Sunday, October 13, 2024

TANZANIA YAADHIMISHA SIKU YA MAAFA DUNIANI OKTOBA 13.

Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya Maafa Duniani ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo Oktoba 13 ili kuendelea kukabiliana na kupunguza madhara yatokanayo na maafa nchini,

Akitoa Tamko la maadhimisho hayo katika Uwanja wa CCM Kirumba leo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema maafa usababisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo, ulemavu wa kudumu, upotevu ,uharibifu wa mali, miundombinu na mazingira huku watoto na vijana wamekuwa wakikabiliwa na athari mbaya zaidi ikiwemo kukatizwa masomo, upungufu wa lishe, athari za kiafya, ulinzi na usalama.

Ameeleza kuwa siku hiyo ilianzishwa kwa Azimio namba 64/200 lililopitishwa na Baraza la Umoja wa Mataifa Disemba 21 mwaka 2009 , huadhimishwa kila mwaka, ili kuunganisha juhudi za kuwalinda watoto na vijana dhidi ya athari za majanga ambapo mikakati mbalimbali imewekwa ikiwemo kutoa mafunzo ya kujikinga na maafa,elimu ya hali ya hewa na jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,kuendeleza tafiti kuhusu madhara ya maafa na kutoa taarifa kwa umma ili kuongeza uelewa.

Akirejea taarifa iliyotolewa na serikali kupitia kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi zote kufuatia mwelekeo wa mvua za vuli katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2024 uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) imeonyesha maeneo  mengi ya nchi yanayopata mvua hizo hayatapata mvua za kutosha hivyo wamejiandaa kuzuia, kupunguza madhara, kujiandaa kukabili na hali hiyo sambamba na  kurejesha hali nzuri.

Akitaja hatua sita za kuzingatia kukabiliana na hali hiyo amezitaka Mamlaka husika ziendelee kuhamasisha na kuwezesha matumizi ya mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi pamoja na utunzaji wa chakula cha binadamu na malisho ya mifugo, mamlaka husika ziimarishe utoaji taaluma ya matumizi ya mbinu za kilimo zinazohitaji maji kidogo pia taasisi za umma ikiwemo za elimu, afya na ofisi mbalimbali ziwe mfano wa kuweka mifumo ya kuvuna, kuhifadhi na kutumia maji ya mvua.

Ameongeza kuwa hatua zingine ni kuimarisha mikakati ya kuzuia milipuko ya magonjwa yanayoweza kujitokeza kutokana na upungufu wa upatikanaji wa maji safi na salama,taasisi husika zishirikiane na taasisi za elimu na mashirika ya maendeleo ili kutoa mafunzo kwa wananchi kuhusu jinsi ya kukabiliana na ukame na Wizara yenye dhamana ya elimu na taasisi zake kuhakikisha wanaendelea kuimarisha mitaala ya elimu ili ijumuishe masuala ya usalama shuleni, kupunguza hatari, na uelewa wa majanga na wakihakikisha mafunzo kwa walimu kuhusu mbinu za kufundisha masuala hayo kwa wanafunzi.

 

"Kaulimbiu ya mwaka huu ni "Elimu ni msingi katika kulinda na kuwawezesha vijana kwa mustakabali wa baadae usio na maafa" ili kuungana na kaulimbiu serikali imeendelea kushirikiana na wadau wa kitaifa na kimataifa kuimarisha mifumo ya elimu inayolenga kutoa maarifa na ujuzi wa kupunguza madhara ya maafa kwa watoto na vijana " anaeleza Mhe.Majaliwa

Pia serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya hali ya hewa nchini ikiwemo kufunga miundombinu ya kisasa ya hali hewa, mafunzo kwa watumishi kwa kuzingatia vigezo vya kitaifa na kimataifa, na kuweka mifumo wezeshi ya usambazaji wa taarifa ya hali ya hewa pamoja na kuimarisha mifumo ya uhakiki wa ubora wa huduma huku uwekezaji wa miundombinu unajumuisha ununuzi wa rada za hali ya hewa.

"Ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, Tanzania itakuwa na rada saba ambapo ni kiwango kikubwa cha rada katika nchi za Afrika Mashariki na kati nitumie fursa hii kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan,  kwa uwekezaji mkubwa katika eneo hilo pia kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa makundi maalumu na kuweka mikakati thabiti inayolenga kuwawezesha vijana kiuchumi na kijamii pamoja na kuhakikisha Serikali inatoa elimu kwa wigo mpana na kuwezesha vijana kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto za majanga na kujenga jamii iliyo na ustawi endelevu." anaeleza Mhe.Majaliwa.

Aidha aliwahimiza wananchi wote, taasisi za elimu, na wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwajengea uwezo vijana kupitia elimu itakayowasaidia kujenga stahimilivu dhidi ya majanga kwa sababu elimu ina nafasi kubwa katika kuhakikisha kizazi cha leo kinakuwa na mbinu za kulinda mazingira, kuzuia uharibifu wa maliasili, na kuhakikisha kuwa tunakuwa na mfumo thabiti wa kukabiliana na majanga.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.