwani mwaka huu wa fedha bado haujamalizika.

Aidha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam Elihuruma Mabelya amesema kuwa moja ya eneo waliloliwekea nguvu ni Konga hiyo kwa kuunga mkono shughuli zao za kiuchumi ili kuhakikisha wanainuka na kufanikiwa katika nyanja mbalimbali za maendeleo



Read More

Wednesday, March 18, 2026

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YARIDHISHWA NA UTEKELEZWAJI MRADI WA KITUO CHA TAIFA CHA UTENGAMAO.


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imetembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Utengamao cha Taifa unaotekelezwa na Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) katika eneo la Itega, jijini Dodoma.

Ziara hiyo imefanyika leo na kuongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Edwin Swale (Mb) ikiwa ni sehemu ya majukumu ya kamati ya kusimamia na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Swale amesema kuwa kamati imeridhishwa na hatua ya utekelezaji  ambayo mradi umefikia kwani unaenda kutimiza  dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kujali Utu na Ustawi wa Watanzania.

Sambamba na hilo, ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu kupitia Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za Kulevya kwa kubuni mbinu ya jinsi ya kusaidia waraibu watokanao na matumizi ya madawa za kulevya.

Awali,Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga amesema kuwa Mradi huo ni endelevu ikiwa ni juhudi ya Serikali katika mapambano dhidi ya Dawa za kulevya na kuahidi kuendelea kushirikiana na Taasisi binafsi katika mapambano dhidi ya matumizi ya Dawa za kulevya Nchini.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na Dawa za kulevya Bw. Aretas Lymo ameongeza kuwa kituo hiko kinatarajia kutoa huduma za matibabu, urekebishaji wa kitabia pamoja programu za kuwawezesha waathirika kurejea katika jamii wakiwa na uwezo wa kujitegemea



Read More

Tuesday, March 17, 2026

NAIBU WAZIRI UMMY ATOA MSUKUMO KWA WATUMISHI KUONGEZA UFANISI, AAGIZA UTEKELEZAJI THABITI WA BAJETI

Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderiananga, amewahimiza watumishi wa ofisi hiyo kuendelea kufanya kazi kwa bidii, ufanisi na weledi ili kuhakikisha malengo yaliyoainishwa katika bajeti ya Serikali yanatekelezwa ipasavyo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika leo Jijini Dodoma, Mhe. Ummy—aliyemwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. William Lukuvi—alisisitiza umuhimu wa watumishi kushirikiana na kuzingatia misingi ya uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Alifafanua kuwa mabaraza ya wafanyakazi yameanzishwa kufuatia Tamko Na. 1 la mwaka 1970 lililotolewa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, likiwa na lengo la kuongeza ufanisi na tija mahali pa kazi.

“Kupitia mabaraza haya, wafanyakazi na waajiri hupata fursa ya kujadili na kubadilishana mawazo kwa manufaa ya taasisi. Ni matumaini yangu kuwa majadiliano yenu yatajikita katika kuimarisha utendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu,” alisema Mhe. Ummy.

Awali, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, alimshukuru Waziri wa Nchi pamoja na Naibu Waziri kwa kushiriki katika kikao hicho muhimu cha Baraza la Wafanyakazi.

Aidha, aliwapongeza viongozi hao kwa ushindi walioupata katika Uchaguzi Mkuu na kwa kuendelea kuaminiwa na Mhe. Rais katika kusimamia sekta hiyo nyeti.

Dkt. Yonazi alieleza kuwa kikao hicho kimewakutanisha Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi ili kujadili bajeti ya ofisi hiyo, ikiwa ni pamoja na kupitia taarifa ya utekelezaji kabla ya kuidhinisha hatua za kuwasilisha bajeti hiyo katika ngazi zinazofuata.



Read More

Monday, March 16, 2026

WANANCHI MKINGA WANUFAIKA NA UWEKEZAJI KATIKA KILIMO CHA MWANI

 


Wananchi wa Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga wanatarajiwa kunufaika zaidi kiuchumi kupitia uwekezaji wa Serikali katika sekta ya kilimo cha mwani, hatua inayolenga kuongeza thamani ya mazao ya bahari na kuboresha maisha ya jamii za pwani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kaushio jipya na mashine mbili za kisasa za kusaga mwani uliofanyika katika Kijiji cha Kichaka Miba, Wilaya ya Mkinga, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Ummy H. Nderiananga, amesema mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuimarisha uchumi wa wananchi wa maeneo ya pwani.

Mradi wa Kuimarisha Usalama wa Bahari unaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), na unatekelezwa na Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP) Tawi la Mwanza kwa ushirikiano na Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga ambapo Lengo lake ni kuimarisha ufuatiliaji na ulinzi wa bahari pamoja na kuongeza thamani ya rasilimali za baharini kwa manufaa ya jamii.

Mhe. Nderiananga amesema kupitia mradi huo, Serikali imenunua boti mbili za doria, kujenga kaushio la kisasa la mwani, kusimika mashine za kusaga mwani na kutoa mafunzo kwa vikundi vya wakulima. Ameongeza kuwa hatua hizo zitaboresha ubora wa mwani, kupanua masoko, kuongeza kipato cha wakulima na kusaidia kuzuia vitendo vya kihalifu baharini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP), Dkt. Guvenail Mkonoko, amesema kabla ya utekelezaji wa mradi huo wataalamu walifanya tathmini iliyobaini changamoto za mbinu duni za kilimo, ukaushaji usio salama na ukosefu wa miundombinu ya kisasa ya uchakataji.

Naye mwakilishi wa wakulima wa mwani, Bi. Mwamvua Bwebwe, Ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kuongeza uzalishaji, kupunguza upotevu wa mazao na kuboresha kipato chao.



Read More

SERIKALI KUIFANYA TANZANIA KITOVU CHA BIASHARA - DKT. YONAZI

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,Uratibu na Wenye Ulemavu Dkt. Jim Yonazi amesema Serikali imefanya juhudi mbalimbali za Kisera, Sheria na Kimkakati ili kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha biashara Afrika Mashariki na Kati.

Dkt. Yonazi aliyasema hayo katika kikao  cha Kikundi Kazi cha Mazingira ya Biashara cha Baraza la Taifa la Biashara TNBC kilichofanyika jijini Dar es salaam.

Alisema Serikali imefanya jitihada za kukuza biashara nchini huku akizitaka sekta binafsi kuendelea kushirikiana na serikali.

“Serikali imefanya juhudi mbalimbali katika uwekezaji nchini ikiwemo mazingira ya ufanyaji wa biashara ya kisera, kisheria na lengo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha biashara Afrika mashariki na kati.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Dkt. Godwill Wanga  alisema kikao hicho kimefanyika ili kujadili maendeleo ya biashara nchini.

Alisema kikao hicho kimejadili vivutio  ambavyo serikali inaweza kufanya uwekezaji zaidi katika sekta ya afya  ili bima ya afya kwa wote itakapoanza iweze kuwa na faida kwa Watanzania.

“Kikao hichi ni muendelezo wa vikao ambavyo tumekuwa tukifanya mara kwa mara katika kujadili maendeleo ya biashara ambapo katika kikao hiki kimejadili kuhusu miundombinu ya mtandao katika  katika nchi yetu.

Aliongeza kuwa :”Tumekubaliana kufanya utafiti kuhusu madhara ya vita katika mashariki ya kati katika uchumi wetu.

 

 

Read More

Friday, March 13, 2026

DKT. YONAZI AONGOZA MKUTANO WA TANZANIA NATIONAL COORDINATING MECHANISM - (TNCM)

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa inayosimamia na kuratibu fedha za Global Fund inayojulikana kama Tanzania National Coordinating Mechanism – (TNCM) ameongoza Kikao cha (TNCM) kilichofanyika katika Ukumbi wa Serengeti, Jengo la FCC, jijini Dar es Salaam.

 Katika mkutano huo, mambo mbalimbali yamejadiliwa ikiwemo maandalizi ya awali ya kuandaa andiko la maombi ya ufadhili wa awamu ya nane ya Mfuko wa Dunia (Global Fund Grant Cycle 8 - GC8). Aidha, Dkt. Yonazi amesisitiza umuhimu wa kuwa na mipango madhubuti na yenye tija ili kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na rasilimali hizo katika mapambano dhidi ya magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu, na Malaria, pamoja na kuimarisha mifumo ya afya kwa ujumla.

Akifunga mkutano huo, Dkt. Yonazi amewahimiza wajumbe na wadau wote kuendeleza ushirikiano na uwazi (Transparency) katika hatua za maandalizi ya GC8, huku akibainisha kuwa ufanisi wa (TNCM) unategemea sauti ya pamoja ya wadau wote wanaowakilishwa.

Mkutano huo uliowahusisha wadau kutoka Serikalini, Sekta Binafsi, Asasi za Kiraia, na Washirika wa Maendeleo, umelenga kujadili masuala mtambuka ya uendeshaji wa taasisi hiyo pamoja na kuweka misingi imara ya upatikanaji wa rasilimali katika sekta ya afya nchini.

Mbali na hayo, katika mkutano huo, wajumbe walimchagua Bw. Godlisten Moshi kuwa Makamu Mwenyekiti mpya wa (TNCM) ili kukamilisha safu ya uongozi na kuongeza ufanisi katika utendaji wa chombo hicho.


Read More

Monday, March 2, 2026

VIJANA WA VYUO VIKUU NA VYUO VYA KATI WASISITIZWA KUENDELEZA MAPAMBANO DHIDI YA VVU NA UKIMWI


Serikali imehamasisha  mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kwa kundi la vijana katika  Chuo cha Uhasibu Arusha  (IAA) na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii ya Tengeru.

Hamasa hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga katika  ziara yake ya  kufuatilia na kutathimini utekelezaji wa Afua za VVU na UKIMWI katika vyuo vya kati na Vyuo Vikuu Jijini Arusha.

Mhe. Nderiananga, ameipongeza Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS)  kwa kazi kubwa ya kusimamia utekelezaji wa Afua za VVU na UKIMWI waliofanya kwenye Taasisi 26 za vyuo vya kati na Vyuo Vikuu nchini, na kuwapongeza vijana wa Vyuo hivyo kwa  kupambana nakuchukua tahadhali na kuzungatia elimu  ya kinga na maambukiz ya Virusi vya UKIMWI waliyoipata kupitia wataalam mbalimbali.

Pia, Mhe. Nderiananga amesisitiza kundi la vijana haswa wa Kiume kuhamasika katika upimaji ili watambue hali za Afya zao na kuhimiza Ufuasi mzuri wa Dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI kwa waathirika wapya, lakini pia amewapongeza Waathirika wote wa VVU  kote nchini kwa matumizi sahihi ya ARV.

Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Mwitikio wa Kitaifa wa UKIMWI kutoka Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Bi Audrey Njelekera, Amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kupitia takwimu zilizopo inamipango madhubuti ya kupunguza na kutokomeza maambukizi ya VVU na UKIMWI nchini kote.

Ameongeza kuwa, takwimu zinaonyesha kuwa kundi la vijana kuanzia miaka 15 hadi 24 ndio linaloathirika zaidi na maambukizi mapya hivyo TACAIDS imeanzisha  Klabu za kijamii kwenye vyuo vya kati na vikuu ili kusaidia  kupunguza unyanyapaa, kuongeza idadi ya wanafunzi kupima na kuongeza ushiriki wa wanafunzi katika mapamabano dhidi ya VVU. Vilevile, kuanzisha programu mbalimbali za kuhamasisha na kuelimisha kupitia mijadala, kuandika machapisho,  vibonzo, picha mjongeo na kampeni za kwenye mitandao ya kijamii.

Nae, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala wa  Chuo cha Uhasibu Arusha, Dkt. Eliakira Nnko amesema kuwa, Chuo kinaendelea kuweka  mipango na mikakati ya utekelezaji wa Afua za UKIMWI mahali pakazi  kwa watumishi na wanafunzi wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI, lengo kuu ni kuhakikisha Wanafunzi na watumishi wanabaki na Afya njema, Kupunguza vifo na kutokomeza unyanyapaa ili kuimarisha utendaji kazi na kuweka  mazingira salama kwa watumishi na  wanafunzi.



Read More

Sunday, March 1, 2026

SERIKALI YA AWAMU YA SITA YASISITIZA UWEZESHWAJI WA WATU WENYE ULEMAVU

 

Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderiananga, amesisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwawezesha kiuchumi watu wenye ulemavu kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri, ikiwemo asilimia 2 inayotengwa mahsusi kwa kundi hilo.

Mhe. Nderiananga ametoa kauli hiyo leo Jijini Arusha alipokutana na watu wenye ulemavu ikiwa ni muendelezo wa Ziara yake iliyoanza Wilaya ya Moshi-Kilimanjaro.

Naibu Waziri Nderiananga, amewapongeza watu wenye ulemavu wa Mkoa wa Arusha kwa nidhamu ya kurejesha mikopo kwa wakati na kuhimiza waliomaliza kurejesha waweze kuomba tena ili kupanua shughuli zao za kiuchumi.

Aidha, ameelekeza kuwa 30% ya manunuzi ya umma kwenye Halmashauri zote za Jiji la Arusha ziende kwenye makundi haya maalum kama vile watu wenye ulemavu, “tunapotengeneza masoko  tutenge maeneo maalumu kwaaajili ya watu wenye ulemavu, na nataka kuona miradi ya watu wenye ulemavu kuwa ni miradi ya kielelezo Nchini’’Mhe. Nderiananga amesema

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Mwinyi Ahmed Mwinyi ameishukuru Serikali ya  Awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kuwakwamua kiuchumi watu wenye ulemavu, na  ameahidi kuandaa hafla kwaajili ya kuwapongeza wanufaika wa Mikopo ya 2% waliofanya vizuri ili iwe kama sehemu ya hamasa na kielelezo kwa wale ambao hawajafanyi vizuri na ambao wanatamani kupata mikopo hiyo.

Awali, Mkurugenzi wa Idara ya watu wenye ulemavu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu Bw. Kizito Wambura amesema Serikali inania thabiti ya kuleta mabadiliko kwa watu wenye ulemavu na  kutatua changamoto zilizobainishwa kupitia mfumo wa kieletroniki wa taarifa za watu wenye ulemavu (PDMIS) ambao tunategemea ufike kwenye maeneo yote ya Tanzania.




Read More