Thursday, October 31, 2024

"UTATUZI WA CHANGAMOTO ZA VIJANA BALEHE NI MSINGI WA TAIFA BORA"-DKT YONAZI.

 


Serikali imejidhatiti kutatua changamoto zinazowakumba vijana balehe kwa kuweka mazingira salama na rafiki kwa vijana kupitia afua mbalimbali zinazowawezesha vijana kufikia malengo yao na utimilifu wao kwa ujumla.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera ,Bunge na Uratibu Dkt.  Jim Yonazi akifungua mkutano wa wadau wanaotekeleza Afua za Vijana Balehe nchini (NAIA)kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum unaofanyika kuanzia 31Oktoba hadi 01 Novemba ,2024 Mkoani Dodoma.

Dkt. Yonazi amefafanua kwamba Ajenda ya Kitaifa ya kuwekeza katika Afya na Maendeleo ya Vijana Balehe nchini  iliyozinduliwa Aprili 17,2021  ilikua na lengo ni kuharakisha utekelezaji wa maeneo ya kipaumbele vinavyohusu afya na maendeleo ya vijana balehe katika Mikoa 13 yenye viashiria visivyoridhisha kuhusu afya na maendeleo ya vijana balehe nchini.

“Utekelezaji wa Ajenda umejikita katika nguzo kuu 6 za ambazo ni kuzuia maambukizi ya VVU, kutokomeza mimba za utotoni, kutokomeza ukatili wa kimwili, kingono na kisaikolojia, kuboresha hali ya lishe, kuhakikisha wavulana na wasichana wanabaki shule kukamilisha mzunguko wao wa elimu, na kuwaendeleza vijana katika ujuzi na ufundi ili wapate fursa ya kujiari na kuajiriwa.” amesema Dkt. Yonazi

Vile vile Dkt. Yonazi ametoa rai kwa wadau wote wanaohusika na masuala ya vijana balehe kufahamu kwamba ili kuwa na Taifa imara la leo na baadae ni vema kuwekeza katika kutatua changamoto za vijana balehe leo ikiwa na maana  ya kutatua changamoto za vijana kwa ajili ya kupata taifa imara.

“Kaulimbiu  ya mkutano huu inayosema Utatuzi wa Changamoto za Vijana balehe kwa taifa imara inachechemua utekelezaji wa Ajenda hii kwa upana wake kwa kuwa ndiyo pekee yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto hizo za vijana kwa sasa hivyo ni matumaini yangu kuwa kupitia mkutano huu, mtapata fursa ya kujadili kwa undani kuhusu changamoto zinazohusu vijana balehe kwa kutumia uzoefu wa utekelezaji wa Ajenda hii kwa kipindi cha miaka mitatu.” amesema Dkt. Yonazi.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju ametambua juhudi za  Mashirika ya Kimataifa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaliyoanzisha miradi mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Vijana Balehe wanapata huduma rafiki za afya, elimu ya afya ya uzazi na kupata ujuzi na maarifa ya kuwafanya vijana wamudu maisha yao.

“Mafanikio haya hayajaja hivi hivi, bali ni jitihada kubwa mlizofanya ninyi Wadau wa Maendeleo kwa kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeunda Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, hivyo nachukua  fursa hii kuwapongeza kwa dhati kwa ushirikiano huo mlioonesha na kufanikisha malengo ya Ajenda hii.” amesema Wakili Mpanju

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu  Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Wilson Mahela amewakumbusha vijana  kujitunza kwa kuzingatia mila na tamaduni za kitanzania zinazofaa na kuepukana kuiga kila wanachokiona kwenye mitandao ya kijamii.

Kwa niaba ya wadau, Mwakilishi kutoka Shirika linaloshughulikia masuala ya Watoto (UNICEF), Edgar Lungu ameishukuru Serikali kwa kuwezesha wadau kuweza kutekeleza afua zao na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuweza kufanikisha kusudio la Serikali kuwa na taifa lililo na vijana imara na taifa imara.

 


Friday, October 25, 2024

TANZANIA YAPIGIWA MFANO, KUKABILI MAAFA, MATUMIZI SAFI YA NISHATI YA KUPIKIA YATAJWA

Serikali ya Tanzania imeendelea kuonesha umahiri wake katika masuala ya menejimenti ya maafa nchini kwa kuzingatia mifumo sahihi ya kukabiliana na maafa na matumizi ya teknolojia ya kisasa pamoja na miongozo, kanuni na sheria mbalimbali zinazoongoza katika uratibu wa maafa hayo.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa Ummy Nderiananga wakati akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Nane wa Ngazi ya Viongozi  kuhusu masuala ya kupunguza athari za maafa pamoja na Kikao cha Tisa cha Jukwaa la Kanda la Afrika la Kupunguza Athari za Maafa na vilivyofanyika jijini Windhoek nchini Namibia   kwa muda wa  siku nne kuanzia Oktoba 21 hadi 24 2024.

Mhe.Nderiananga ameeleza kuwa, uwekezaji mkubwa umefanywa na Serikali ya Tanzania hususan katika kuhakikisha teknolojia inavusha Taifa katika kukabili maafa ambapo Serikali ilianzisha Kituo cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga  katika Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura nchini Tanzania ambacho kimeifanya nchi  kuwa mahiri katika masuala ya menejimenti ya maafa hususan katika kuzuia, kupunguza kujiandaa na kukabili maafa pindi yanapotokea.

Katika hatua nyingine Mhe.Nderiananga amezungumzia kuhusu mkakati wa miaka kumi wa Nishati safi ya Kupikia ambao utekelezaji wake umeanza mwaka 2024 hadi 2034,  ameeleza kuwa unalenga kuhifadhi mazingira, kulinda afya kwa kuzuia matumizi ya kuni na mkaa ili kuepuka athari za mabadiliko ya tabia nchi.

“Suala ya mabadiliko ya tabia nchi linaathiriwa na ukataji wa miti inayopelekea uharibifu mkubwa wa mazingira na kuchagiza ukosefu wa mvua za kutosha, uwepo wa ukame unaoathiri uzalishaji wa chakula, tunampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuzindua mkakati huo,”alisema

Amesema moja ya mikakati ambayo Tanzania imejiwekea ni kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.

"....Kama nchi tumejipanga kuhakikisha Taasisi za Serikali na Mashirika binafsi yanawekeza ipasavyo katika matumizi ya nishati safi kwa maslahi mapana ya mazingira safi na salama, Afya zetu na Afrika kwa ujumla " amesisitiza Mhe.Nderiananga

Kufuatia hatua huyo Mhe.Nderianga ametoa  wito kwa Mataifa mbalimbali duniani kufuata nyayo za Tanzania kwa kuhakikisha zinaweka mikakati madhubuti ya muda mfupi na mrefu ya Nishati safi ya Kupikia ili kuifanya Dunia kuwe mahali safi na salama pa kuishi.

Awali akifungua mkutano huo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Kazi na Uchukuzi Nchini Namibia Mhe. John Mutorwa amesema mikutano hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa ambapo awamu hii imefanyika nchini Namibia na kuwakutanisha wadau zaidi ya elfu moja wa  maafa kwa nchi za Afrika  wakiwemo wataalamu kutoka  katika ngazi za kitaifa, Serikali za mitaa, Mashirika ya Umoja wa Kitaifa na Kimataifa, Asasi za Kiraia, sekta binafsi, taasisi za elimu na utafiti na wanahabari, na hii imetajwa kuwa ni mafanikio makubwa kwa bara la Afrika.

“Tunashukuru kwa namna nchi zilivyojitokeza kushiriki mikutano hii muhimu katika kuhakikisha masuala ya maafa yanakabiliwa na kuwa na Afrika stahimilivu katika maafa, tunawashukuru sana Mawaziri mlioweza kushiriki mikutano hii, nasi tumepata heshima kama nchi, na tunaahidi kuendelea kuimarisha mashirikiano yetu kama Bara la Afrika,”alisema Mhe. Mutorwa

Aidha, alitoa rai kwa kila nchi kuona umuhimu wa kujipanga kukabili maafa bila kujali utofauti na hali za Mataifa ya Afrika, lengo kuyafikia na kuyaishi malengo na kuwa tayari kusimamia masuala haya.

“Maafa si jambo la kulifurahia, yanapaswa kupewa mwitikio mkubwa na mikakati yenye mashiko na inayotekelezeka lengo ni kulinda jamii zetu na kuweza kuifanya Dunia sehemu salama ya kuishi,hili litafanikiwa tukiendelea kushikamana kwa umoja wetu wa Afrika” alisisitiza




 

Thursday, October 24, 2024

SERIKALI YAPONGEZWA KUENDELEA KUONGEZA AFUA ZA UKIMWI

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Elibariki Emmmanuel Kingu ameipongeza Serikali na wadau wa maendeleo wanaoshirikiana na Serikali katika kutoa afua mbalimbali kukabiliana na ugonjwa wa Virusi vya UKIMWI.

Kauli hiyo ameitoa katika Ukumbi wa Bunge, Jijini Dodoma wakati kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI walipokutana mashirika yasiyo ya kiserikali ya Medical Reseach International(HJMFRI), International Centre for AIDS Care and Treatment Progaram (ICAP) na Management and Development for Health (MDH) yanayofanya kazi chini ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) katika semina ya kujengea uwezo kamati.

Ameeleza umuhimu wa Semina hiyo katika kutambua wadau wanaoshirikiana na Serikali kwa karibu na kuishauri serikali katika kuongeza muitikio wa kisiasa wa kuendelea kushawishi wadau hao kuwa na mkakati  stahimilivu katika kusaidia afua za UKIMWI.



Wednesday, October 23, 2024

DKT. YONAZI ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI NAMIBIA

 


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ametembelea Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Namibia, ikiwa ni ziara yake ya kikazi nchini humo, lengo ni kushiriki Kikao cha Tisa cha Jukwaa la Kanda la Afrika la Kupunguza Athari za Maafa na Mkutano wa Nane wa Ngazi ya Viongozi (High Level Meeting) kuhusu masuala ya kupunguza athari za maafa vinavyofanyika Windhoek nchini Namibia.

Dkt. Yonazi ameambatana na Timu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwemo Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi hiyo Brig. Jenerali Hosea Ndagala, Mkurugenzi wa Tathmini na Ufuatiliaji Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Charles Msangi, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Bw. January Kitunsi pamoja na Afisa Habari wa Ofisi hiyo Bi. Nyamagory Kitwara.

Aidha, katika mazungumzo na mwenyeji wake ambaye ni Afisa Mambo ya Nje Mkuu na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Namibia Bw. Elias Tamba ameeleza kuwa, nchi ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Naminia katika masuala mbalimbali kwa kuzingatia urafiki uliopo baina ya Mataifa hayo mawili toka kipindi ya Uhuru wa Namibia ambapo Tanzania inakumbukwa kwa mchango wake.



TANZANIA YANG’ARA KIMATAIFA KWA KUWA NA KITUO CHA UFUATILIAJI MAJANGA, WADAU WA MAAFA WAVUTIWA



Tanzania imetajwa kuwa  nchi ya kwanza barani Afrika kwa kuwa na Kituo cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga na Tahadhari ya Mapema (National Emergency Operation and Communication Center Situation Room) katika Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura nchini Tanzania ambacho kimeifanya nchi  kuwa kinara  katika masuala ya menejimenti ya maafa hususan katika kuzuia, kupunguza kujiandaa na kukabili maafa pindi yanapotokea.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ametoa kauli hiyo jijini Windhoek nchini Namibia wakati akiwasilisha  mada katika Kikao cha Tisa cha Jukwaa la Kanda la Afrika la Kupunguza Madhara ya Maafa na Mkutano wa Nane wa Ngazi ya Viongozi kuhusu masuala ya kupunguza madhara ya maafa.

Akizungumzia umuhimu wa kituo hicho, Dkt. Yonazi amesema kituo hicho  kimeendelea kutumika  kufanya ufuatiliaji wa uwezekano wa kutokea kwa majanga kwa kutumia mifumo ya kiteknolojia ya kijiografia kwa majanga yanayotokana na hali ya hewa na haidrolojia kwa kutumia jukwaa la kielektroniki la MyDEWETRA.

“Mfumo huu umerahisisha ufuatiliaji wa mwenendo wa janga lililotabiriwa na kufanya uchambuzi wa kiwango cha madhara kwa jamii, miundombinu na mazingira, kuandaa taarifa za tahadhari ya mapema ya hatua za kuchukua ili kuzuia, kujiandaa na kukabili maafa, kuandaa taarifa ya mwenendo wa tukio na kusambaza kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya kusaidia uratibu na utekelezaji wa shughuli za kukabili na kurejesha hali,” Amesema  Dkt. Yonazi

Dkt. Yonazi amesema kuwa uanzishwaji wa kituo hicho cha ufuatiliaji wa majanga na tahadhari ya mapema umefanikiwa kutokana na mradi ulioanzishwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Madhara ya Maafa katika Kanda ya Afrika na  kufadhiliwa na Serikali ya Nchi ya Italia kupitia Shirika la Maendeleo la Italia (Italian Agency for Development Cooperation) ambapo Taasisi ya CIMA Research Foundation ya Italia imesadia kutoa utaalam wa utekelezaji wa shughuli zote.

Ameongeza kuwa  uwepo wa kituo hicho umesaidia sana Tanzania kuendelea kuwa kinara namba moja katika kukabiliana na  maafa kabla hayajaleta madhara.

Kufuatia umuhimu wa kituo hicho, Dkt. Yonazi ametoa wito kwa  Nchi  wanachama  pamoja na  mataifa mengine kuja Tanzania kwa lengo la  kujifunza na kubadilishana uzoefu kwa kuzingatia umuhimu wake.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoshiriki katika Kikao hicho cha siku nne ambacho kinatajia kumalizika   Oktoba 24, 2024 ambapo kikao hicho kimefanikiwa kuwakutanisha wadau zaidi ya elfu moja wa  maafa kwa nchi za Afrika  wakiwemo wataalamu kutoka  katika ngazi za kitaifa, Serikali za mitaa, Mashirika ya Umoja wa Kitaifa na Kimataifa, Asasi za Kiraia, sekta binafsi, taasisi za elimu na utafiti na wanahabari.



 

Monday, October 21, 2024

ENDELEENI KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA VIRUSI VYA UKIMWI” MHE. NDERIANANGA


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga ameihimiza jamii kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI nchini kwa kuendelea kuzingatia elimu inayotolewa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) ili kuunga mkono jitihada za Serikali dhidi ya mapambano hayo na kuyafikia malengo yaliyopo.

Mhe. Nderiananga ametoa wito huo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa ya utekelezaji wa Mkakati wa Tano wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26 iliyowasilishwa katika ukumbi wa Bunge, jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo Dkt. Jerome Kamwele katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI.

Alisema, jamii haina budi kuendelea kujilinda na kuwalinda wengine kwa kuzingatia ushauri na elimu inayotolewa ili kuhakikisha hali ya maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI nchini ipungue na kuyafikia malengo ya kuzifikia sifuri tatu ifikapo 2030.

“Suala la UKIMWI siyo la TACAIDS na Ofisi ya Waziri Mkuu peke yake, Wizara ya Afya inapambania kuboresha huduma ya mama na Mtoto, Ofisi ya Rais TAMISEMI ndio imejenga miundombinu  na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewekeza Ujenzi hadi ngazi ya Kata kuna vituo Vya afya yote hii ni kusogeza huduma karibu na wananchi na uwekezaji huu tutaona matunda yake katika mapambano dhidi  ya VVU,”Alieleza Mhe. Nderiananga.

Pia aliishukuru TACAIDS kwa kufanya kazi nzuri ya kuifikia jamii kwa njia ya elimu huku akiwahimiza kuendelea kuongeza nguvu kwa vijana kwani ndilo kundi linaloongoza kwa maambukizi bila kusahau ni kundi muhimu katika uzalishaji na kujiletea maendeleo.

Awali akiwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa Mkakati wa Tano wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo Dkt. Jerome Kamwele alieleza kwamba, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi Oktoba 2024, tume hiyo imefanikiwa kuratibu kwa ufanisi utekelezaji wa mkakati katika sekta zote ndani ya Serikali na sekta binafsi, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Taasisi za dini na wadau mbalimbali.

“Tume pia tumefanikiwa kupunguza maambukizi mapya ya VVU kutoka maambukizi 61,281 mwaka 2020 hadi maambukizi 60,000 mwaka 2023, kupungua kwa vifo vitokanavyo na UKIMWI kutoka vifo 32,639 mwaka 2020 hadi vifo 25,000 mwaka 2023 na kupungua kwa kiwango cha ubaguzi na unyanyapaa unaogokana na VVU kutokana na elimu ambayo imeendelea kutolewa kwa jamii na wadau,” alieleza Dkt. Kamwele.

Alifafanua kwamba mafanikio mengine ni pamoja na kufikia lengo la utekelezaji wa shabaha za Kimataifa 95-95-95 zinazohusu kupima na kutibu ifikapo 2026 ambapo asilimia 98 ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI  (WAVIU) wameanza tiba huku utafiti ukionyesha mwelekeo mzuri wa kufikia shabaha ya asilimia 95 ya tatu inayohusu kufubaza Virusi vya UKIMWI na kusisitiza ushirikiano wa pamoja kufikia asilimia 95 ya kwanza inayohusu watu wote wanaoishi na VVU kupima na kujua hali zao.

“Serikali inaendelea kuweka mkazo katika utekelezaji wa afua zinazolenga kupunguza kasi ya maambukizi mapya ya VVU hasa makundi maalum, kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha watu kupima kujua hali zao, kuongeza nguvu kuyafikia makundi maaalum hasa vijana, wanawake, wanaume, Watoto, watu wenye ulemavu na wanaoishi katika mazingira hatarishi,” alifafanua.

Aidha Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Bernadeta Mushashu aliipongeza TACAIDS kwa jitihada zake ikishirikiana na wadau kuhakikisha wananchi wanafanya shughuli zao za kiuchumi wakiwa katika hali njema ya kiafya.

Sunday, October 13, 2024

TANZANIA YAADHIMISHA SIKU YA MAAFA DUNIANI OKTOBA 13.

Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya Maafa Duniani ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo Oktoba 13 ili kuendelea kukabiliana na kupunguza madhara yatokanayo na maafa nchini,

Akitoa Tamko la maadhimisho hayo katika Uwanja wa CCM Kirumba leo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema maafa usababisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo, ulemavu wa kudumu, upotevu ,uharibifu wa mali, miundombinu na mazingira huku watoto na vijana wamekuwa wakikabiliwa na athari mbaya zaidi ikiwemo kukatizwa masomo, upungufu wa lishe, athari za kiafya, ulinzi na usalama.

Ameeleza kuwa siku hiyo ilianzishwa kwa Azimio namba 64/200 lililopitishwa na Baraza la Umoja wa Mataifa Disemba 21 mwaka 2009 , huadhimishwa kila mwaka, ili kuunganisha juhudi za kuwalinda watoto na vijana dhidi ya athari za majanga ambapo mikakati mbalimbali imewekwa ikiwemo kutoa mafunzo ya kujikinga na maafa,elimu ya hali ya hewa na jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,kuendeleza tafiti kuhusu madhara ya maafa na kutoa taarifa kwa umma ili kuongeza uelewa.

Akirejea taarifa iliyotolewa na serikali kupitia kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi zote kufuatia mwelekeo wa mvua za vuli katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2024 uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) imeonyesha maeneo  mengi ya nchi yanayopata mvua hizo hayatapata mvua za kutosha hivyo wamejiandaa kuzuia, kupunguza madhara, kujiandaa kukabili na hali hiyo sambamba na  kurejesha hali nzuri.

Akitaja hatua sita za kuzingatia kukabiliana na hali hiyo amezitaka Mamlaka husika ziendelee kuhamasisha na kuwezesha matumizi ya mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi pamoja na utunzaji wa chakula cha binadamu na malisho ya mifugo, mamlaka husika ziimarishe utoaji taaluma ya matumizi ya mbinu za kilimo zinazohitaji maji kidogo pia taasisi za umma ikiwemo za elimu, afya na ofisi mbalimbali ziwe mfano wa kuweka mifumo ya kuvuna, kuhifadhi na kutumia maji ya mvua.

Ameongeza kuwa hatua zingine ni kuimarisha mikakati ya kuzuia milipuko ya magonjwa yanayoweza kujitokeza kutokana na upungufu wa upatikanaji wa maji safi na salama,taasisi husika zishirikiane na taasisi za elimu na mashirika ya maendeleo ili kutoa mafunzo kwa wananchi kuhusu jinsi ya kukabiliana na ukame na Wizara yenye dhamana ya elimu na taasisi zake kuhakikisha wanaendelea kuimarisha mitaala ya elimu ili ijumuishe masuala ya usalama shuleni, kupunguza hatari, na uelewa wa majanga na wakihakikisha mafunzo kwa walimu kuhusu mbinu za kufundisha masuala hayo kwa wanafunzi.

 

"Kaulimbiu ya mwaka huu ni "Elimu ni msingi katika kulinda na kuwawezesha vijana kwa mustakabali wa baadae usio na maafa" ili kuungana na kaulimbiu serikali imeendelea kushirikiana na wadau wa kitaifa na kimataifa kuimarisha mifumo ya elimu inayolenga kutoa maarifa na ujuzi wa kupunguza madhara ya maafa kwa watoto na vijana " anaeleza Mhe.Majaliwa

Pia serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya hali ya hewa nchini ikiwemo kufunga miundombinu ya kisasa ya hali hewa, mafunzo kwa watumishi kwa kuzingatia vigezo vya kitaifa na kimataifa, na kuweka mifumo wezeshi ya usambazaji wa taarifa ya hali ya hewa pamoja na kuimarisha mifumo ya uhakiki wa ubora wa huduma huku uwekezaji wa miundombinu unajumuisha ununuzi wa rada za hali ya hewa.

"Ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, Tanzania itakuwa na rada saba ambapo ni kiwango kikubwa cha rada katika nchi za Afrika Mashariki na kati nitumie fursa hii kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan,  kwa uwekezaji mkubwa katika eneo hilo pia kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa makundi maalumu na kuweka mikakati thabiti inayolenga kuwawezesha vijana kiuchumi na kijamii pamoja na kuhakikisha Serikali inatoa elimu kwa wigo mpana na kuwezesha vijana kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto za majanga na kujenga jamii iliyo na ustawi endelevu." anaeleza Mhe.Majaliwa.

Aidha aliwahimiza wananchi wote, taasisi za elimu, na wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwajengea uwezo vijana kupitia elimu itakayowasaidia kujenga stahimilivu dhidi ya majanga kwa sababu elimu ina nafasi kubwa katika kuhakikisha kizazi cha leo kinakuwa na mbinu za kulinda mazingira, kuzuia uharibifu wa maliasili, na kuhakikisha kuwa tunakuwa na mfumo thabiti wa kukabiliana na majanga.

Saturday, October 12, 2024

VIONGOZI WAHIMIZWA KUWEKA MKAZO, WATU KUJITOKEZA KUJIANDIKISHA

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe William Lukuvi ametoa rai kwa viongozi wa vyama vya siasa viongozi wa dini viongozi wa kimila na viongozi wengine kushirikiana katika kuhimiza wananchi kwenda kujiandikisha kwa sababu ni haki yao.

Wito huo umetolewa leo wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa uliofanyika katika Ukumbi wa LAPF Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi wa vyama Siasa.

Ameeleza kwamba haki ya mtu kujiandikisha inabaki pale pale awe mwanachama wa chama cha siasa au bila kuwa mwanachama wa chama cha siasa.

Waziri Lukuvi amesema, “tukijumlisha wanachama wetu wote kuna watu wanabaki  ambao hawako kwenye fungu lolote  katika vyama hivi vya siasa 19, lakini bado tunao ushawishi wa kutumia sauti zetu kuhimiza  wananchi wote wenye umri wa kujiandikisha wajiandikishe  na hatimae watumie nafasi hiyo kupiga kura”

Tunaowajibu kama viongozi wa vyama vya siasa kwa pamoja kuufanya uchaguzi huu uwe mzuri.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha (UDP) Mhe. John Cheyo amesema kuna changamoto moja ya matumizi wa mhuri wa chini ambao bado haieleweki vizuri, nadhani sisi kama wadau wa siasa tunayo nafasi kukubaliana kwa kuwa na kauli moja ya kusimamia uchaguzi kulingana na kanuni na sheria ambazo tumejiwekea.

“Tunadhamira ya kuwa na uchaguzi huru na haki kwa kila mmoja wetu na kama ilivyoelezwa na Waziri Lukuvi na hiyo ndiyo dhamira ya Mhe, Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassani,” alisema Mhe. Cheyo

Awali Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, Joseph Selasini amesema huu ni mkutano ambao umeandaliwa tukiwa tunaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kujipanga katika maandalizi ya chaguzi zinazoendelea.

Thursday, October 10, 2024

JAMII YAKUMBUSHWA KULINDA MAZINGIRA KUEPUKA MAGONJWA YA MLIPUKO

 


 Mratibu wa Maafa kutoka  Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bi. Numpe Mwambenja ameikumbusha jamii kuendelea kulinda mazingira ili kuepuka uwezekano wa kukumbwa na magonjwa ya milipuko ikiwemo kipindupindu.

Ameyasema hayo wakati akifungua semina kuhusu ya masuala ya menejimenti ya maafa kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW) katika Kata ya Kirumba Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza, katika kuelekea Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Maafa Dunia  ambapo Kitaifa mwaka huu yanaadhimishwa Mkoani Mwanza yakiwa na kauli mbiu isemayo “Elimu ni Msingi katika Kulinda na Kuwawezesha Vijana kwa Mustakabali wa Baadae usio na Maafa”.

Kwa upande wake Mratibu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa Maendeleo kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la ActionAid Bw. Tema Hassan amesema masuala ya kukabiliana na maafa yanahitaji elimu mahususi huku akisisitiza matumizi ya   teknolojia ya kisasa ili kuifikia jamii iliyokusudiwa.

“Teknolojia ni muhimu katika kuifikia jamii kiurahisi, hivyo ni vyema kuwekeza katika matumizi ya simu na mifumo ya kisasa kwa kuzingatia makundi yanayokusudiwa,” alisema Temu

Kufuatia hatua hiyo Bw.Temu amesema  kuwa Shirika la ActioAid litaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukabiliana na maafa nchini kwa kuzingatia unyeti wa masuala hayo na kuhakikisha jamii inaendelea kuwa stahimilivu katika masuala ya maafa.

Kwa upande wake Afisa Afya wa Kata ya Kirumba Bi. Veronica Massawe amesema usafi wa mazingira ni jambo lisiloepukika huku akiitaka jamii kuzingatia  maelekezo yanayotolewa na wataalamu  ili kujikinga na magonjwa ya milipuko.

“Ni muhimu  kulinda afya zetu kwani, Afya ndiyo  mtaji wetu sote" amesisitiza Bi. Veronica Massawe.

Ameongeza kuwa " Tumejiandaa, kukabiliana na maafa ikiwa na pamoja na kujiepusha na mazingira hatarishi yanayoweza kutuletea maafa katika kata yetu, usafi ni wajibu wa msingi kuwa na vyoo bora na kuvitumia katika kupambana na magonjwa ya mlipuko"

Naye Mwenyekiti wa Wahudumu wa Afya ya Jamii Kata ya Kirumba Bw. Wilfred Roman amesema watatumjia elimu waliyopewa katika semina hiyo kwa kuwaelimisha wahudumu wa afya ngazi ya jamii kwa kufanya afya shirikishi.

“Elimu tuliyopewa katika semina ni nyenzo muhimu tutakayoitumia katika kupambana na magonjwa ya mlipuko,” amesema Wilfred.

 

 

Wednesday, October 9, 2024

“MRADI WA TANKI LA MAJI BANGULO MBIONI KUKAMILIKA” WAZIRI LUKUVI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi amesema ujenzi unaoendelea wa tanki kubwa la kuhifadhia maji safi kutoka Ruvu unatarajia kukamilika mapema mwakani ambapo litasaidia kuondoa kero ya maji Jijini Dar es salaam.

Waziri ametoa kauli hiyo alipofanya ziara ya kutembelea na kujionea maendeleo ya mradi na kuzungumza na wananchi wa Banguko katika Jimbo la Ukonga jijini Dar es salaam.

Ameeleza ujenzi wa bwawa hilo utanufaisha wananchi takribani 450000 hasa wa Jimbo la Ukonga na Segerea na Mkandarasi ameshalipwa fedha zote hivyo mradi utakapokamilika wananchi wote wataunganishwa na mtandao wa maji.

“Hivyo tutashuhudia kata saba katika Jimbo la Ukonga zitakazoondokana na adhaa ya upatikanaji wa maji,” alisema Waziri Lukuvi.

Aidha tunashuhudia fedha nyingi zinatolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji na barabara na tumekubaliana usanishaji wa mikataba ufanyike katika maeneo husika ya ujenzi wa miradi.

Ujenzi wa Miradi ya Maendeleo ni hatua lakini sisi tumekwenda kasi sana katika utekelezaji wake hivyo wananchi mukiona vinaelea vimeundwa,

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe, Albert Chalamila amesema Mkoa umejikita sana katika kulinda amani na kuendelea kulinda raia na mali zao, ili wananchi waweze kujikita katika shughuli za uzalishaji.

“Mwenyeviti wa Serikali za Mitaa na kamati za ulinzi kwa kushirikisha na polisi jamiii, hakikisheni Madhila ya wananchi kuogopa wahalifu yanadhibitiwa katika maeneo yenu,“ alisema Mkuu wa Mkoa Chalamila.

Awali Mkuu wa wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amesema Serikali imejenga madarasa ya ghorofa zaidi ya 80 na madarasa ya kawaida 465 kwa shule za sekondari, na kwa upande wa shule za msingi madarasa zaidi ya 437 yamejengwa.

“Mafanikio haya yanakuja kutokana na mahusiano tuliyonayao na wawakiishi wa wananchi wanaochagiza kwa kiasi kikubwa maendeleo ya miradi ya maendeleo,” alisema Mkuu wa wilaya Mpogolo.

Ikumbukwe katika ziara hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe William Lukuvi, alizindua Mradi wa Barabara ya Tukuyu Ilala na Kuweka Jiwe la Msingi katika sekondari Liwiti.

Tuesday, October 8, 2024

“SERIKALI KUENDELEA KUTHAMINI MCHANGO WA VYAMA VYA SIASA KATIKA KUDUMISHA AMANI” WAZIRI LUKUVI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe William Lukuvi amesema Serikali itaendelea kuheshimu misingi iliyowekwa na vyama vya siasa katika kujenga   amani na utulivu kwa watanzania wote.

Kauli hiyo ameitoa Jijini Dar es Salaam katika ziara yake ya kutembelea Makao Makuu ya Ofisi za Vyama vya UDP, NCCR MAGEUZI, CUF na NLD ambapo amepata nafasi ya kukutana na kufanya mazungumzo na Viongozi Wakuu wa Vyama hivyo.

Ameeleza kwamba tangu mfumo wa vyama vingi umeanza nchini Vyama vya Siasa kwa kushirikiana na Chama Tawala vimekuwa mhimili wa kujenga  amani na umoja, hivyo nawapongeza kwa kazi nzuri ya uzalendo mnayofanya.

“Niombe Viongozi wa Vyama mhimize wananchi kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ndani ya demokrasia ya vyama mnaweka wagombea ili washindane na vyama vingine kupata viongozi,” alisema Waziri Lukuvi

Aidha Serikali itahakikisha matangazo yote ya vijiji yanawekwa kwenye tovouti za Serikali ili wananchi wafahamu vijiji, vitongoji na mitaa inayogombaniwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha (UDP) Mhe. John Cheyo amemshukuru Waziri wa Nchi kwa kufanya ziara katika Ofisi za Makao Makuu ya Vyama kwa sababu imeonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kutekeleza falsafa ya 4R.

Mhe. Cheyo amesema “sisi kama wadau wa siasa tunataka kushiriki katika kuona nchi inatawalika kwa amani na kuchagiza maendeleo makubwa”

Monday, October 7, 2024

SERIKALI KUENDELEA KUTOA KIPAUMBELE USIMAMIZI WA MAAFA NCHINI

 

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kutoa kipaumbele katika usimamizi wa masuala ya maafa ambapo miongoni mwa hatua mbalimbali zimechukuliwa.

Kauli hiyo imetolewa  Jijini Dodoma na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga, wakati akifungua mafunzo ya usimamizi wa maafa kwa Waratibu wa maafa wa Wizara na Taasisi, Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Kimataifa na Asasi za Kiraia.

Akibainisha baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali, Mhe. Ummy amesema kuwa serikali imeweza kutunga Sheria mpya na kuandaa miongozo ya usimamizi wa maafa na kutoa vifaa vya misaada ya kibinadamu kwa wananchi walioathirika na maafa katika Halmashauri mbalimbali nchini.

“Serikali pia, imeendesha mazoezi ya mezani ya nadharia ya kujiandaa na kukabiliana na maafa kwa majanga ya mafuriko, vimbunga na tsunami; kuimarisha maghala ya kuhifadhi vifaa vya msaada katika kanda sita kwa kuongeza vifaa vya kutolea huduma za kibinadamu” ameongeza Mhe. Ummy.

Aidha, ameeleza kuwa serikali imefanya mafunzo kwa kamati za usimamizi wa maafa za mikoa na wilaya na voluntia pamoja na kutoa elimu kwa umma, wataalam wanaosimamia asasi za kiraia na waandishi wa habari kutoka katika redio za kijamii nchini kuhusu masuala ya usimamizi wa maafa.

Mbali na hayo Mhe. Ummy amebainisha kuwa, mafunzo hayo ni hatua ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya chama tawala ya Mwaka 2020 – 2025 ambayo katika Ibara ya 107 inaelekezwa Serikali kuchukua hatua za kuimarisha mifumo ya utendaji ya wizara, taasisi na mamlaka za serikali za mitaa ikiwemo kutoa elimu ya usimamizi wa maafa.

Nae, Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Eleuter Kihwele, amesema kuwa, mafunzo hayo yanayotolewa kwa siku mbili yataleta mchango katika kukabiliana na masuala ya majanga nchini.

Mkurugenzi Mtendaji, Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Makame Khatibu Makame ameeleza kuwa Zanzibar ipo salama na inaendelea kupambana na usimamizi wa maafa hivyo uwepo wa mafunzo hayo ni fursa kwao kujifunza mifumo ya kisasa ya namna ya kukabiliana na masuala ya maafa.

Kwa upande wake, Naibu Mwakilishi Mkazi, Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) Bw. Patrick Codja, amesema kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na serikali katika kutatua masuala mbalimbali yanayotoka na maafa.

WAZIRI LUKUVI, AHIMIZA VYAMA VYA SIASA KUSHIRIKI UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi amewahamasisha na kuwahimza viongozi wa Vyama vya Siasa juu ya umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

 Waziri amesema hayo wakati alipotembelea ya Makao Makuu Vyama Vinne vya Siasa katika ziara yake iliyolenga kuendelea kuimarisha mahusiano na falsafa ya Mhe. Rais. Dkt, Samia Suluhu Hassan ya 4R.

Amesema lengo ni kuvifikia vyama vyote 19 kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa ikiwa ni pamoja na kutoa salamu za upendo za Mhe, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuwapa pongezi viongozi wapya waliochaguliwa hivi karibuni.

“Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unasimamiwa na TAMISEMI na una kanuni na taratibu  za uendeshaji wake zinazohusisha Vyama vya Siasa, hivyo natumia fursa hii kuhimiza wananchi wote kujitokeza kujiandikisha katika zoezi linaloanza tarehe 11-20 /10/2024 kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili wapate nafasi ya kuchagua na kuchaguliwa” alisema Waziri Lukuvi.

Aidha amewaomba viongozi wa kisiasa kuendelea kutoa ushauri kwa Serikali bila kusubiri vikao vya baraza vinavyoitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa na badala yake wanaweza kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kama kiungo ili waweze kuishauri Serikali wakati wowote.

Waziri Lukuvi amesema, “ni wajibu wetu kudumisha amani na upendo kama alivyotuasa Mhe. Rais kwa kushindanisha sera zetu kwa hoja na tukishapata matokeo tuwachie waliochaguliwa ambao watakuwa ni Wenyeviti wa vijiji, Wenyeviti wa Mitaa na Wenyeviti wa Vitongoji watekeleze wajibu wao.”

Nashukuru sana kwa sababu vyama vyote wamekubali kutembelewa kwa ratiba ambayo itakuwa imepangwa,

Kwa upande wake Bi, Doroth Temu Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT amesema wao kama wadau wanaendelea na kazi ya msingi ya kuelimisha uma juu ya umuhimu wa uchaguzi  na kuendelea kuwasilisha Serikalini maoni yote wanayoyapata kwa wananchi.  

“Tutaendelea kuwakumbumbusha wananchi kwamba uchaguzi ni jukumu muhimu:  na kuwahimiza kushiriki kwao kama raia wa Tanzania katika kuchagua viongozi nasi tukitegemea uchaguzi kuwa huru na wakuaminika,” alisema Makamu Mwenyekiti Bi, Doroth Temu.

Ikumbukwe kwamba katika siku ya kwanza ya ziara ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) ametembelea na kukutana na Viongozi wa Vyama vya CHAUMMA, ACT Wazalendo, CCK na  UPDP.

“SERIKALI IMEENDELEA KUCHUKUA HATUA ZA KUIMARISHA MASUALA YA MENEJIMENTI YA MAAFA NCHINI ”DKT. YONAZI

 


Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu imesema itaendelea kuimarisha masuala ya menejimenti ya maafa kwa lengo la kuimarisha ustahimilivu dhidi ya maafa nchini.

Kauli hiyo imetolewa Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi wakati akifungua  Kikao Kazi cha Kukabidhi Nyaraka za Usimamizi wa Maafa za Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ pamoja na kupokea Taarifa ya Tathmini ya Jiolojia, Haidrolojia na Mazingira.

Dkt. Yonazi amesema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuwekwa kwa mfumo wa kisera, kisheria na kitaasisi wa utaratibu wa masuala ya maafa kwa kutunga Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Na. 6 ya mwaka 2022 lengo likiwa  ni kuendelea kuimarisha masuala ya usimamizi wa maafa.

Amefafanua kuwa, Sheria hiyo imebainisha majukumu na imeweka mfumo wa usimamizi wa maafa kupitia Kamati za Usimamizi wa Maafa kutoka ngazi ya Taifa hadi Kijiji/Mtaa.

Amesema lengo ni kuhakikisha Wizara, Idara, Taasisi za Serikali na zisizo za Serikali, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zinashiriki kikamilifu katika kutekeleza shughuli za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga pamoja na kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali kwa ubora pindi maafa yanapotokea.

Dkt. Yonazi alieleza kwamba ili kuwezesha utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa maafa kwa ufanisi, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu kwa kushirikiana na wadau pia imeendelea kuboresha utaratibu wa utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa maafa nchini kwa kuandaa nyaraka zinazoainisha majukumu ya msingi kwa wadau na zinazotoa mwongozo wa majukumu kwa wadau.

Aidha Nyaraka hizo ni pamoja na Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na kukabiliana na Maafa (2022), Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano Wakati wa Maafa (2022 na Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa (2022).

 Dkt.Yonazi amesema nyaraka ziwe ni chachu ya kuongeza ushirikishwaji wa jamii na wadau pamoja na  kupunguza madhara ya majanga na kujiandaa na kukabiliana na maafa”alieleza Dkt. Yonazi

“Natambua, kwa sasa Halmashauri inaendelea kutekeleza shughuli za kurejesha hali baada ya maafa makubwa yaliyosababishwa na janga la maporomoko ya ardhi katika mlima Hanang yaliyotokea mwaka jana,  niendelee kusisitiza kuwa, muendelee  kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kuzuia na kupunguza madhara ya majanga na kujiandaa na kukabiliana na maafa na kuwahamasisha wananchi kutokutekeleza shughuli za kiuchumi na ujenzi katika maeneo hatarishi kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu,”amesema Dkt.Yonazi

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Hanang’ na Mwenyekiti wa Kamati Elekezi ya Usimamizi wa Maafa ya Wilaya Mhe. Almishi  Hazali ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendelea kuratibu maafa nchini, huku akipongeza hatua ya uzinduzi wa nyaraka hizo muhimu katika Wilaya hiyo na kueleza kuwa, ni nyenzo muhimu katika kuendeleza jitihada juu ya majanga na maafa nchini.

 

 


Wednesday, October 2, 2024

“HALI YA LISHE INAENDELEA KUIMARIKA NCHINI” DKT. YONAZI

 


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amesema hali ya lishe nchini imeendelea kuimarika kwa kwa kuzingatia Takwimu zinaonesha kupungua kwa viwango vya utapiamlo kwa baadhi ya viashiria ikiwemo kiwango cha udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambacho ndio kiashiria kikuu cha utapiamlo kimepungua kutoka asilimia 32 mwaka 2018 hadi asilimia 30 mwaka 2022 (DHS 2022).

Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe nchini unaofanyika ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Malaika Jijini Mwanza uliowakutanisha wadau wa afua za lishe kwa lengo la kupokea na kujadili hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha mwaka wa tatu 2023/2024 katika maeneo mahsusi yaliyoanishwa kwenye Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe (2021/22-2025/26).

Alieleza kuwa Mkutano huo unatoa fursa kwa wadau wote wa lishe kujadili namna utekelezaji ulivyofanyika, changamoto na mikakati ya kufanikisha utekelezaji katika kipindi kilichobaki cha utekelezaji wa mpango huo hususan mwaka 2025/26. Pia Mkutano huu unatazamiwa kuongeza msukumo mpya wa utekelezaji wa afua za lishe miongoni mwa wadau kama moja ya nguzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Akiongelea kuhusu hali ya lishe amesema kuwa kiwango cha ukondefu pia kimepungua kutoka asilimia 3.8 mwaka 2014 hadi asilimia 3.5 mwaka 2018, ingawa takwimu hizi zilibadilika mwanzoni mwa mwaka 2023 baada ya kupata matokeo ya utafiti uliofanywa Machi - Julai 2022 na Taasisi ya Chakula na Lishe na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.

 

Dkt. Yonazi alisema kuwa, uwepo wa wadau katika mkutano huo ni uthibitisho tosha wa ushirikiano uliopo na utayari wao katika kuboresha hali ya lishe kwa Watanzania, hususan makundi yanayoathirika zaidi ambayo ni watoto wadogo na wachanga, watu wenye mahitaji maalum, wanawake wajawazito na wale walio katika umri wa uzazi.

“Naomba ushirikiano huo uendelee wakati wote wa utekelezaji wa mpango na hususan wakati kama huu ambao tunakutana kujadili utekelezaji Sote tunajua kuwa ili tuweze kuwa na maendeleo ya kiuchumi na kijamii ni lazima Taifa liwe na watu wenye lishe na afya bora ili kuwa na uwezo wa kufikiri, kutenda na kufanya kazi kwa bidii. Hivyo, juhudi hizi na nyingine ni muhimu kuwa endelevu ili kutuwezesha kufikia malengo,” alisisitiza Dkt. Yonazi.

Aidha Dkt. Yonazi alitumia mkutuno huu kuiasa  jamii kuendelea kushiriki kikamilifu na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha hali ya lishe kwa Watanzania inaendelea kuimarika huku akisema kuwa Serikali inaahidi kuendelea kuunga mkono juhudi zilizopo na nyingine za wadau ili kuhakikisha Taifa linapata mafanikio dhidi ya mapambano ya tatizo la utapiamlo.

Kwa upande wake Mheshimiwa Mizengo Pinda Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema, Serikali imeendelea kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha jamii inaendelea na mapambano haya ya lishe duni na kuhakikisha Taifa linaendelea kuwa na watu wenye afya bora, na kukumbusha jamiii kuwa mstari wa mbele katika masuala ya afua za Lishe.

“Jambo hili la mapambano dhidi ya lishe ni Mtambuka, hakuna Wizara itakwepa, hivyo ni wakati sahihi na tuone njia sahihi za kutumia katika mapambano haya,ifike mahali tuizungumze dhana ya lishe katika wizara na kuhimiza agenda hii iwe ya kila mmoja,” alisema Mhe. Pinda

Aliongezea kuwa, masuala ya lishe yawekewe mkazo zaidi kuanzia katika elimu ya  msingi hasa kupitia uwepo wa Klabu maalum zinazochagiza masuala ya afua za lishe nchini lengo ni kuwajengea uelewa watoto kuwa na elimu ya kina kuhusu masuala haya.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka alizungumza wakati wa mkutano huo alieleza jitihada zinazofanywa na mkoa wake katika mapambano dhidi ya Utapiamlo na masuala yote ya lishe amesema ni wakati sahihi kuwa na mikakati inayotekelezeka ili kuwa na jamii yenye lishe na afya bora.

Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe nchini umeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, na umebebwa na kauli mbiu isemayo “Kuchagiza Mchango wa Wadau wa Kisekta ili Kudumisha Matokeo Bora ya Hali ya Lishe Nchini Tanzania” ukilenga kufanya tathmini ya  utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa pili wa Taifa wa Lishe ili kuendelea kukabiliana na changamoto za utapiamlo nchini.