Tanzania imeungana na mataifa
mengine duniani kuadhimisha siku ya Maafa Duniani ambayo hufanyika kila mwaka
ifikapo Oktoba 13 ili kuendelea kukabiliana na kupunguza madhara yatokanayo na
maafa nchini,
Akitoa Tamko la maadhimisho
hayo katika Uwanja wa CCM Kirumba leo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema maafa
usababisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo, ulemavu wa kudumu, upotevu
,uharibifu wa mali, miundombinu na mazingira huku watoto na vijana wamekuwa
wakikabiliwa na athari mbaya zaidi ikiwemo kukatizwa masomo, upungufu wa lishe,
athari za kiafya, ulinzi na usalama.
Ameeleza kuwa siku hiyo
ilianzishwa kwa Azimio namba 64/200 lililopitishwa na Baraza la Umoja wa
Mataifa Disemba 21 mwaka 2009 , huadhimishwa kila mwaka, ili kuunganisha juhudi
za kuwalinda watoto na vijana dhidi ya athari za majanga ambapo mikakati
mbalimbali imewekwa ikiwemo kutoa mafunzo ya kujikinga na maafa,elimu ya hali
ya hewa na jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,kuendeleza tafiti
kuhusu madhara ya maafa na kutoa taarifa kwa umma ili kuongeza uelewa.
Akirejea taarifa iliyotolewa
na serikali kupitia kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi zote kufuatia
mwelekeo wa mvua za vuli katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2024
uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) imeonyesha maeneo mengi ya nchi yanayopata mvua hizo hayatapata
mvua za kutosha hivyo wamejiandaa kuzuia, kupunguza madhara, kujiandaa kukabili
na hali hiyo sambamba na kurejesha hali
nzuri.
Akitaja hatua sita za
kuzingatia kukabiliana na hali hiyo amezitaka Mamlaka husika ziendelee
kuhamasisha na kuwezesha matumizi ya mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi pamoja na
utunzaji wa chakula cha binadamu na malisho ya mifugo, mamlaka husika
ziimarishe utoaji taaluma ya matumizi ya mbinu za kilimo zinazohitaji maji
kidogo pia taasisi za umma ikiwemo za elimu, afya na ofisi mbalimbali ziwe
mfano wa kuweka mifumo ya kuvuna, kuhifadhi na kutumia maji ya mvua.
Ameongeza kuwa hatua zingine
ni kuimarisha mikakati ya kuzuia milipuko ya magonjwa yanayoweza kujitokeza
kutokana na upungufu wa upatikanaji wa maji safi na salama,taasisi husika
zishirikiane na taasisi za elimu na mashirika ya maendeleo ili kutoa mafunzo
kwa wananchi kuhusu jinsi ya kukabiliana na ukame na Wizara yenye dhamana ya
elimu na taasisi zake kuhakikisha wanaendelea kuimarisha mitaala ya elimu ili
ijumuishe masuala ya usalama shuleni, kupunguza hatari, na uelewa wa majanga na
wakihakikisha mafunzo kwa walimu kuhusu mbinu za kufundisha masuala hayo kwa
wanafunzi.
"Kaulimbiu ya mwaka huu
ni "Elimu ni msingi katika kulinda na kuwawezesha vijana kwa mustakabali
wa baadae usio na maafa" ili kuungana na kaulimbiu serikali imeendelea
kushirikiana na wadau wa kitaifa na kimataifa kuimarisha mifumo ya elimu
inayolenga kutoa maarifa na ujuzi wa kupunguza madhara ya maafa kwa watoto na
vijana " anaeleza Mhe.Majaliwa
Pia serikali imefanya
uwekezaji mkubwa katika sekta ya hali ya hewa nchini ikiwemo kufunga
miundombinu ya kisasa ya hali hewa, mafunzo kwa watumishi kwa kuzingatia vigezo
vya kitaifa na kimataifa, na kuweka mifumo wezeshi ya usambazaji wa taarifa ya
hali ya hewa pamoja na kuimarisha mifumo ya uhakiki wa ubora wa huduma huku
uwekezaji wa miundombinu unajumuisha ununuzi wa rada za hali ya hewa.
"Ifikapo mwishoni mwa
mwaka huu, Tanzania itakuwa na rada saba ambapo ni kiwango kikubwa cha rada
katika nchi za Afrika Mashariki na kati nitumie fursa hii kumshukuru Rais Samia
Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa
katika eneo hilo pia kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa makundi maalumu na
kuweka mikakati thabiti inayolenga kuwawezesha vijana kiuchumi na kijamii
pamoja na kuhakikisha Serikali inatoa elimu kwa wigo mpana na kuwezesha vijana
kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto za majanga na kujenga jamii iliyo na
ustawi endelevu." anaeleza Mhe.Majaliwa.
Aidha aliwahimiza wananchi
wote, taasisi za elimu, na wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na
Serikali katika kuwajengea uwezo vijana kupitia elimu itakayowasaidia kujenga
stahimilivu dhidi ya majanga kwa sababu elimu ina nafasi kubwa katika
kuhakikisha kizazi cha leo kinakuwa na mbinu za kulinda mazingira, kuzuia
uharibifu wa maliasili, na kuhakikisha kuwa tunakuwa na mfumo thabiti wa
kukabiliana na majanga.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.