SERIKALI imedhamiria kuendelea
kushirikiana na wadau katika kutekeleza
dhana ya Afya Moja nchini hasa maeneo ya kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na
milipuko ya magonjwa na hatari nyingine za afya zinazohitaji ushiriki wa sekta
zaidi ya moja na taaluma mbalimbali.
Akizungumza leo Jumatano
Novemba 6, 2024 wakati akifunga Mkutano wa Afya Moja uliofanyika katika Kituo
cha Mikutano cha Kimataifa wa Arusha (AICC) Jijini Arusha, Katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi
amesema lengo la Dhana ya Afya Moja ni kupanua na kuimarisha ushirikiano baina
ya sekta pamoja na taaluma mbalimbali katika hatua zote za kuzuia, kujiandaa na
kukabiliana na milipuko ya magonjwa na hatari nyingine za afya zinazohitaji
ushiriki wa sekta zaidi ya moja na taaluma mbalimbali katika kutekeleaji wa Afua hizo.
“Ni wakati sahihi kuendelea
kushirikiana kwa pamoja na wadau wengine ikiwemo jamii, kwa kuongozwa na wizara
za msingi ambazo ni Afya ya Binadamu, Wanyama (Mifugo na Wanyama Pori),
Mazingira na Kilimo katika ngazi zote ili kuhakikisha nguvu ya pamoja
inatuvusha hapa tulipo na kuendelea kuipa nguvu dhana ya afya moja,” alisema
Dkt. Yonazi
Aliongezea kuwa, Dawati la
Uratibu wa Afya Moja lipo chini ya Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya
Waziri Mkuu ambayo utekelezaji wa majukumu yake unaongozwa na Sera ya Taifa ya
Usimamizi wa Maafa ya Mwaka 2004 inayoweka umuhimu katika usalama wa maisha ya
watu na mali zao kwa kupunguza athari za kiuchumi na kijamii katika kuipa nguvu
Sera ya Usimamizi wa Maafa ya mwaka 2004, Serikali ilitunga Sheria ya Usimamizi
ya Maafa Namba 7 ya Mwaka 2015 inayosimamia utekelezaji wa shughuli za idara.
Dkt. Yonazi alizikumbusha
sekta zote kuendelea kushirikiana katika kutatua changamoto ya magonjwa ya
zoonotiki, usalama wa chakula, mabadiliko ya tabia nchi na usugu wa dawa dhidi
ya vimelea vya magonjwa.
Aidha ameyataja maeneo ya
kuimarisha ushirikiano kwa sekta pamoja na wadau wote wanaotekeleza Dhana hiyo
ikiwemo ya kuongeza ushiriki wa sekta ya mazingira na sekta ya kilimo katika
utekelezaji wa dhana ya Afya Moja, kuandaa miongozo ya namna sekta
zitakavyobadilishana taarifa za magonjwa na matukio yenye athari kwa binadamu,
wanyama na mazingira chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na
kuhuisha orodha ya magonjwa ya kizoonotoki na kutekeleza miongozo na mipango
mbalimbali ya kudhibiti magonjwa hayo.
Maeneo mengine ni kuendelea
kuzijengea uwezo Kamati za Usimamizi wa Maafa kuhusu uratibu na utekelezaji wa
dhana ya Afya Moja, kuendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Afya Moja
(2022-2027) katika maeneo yote pamoja na kuendelea kushiriki katika tafiti na
uchunguzi wa pamoja kuhusu milipuko ya magonjwa na matukio mbalimbali nchini.
Kwa hatua nyingine Dkt. Yonazi
amepongeza washiriki wote ikiwemo wawasilisha mada kwa siku zote na kueleza
kuwa zitaendelea kuongeza tija katika miradi mbalimbali nchini ikiwemo ya
kichaa cha mbwa, kimeta na homa ya bonde
la ufa.
“Mmetoa michango mingi na
mizuri hakika itatufaa katika utekelezaji wa dhana ya Afya Moja na kuboresha
afya za binadamu, wanyama, mimea na mifumo yaikolojia ,”alieleza Dkt. Yonazi.
Aidha amewashukuru wadau
waliofanikisha kufanyika kwa mkutano huo muhimu huku akiwasihii kuendelea
kuimarisha mashirikiano yaliyopo ili kuendelea kuipa nguvu Dhana ya Afya Moja
na kuyafikia malengo yake.
“Kipekee niwashukuru COHESA,
FAO, USAID na One Health Society kwa kusaidia na kufanikisha mkutano huu.
Aidha, niwapongeze USAID kupitia mradi wao wa Breakthrough Action, MDH, Chuo
cha Nelson Mandela kupitia mradi wa CEREBLAM, AFROHUN, KCMC/KCRI na Chuo Kikuu
cha Dodoma (UDOM) kwa kushiriki kikamilifu katika maonesho ya Mkutano huu,”
Alisisitiza
Kwa upande wake Katibu Tawala
Mkoa wa Arusha Ndugu Missaile Musa ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa
kuratibu Mkutano huo wenye tija kwa Mkoa na Taifa kwa ujumla huku akisema
mkutano huo umefanikiwa kukutanisha wadau na kujengewa uwezo pamoja na kuweka
mikakati itakayowezesha kuyafikia malengo yaliyokusudiwa.
“Malengo na mkutano huu
yamefanikiwa sana, kama mkoa tunaamini kuwa yote yaliyowasilishwa hapa
yanamchango katika kuimarisha afya zetu pamoja na za wanyama, tutaendelea kuwa
salama endapo haya tutayapa kipaumbele hivyo tuendelee kuwalinda na kujilinda
kuwa na jamii salama,”alisema Missaile
Katika Mkutano huo uliofanyika
kwa muda wa siku tatu kuanzia Novemba
4 hadi 6, 2024 na kuhudhuriwa na zaidi
ya washiriki 320 kutoka ndani na nje ya nchi ikiwemo; Kenya, Uganda, Zimbabwe,
Namibia, Rwanda, Nigeria, Ghana, Sudani ya Kusini, Cameroon, Senegal, Scotland
na Ujerumani umekuwa ni muhimu sana.