Naibu
Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe.
Ummy Nderiananga, amewahimiza watumishi wa ofisi hiyo kuendelea kufanya kazi
kwa bidii, ufanisi na weledi ili kuhakikisha malengo yaliyoainishwa katika
bajeti ya Serikali yanatekelezwa ipasavyo.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika leo Jijini Dodoma, Mhe.
Ummy—aliyemwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu
na Wenye Ulemavu), Mhe. William Lukuvi—alisisitiza umuhimu wa watumishi
kushirikiana na kuzingatia misingi ya uwajibikaji katika utekelezaji wa
majukumu yao ya kila siku.
Alifafanua
kuwa mabaraza ya wafanyakazi yameanzishwa kufuatia Tamko Na. 1 la mwaka 1970
lililotolewa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, likiwa
na lengo la kuongeza ufanisi na tija mahali pa kazi.
“Kupitia
mabaraza haya, wafanyakazi na waajiri hupata fursa ya kujadili na kubadilishana
mawazo kwa manufaa ya taasisi. Ni matumaini yangu kuwa majadiliano yenu
yatajikita katika kuimarisha utendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu,” alisema Mhe.
Ummy.
Awali,
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu),
Dkt. Jim Yonazi, alimshukuru Waziri wa Nchi pamoja na Naibu Waziri kwa
kushiriki katika kikao hicho muhimu cha Baraza la Wafanyakazi.
Aidha,
aliwapongeza viongozi hao kwa ushindi walioupata katika Uchaguzi Mkuu na kwa
kuendelea kuaminiwa na Mhe. Rais katika kusimamia sekta hiyo nyeti.
Dkt.
Yonazi alieleza kuwa kikao hicho kimewakutanisha Menejimenti ya Ofisi ya Waziri
Mkuu pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi ili kujadili bajeti ya ofisi
hiyo, ikiwa ni pamoja na kupitia taarifa ya utekelezaji kabla ya kuidhinisha
hatua za kuwasilisha bajeti hiyo katika ngazi zinazofuata.


EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.