Serikali imejidhatiti kutatua
changamoto zinazowakumba vijana balehe kwa kuweka mazingira salama na rafiki
kwa vijana kupitia afua mbalimbali zinazowawezesha vijana kufikia malengo yao
na utimilifu wao kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa na Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera ,Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi akifungua mkutano wa wadau
wanaotekeleza Afua za Vijana Balehe nchini (NAIA)kwa niaba ya Katibu Mkuu
Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum unaofanyika
kuanzia 31Oktoba hadi 01 Novemba ,2024 Mkoani Dodoma.
Dkt. Yonazi amefafanua kwamba
Ajenda ya Kitaifa ya kuwekeza katika Afya na Maendeleo ya Vijana Balehe
nchini iliyozinduliwa Aprili
17,2021 ilikua na lengo ni kuharakisha
utekelezaji wa maeneo ya kipaumbele vinavyohusu afya na maendeleo ya vijana
balehe katika Mikoa 13 yenye viashiria visivyoridhisha kuhusu afya na maendeleo
ya vijana balehe nchini.
“Utekelezaji wa Ajenda
umejikita katika nguzo kuu 6 za ambazo ni kuzuia maambukizi ya VVU, kutokomeza
mimba za utotoni, kutokomeza ukatili wa kimwili, kingono na kisaikolojia,
kuboresha hali ya lishe, kuhakikisha wavulana na wasichana wanabaki shule
kukamilisha mzunguko wao wa elimu, na kuwaendeleza vijana katika ujuzi na
ufundi ili wapate fursa ya kujiari na kuajiriwa.” amesema Dkt. Yonazi
Vile vile Dkt. Yonazi ametoa
rai kwa wadau wote wanaohusika na masuala ya vijana balehe kufahamu kwamba ili
kuwa na Taifa imara la leo na baadae ni vema kuwekeza katika kutatua changamoto
za vijana balehe leo ikiwa na maana ya
kutatua changamoto za vijana kwa ajili ya kupata taifa imara.
“Kaulimbiu ya mkutano huu inayosema Utatuzi wa
Changamoto za Vijana balehe kwa taifa imara inachechemua utekelezaji wa Ajenda
hii kwa upana wake kwa kuwa ndiyo pekee yenye uwezo wa kukabiliana na
changamoto hizo za vijana kwa sasa hivyo ni matumaini yangu kuwa kupitia
mkutano huu, mtapata fursa ya kujadili kwa undani kuhusu changamoto zinazohusu
vijana balehe kwa kutumia uzoefu wa utekelezaji wa Ajenda hii kwa kipindi cha
miaka mitatu.” amesema Dkt. Yonazi.
Kwa upande wake Naibu Katibu
Mkuu wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon
Mpanju ametambua juhudi za Mashirika ya
Kimataifa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaliyoanzisha miradi mbalimbali kwa
ajili ya kuhakikisha kwamba Vijana Balehe wanapata huduma rafiki za afya, elimu
ya afya ya uzazi na kupata ujuzi na maarifa ya kuwafanya vijana wamudu maisha
yao.
“Mafanikio haya hayajaja hivi
hivi, bali ni jitihada kubwa mlizofanya ninyi Wadau wa Maendeleo kwa
kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu
Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeunda Wizara hii ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, hivyo nachukua fursa hii kuwapongeza kwa dhati kwa
ushirikiano huo mlioonesha na kufanikisha malengo ya Ajenda hii.” amesema
Wakili Mpanju
Kwa upande wake Naibu Katibu
Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia Dkt. Wilson Mahela amewakumbusha vijana kujitunza kwa kuzingatia mila na tamaduni za
kitanzania zinazofaa na kuepukana kuiga kila wanachokiona kwenye mitandao ya
kijamii.
Kwa niaba ya wadau, Mwakilishi
kutoka Shirika linaloshughulikia masuala ya Watoto (UNICEF), Edgar Lungu
ameishukuru Serikali kwa kuwezesha wadau kuweza kutekeleza afua zao na kuahidi
kuendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuweza kufanikisha kusudio la
Serikali kuwa na taifa lililo na vijana imara na taifa imara.