Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu imesema itaendelea kuimarisha masuala ya menejimenti ya maafa kwa lengo la kuimarisha ustahimilivu dhidi ya maafa nchini.
Kauli hiyo imetolewa Wilayani
Hanang’ Mkoani Manyara na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia
masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi wakati akifungua Kikao Kazi cha Kukabidhi Nyaraka za Usimamizi
wa Maafa za Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ pamoja na kupokea Taarifa ya
Tathmini ya Jiolojia, Haidrolojia na Mazingira.
Dkt. Yonazi amesema miongoni
mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuwekwa kwa mfumo wa kisera, kisheria na
kitaasisi wa utaratibu wa masuala ya maafa kwa kutunga Sera ya Taifa ya
Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Na. 6 ya
mwaka 2022 lengo likiwa ni kuendelea
kuimarisha masuala ya usimamizi wa maafa.
Amefafanua kuwa, Sheria hiyo
imebainisha majukumu na imeweka mfumo wa usimamizi wa maafa kupitia Kamati za
Usimamizi wa Maafa kutoka ngazi ya Taifa hadi Kijiji/Mtaa.
Amesema lengo ni kuhakikisha
Wizara, Idara, Taasisi za Serikali na zisizo za Serikali, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa zinashiriki kikamilifu katika kutekeleza shughuli za kuzuia
na kupunguza madhara ya majanga pamoja na kujiandaa, kukabiliana na kurejesha
hali kwa ubora pindi maafa yanapotokea.
Dkt. Yonazi alieleza kwamba
ili kuwezesha utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa maafa kwa ufanisi,
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu kwa kushirikiana
na wadau pia imeendelea kuboresha utaratibu wa utekelezaji wa shughuli za
usimamizi wa maafa nchini kwa kuandaa nyaraka zinazoainisha majukumu ya msingi
kwa wadau na zinazotoa mwongozo wa majukumu kwa wadau.
Aidha Nyaraka hizo ni pamoja
na Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na kukabiliana na Maafa (2022), Mkakati wa
Taifa wa Mawasiliano Wakati wa Maafa (2022 na Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa
Maafa (2022).
“Natambua, kwa sasa
Halmashauri inaendelea kutekeleza shughuli za kurejesha hali baada ya maafa
makubwa yaliyosababishwa na janga la maporomoko ya ardhi katika mlima Hanang
yaliyotokea mwaka jana, niendelee
kusisitiza kuwa, muendelee kutoa elimu
kwa jamii kuhusu namna ya kuzuia na kupunguza madhara ya majanga na kujiandaa
na kukabiliana na maafa na kuwahamasisha wananchi kutokutekeleza shughuli za
kiuchumi na ujenzi katika maeneo hatarishi kwa kuzingatia ushauri wa
kitaalamu,”amesema Dkt.Yonazi
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya
ya Hanang’ na Mwenyekiti wa Kamati Elekezi ya Usimamizi wa Maafa ya Wilaya Mhe.
Almishi Hazali ameishukuru Ofisi ya
Waziri Mkuu kwa kuendelea kuratibu maafa nchini, huku akipongeza hatua ya uzinduzi
wa nyaraka hizo muhimu katika Wilaya hiyo na kueleza kuwa, ni nyenzo muhimu
katika kuendeleza jitihada juu ya majanga na maafa nchini.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.