Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amesema
hali ya lishe nchini imeendelea kuimarika kwa kwa kuzingatia Takwimu zinaonesha
kupungua kwa viwango vya utapiamlo kwa baadhi ya viashiria ikiwemo kiwango cha
udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambacho ndio kiashiria
kikuu cha utapiamlo kimepungua kutoka asilimia 32 mwaka 2018 hadi asilimia 30
mwaka 2022 (DHS 2022).
Ameyasema hayo wakati wa
ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe nchini unaofanyika ukumbi wa
Mikutano wa Hoteli ya Malaika Jijini Mwanza uliowakutanisha wadau wa afua za
lishe kwa lengo la kupokea na kujadili hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa
afua za lishe kwa kipindi cha mwaka wa tatu 2023/2024 katika maeneo mahsusi
yaliyoanishwa kwenye Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe (2021/22-2025/26).
Alieleza kuwa Mkutano huo
unatoa fursa kwa wadau wote wa lishe kujadili namna utekelezaji ulivyofanyika,
changamoto na mikakati ya kufanikisha utekelezaji katika kipindi kilichobaki
cha utekelezaji wa mpango huo hususan mwaka 2025/26. Pia Mkutano huu
unatazamiwa kuongeza msukumo mpya wa utekelezaji wa afua za lishe miongoni mwa
wadau kama moja ya nguzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Akiongelea kuhusu hali ya
lishe amesema kuwa kiwango cha ukondefu pia kimepungua kutoka asilimia 3.8
mwaka 2014 hadi asilimia 3.5 mwaka 2018, ingawa takwimu hizi zilibadilika
mwanzoni mwa mwaka 2023 baada ya kupata matokeo ya utafiti uliofanywa Machi -
Julai 2022 na Taasisi ya Chakula na Lishe na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Dkt. Yonazi alisema kuwa,
uwepo wa wadau katika mkutano huo ni uthibitisho tosha wa ushirikiano uliopo na
utayari wao katika kuboresha hali ya lishe kwa Watanzania, hususan makundi
yanayoathirika zaidi ambayo ni watoto wadogo na wachanga, watu wenye mahitaji
maalum, wanawake wajawazito na wale walio katika umri wa uzazi.
“Naomba ushirikiano huo
uendelee wakati wote wa utekelezaji wa mpango na hususan wakati kama huu ambao
tunakutana kujadili utekelezaji Sote tunajua kuwa ili tuweze kuwa na maendeleo
ya kiuchumi na kijamii ni lazima Taifa liwe na watu wenye lishe na afya bora
ili kuwa na uwezo wa kufikiri, kutenda na kufanya kazi kwa bidii. Hivyo, juhudi
hizi na nyingine ni muhimu kuwa endelevu ili kutuwezesha kufikia malengo,”
alisisitiza Dkt. Yonazi.
Aidha Dkt. Yonazi alitumia
mkutuno huu kuiasa jamii kuendelea
kushiriki kikamilifu na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha
hali ya lishe kwa Watanzania inaendelea kuimarika huku akisema kuwa Serikali
inaahidi kuendelea kuunga mkono juhudi zilizopo na nyingine za wadau ili
kuhakikisha Taifa linapata mafanikio dhidi ya mapambano ya tatizo la utapiamlo.
Kwa upande wake Mheshimiwa
Mizengo Pinda Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema,
Serikali imeendelea kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha jamii inaendelea na
mapambano haya ya lishe duni na kuhakikisha Taifa linaendelea kuwa na watu
wenye afya bora, na kukumbusha jamiii kuwa mstari wa mbele katika masuala ya
afua za Lishe.
“Jambo hili la mapambano dhidi
ya lishe ni Mtambuka, hakuna Wizara itakwepa, hivyo ni wakati sahihi na tuone
njia sahihi za kutumia katika mapambano haya,ifike mahali tuizungumze dhana ya
lishe katika wizara na kuhimiza agenda hii iwe ya kila mmoja,” alisema Mhe.
Pinda
Aliongezea kuwa, masuala ya
lishe yawekewe mkazo zaidi kuanzia katika elimu ya msingi hasa kupitia uwepo wa Klabu maalum
zinazochagiza masuala ya afua za lishe nchini lengo ni kuwajengea uelewa watoto
kuwa na elimu ya kina kuhusu masuala haya.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe,
Mhe. Anthony Mtaka alizungumza wakati wa mkutano huo alieleza jitihada
zinazofanywa na mkoa wake katika mapambano dhidi ya Utapiamlo na masuala yote
ya lishe amesema ni wakati sahihi kuwa na mikakati inayotekelezeka ili kuwa na
jamii yenye lishe na afya bora.
Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau
wa Lishe nchini umeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Taasisi
ya Chakula na Lishe Tanzania, na umebebwa na kauli mbiu isemayo “Kuchagiza
Mchango wa Wadau wa Kisekta ili Kudumisha Matokeo Bora ya Hali ya Lishe Nchini
Tanzania” ukilenga kufanya tathmini ya
utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa pili wa Taifa wa Lishe ili kuendelea
kukabiliana na changamoto za utapiamlo nchini.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.