Tanzania
imetajwa kuwa nchi ya kwanza barani
Afrika kwa kuwa na Kituo cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga na Tahadhari ya
Mapema (National Emergency Operation and Communication Center Situation Room)
katika Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura nchini Tanzania
ambacho kimeifanya nchi kuwa kinara katika masuala ya menejimenti ya maafa
hususan katika kuzuia, kupunguza kujiandaa na kukabili maafa pindi yanapotokea.
Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu
Dkt. Jim Yonazi ametoa kauli hiyo jijini Windhoek nchini Namibia wakati
akiwasilisha mada katika Kikao cha Tisa
cha Jukwaa la Kanda la Afrika la Kupunguza Madhara ya Maafa na Mkutano wa Nane
wa Ngazi ya Viongozi kuhusu masuala ya kupunguza madhara ya maafa.
Akizungumzia
umuhimu wa kituo hicho, Dkt. Yonazi amesema kituo hicho kimeendelea kutumika kufanya ufuatiliaji wa uwezekano wa kutokea
kwa majanga kwa kutumia mifumo ya kiteknolojia ya kijiografia kwa majanga
yanayotokana na hali ya hewa na haidrolojia kwa kutumia jukwaa la kielektroniki
la MyDEWETRA.
“Mfumo
huu umerahisisha ufuatiliaji wa mwenendo wa janga lililotabiriwa na kufanya
uchambuzi wa kiwango cha madhara kwa jamii, miundombinu na mazingira, kuandaa
taarifa za tahadhari ya mapema ya hatua za kuchukua ili kuzuia, kujiandaa na
kukabili maafa, kuandaa taarifa ya mwenendo wa tukio na kusambaza kwa wadau
mbalimbali kwa ajili ya kusaidia uratibu na utekelezaji wa shughuli za kukabili
na kurejesha hali,” Amesema Dkt. Yonazi
Dkt.
Yonazi amesema kuwa uanzishwaji wa kituo hicho cha ufuatiliaji wa majanga na
tahadhari ya mapema umefanikiwa kutokana na mradi ulioanzishwa na Ofisi ya
Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Madhara ya Maafa katika Kanda ya Afrika na kufadhiliwa na Serikali ya Nchi ya Italia
kupitia Shirika la Maendeleo la Italia (Italian Agency for Development
Cooperation) ambapo Taasisi ya CIMA Research Foundation ya Italia imesadia
kutoa utaalam wa utekelezaji wa shughuli zote.
Ameongeza
kuwa uwepo wa kituo hicho umesaidia sana
Tanzania kuendelea kuwa kinara namba moja katika kukabiliana na maafa kabla hayajaleta madhara.
Kufuatia umuhimu wa kituo hicho, Dkt. Yonazi ametoa wito kwa Nchi wanachama pamoja na mataifa mengine kuja Tanzania kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kwa kuzingatia umuhimu wake.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoshiriki katika Kikao hicho cha siku nne ambacho kinatajia kumalizika Oktoba 24, 2024 ambapo kikao hicho kimefanikiwa kuwakutanisha wadau zaidi ya elfu moja wa maafa kwa nchi za Afrika wakiwemo wataalamu kutoka katika ngazi za kitaifa, Serikali za mitaa, Mashirika ya Umoja wa Kitaifa na Kimataifa, Asasi za Kiraia, sekta binafsi, taasisi za elimu na utafiti na wanahabari.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.