Monday, October 7, 2024

SERIKALI KUENDELEA KUTOA KIPAUMBELE USIMAMIZI WA MAAFA NCHINI

 

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kutoa kipaumbele katika usimamizi wa masuala ya maafa ambapo miongoni mwa hatua mbalimbali zimechukuliwa.

Kauli hiyo imetolewa  Jijini Dodoma na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga, wakati akifungua mafunzo ya usimamizi wa maafa kwa Waratibu wa maafa wa Wizara na Taasisi, Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Kimataifa na Asasi za Kiraia.

Akibainisha baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali, Mhe. Ummy amesema kuwa serikali imeweza kutunga Sheria mpya na kuandaa miongozo ya usimamizi wa maafa na kutoa vifaa vya misaada ya kibinadamu kwa wananchi walioathirika na maafa katika Halmashauri mbalimbali nchini.

“Serikali pia, imeendesha mazoezi ya mezani ya nadharia ya kujiandaa na kukabiliana na maafa kwa majanga ya mafuriko, vimbunga na tsunami; kuimarisha maghala ya kuhifadhi vifaa vya msaada katika kanda sita kwa kuongeza vifaa vya kutolea huduma za kibinadamu” ameongeza Mhe. Ummy.

Aidha, ameeleza kuwa serikali imefanya mafunzo kwa kamati za usimamizi wa maafa za mikoa na wilaya na voluntia pamoja na kutoa elimu kwa umma, wataalam wanaosimamia asasi za kiraia na waandishi wa habari kutoka katika redio za kijamii nchini kuhusu masuala ya usimamizi wa maafa.

Mbali na hayo Mhe. Ummy amebainisha kuwa, mafunzo hayo ni hatua ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya chama tawala ya Mwaka 2020 – 2025 ambayo katika Ibara ya 107 inaelekezwa Serikali kuchukua hatua za kuimarisha mifumo ya utendaji ya wizara, taasisi na mamlaka za serikali za mitaa ikiwemo kutoa elimu ya usimamizi wa maafa.

Nae, Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Eleuter Kihwele, amesema kuwa, mafunzo hayo yanayotolewa kwa siku mbili yataleta mchango katika kukabiliana na masuala ya majanga nchini.

Mkurugenzi Mtendaji, Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Makame Khatibu Makame ameeleza kuwa Zanzibar ipo salama na inaendelea kupambana na usimamizi wa maafa hivyo uwepo wa mafunzo hayo ni fursa kwao kujifunza mifumo ya kisasa ya namna ya kukabiliana na masuala ya maafa.

Kwa upande wake, Naibu Mwakilishi Mkazi, Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) Bw. Patrick Codja, amesema kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na serikali katika kutatua masuala mbalimbali yanayotoka na maafa.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.