WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeadhimia kupambana vilivyo
dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya na kuhakikisha inakuwa
historia nchini.
Pia
ametoa wito kwa wazazi wote nchini waendelee kufuatilia nyendo za
watoto ili wasijiingize kwenye mtego wa dawa za kulevya na wala
wasisubiri vijana wao waanze kutumia.
Ametoa
kauli hiyo leo (Alhamisi, Juni 29, 2017) kwenye maadhimisho ya Kitaifa
ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani, iliyoadhimishwa mjini
Dodoma.
Kufuatia
hali hiyo Waziri Mkuu amesema Serikali imejidhatiti kuhakikisha kuwa
uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya unadhibitiwa
kikamilifu nchini.
Amesema
katika kutimiza azma hiyo, ambayo pia inaelekezwa na Ilani ya Uchaguzi
ya CCM, Serikali ilifanya mabadiliko ya Sheria ya Dawa za Kulevya kwa
kuanzisha chombo cha kisheria cha kupambana na biashara hiyo, ambayo
imeongeza adhabu kwa wanaoshiriki.
Waziri
Mkuu amesema Serikali itaendelea kuimarisha chombo hicho kinachoongoza
mapambano ya dawa za kulevya ili kiendelee kufanya kazi kwa weledi na
kwa kutumia mbinu za kisayansi.
“Tunaponadi
uchumi wa viwanda lazima tuwe na nguvu kazi yenye siha njema kuweza
kushiriki kwenye kazi halali za kujenga Taifa letu na yeyote anayetaka
kudhohofisha nguvu kazi ya Taifa letu au kuhujumu jitihada za uchumi wa
viwanda atashughulikiwa bila huruma,” amesema.
Aidha, kauli mbiu ya maadhimisho hayo kitaifa ni ‘Tuwasikilize na Kuwashauri Vijana na Watoto ili Kuwaepusha na Dawa za kulevya.’
Waziri
Mkuu amesema kauli mbiu hiyo imetokana nan a takwimu za waathirika
wakubwa wa dawa za kulevya ambao ni vijana wenye umri kati ya miaka
15-35.
“Hili
ndilo kundi kubwa kwenye jamii jetu na ndilo tegemeo kubwa kwa ustawi
wa nchi yetu. Hili ndilo kundi litakalotoa askari wa kulinda Nchi yetu,
wanasiasa wa kuongoza Taifa letu na wataalamu mbalimbali wa kuisaidia
Tanzania,” amesema.
Awali Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu),
Mheshimiwa Jenista Mhagama alisema matumizi ya dawa za kulevya
yamelisababishia Taifa madhara makubwa ya kiafya na kiuchumi hivyo kila
mwananchi ashiriki katika mapambano hayo.
Mapema Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi
la Kituo cha Kutoa Huduma ya Tiba kwa Waathirika wa Dawa za Kulevya
katika eneo la Itega mkoani Dodoma na kuwashauri wakazi wa mkoa huo
kutojihusisha na biashara hiyo.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.