Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Doto Biteko amezitaka taasisi za ufutiliaji na tathmini kufanya kazi kwa weledi na kuimarisha eneo hilo ili kuendana na mahitaji yanayolenga kuleta tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hayo yameelezwa leo Zanzibar na Dkt. Biteko wakati akimwakilisha Waziri Mkuu, Mhe. Kassim
Majaliwa katika Kongamano la Tatu la
Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza.
Amesema wataalam wa
ufuatiliaji na tathmini wanawajibika kuilinda taaluma hiyo na kuwashawishi kwa
hoja wakuu wa taasisi husika kupenda kazi zinazotokana na taaluma hiyo badala
ya kujisikia wanyonge kitaaluma.
Aidha, Dkt. Biteko amewataka
washiriki muda wote kusisitiza misingi ya taaluma hiyo na baadaye kuleta
matokeo chanya kwa maendeleo ya Taifa na watu wake. “Inawezekana katika maeneo
yenu ya kazi wakawepo wakuu wa taasisi au viongozi wa serikali ambao hawapendi
mfanye kazi yenu vizuri, kukubaliana na hilo ni kujiua wenyewe. Mnapotoka hapa
mkafanye mkuu wa taasisi au kiongozi aone umuhimu wenu katika shirika.” Amesema
Dkt. Biteko.
Aidha, amewataka wataalamu hao
kusema ukweli na kusimamia taaluma yao. “ Nataka niwaombe mkajiamini Rais Samia
ameahiza na kuelekeza uwepo wa vitengo vya tathmini ndani ya Serikali, Ofisi ya Rais, Mipango na
Uwekezaji wafanyekazi na kitengo cha ufuatiliaji kilichopo Ofisi ya Waziri Mkuu
mfuatilie fedha zinazopelekwa kwenye miradi na matokeo yake kwenye kubadilisha
hali za maisha ya watu.” Amesisitiza Dkt. Biteko.
Kupitia kikao hicho, ametoa
maagizo matano yakilenga kuboresha ufuatiliaji, tathmini na kujifunza.
“ Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Bunge na Uratibu ikamilishe mapema Mfumo Ufuatiliaji na Tathmini na kuwezesha
taarifa za utendaji wa Serikali kupatikana kwa urahisi.Tume zetu za Mipango
zikamilishe uchambuzi wa miradi yote inayotekelezwa ndani ya Serikali na kila
mwaka kutoa taarifa ya utekelezaji. Namna hii itawezesha Serikali kuona tija ya
miradi inayoidhinishwa na kutekelezwa hapa nchini.” Amesema Dkt. Biteko.
Aidha ameielekeza Ofisi hiyo kukamilisha
Sera ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ili iwezeshe utekelezaji sahihi wa
eneo la ufuatiliaji na tathmini nchini. Sambamba na TanEA na ZaMEA kuweka
mikakati ya kujiimarisha kiuchumi ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa
mujibu wa uanzishwaji wake.
Aidha, Dkt. Biteko aziagiza
TanEA na ZaMEA kuwa Sera pamoja na mikakati yake ziwe zinafanyiwa Tathimini
kila baada ya miaka mitatu baada ya kuandaliwa. Hii itasaidia kujua kila hatua
inayofikiwa kwa utelezaji wake pamoja na utatuzi wa changamoto za utelezaji na
maboresho wakati wa uhuishaji wa Sera.
Kwa upande wake, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. William Lukuvi amesema
kuwa Kongamano hilo la tatu la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza lenye kauli
mbiu isemayo ‘Kuimarisha utoaji wa
huduma kwa wananchi kwa kutumia teknolojia katika ufuatiliaji na tathmini
na matumizi ya matokeo ya tathmini katika kufanya maamuzi’ limepata mwitikio
mkubwa kutoka kwa wadau na washiriki.
Ametaja lengo la Kongamano
hilo kuwa ni kuweka msisitizo kwenye
lengo kuu la Serikali la kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi na kuwa
katika kutimiza azma hiyo, washiriki wamehamasishwa kutumia vizuri taaluma na
mafunzo mbalimbali wanayoyapata kuhakikisha wanakuwa jicho la Serikali katika
mipango yake, utendaji wake na utekelezaji wa miradi ili iweze kupata
maendeleo.
Aidha Mhe. Lukuvi amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe.
Dkt. Hussein Ali Mwinyi wamekuwa vinara wa ufuatiliaji na tathmini katika
utendaji wa Serikali kwa ujumla wake, utekelezaji wa miradi yote nchini na
utoaji wa huduma bora kwa wakati kwa wananchi wote.
Amesema kuwa marais hao
wanafanya hayo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya
mwaka 2020 ambapo kwa sekta zote umewekwa mkazo wa ufuatiliaji na tathmini
katika utendaji, utekelezaji wa miradi na utoaji huduma.
“ Katika kuimarisha Sekta ya
Fedha, ibara ya 20 (f) ya Ilani ya CCM inaitaka Serikali kuimarisha ufuatiliaji
na tathmini ya mashirika na taasisi zilizobinafsishwa ili kuhakikisha mikataba
inatekelezwa ipasavyo na Sekta ya Ujenzi, ibara ya 51(a)(ii) ya Ilani inaitaka Serikali kuboresha mfumo wa
ufuatiliaji na tathmini wa shughuli za barabara kwa kuhakikisha thamani ya
ubora wa kazi inaendana na fedha zilizotumika.” Amesema Mhe. Lukuvi.
Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa kupitia
Kongamano hilo wamepata fursa mbalimbali ikiwemo kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uwezo wa
wataalamu. Sambamba na washiriki kujifunza mbinu mpya za kuboresha mifumo ya
Ufuatiliaji na Tathmini, hasa kwa kutumia teknolojia na takwimu sahihi ili
kufanya maamuzi sahihi na yenye tija.
“ Kongamano hili limesisitiza
umuhimu wa wananchi kushiriki katika mchakato mzima wa Ufuatiliaji na Tathmini
ili kuimarisha uwazi, uwajibikaji na kuhakikisha Serikali na wahisani wanatoa
huduma zenye tija. Pia, ushirikishwaji wa waananchi utasaidia kuhakikisha kuwa
miradi ya maendeleo inawafaidisha moja kwa moja.” Amesema Dkt. Yonazi.
Vilevile ameongeza kuwa,
kongamano hilo limelenga kukuza uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa sera
na miradi ya maendeleo, kwa kuleta pamoja wadau mbalimbali wakiwemo watendaji
wa serikali, wabunge, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wananchi, aidha,
limetoa jukwaa la kujadili jinsi ufuatiliaji na tathimini unavyoweza kutumika
kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi na uwajibika.
Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya
Mipango, Dkt. Ameir Haji Sheha amesema kuwa ushiriki wa Kongamano hili limeibuwa
haja na mahitaji mbalimbali na kuwa Kongamano hilo limejumuisha washiriki 738
na ameishukuru Ofisi ya Waziri, Sera, Bunge na Uratibu kwa ushirikiano wakati
wote wa maandalizi wa Kongamano hilo.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.