Naibu Waziri Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga ameihimiza
jamii kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya Virusi vya
UKIMWI nchini kwa kuendelea kuzingatia elimu inayotolewa na Tume ya Kudhibiti
UKIMWI Tanzania (TACAIDS) ili kuunga mkono jitihada za Serikali dhidi ya
mapambano hayo na kuyafikia malengo yaliyopo.
Mhe. Nderiananga ametoa wito
huo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa ya utekelezaji wa Mkakati wa Tano wa
Taifa wa kudhibiti UKIMWI wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26 iliyowasilishwa katika
ukumbi wa Bunge, jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo Dkt.
Jerome Kamwele katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI.
Alisema, jamii haina budi
kuendelea kujilinda na kuwalinda wengine kwa kuzingatia ushauri na elimu
inayotolewa ili kuhakikisha hali ya maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI
nchini ipungue na kuyafikia malengo ya kuzifikia sifuri tatu ifikapo 2030.
“Suala la UKIMWI siyo la
TACAIDS na Ofisi ya Waziri Mkuu peke yake, Wizara ya Afya inapambania
kuboresha huduma ya mama na Mtoto, Ofisi ya Rais TAMISEMI ndio imejenga
miundombinu na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania amewekeza Ujenzi hadi ngazi ya Kata kuna vituo Vya afya yote hii ni
kusogeza huduma karibu na wananchi na uwekezaji huu tutaona matunda yake katika
mapambano dhidi ya VVU,”Alieleza Mhe. Nderiananga.
Pia aliishukuru TACAIDS kwa
kufanya kazi nzuri ya kuifikia jamii kwa njia ya elimu huku akiwahimiza
kuendelea kuongeza nguvu kwa vijana kwani ndilo kundi linaloongoza kwa
maambukizi bila kusahau ni kundi muhimu katika uzalishaji na kujiletea
maendeleo.
Awali akiwasilisha taarifa
kuhusu utekelezaji wa Mkakati wa Tano wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI wa mwaka
2021/22 hadi 2025/26 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo Dkt. Jerome Kamwele
alieleza kwamba, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi Oktoba 2024, tume
hiyo imefanikiwa kuratibu kwa ufanisi utekelezaji wa mkakati katika sekta zote
ndani ya Serikali na sekta binafsi, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Taasisi za
dini na wadau mbalimbali.
“Tume pia tumefanikiwa
kupunguza maambukizi mapya ya VVU kutoka maambukizi 61,281 mwaka 2020 hadi
maambukizi 60,000 mwaka 2023, kupungua kwa vifo vitokanavyo na UKIMWI kutoka
vifo 32,639 mwaka 2020 hadi vifo 25,000 mwaka 2023 na kupungua kwa kiwango cha
ubaguzi na unyanyapaa unaogokana na VVU kutokana na elimu ambayo imeendelea
kutolewa kwa jamii na wadau,” alieleza Dkt. Kamwele.
Alifafanua kwamba mafanikio
mengine ni pamoja na kufikia lengo la utekelezaji wa shabaha za Kimataifa
95-95-95 zinazohusu kupima na kutibu ifikapo 2026 ambapo asilimia 98 ya watu
wanaoishi na virusi vya UKIMWI (WAVIU) wameanza tiba huku utafiti
ukionyesha mwelekeo mzuri wa kufikia shabaha ya asilimia 95 ya tatu inayohusu
kufubaza Virusi vya UKIMWI na kusisitiza ushirikiano wa pamoja kufikia asilimia
95 ya kwanza inayohusu watu wote wanaoishi na VVU kupima na kujua hali zao.
“Serikali inaendelea kuweka
mkazo katika utekelezaji wa afua zinazolenga kupunguza kasi ya maambukizi mapya
ya VVU hasa makundi maalum, kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha watu kupima
kujua hali zao, kuongeza nguvu kuyafikia makundi maaalum hasa vijana, wanawake,
wanaume, Watoto, watu wenye ulemavu na wanaoishi katika mazingira hatarishi,”
alifafanua.
Aidha Makamu Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Bernadeta Mushashu
aliipongeza TACAIDS kwa jitihada zake ikishirikiana na wadau kuhakikisha
wananchi wanafanya shughuli zao za kiuchumi wakiwa katika hali njema ya kiafya.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.