Thursday, January 29, 2026

WANANCHI KUNUFAIKA NA MRADI WA RAMANI ZETU, SAUTI ZETU


 Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu imezindua mradi wezeshi wa “Ramani Zetu, Sauti Zetu”, unaolenga kuwajengea uwezo Wananchi wa Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Pwani katika kukabiliana na Majanga.

Akizungumza katika Uzinduzi huo uliofanyika leo Jijini Morogoro Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni na Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu) Kanali Selestine Masalamado amesema, mradi huo umekuja wakati mufaka ambao jitihada kubwa zikiwa zinaendelea za kuzuia majanga ya asili maeneo mbalimbali ya nchi.

Aidha, ameeleza kuwa “tunahitaji uwepo wa data sahihi za wakati bila kusahau ushirikishwaji wa moja kwa moja wa jamii katika kuendelea kukabiliana na majanga ya asili na athari zake”

“Mpango huu unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inayolenga kujenga taifa lenye jamii imara yenye uwezo wa kutumia maarifa ya teknolojia katika kufanya maamuzi ya maendeleo” aliongeza Kanali Masalamado.

Naye, Mkurugenzi wa Taasisi ya OpenMap Development Tanzania (OMDTZ) Bw. Innocent Maholi, amesema Mradi huo unalenga kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema, ikiwa ni pamoja maandalizi na usimamizi wa maafa kwa kutumia teknolojia na ushiriki wa wananchi katika ukusanyaji wa taarifa muhimu za maeneo yao.

“serikali itaendelea kuuunga mkono juhudi hatua za usimamizi madhubuti wa maafa ambazo sehemu muhimu ya safari ya kuelekea maendeleo endelevu na uchumi imara wa wananchi,” alibainisha

Read More

Tuesday, January 27, 2026

DKT. KILABUKO AZINDUA NYARAKA ZA USIMAMIZI WA MAAFA NKASI


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Dkt. James Kilabuko amezindua nyaraka za usimamizi wa maafa katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa huku akisisistiza nyaraka hizo kutekelezwa kwa vitendo.

Dkt. Kilabuko amesema hayo wakati wa uzinduzi huo na kusema kuwa, hatua hiyo ni mwanzo wa kuanza kazi rasmi endapo kutatokea janga lolote, na kutoa wito kwa idara, vitengo na taasisi ngazi ya wilaya kuzingatia nyaraka hizo kwa kuhakikisha zinakuwa chachu ya kuongeza ushirikishwaji wa jamii na wadau katika masuala ya menejimenti ya maafa.

Ameongeza kuwa, hatua hiyo itasaidia kujenga uelewa wa jamii kuhusu masuala ya usimamizi wa maafa, kuimarisha mfumo wa utoaji wa tahadhari awali, kujenga uwezo wa kuzuia, kupunguza madhara na kujiandaa na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea.

Dkt. Kilabuko alifafanua kuwa, nyaraka hizo zimekuja wakati sahihi kwa  kuzingatia kuwa, Wilaya imekuwa ikikabiliwa na maafa yanayosababishwa na majanga hasa ya upepo mkali, magonjwa ya mlipuko kwa binadamu na wanyama, mafuriko pamoja na mgongano wa wanyamapori na binadamu ambayo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara.

“Nimeelezwa kuwa matokeo ya tathmini ya maafa iliyofanyika katika Halmashauri ya Nkasi mwezi Januari, 2026 yalionesha kuwa yapo majanga mengine ambayo yamekuwa yakijitokeza japo hayajaleta athari kubwa ikiwemo wadudu waharibifu wa mazao, ajali za barabarani, moto, ajali za majini, tetemeko la ardhi, radi pamoja na maporomoko ya ardhi.Natambua kuwa Wilaya imekuwa ikikabiliwa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu,nitumie fursa hii kuwapongeza kwa jitihada mnazoendelea nazo katika kukabiliana na ugonjwa huo,”Alisema Dkt. Kilabuko

Kwa hatua nyingine, Ameshukuru Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) kwa ufadhili ambao umewezesha kuchangia jitihada za Serikali katika kuandaa Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa pamoja na Mkakati wa Kupunguza Vihatarishi vya Maafa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.

Naye Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Brigedia Generali Hosea Ndagala amesema Idara hiyo imekuwa ikichukua hatua za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Aliongezea kuwa,Serikali kwa kutambua hilo na katika kuhakikisha nchi inakuwa stahimilivu dhidi ya maafa, imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali. Jitihada hizo ni pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa kushughulikia masuala ya maafa kwa kutunga Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004, Toleo la Mwaka 2025 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa Sura ya 242 ambayo imeweka mfumo mzuri wa usimamizi wa maafa kutoka ngazi ya Taifa hadi Kijiji/Mtaa.

“Ni muhimu kwa Halmashauri kuendelea kutenga fedha katika bajeti juu ya utekelezaji wa Mpango huu uliozinduliwa leo na kuendelea kutoa elimu kuhusu namna bora ya wananchi kuendelea kuchua hatua za awali kwa kuzingatia maafa ni suala mtambuka na linaanza na mtu mmoja,” alisisitiza

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mheshimiwa Peter Lijualikali ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu na UNICEF kwa kazi nzuri ya uandaaji wa nyaraka za usimamizi wa maafa na kutoa elimu juu ya masuala ya menejimenti ya maafa kwa Wilaya ya Nkasi na kuahidi kuzifanyia kazi nyaraka hizo.

“Wilaya imepata kitu chema kitakachotufaa, nasi tunaahidi kuzitumia kama miongozo sahihi ya kuleta matokeo kwa kuzingatia Serikali imeweka fedha katika kuhakikisha mipango inaleta matokeo yaliyokusudiwa, hivyo tusiwe nyuma, tufanyie kazi kwa tija ya Halmashauri nzima,” alisema Lijualikali

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Nkasi Mheshimiwa Richard Leonard Masai akitoa Salam ameshukuru uratibu mzuri wa uandaaji wa nyaraka hizo na kutoa rai kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhali za awali na kuzingatia taarifa za tahadhali zinazotolewa na wataalamu ili kuendeala kuwa na jamii iliyo salama na yenye kujiletea maendeleo yake.

 

Read More

Friday, January 23, 2026

KAMATI YAPONGEZA JUHUDI ZA SERIKALI UBORESHWAJI HUDUMA ZA AFYA

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Dkt. Lembulung Lukumay ameipongeza Serikali kwa kuwekeza fedha katika ujenzi wa miundombinu ya sekta ya afya pamoja na uboreshaji wa upatikanaji vifaa tiba.

Dkt. Lukumay ametoa pongezi hizo leo Jijini Dodoma wakati akipokea taarifa ya Muundo na Majukumu ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) iliyo chini Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu.

 “Serikali imeongeza idadi ya madaktari wabobezi katika jitihada za kuboresha huduma za afya ikiwemo kuweka utaratibu mzuri wa kuendelea kuwezesha afua za UKIMWI kwa kutegemea fedha zetu za ndani ili kuendeleza upatikanaji wa dawa,” alieleza Dkt. Lukumay.

 Aidha, amebainisha kuwa, wananchi hawana budi kuelezwa juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais, Dkt, Samia Suluhu Hassan katika uimarishaji wa huduma za afya, katika ngazi ya Zahanati, Vituo vya afya, hospitali za Wilaya na hospitali za Mikoa.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. William Lukuvi ameahidi kuendelea kushirikiana na kamati kwa ukaribu  na kufanyia kazi kwa ukamilifu ushauri na maelekezo yatakayotolewa na kamati




Read More

Thursday, January 22, 2026

NDUMBARO AIPONGEZA OFISI YA WAZIRI MKUU KWA UTENDAJI BORA


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Damas Daniel Ndumbaro, ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) pamoja na taasisi zake kwa utendaji mzuri katika kuratibu shughuli za Serikali zinazogusa maisha ya wananchi.

Pongezi hizo zimetolewa leo jijini Dodoma wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Ofisi ya Waziri Mkuu mbele ya Kamati hiyo ya Bunge.

Mhe. Ndumbaro amesema maeneo ya uratibu wa maafa na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi yanahitaji kuendelea kupewa kipaumbele ili Serikali iendelee kuwafikia wananchi kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Ummy Nderiananga, amesema Serikali imetenga fungu maalum la fedha kwa ajili ya afua za UKIMWI pamoja na kushughulikia masuala ya maafa kila mwaka wa bajeti, hatua itakayohakikisha utekelezaji endelevu wa majukumu hayo nchini.



Read More

Wednesday, January 21, 2026

SERIKALI KUSHIRIKIANA NA VYUO VIKUU KUIMARISHA UWAJIBIKAJI KATIKA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA UMMA


 

Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, kupitia Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Serikali, imesaini Hati za Mashirikiano (MoU) na Vyuo Vikuu vinne ambavyo ni Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha na Taasisi ya Uhasibu Tanzania kwa lengo la kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini unaotumia ushahidi katika kupanga na kutekeleza sera, mipango, programu na miradi ya maendeleo. 

Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika leo  jijini Dodoma, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (SBUU) Dkt. Jim Yonazi amesema kupitia mashirikiano hayo, Serikali na Vyuo Vikuu vitashirikiana katika kuimarisha uwezo wa wataalamu wa ufuatiliaji na tathmini, kufanya tathmini za pamoja za miradi ya maendeleo, kuendeleza tafiti bunifu na kuhakikisha maarifa yanayozalishwa vyuoni yanatumika kuboresha utendaji wa Serikali.

"Mafanikio ya MoU hizo yatapimwa kwa utekelezaji wake, kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yenye msisitizo wa matokeo yanayopimika na manufaa halisi kwa wananchi" ameongeza Dkt. Yonazi.

Awali, akizungumza kwa niaba ya Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu vilivyoshiriki katika hafla hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Prof. Lughano Kusiluka amesema kuwa, Ufuatiliaji na Tathmini ni eneo muhimu kwa ajili ya maendeleo ya taifa na Vyuo Vikuu vinaahidi kushirikiana na serikali katika kuhakikisha tunafanya vizuri katika eneo hilo ili nchi zinazotuzunguka wajifunze kutoka Tanzania.

Aidha, Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Serikali Bi. Sakina Mwinyimkuu amesema kuwa ushirikiano huo wenye nia ya pamoja una malengo ya kuongeza nguvu ya kusaidia taifa na kujenga tamaduni ya uwajibikaji.

Read More

Tuesday, January 20, 2026

MHE. LIJUALIKALI ATOA NENO KWA KAMATI ELEKEZI YA WILAYA YA USIMAMIZI WA MAAFA

 


Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mheshimiwa Peter Lijualikali amepongeza Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu kwa namna ilivyoratibu zoezi la uandaaji wa Rasimu za Nyaraka za Usimamizi wa Maafa kwa Wilaya yake huku akiwasihi wajumbe wa kamati kuzitumia kama ilivyokusudiwa mara baada ya uzinduzi utakaofanyika hivi karibuni.

Ameyasema hayo leo wakati wa kikao cha Kamati Elekezi ya Wilaya ya Usimamizi wa Maafa ikihudhuriwa na timu ya wajumbe hao wakiongozwa na mkuu wa Wilaya huyo ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati.

“Kipekee nawapongea Ofisi ya Waziri Mkuu na UNICEF kwa kuona umuhimu wa kuja katika Wilaya yetu ya Nkasi, na tutahakikisha kile mlichokifanya hapa Nkasi kinaleta matokeo chanya hasa kwa elimu tuliyoipata ya masuala ya usimamizi wa maafa hususani katika kuzuia na kujiandaa ili kusiwe na athari kubwa endapo majanga yatatokea,” alieleza Mhe. Lijualikali.

Naye Mratibu wa Maafa Mkoa wa Rukwa Bi. Aziza Kalyatila amesema ipo haja ya kuendelea kupewa elimu zaidi ya masuala ya usimamizi wa maafa kwani itasaidia katika kuwajengea uwezo wa kuzuia, kujiandaa, kukabili, na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea.

Kikao hicho kimeandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) pamoja na timu ya wataalamu kutoka ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kikilenga kuwapitisha katika nyaraka zilizoandaliwa kwa ajili ya matumizi ya Halmashauri ambazo ni Tathmini ya Vihatarishi vya Majanga, Uwezekano wa Kuathirika na Uwezo wa Kukabiliana na Majanga, rasimu ya Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa pamoja na rasimu ya Mkakati wa kupunguza vihatarishi vya maafa.

 

Read More

Monday, January 19, 2026

NKASI YAJENGEWA UWEZO MASUALA YA MENEJIMENTI YA MAAFA


Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu imewajengea uwezo wajumbe wa Kamati ya Wataalamu ya Usimamizi wa Maafa ya Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa ili kuhakikisha jamii inakuwa stahimilivu wakati wa majanga.

Elimu hiyo imetolewa na timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa kikao cha kupitia Rasimu za Nyaraka za Usimamizi wa Maafa za Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kwa Kamati za Usimamizi wa Maafa wilayani humu ikiongozwa na  na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo.

Kikao hicho kimeandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na timu ya wataalamu kutoka ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kikilenga kuwapitisha katika nyaraka zilizoandaliwa kwa ajili ya matumizi ya Halmashauri ambazo ni Tathmini ya Vihatarishi vya Majanga, Uwezekano wa Kuathirika na Uwezo wa Kukabiliana na Majanga, Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa pamoja na Mkakati wa kupunguza vihatarishi vya maafa.

Akitoa neno la shukran mara baada ya kikao hicho Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Bw. Eliud Njogellah amepongeza kazi iliyofanyika na timu ya kuandaa nyaraka hizo huku akieleza kuwa zimekuja kwa wakati sahihi ambapo Halmashauri imekuwa ikikumbwa na majanga na maafa mbalimbali hivyo zitatumika kwa uzito wake na tija iliyokusudiwa.

Read More

WAJUMBE BARAZA KUU JUMUIYA YA WAZAZI CCM TAIFA WAIPONGEZA SERIKALI KWA UJENZI WA MJI WA SERIKALI MTUMBA

 


Wajumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, wakiongozwa na Mwenyekiti Fadhili Maganya, wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa ujenzi wa mji wa Serikali, Mtumba.

Bw. Maganya ametoa pongezi hizo alipoongoza ujumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa kutembelea Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

"Tunaona namna Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais na Mwenyekiti wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan inavyotekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa ujenzi wa Mji huu wa kisasa ambao sio tuu watu kuja kufanya kazi bali hata kukuza  utalii wa ndani" amesema Bw. Maganya.

Aidha, Bw. Maganya ameongeza kuwa, ujenzi wa barabara, majengo ya kisasa na matumizi ya samani zilizotengenezwa ndani ya nchi vinaonesha thamani ya fedha zinazotolewa na Serikali na kuahidi kushirikiana na Serikali katika upandaji wa miti ili kuwa sehemu ya kutimiza malengo ya utunzaji wa mazingira katika mji huo.

 Awali, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Mheshimiwa Ummy Nderiananga amesema, Ofisi ya Waziri Mkuu (SBUU) itaendelea na uratibu wa ujenzi wa mji wa Serikali kwa kiwango kinachohitajika na amewashukuru Jumuiya ya Wazazi Taifa kwa  kutenga muda wa kutembelea Mji wa Serikali ili kujionea kwa macho utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akiwakaribisha Wajumbe hao, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Paul Sangawe amesema, Ofisi ya Waziri Mkuu inapokea wageni mbalimbali wanaotaka kutembelea Mji wa Serikali Mtumba na kuufanya Mji huo kuwa kivutio cha utalii.

Read More